Wednesday, August 10, 2022

WANAMUZIKI WA SASA WANAKUBALI KUKOSOLEWA?

 

Top Ten Show 1989

Jana nilikuwa naangalia maktaba yangu ya kanda za video za zamani, nikaiona kanda moja iliyonirudisha miaka mingi sana nyuma. Ilikuwa ni kanda ya video ya onyesho moja la bendi ya Tancut Almasi Orchestra lililofanyika katika ukumbi wa klabu ya bendi hiyo eneo la Sabasaba pale Iringa.
Mwaka 1989 yalianza kufanyika mashindano ya bendi yaliyoitwa Top Ten Show, mashindano haya yalifikia kilele mwaka 1990. Yalikuwa ni mashindano makubwa sana ya muziki wa dansi na mpaka leo hayajawahi kufanyika mashindano ya bendi yenye ukubwa ule. Mashindano haya yaliyotayarishwa kwa ushirikiano wa CHAMUDATA, Radio Tanzania na Umoja wa Vijana wa CCM, yalianza tarehe 29 Julai 1989 na kufikia kilele tarehe 25 November 1989. Bendi zilizoshiriki zilikuwa 50 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Arusha , Kilimanjaro, Tanga, Iringa,  Mbeya,  Morogoro, Rukwa , Kigoma na Pwani. Hii ilikuwa maendeleo kwani Top Ten Show ya mwaka 1988 ilikuwa na bendi 27 tu. Wafanyakazi wa Radio Tanzania Dar es Salaam  walizunguka katika mikoa mbalimbali na bendi za huko zilifanya maonyesho ambayo yaliyorushwa ‘live’  redioni na hivyo kuwapa wasikilizaji nchi nzima nafasi ya kusikiliza na kufuatilia mashindano hayo katika hatua zote.  Mwaka huo nilishiriki mashindano haya wakati nikiwa mmoja wa wanamuziki wa bendi ya TANCUT Almasi Orchestra iliyokuwa na masikani yake mjini Iringa.  Masharti ya mashindano tulipewa mapema sana. Kila bendi ilitakiwa ijitayarishe kwa nyimbo tatu, mmoja uwe unaitwa Nakulilia Afrika, wimbo wa pili ulikuwa lazima utokane na wimbo wa tuni ya asili ya kabila mojawapo la Tanzania na wimbo wa tatu uwe wimbo wowote ambao bendi ilipendelea kuupiga. Tulianza kufanya mazoezi makali  ya nyimbo hizo. Marehemu Kasaloo Kyanga na pacha wake Kyanga Songa wakaja na tungo yao ya wimbo Afrika Nakulilia, na mimi nikatoa mchango wa wimbo wa asili ya Kihehe ulioitwa Lung’ulye, kwa pamoja tukaamua kuwa wimbo wetu wa tatu uwe Ngoma za Afrika uliokuwa utunzi wa Kalala Mbwebwe.
Baada ya mazoezi makali tuliamua kufanya onyesho lisilo la kiingilio na kuwakaribisha wapenzi wa muziki wa dansi pale Iringa kuja kutoa maoni yao kuhusu matayarisho yetu hayo.  Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati huo, Mama Mary Chipungahelo alikuwa mgeni rasmi  wa onyesho hilo. Kilichofanyika pale siku ile, kilikuwa si kitu ambacho naona kitawezekana kwa urahisi katika zama hizi. Baada ya kupiga nyimbo zile wapenzi walikaribishwa jukwaani  kuongea ukweli kuhusu nyimbo zile, tuliomba waliotaka kutoa sifa wakae nazo, tulichokuwa nania nacho ni mapungufu katika matayarisho hayo. Hakika kulikuweko maneno makali ambayo sidhani wasanii wengi siku hizi wangekubali kukosolewa vile. Kulikuwa na kukosoa kuanzia mavazi, uchezaji na hata tungo zenyewe. Tungo ya Afrika Nakulilia iliyotungwa na akina Kasaloo ilikataliwa kwani ilionekana ilitokana na wimbo wa Pepe Kalle, hivyo muimbaji Kalala Mbwebwe na mpiga gitaa la solo Kawele Mutimwana wakaleta tungo nyingine ambayo ndio ilikuwa moja ya kete zetu katika mashindano yale.



Baada ya kuvuka kigingi cha wapenzi wetu wa Iringa, tulikuja Dar es Salaam na tulikuwa tumepangiwa katika kituo cha ukumbi wa Silent Inn uliokuwa eneo la Mpakani Dar es Salaam. Katika onyesho hilo, tulikuwa jukwaani pamoja na bendi iliyokuwa ikiitwa Orchestra Linga Linga Stars wakati huo muimbaji wake mahiri alikuwa Karama Regesu ambaye kwa sasa yupo Msondo Music Band. Tancut tukaibuka kuwa katika bendi kumi bora na kuja kushiriki fainali za onyesho lile zilizofanyika uwanja wa Taifa. 
Baadhi ya bendi zilifika kumi bora  zilikuwa, Tancut Almasi, Super Matimila, MK Group, Salna Brothers, Varda Arts, Bima Lee, Kilimanjaro Band na Vijana Jazz Band, hakika Uwanja wa Taifa palipendeza siku ile. Lakini kwangu mimi mambo yalikuwa na utata kidogo kwani siku ya fainali, nilikuwa nimeshamia Vijana Jazz Band, lakini kwa siku hiyo nilirudi bendi yangu ya zamani ya  Tancut Almasi  kwani wakati wa mashindano nilishiriki katika bendi hiyo. Uwanja wa Taifa ulijaa wanamuziki wengi sana, na kwa kuwa bendi zilikuwa na ustaarabu wa kuvaa sare, basi sare za aina mbalimbali zilitawala siku hiyo.

Ushindi wa TANCUT

 Hatimae matokeo yalitangazwa na kila wimbo ulikuwa na mshindi wa kwanza mpaka wa kumi, washindi watatu wa kwanza wakipata zawadi mbalimbali. Wimbo wangu wa asili ya Kihehe, ulishinda zawadi ya kwanza katika nyimbo za kiasili na washiriki wote tulipewa ‘radio cassette’ zilizotolewa na Ubalozi wa Uholanzi. Wimbo Afrika Nakulilia ulishika nafasi ya pili na wimbo uliokuwa chaguo la bendi ulikuwa Ngoma za Kwetu uliokuwa utunzi wa Kalala Mbwebwe ulichukua nafasi ya nne katika kundi lake, Kwa ujumla matokeo yalikuwa mazuri sana kwa bendi ya TANCUT Almasi.
Wanamuziki na viongozi wa TANCUT ALMASI Orchestra wakiwa na zawadi zao


 Art Critic

Katika nchi ambazo sanaa imekuwa, huwa kuna watu wanaoitwa ‘art critics’, hawa kwa kweli ni mabingwa katika fani za sanaa wanazo shughulikia na wao kazi yao moja kubwa ni kukosoa kazi mbalimbali za sanaa na hatimae hata kuzipa grade. Kwa mtizamo wa haraka haraka utaweza kudhani kuwa kukosoa kwao kunaweza kuharibu soko la sanaa husika, lakini kwa kuwa hawa watu huwa wakweli na wenye uzoefu, wasanii huwa wanafuatia sana watu hawa wanasemaje kuhusu kazi zao. Kupasishwa na watu hawa hupandisha thamani ya sanaa husika. Wakosoaji hawa pia huwafanya wasanii wawe makini katika kazi zao na hivyo ubora wa sanaa nzima unapanda.  Kitendo cha bendi ya TANCUT kuruhusu kukosolewa kabla ya kuingia katika mashindano ilikuwa sababu moja wapo ya bendi kupata ushindi mnono katika mashindano yale. Wasanii wa sasa hapa nchini wako tayari kukosolewa?

Friday, August 5, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU ARUSHA NA MOSHI

 

The Ambassador Band ya AICC

Safari ya kuzikumbuka bendi zetu leo inatufikisha miji ya kaskazini mwa nchi yetu. Jiji la Moshi na jiji la Arusha. 
Tuanze na jiji la Moshi, hakika  ukisikiliza hadithi mtaani za siku hizi unaweza ukadhani Moshi si mji wa kuwepo katika historia ya muziki, lakini kinyume kabisa, huwezi kuongelea historia ya muziki Tanzania bila kutaja Moshi. Kwanza kuna mchango mkubwa wa wanamuziki waliotoka Moshi, na pili kati ya wawekezaji wakubwa katika muziki waliowahi kutokea Tanzania, waliotoka Moshi.
Taja bendi karibu zote zilizokuwa kubwa miaka ya sitini na sabini utaukuta mkono wa muwekezaji toka Moshi.
Wanamuziki wa Moshi walianza kuiweka Tanzania katika ramani ya muziki wa Afrika ya Mashariki kuanzia miaka ya 50. Mabingwa kama Frank Humplick na Dada zake, ambao walikuwa watoto wa  baba muhandisi kutoka Austria na mama Mchaga,  Dr Hosea Macha na mke wake, Dr Hosea alikuwa baba mzazi wa mwandishi na msanii maarufu Freddy Macha,  Kimambo Brothers na wengine wengi waliweza kurekodi nyimbo zao kwa mtindo ule wa kutumia gitaa kavu, yaani gitaa lisilotumia umeme. Frank Humplick alirekodi nyimbo nyingi na wasanii wa Kenya chini ya lebo ya Jambo, ukiwemo wimbo maarufu Mi Francois mi naimba,ambao alifanya ‘kolabo’ na mwanamuziki kutoka Kongo Edward Mazengo, mambo yote hayo kabla ya Uhuru.
Baadhi ya bendi nyingine  zilizokuweko Moshi ni Ringo Jazz, halafu kulikuweko na Black Beatles, hawa walikuwa wakivaa kama wale wanamuziki wa Beatles wa Uingereza, walikuwa na gari lao la Combi ambalo waliliandika maandishi makubwa Black Beatles.  Moshi pia ilikuweko bendi maarufu ya Zaire Success, hii ilikuwa bendi ya vijana wa Kikongo. Kulikuwa na hadithi zamani ikisema hawa walikuwa ni kundi lililovunjika kutoka kutoka kwa kundi la Orchestra Fauvette la akina King Kiki na Ndala Kasheba Supreme, hata lile kundi la bendi ya Wakongo la Mwanza lilioitwa Orchestra Super Veya nayo husemekana ilitokana na mpasuko wa Orchestre Fauvette.
Mara ya mwisho kuingia muziki wa Zaire Success ilikuwa mwaka 1974 walipopiga community center Same, siku ilipofunguliwa Benki ya kwanza mji huo. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bwana Peter Kisumo. Mimi na rafiki zangu tulizuiliwa kuingia kwa kuwa kulikuwa na mgambo mlangoni kazi yake ilikuwa kuangalia waliovaa nguo zisizofaa,  tulikuwa tumevaa suruali zetu zilizokuwa pana chini, maarufu kwa jina la bugaluu. Ikalazimu kwenda kubadili ili kuweza kuingia dansi lile.  Nigusie hapa kuwa kuwa Same pia kulikuwa na bendi iliyoitwa TANU Youth League Jazz Band, kuna Askofu maarufu alikuwa mwanamuziki wa bendi hiyo miaka hiyo ya 70.

Chuo cha Polisi cha Moshi maarufu kwama Police Training School, PTS, kwa miaka mingi ilikuwa na bendi moja nzuri iliyokuwa ikitumbuiza mjini Moshi mara kwa mara. Moshi pia kulikuwa na bendi iliyokuwa inaitwa Bana Afrika Kituli, awali ilikuwa bendi kubwa ikaapoteza umaarufu mpaka ikawa inapiga kwenye vilabu vya mbege. Mmoja wa wanamuziki wa bendi hii niliwahi kumkuta Tanga akiwa amebadili taaluma na kuwa mganga wa kienyeji. Ni jambo la ajabu kidogo lakini kuna wanamuziki wengi sana ambao walikuja kuacha muziki na mkuwa waganga wa kienyeji.
Shule ya sekondari ya Old Moshi na hata Shule ya Ufundi ya Moshi ( Moshi Tech), zote zilikuwa na bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki kwa umahiri wa hali ya juu. Bendi ya shule ya Old Moshi walijiita Orchestra Mosesco. Baadhi ya wanamuziki wa bendi hii walikuwa Joseph Mkwawa, Pelegrin, Mwakibete, Tamba, Kufakunoga  na kadhalika.
Tuhamie Arusha, mji ambao katika miaka ya mwanzo ya sabini ulikuwa umechangamka sana kutokana na kuwa na wafanyakazi wengi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, halafu ukijumlisha na  biashara ya utalii, hakika mji ulikuwa na burudani nyingi. Hoteli za kitalii zilizokuwa chini ya Shirika la utalii Tanzania, karibu zote zilikuwa zikishindana kuwa na bendi bora hotelini, bendi kama The Revolutions, ambayo baade iliitwa Kilimanjaro Band, The Bar Keys ambayo ikaja kuitwa Tanzanites ni baadhi ya bendi ambazo zilitamba sana kwenye mahoteli ya Arusha. Bendi chache nyingine zilizokuwa zikipiga mahotelini ni Juju Masai ya akina Sabuni, hawa walikuwa ndugu waliokuwa mahiri sana katika muziki,  Crimson Rage, Ambassadors akina Andy Swebe na Likisi matola (wanaoonekana pichani), Tonics ya David Marama  na kadhalika.

Kwenye uwanja wa muziki wa Rumba kulikuwa na bendi kama Orchestra National, bendi ambayo ndio aliyoanzia muimbaji mahiri sana Hassan Bitchuka kabla ya kuonekana na NUTA Jazz Band. Kulikuwana Arusha Jazz Band, bendi iliyokuwa ya akina Wilson Peter na wenzie baada ya kuihama Jamhuri Jazz Band ya Tanga. Arusha Jazz Band ilihamia Mombasa na ndipo ikabadili jina na kujiita Simba wa Nyika, umaarufu wa bendi hiyo unafahamika kwa wapenzi wote wa muziki wa zamani. Arusha pia kulikuwa na bendi ya Chuo Cha Jeshi Monduli, bendi iliyoitwa Les Mwenge, bendi iliyokuja kupata umaarufu mkubwa kutokana na album ya wimbo Kila munu ave na kwao wa Halila Tongolanga.

Ukurugenzi wa Mkoa wa Arusha  ulianzisha bendi, nadhani ulikuwa ukurugenzi wa kwanza kufanya hivyo baadae mikoa mingine ikafuatisha. Bendi hiyo  iliundwa na  wanamuziki wa bendi ya Orchestra Lombelombe, bendi iliyokuwa ni matokeo ya mpasuko wa Morogoro Jazz band. Bendi hiyo mpya ikaitwa Kurugenzi Arusha. Kurugenzi Arusha ilitunga nyimbo kadhaa zilizotikisa anga ya muziki nchini, nyimbo  kama vile Wivu na Ujamaa mpaka leo bado zina wapenzi lukuki. Mwisho huwezi kuongelea bendi za Arusha bila kuitaja  Serengeti Band, bendi iliyoanzishwa na mmoja ya wanamuziki wa Orchestra Mkwawa iliyokuwa bendi ya shule ya Mkwawa, mwandishi mkongwe Danford Mpumilwa, hakika bendi hii nayo ilichangamsha jiji la Arusha.

Thursday, July 28, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 6 -MBEYA

 


Hebu tuendelee na safari ya kukumbuka bendi mbalimbali nchini, leo tuanzie mkoa wa Mbeya, tuanze na wilaya ya Mbeya, wilaya ambayo kabla ya mwaka 1927 ilikuwa ikijulikana kama wilaya ya Igali.
Mbeya ilikuja kuanza kupata umaarufu kutokana na kugundulika kwa dhahabu sehemu mbalimbali za kuzungukia mji huu kuanzia mwaka1906, hali iliyoendelea kwa karibu miaka ishirini baada ya hapo. Mji ukapata wageni kutoka kila kona ya Afrika Mashariki na Kati mpaka visiwa vya Ngazija, watu wakaja Mbeya na miji jirani kutafuta utajiri.

Popote penye vijana wengi, tena wakiwa wanatafuta pesa, hakukosekani burudani na hasa burudani ya muziki. Bahati mbaya si mengi yaliyohusu burudani za wakati huo yaliyowekwa kwenye kumbukumbu,lakini kati ya machache tuanze na historia ya mtu moja aliyekuwa maarufu sana aliyeitwa John Benedict Mugogo Mwakangale, mwenyewe alipendelea kuitwa JBM. John Mwakangale, JBM alikuwa mwanasiasa mashuhuri katika harakati za kupigania Uhuru na baadae katika siasa ya kutafuta umoja wa Afrika. Alifanya kazi kubwa ya kutambuliwa na hatimae alikuweko katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Tanganyika huru chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na akateuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa Kazi, pia alikuwa Mbunge wa Nyanda za juu kusini kwa kipindi kirefu, kabla ya Uhuru na hata baada ya Uhuru. Pamoja na yote hayo JBM pia alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki. Kati ya mwaka 1959 na mwaka 1960 alikwenda Zambia, wakati huo ikiitwa Northern Rhodesia, alikwenda kununua vyombo vya muziki kwa ajili ya bendi yake iliyoitwa Free Mwakangale Jazz. Alipokuwa huko akakutana na vijana kutoka jimbo la Luanshya waliokuwa  na kundi lao      wakipiga vizuri sana muziki, akaongea nao na hatimae wakakubaliana kuondoka kwao na kuingia Tanganyika kujiunga na Free Mwakangale Jazz, mmoja wa vijana hao alikuwa Michael Enoch. Michael Enoch baadae alikuja kuchukuliwa na Dar es Salaam Jazz Band na kuiendeleza kwa miaka mingi akiwa mpiga solo, kisha akahamia Dar es Salaam International akiwa mpiga saksafon  na hatimae Mlimani Park Orchestra alikoendeleza umahiri wake katika saksafon, na kupewa majina mengi ya sifa, King Enoch, na Teacher, Michael alikutwa na mauti  alipokuwa DDC Mlimani Park Orchestra.
Bendi ya Free Mwakangale Jazz makao yake makuu yalikuwa mji uliopewa jina la Neu Langenburg na Wajerumani lakini wote tunaufahamu siku hizi kama Tukuyu, , pamoja na Michael Enoch bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki wengine wanaokumbukwa ni Ben Jack na Saiz Vera.
Kuna hadithi ya kuchekesha na kusikitisha kuhusu kisa kilichofanya Free Mwakangale Jazz ife na Michael Enoch atue Dar es Salaam Jazz Band.
Siku moja  bendi ya Free Mwakangale Jazz ilipata safari ya kwenda Mwanza na baada ya kufika huko ilifanya maonyesho kadhaa, siku moja vijana hawa walikodi gari ili kubeba vyombo vyao, pengine wakati huo kwa ugeni na pengine hata Kiswahili walikuwa hawajakifahamu sawasawa, dreva wa gari akawaomba wamsubiri akaweke mafuta, wakamruhusu, alipoondoka hakuonekana tena ukawa ndio mwisho wa Free Mwakangale Jazz. Wanamuziki wakajikuta wamekwama Mwanza, bahati nzuri baada ya muda mfupi walipata kazi ya kupiga muziki katika bendi moja pale Mwanza, wakiwa katika bendi hiyo, muwakilishi wa Dar es Salaam Jazz Band , marehemu Limi Ally,ambaye alikuwa katika harakati za kumtafuta mpiga gitaa la solo akamuona Michael Enoch, na ndipo wakakubaliana kurudi nae Dar es Salaam kujiunga na Dar es Salaam Jazz Band.

Bendi nyingine ya Mbeya ilikuwa TANU Youth League Jazz Band, bendi iliyokuwa maarufu miaka ya sitini na ilirekodi nyimbo kadhaa RTD, kati ya nyimbo zake zilizokuwa maarufu ni ule ulioitwa Nampenda Firida mwenye macho mazuri. Kulikuwa na bendi nyingine ambayo ilisemekana ilitokana na kufa kwa TANU Youth League Jazz Band ilikuwa ikiitwa  bendi ya Lemi au Remi.

Bendi nyingine iliyokuweko Mbeya ni hiyo iliyoko kwenye picha ambayo iliitwa Azimio Co Bantou Jazz Band. Ukiangalia vizuri picha hiyo, utaona ilipigwa katika kota zilizokuwa za wafanyakazi wa  serikali zilizokaribu na mitaa ya Ghana, pengine hapo ndipo yalikuwa masikani ya bendi hii.

Katika tasnia ya muziki wa bendi kuna utamaduni wa kuigana majina, kwa mfano baada ya kuundwa bendi ya Dar es Salaam International Orchestra, bendi nyingi ziliibuka na kujiita international, zikiwemo Dodoma International Orchestra, Tanga International Orchestra, Ruaha International Orchestra na kadhalika. Kule Sumbawanga ikaundwa bendi iliyoitwa Rukwa International Orchestra, bendi hii ilijitokea sana na kushiriki matukio ya kitaifa. Rukwa International Orchestra ilikuwa mojawapo ya bendi zilizojitokeza kushiriki Mashindano ya Bendi Bora (MASHIBOTA) yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam miaka ya 90.

Thursday, July 21, 2022

KAMIKI WIMBO WA MIAKA YA SABINI UNAOKUMBUKWA NA WAZEE MPAKA LEO

Kamiki yeye motema aaa, Kamiki yeye motema oooo. Wapenzi wa muziki wa kavasha wa miaka ya 70 na 80, hawakosi kuanza kutabasamu, mistari hiyo niliyoanzia habari hii ilikuwa ni maneno ya mwanzo ya wimbo maarufu enzi hizo, wimbo ulioitwa Kamiki. Wimbo huu ulipigwa na bendi  iliyoitwa Orchestra Kiam kutoka Kongo. Bendi hii ilikuwa na nyimbo nyingi sana zilizopendwa sana karibu Afrika nzima. Wakati huo ulikuwa ndio wakati ambapo vijana waliojiona wa kisasa Afrika nzima walikuwa wakivaa suruali pana zilizoitwa Bugaluu na viatu vyenye soli ndefu ambavyo vilifahamika kama platform. Shati zilikuwa ni zenye kubana sana na siliitwa ‘slimfit’, huku kichwani kila kijana mjanja alikuwa nafuga nywele ndefu zilizokuwa zikichanwa kwa mtindo wa Afro. Vijana wa kiume walikuwa wakitumia sana chanuo za chuma ambazo zilipashwa moto kisha kunyoosha nywele ili ziwe ndefu. Lakini turudi kwa Orchestra Kiam, historia ya kundi hili ilianza baada ya Papa Noel, mwanamuziki mkongwe wa Kongo aliyepigia bendi nyingi maarufu za Kongo ikiwemo TP OK Jazz, kuwa na taratibu za kusaidia vijana waliotaka kujiendeleza kimuziki waliokuwa wakiishi jirani na kwake, hivyo basi  alitengeneza bendi iliyoitwa Orchestra Bamboula, bendi hii haikuwa na vyombo, vijana walifanya mazoezi kwa magitaa makavu nyumbani kwa mkongwe huyu na walipo bahatika kupata sehemu za kufanya  onyesho, Papa Noel alikuwa akikodi vyombo na bendi kuweza kupiga, lakini kwa mtindo huu mara nyingi hawakupata malipo mazuri, lakini nia yao ilikuwa kupiga muziki na si kusaka fedha.
Siku moja Papa Noel alisafiri na TP OK Jazz kwenda kufanya onyesho nchini Algeria aliporudi alikuta vijana wake wamesambaratika, basi akatafuta vijana wengine na kuunda kundi jipya lililofanya mazoezi miezi sita. Baada ya muda huo Papa Noel alienda kwenye studio ya mkongwe mwingine wa muziki  wa Kongo ,Verckys, na kulipia gharama za kurekodi, kundi la Bamboula  likaingia studio na kurekodi na chini ya fundi mitambo wa studio hiyo Kidiata M’Pole, bendi hiyo ikarekodi  nyimbo nne katika muda wa masaa machache, kama ilivyokuwa taratibu miaka hiyo.
Ilikuwa ni kawaida ya Verckys kusikiliza nyimbo  zilizorekodiwa katika studio yake, na aliposikia nyimbo hizo mpya akamtuma meneja wake kuwatafuta vijana waliopiga muziki  huo. Meneja wake aliyekuwa anamfahamu Frank Muzola Ngunga, akaanza msako. Muzola alipopatikana alisema wana nyimbo nyingine pia ambazo hawajazirekodi, wakaalikwa kuzirekodi zote, Muzola akasita kurekodi nyimbo hizo kwani alihisiki atakuwa anamsaliti Papa Noel, wenzie wakamshinikiza hatimae akakubali. Wakati huo Papa Noel alikuwa akitafuta fedha za kukamilisha malipo ya kuweza kutengeneza santuri ya nyimbo nne zilizorekodiwa na pia kumlipa fundi mitambo aliyezirekodi. Kesho yake Papa Noel alikwenda studio kukamilisha malipo alishangaa kukuta kundi lake likiwa studio linarekodi likiwa linasikilizwa na Verckys, ugomvi mkubwa ukaanza hapohapo, lakini hatimae Verckys alimzidi kete Papa Noel kwa kumtaka aonyeshe mkataba wake na wana muziki hao. Papa Noel aliondoka kwa hasira hakuna anaejua alizipeleka wapi nyimbo zile nne zilizorekodiwa kwani hata yeye alipoulizwa miaka mingi baadae alisema hakumbuki.
Verckys aliamua kuliita kundi lake jipya,  Orchestra Kiam, Kiam ikiwa kifupi cha Kiamwangana jina halisi la Verckys. Wanamuziki waanzilishi wa kundi hili walikuwa Frank Muzola Ngunga, Bakolo Keta, Jeannot Botuli Ilonge na Mboyo Bola Eddie waimbaji, wapiga gitaa la solo walikuwa  Guyno na Souza Vangu (Souza alijiunga miezi michache baadae), wapiga gitaa la  rhythm walikuwa  Lélé Nsundi na Djo Morena, kwenye gitaa la bezi alikuweko Vieux Kody na mpiga drums  Suké Ngonge. Wanamuziki hawa wakaingia mkataba na Verkcys akampa kila mmoja wao fungu la bonas ya kujiunga na bendi na kisha wakawa wanalipwa mshahara, shilingi alfu thelathini katikati ya mwezi na shilingi alfu sabini mwisho wa mwezi, na wengine pia wakanunuliwa samani kwa ajili ya vyumba vyao, hakika walijiona wamepata mfadhili wa kweli ukikumbuka kuwa kwa Papa Noel, walikuwa wakiishi kwa kubahatisha. Walikabidhiwa vyombo vipya wakawa wanafanya mazoezi siku tatu kwa wiki na siku za wikiendi wakawa wanapiga katika kumbi mbalimbali ambazo zilikuwa zimeingia mkataba na Verckys. Verckys aliendeleza utaratibu huu wa kuwa na bendi alizozilipa mshahara mdogo na kupata mapato makubwa kutokana na kuzikodisha kwenye kumbi na pia kuuza santuri za bendi zilizokuwa chini yake.
Mwaka 1974 Orchestra Kiam waliingia studio na kurekodi wimbo wa Nina, wimbo wao wa kwanza kupendwa sana, ulikuwa utunzi wa  Bakolo Keta, utunzi mwingine wa Bokolo ulioitwa  Baya-Baya ulisaidia sana umaarufu wa bendi hii. Umaarufu wa Kiam ukaanza kuwapa uchu matajiri wengine kuimiliki bendi hii. Mfanya biashara mmoja Mbuta Suka alianzisha label yake aliyoiita Mabele Productions, na  mwanzoni mwa mwaka 1975 aliwashawishi wanamuziki kadhaa wa Kiam kuja kurekodi kwa kutumia label yake  kwa kutumia utaratibu  ulioitwa zong zing, yaani kurekodi nje ya bendi. Kundi kubwa la Kiam lilishiriki kazi hii na kurekodi nyimbo nne. Mbuta Nsuka alianza kusambaza santuri za nyimbo hizo na kuzitambulisha kuwa zimepigwa na Orchestra Baya-Baya, Verckys alipozisikia nyimbo hizo alijua ni bendi yake akawasimamisha kazi wanamuziki wote walioshiriki. Mbuta Nsuka akatumia fursa hiyo kuwashawishi wanamuziki hao waachane na Verckys, na ndipo rasmi ikaundwa bendi ya Orchestra Baya- Baya.

Huku Orchestra Kiam kikawa kilio maana waliobaki walikuwa ni muimbaji Frank Muzola Ngunga, mpiga bezi  Vieux Kody na mpiga rhythm Djo Morena. Muzola Ngunga akapewa kazi ya kutafuta wanamuziki wengine kufufua bendi.  Baada ya kama mwezi kundi likafufuka na waimbaji Germain Kanza, Adoly Bamweniko na Otis Mbuta, kwenye magitaa akapatikana mpiga solo Adamo Lewis na  Djuké, kwenye gitaa la rhythm akaweko Antoine Denewadé. Baada ya mazoezi ya miezi michache Kiam wakarudi tena studio. Hapo ndipo vikatoka vibao maarufu kama Memi, Yanga Yanga na Kobondela .

Wakati huo Orchestra Baya-Baya walianza safari ya kuzunguka kupiga muziki miji mbalimbali, muda si mrefu bendi ikakwama  katika mji wa Bandaka kutokana  na kukosekana mapato.  Ukawa mwisho wa Orchestra Baya- Baya, Lélé Nsundi ,Bakolo Keta na Suké Ngonge wakarudi Orchestre Kiam. Huyu Lélé Nsundi alikuwa mpangaji mzuri sana wa muziki hivyo ilianza kazi  nzuri sana ya  nyimbo mpya ikianzia na wimbo maarufu wa Kamiki , wimbo huu ulitungwa na Muzola Ngunga kumsifia mwanamke aliye kuwa akiishi nae wakati huo. Wimbo huo ulipendwa Afrika nzima wakati huo na hata leo. Mpaka mwaka 1977 Kiam waliendelea kutoa vibao motomoto kama Ifantu, Bomoto, Ya Yona, Mbale, Bakule, Masumu na kadhalika. Mwezi Agosti mwaka 1978, Kiam walirekodi wimbo ulioitwa Exode  wakiwa na muimbaji mualikwa kutoka Gabon alieitwa Mack Joss. Mark akawazindua kuhusu hakimiliki na jinsi Verkcys alivyokuwa akiwadhulumu haki zao hizo, kwa kuwapa mshara tu bila kuwapa mirabaha iliyotokana na mauzo ya santuri walizotunga na kushiriki. Elimu hii ikawafanya  Bakolo Keta , Lélé Nsundi na Adoly Bamweniko, kuondoka Kiam mara moja. Lilikuwa pigo kubwa kwa Kiam kwani baada ya hapo hawakuweza kutoa tena nyimbo za kutikisa wapenzi wao.

Verckys alijitahidi sana kulitambulisha kundi la Kiam Afrika ya Mashariki na Afrika ya Magharibi, jambo ambalo lilifanya kundi hili kukumbukwa zaidi katika maeneo haya kuliko Kinshasa kwenyewe mpaka leo. Lakini hatimae mwaka 1983, Muzola Ngunga na Verckys waliamua kulivunja rasmi kundi la Orchestra Kiam.

 

Wednesday, July 20, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 5

Katika safari yetu ya kuzikumbuka bendi mbalimbali nchini, kuna kitu kinaonekana wazi kabisa, katika swala la muziki kwa ujumla tumerudi nyuma sana. Kulikuwa na bendi binafsi, bendi za serikali , bendi za chama tawala na karibu kila mji ulikuwa na zaidi ya bendi moja. Watu walikuwa wachache sana kuliko siku hizi lakini walikuwa na na nafasi za uchaguzi wa burudani kuliko siku hizi. Sababu ni nyingi lakini si nia ya makala hizi kuongelea hayo japo baada ya mzunguko wa nchi nzima pengine italazimika kujiuliza tumefikaje huku tuliko? Kabla ya kuendelea na safari kuna kitu kiko wazi kinajitokeza, wakati wa awamu tatu za mwanzo za uongozi wa nchi hii, wasanii wa kila mahala walithaminika, ndio maana unakuta kila mkoa kulikuweko na makundi ya muziki ambayo hatimae yaliweza kujitokeza na kufahamika nchi nzima. Siku hizi ni kawaida kabisa viongozi wa juu kuoneka wakisindikizwa na wasanii ‘wakubwa ‘ wa kutoka Dar es Salaam, utadhani huko wanakokwenda hakuna wasanii, au wanaenda nchi nyingine kutangaza sanaa ya nchi yao.
Safari yetu leo inatupeleka mikoa ya kusini, mikoa hii haikuwa nyuma kabisa katika mambo ya dansi, kulikuweko na bendi toka enzi ya mkoloni. Kati ya bendi ambazo nina kumbukumbu nazo, nianze na White Jazz Band iliyokuwa na masikani yake mjini Lindi,  bendi hii kama zilivyokuwa bendi nyingine ilipitisha wanamuziki wengi lakini kati ya wanamuziki waliokuja kung’aa nchini waliopitia bendi hii ni marehemu Mzee Kasim Mapili, yeye alinza kupiga muziki katika bendi hii mwaka 1958, kuna kila sababu kuamini kuwa ilikuweko kabla ya mwaka huo. Mwaka 1963 tayari kulikuwa na bendi iliyokuwa inaitwa Jamhuri Jazz Band mjini Lindi, bendi hii ilikuwa mali ya TANU Youth League, au Jumuiya ya Vijana wa TANU. Jamhuri Jazz Band hii ya  ilikuweko kabla ya Jamhuri Jazz Band ile ya Tanga, japo tutakapofika mkoa wa Tanga tutapata historia ndefu zaidi ya bendi hiyo.

Wakati tukiwa bado Lindi, haiwezekani kutoitaja Mitonga Jazz Band. Bendi hii ilifanya makubwa kwa kutoa mfululizo wa vibao pendwa, kikiwemo Mariana na Sitaoa tena Mchinga, ambavyo vikipigwa mpaka leo bado wanaovisikia hata kwa mara ya kwanza huvipenda. Album ya wimbo Mariana ilirekodiwa na mafundi mitambo wa Radio Tanzania Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Polisi pale Lindi, lakini ubora wake unazishinda nyimbo nyingi zilizorekodiwa kwenye studio za kisasa, jambo linaloonyesha umahiri wa wanamuziki wa bendi hiyo, na umahiri wa mafundi mitambo.
Tukitoka Lindi tuingie mji wa Masasi, mji huu nao ulikuwa na bendi nyingi na ni mji ambao umewahi kutoa wanamuziki wengi ambao walikuja kuwa maarufu Afrika ya Mashariki nzima. Tuanze na Masasi Jazz Band, bendi hii ilitoa wanamuziki  maarufu kama  Gerald Nangati, wapiga gitaa la rhythm wawili mahiri, Ally Makunguru aliyekuja kupigia bendi za JKT Kimbunga Stereo, Mlimani Park, International Orchestra Safari Sound na hatimae kuhamia Kenya ambako pia alipiga muziki katika bendi kubwa maarufu za huko. Masasi Jazz Band ndiko alikotoka  Charles Kasembe ambaye alikuja kupiga na Mbaraka Mwinshehe, akapitia Dodoma International Orchestra na hatimae akahamia Kenya alikokuwa na bendi yake ya Les Volcano.

Bendi nyingine iliyokuweko Masasi ilikuwa Umoja Jazz Band, pia kulikuweko na TANU Youth League Jazz Band katika mji huo, jambo lililokuwa kawaida katika miji mingi, ni wazi kulikuwa na sera za makusudi za TANU kuhakikisha kila wilaya kuna kuwa na bendi ya vijana wa TANU. Bendi hii ya TANU Youth League Jazz Band ndio ilikuwa bendi ya kwanza ya mwanamuziki mwingine aliyekuja kuwa mpiga solo mahiri sana katika bendi za JKT Kimbunga Stereo na DDC Mlimani Park Orchestra Mzee Henry Mkanyia.
Kwa mara ya kwanza nilipokutana na Ally Makunguru mwaka 1975, alinambia kuwa alipokuwa Masasi pia alikuwa akipigia bendi iliyokuwa ikiitwa Kochoko Jazz band, hiyo ni bendi nyingine ya mji huyo. Masasi ulikuwa mji mdogo sana wakati huo lakini ulikuwa na bendi nyingi kiasi hiki, na hizi nilizotaja hapa, ni zile zilizoko katika kumbukumbu zangu tu.

Nachingwea nako hakukuwa kimya kulikuwa na bendi iliyoitwa Mondomondo Jazz band, bendi iliyokuwa ikileta burudani kwa wakazi wa mji huo.
Mtwara ulikuwa mji mwingine wa maraha kule kusini mwa Tanzania, toka miaka hiyo mpaka leo Mtwara imeendelea kutoa wanamuziki mahiri ambao wamekuwa waking’aa kitaifa na kimataifa. Kati ya bendi zilizowahi kuweko Mtwara tuanze na bendi iliyochukua jina la mji huo Mtwara Jazz Band, pia mapema baada ya Uhuru ilikuweko bendi iliyoitwa Honolulu Jazz Band. Mamlaka ya Bandari katika miaka ya zamani ilikuwa inajihusisha sana katika michezo na utamaduni, na hapo Mtwara ikaanzisha bendi ilioyoitwa Bandari Mtwara Jazz Band. Lakini pia ziliwahi kuweko bendi nyingine zaidi katika mji huu, kulikuwa na Mambo Jazz Band na bendi nyingine iliyoitwa Bantu Jazz Band… Kwa leo nimalizie kwa kuitaja bendi iliyokuweko mji ambao hautajwi sana linapokuja swala la bendi nao ni Kilwa Masoko. Mji huu nao ulikuwa na bendi yake iliyoitwa Lucky Star Jazz Band


Friday, July 15, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 4

Kama Franco Luambo Luanzo angekuwa hai mwaka huu angekuwa anatimiza miaka 84 kwani alizaliwa tarehe 6 Julai 1938, lakini kwa mapenzi ya Mungu alifariki tarehe 12 Oktoba 1989 akiwa na umri wa miaka 51 tu. Wakati Franco akiwa na umri wa miaka 6 tu Morogoro Jazz Band ilianzishwa katika mji wa Morogoro. Kuna somo kubwa hapa, kwa bahati mbaya kutokana na Tanzania kutokuandika historia yake ya muziki, watu wengi na hata wanamuziki wengi wa kizazi hiki hudhani kuwa nchi yetu iliiga toka Kongo maswala ya muziki wa bendi, lakini historia inaonyesha kuwa mambo hayakuwa hivyo hata kidogo kama tarehe hizo hapo juu zinavyoashiria wazi, pengine wanamuziki wetu wa zama hizo hawakujua hata kama Kongo kuna wanamuziki.

Leo safari yetu ya kuzikumbuka bendi zetu, imetuleta mkoa wa Morogoro, na kama unavyoona wakazi wa Morogoro tayari waliakuwa wakifurahia muziki wa bendi kabla hata ya vita ya piti kumalizika.
Morogoro Jazz band inajulikana na wengi mpaka leo hasa katika kipindi alichokuwepo Mbaraka Mwinyshehe Mwaluka. Wimbo maarufu wa Jogoo la shamba ni moja kati ya nyimbo za bendi hiyo ambazo hata watoto wadogo wa kizazi hiki wanaufahamu, na kuutumia katika kutaniana tena kwa utani unaofanana sana na nia ya kutungwa kwa wimbo huo.

Mwaka 1948 nguli mwingine wa Morogoro, Salum Yazidu Abdallah (SAY), mwanamuziki aliyezaliwa kutoka kwa baba Mwarabu na mama Mlugulu, alianzisha bendi yake aliyoiita La Paloma, neno la Kispayola likiwa na maana Njiwa. Wanamuziki na wapenzi wa rumba miaka hiyo, kwa ujumla walikuwa wakisikiliza santuri z Kispanyola kutoka Cuba. Santuri hizo zilizokuwa na namba zilizoanzia GV 1 na kuendelea hadi zaidi kidogo ya GV 200 zilikuwa na muziki kutoka bendi mbalimbali za Cuba, wanamuziki wa huku wakawa wanapiga muziki kuiga huo wa Cuba na hata kuunda bendi zao nazo kuzipa majina ya bendi zile za kule Cuba, ndio maana tukaziona bendi za Sextet Jazz ya Dodoma na Habanero Jazz Band ya Iringa. 
Salum Abdallah aliwahi kutoroka toka kwao Morogoro  na kwenda Mombasa ili azamie meli na kwenda Cuba kujifunza muziki, bahati mbaya kipindi hicho vita ya dunia ya pili ilikuwa imepamba moto na hivyo safari yake ikaishia Mombasa, alipata taabu sana Mombasa hatimae Umoja wa Waarabu wa Mombasa walimtaarifu baba yake aliyekuja kumrudisha mwanawe Morogoro.
Aliporudi Morogoro ndipo akaanzisha bendi yenye jina la ‘La Paloma’ jina lilitokana na wimbo maarufu wa Cuba ambao mpaka leo bado unapigwa na bendi zetu nyingi kama muziki wa ala mapema kabla ya kuanza rasmi kwa dansi.
La Paloma Band ilibadili jina na kujiita Cuban Marimba Band mwaka 1952, chini ya Salum Abdallah bendi ilirekodi nyimbo nyingi ambazo mpaka leo bado zinapendwa hata na vijana wa leo. Nyimbo kama Wangu Ngaiye, Shemeji Shemeji wazima taa, Wanawake na kadhalika  si ngeni masikioni mwa wapenzi wa muziki hata leo. Cuban Marimba ilikuwa maarufu kiasi cha kampuni za kurekodi kutoka Mombasa zilikuwa zikiifuata bendi  Morogoro ili kuirekodi. Wimbo maarufu wa Wanawake Tanzania ulirekodiwa Korogwe, baada ya kampuni ya kurekodi ya Assanand kuifuata bendi Morogoro na kukuta imesafiri. Baada ya kuitafuta hatimae wakakutana Korogwe. Wakati Assand akiwa njiani gari lake lilikwama kwenye matope, na aliomba msaada wa kusukumwa, wanawake wakajitokeza na kulisukuma gari lile. Asanand  alipomuhadithia mkasa ule Salumu Abdallah ndipo ulipotungwa wimbo maarufu wa Wanawake Tanzania.
Kwa mapenzi ya Mungu Salum Abdallah alifariki katika ajali ya ajabu mwaka 1965. Cuban Marimba ikawa chini ya Juma Kilaza. Kilaza aliendelea na bendi hiyo miaka kadhaa alipoiacha akaanzisha bendi yake iliyoitwa TK Lumpopo, ambayo mata nyingine alikuwa akiita TK Lumpopo National. Mbaraka Mwinyshehe nae alikuja kuicha Morogoro Jazz Band na kuanzisha bendi yake ya Super Volcano.
Kwa kipindi kifupi kwenye mwaka 1985 ilitokea bendi iliyoitwa Les Cuban. Vyombo vya bendi hii vilikuwa mali ya Chama Cha Mapinduzi  mkoa wa Morogoro, na alikabidhiwa Mzee Juma Kilaza ili kuona uwezekano wa kurudisha hadhi ya muziki Morogoro. Mzee Kilaza aliwaleta wanamuziki wa bendi ya Orchestra Vina Vina toka Nairobi, vijana aliyorekodi nao huko na kuwaona wako vizuri sana. Kati ya waliokuja na Orchestra Vina Vina alikuweko muimbaji mlemavu wa macho Nico Zengekala. Les Cuban  ikawa sasa inajitambulisha kwa mtindo wa Vina vina, ili kutokupoteza jina lao la awali, walifanya kazi kubwa ya kukumbukwa, nyimbo kama Kifuko cha Zambarau au Jackie ni wimbo bado maarufu mpaka leo. Lakini bendi iliingia katika matatizo ya kiutawala na kufa mapema sana.

Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza wa kwanza kulia




Tukirudi nyuma katika miaka ya sitini na sabini, bendi hizi mbili, Morogoro Jazz Band na Cuban Marimba Band ziliuchangamsha sana mji wa Morogoro kiasi cha kwamba siku za mwisho wa wiki, wapenzi wa muziki walikuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kustarehe. Wakati huo usafiri ulikuwa mgumu kwani sehemu kubwa ya barabara kati ya miji hii miwili ilikuwa ni ya vumbi.
Watu wa mkoa wa Morogoro hupenda sana muziki, kulikuwa na bendi. Inawezekana kabisa kuwa katika miaka ya 70 na 80 mkoa wa Morogoro ndio ulikuwa na bendi nyingi zaidi. Hasa ukizingatia kuwa karibu kila wilaya ilikuwa na bendi na tena zilizokuwa zikifahamika Kitaifa.
Kati ya bendi za Mkoa wa Morogoro zilizokuwa Mahenge ni Mahenge Jazz Band na Taifa Jazz Band, hii bendi ya pili ilianzishwa na  Joakim Ufuta ‘Dokta’, huyu alikuja kuwa mpiga gitaa  la solo maarufu sana katika bendi ya Cuban Marimba na TK Lumpopo. Mahenge pia kulikuwa na bendi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kwiro, Kwiro Jazz Band. Bendi hii ilirekodi mara kadhaa RTD, na wanamuziki wa bendi hiyo si mara moja walilalamika kuwa Morogoro Jazz Band iliwaibia mtindo wao wa Mahoka. Mpiga solo wa bendi ya shule ya sekondari ya Mkwawa, Orchestra Mkwawa, Simon Sewando alikuwa fundi mitambo wa bendi ya Kwiro kabla hajahamia shule ya Mkwawa. Alijulikana kwa jina ya ‘The mad scientist’ kutokana na kufumua fumua na kutengeneza amplifaya za bendi hiyo. Sewando amestaafu akiwa mwalimu wa electronics Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kulikuwa na Kilosa Jazz band ambako alitokea Abel Balthazar na mkasa wake wa kuhamia Dodoma Jazz band niliuandikia katika makala kuhusu bendi za mkoa wa Dodoma. Kulikuweko na Ifakara Jazz Band pia  Sukari Jazz band bendi iliyokuwa mali ya kiwanda cha Sukari cha Kilombelo, kulikuweko na  Ulanga Jazz band toka Ulanga na bila kusahau Njohole Jazz Band. Njohole Jazz Band walikuwa na nyimbo zao nyingi maarufu Afrika ya Mashariki nzima, kwa sababu walikuwa wakienda Nairobi kurekodi santuri za nyimbo zao. Lakini bendi hii ilikufa kutokana na mkasa wa kusikitisha sana. Walikuwa wakisafiri katika lori ambalo ndani yake pia kulikuwa na mzigo wa vinywaji, gari lile likapinduka na wanamuziki wote wakafa palepale, akabaki kiongozi wao tu aliyekuwa ametangulia kwa usafiri mwingine. Mungu awalaze pema…..Safari Iendelee.

Thursday, July 14, 2022

ZAMANI WATU WALIENDA DANSINI WAKAKUTA POMBE, SIKU HIZI WANAENDA KWENYE POMBE WANAKUTA DANSI

 

Kumbukumbu zangu huwa zinanirudisha Iringa nilipokuwa na umri wa miaka sita au saba hivi. Nadhani ndipo nilipoanza kutambua kuwa watu huwa wanaenda dansini. Maana mara kwa mara wazazi wangu walikuwa wanajitayarisha wanavaa nguo nzuri halafu wanatuaga ‘Haya laleni sisi tunaenda dansini’.
Moja ya dansi nakumbuka lilikuwa limepigwa na Cuban Marimba wakiongozwa na Salum Abdallah, nakumbuka kwa sababu kesho yake Mwalimu Nyerere alikuja kuhutubia watu wa Iringa kwenye uwanja ambapo upo sasa ni uwanja wa Samora. Wakati huo ulikuwa ni uwanja wa mpira wa shule ya Mshindo Middle School, na baba yangu alikuwa Headmaster wa shule ile. Nyumba yetu ilikuwa pembeni tu ya uwanja huo wa mpira. Siku hiyo alipokuja kuhutubia Mwalimu Nyerere, wimbo uliokuwa ukisikika kwenye spika ukirudia rudia, ulikuwa wimbo wa Cuban Marimba na baadhi ya  maneno yake yalikuwa ‘ Tutie jembe mpini, twendeni tukalime’, lazima ilikuwa baada ya Uhuru maana ndio nyimbo baada ya Uhuru zilivyokuwa na ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujenga nchi mkoloni kisha ondoka.
 Wakati wimbo huo ukiimba, mama yangu akatuambia na wadogo zangu kuwa wimbo huo walikuwa wameucheza jana yake dansini. 

Kwa kweli toka nikiwa mtoto, dansi kwangu ni neno la furaha  kwenye maisha yangu. Nikiwa mdogo  wazazi wangu walikuwa wakituonyesha namna ya kucheza aina mbalimbali za dansi, zikiwemo tap dancing, aina ya dansi ambayo visigino vya viatu lazima uvigonge kwa nguvu sakafuni wakati wa kucheza kufuatia mapigo ya muziki, hivyo basi vinatoa beat fulani kufuatana na wimbo, dansi moja ngumu kuicheza maana inachosha baada ya dakika moja tu. Tulifundishwa kucheza  chachacha, waltz, foxtrot na aina nyingine za dansi ambazo sijapata hata  kujua majina yake.

Nyakati hizo na miaka mingi baadae, mtu akiaga anakwenda dansini, jambo la muhimu atakalolifanya huko ni kucheza nyimbo nyingi kadri atavyoweza. Kesho yake mazungumzo kuhusu dansini ni kuulizana nyimbo ngapi zilichezesha. Mpenzi wa muziki kurudi nyumbani akiwa kachoka kwa kucheza ilikuwa ndio dalili ya kufurahia kwa usiku ule.

Miaka mingi baadae hatimae nikaja kuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi.  Hii aina ya muziki  uliokuja kuitwa muziki wa dansi, ulipewa jina hili kuanzia mwaka 1986 baada ya mkutano mkubwa wa wanamuziki ulioitishwa na Baraza la Muziki Tanzania kuja na wazo la kuwa na vyama vya muziki, ili kutofautisha na muziki wa Taarab, ndipo kikaundwa Chama cha Muziki wa Dansi na dhana ya muziki wa bendi ambao nia yake ilikuwa kucheza ukaitwa 'muziki wa dansi'.

Muziki wa bendi ambao sasa unaitwa muziki wa dansi, ulitungwa na hatimae kupigwa kwa vifaa vya kisasa na lengo kubwa ni kuwa wapenzi wa muziki huo watacheza.  Katika miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini, bendi zilikuwa zikitangaza aina muziki itakaoupiga, kwa mfano kiongozi wa bendi aliweza kutoa maelezo yafuatayo kabla ya kupiga wimbo. ‘Muziki ufuatao unaitwa Dada Adija, umepigwa katika mtindo wa Cha Cha’. Basi muziki ukianza wapenzi wa muziki wangeingia uwanjani na kucheza ChaCha. Na hivyo hivyo kama wimbo ni Twist, Bolelo, Charanga na kadhalika, hata kucheza kulikuwa na mpangilio unaoeleweka.

Tungo za zamani zilikamilishwa kwa muungano wa mawazo kutoka kwa wanamuziki mbalimbali katika bendi. Mtunzi wa awali aliweza kuleta  mashahiri, mara nyingine yakiambatana na melodia na kuwaimbia wenzie ambao walianza kutunga vipande vyao kupitia  vyombo mbalimbali wanavyovipiga. Tungo nyingi za awali zilianza kwa rumba, na ilipofika katikati mwendo ulibadilika na kuingia katika kile tulichokuwa tukikiita ‘chemka’.
 Chemka mara nyingi ilianza kwa kuimba na kisha kuingia kipande cha gitaa la solo. Hapa ndipo wapiga solo walikuwa wakipimwa kwa umahiri wao wa kutunga na kupiga vipande vya solo ambavyo vingeweza kuwateka akili wasikilizaji na kuwafanya wacheze dansi.



Katika bendi nilizopitia kama vile TANCUT Almasi na Vijana Jazz Band, baada ya bendi kukamilisha kuufanyia mazoezi wimbo, wimbo huo ulianza kupigwa katika maonyesho mbalimbali, lakini jambo la muhimu ambalo wanamuziki wote tulikuwa tukiliangalia lilikuwa ni Je, watu wanaucheza wimbo mpya? Ikionekana wimbo  umekosa hamasa ya kuwasimamisha  wachezaji, wimbo huo ulirudishwa mazoezini na kubadilisha vitu tulivyohisi vinafanya watu wasipende kucheza wimbo ule. Na mara nyingine wimbo huo ulitupwa pembeni moja kwa moja, mamia ya nyimbo  katika bendi mbalimbali ziliishia kupigwa kwenye kumbi mara moja tu na hazikurudiwa tena, kwa kuwa tu watu hawakuchangamkia kuzicheza.
Siku hizi mambo yako tofauti kabisa, unaweza kuingia kwenye onyesho la muziki wa Taarab, muziki ambao zamani ulikuwa ukisifika kwa kuwa muziki wa kusikiliza tu, ukakuta wapenzi wakitiririka jasho kwa kucheza nyimbo mbalimbali za Taarab. Na ukaingia katika onyesho la ‘muziki wa dansi’, ukakuta waimbaji wakitoka mishipa ya shingo, solo likapigwa kwa ufasaha, vyombo vingine vikachangia lakini hakuna anaeshughulika kucheza dansi hilo. Kama ingekuwa  zamani, hiyo ni dalili ya moja kwa moja kuwa muziki huo hauwafurahishi wapenzi. Lakini hizi ni zama nyingine.

Katika zama hizi, bendi huwa na wacheza show wake au hata waimbaji wa bendi nao wakatengeneza show yao, kisha wakawa wanapiga muziki na kucheza wao wenyewe. Ni kama nilinganishe na msemo maarufu wa  'kujitekenya halafu kucheka mwenyewe'. Wimbo ukiisha  wanamuziki huanza wimbo mwingine bila  kuhisi kuwa kuna tatizo.
Teknolojia imeleta aina nyingine ya kuonyesha upenzi na unazi wa muziki. Wapenzi wa muziki siku hizi huonyesha upenzi wao wa muziki kwa kuchukua simu na kurekodi  bendi ikiimba na kucheza, hawachezi wala kutikisika, kazi yao ni kunyanyua simu na kurekodi. Vipande hivi vya video husambazwa kwenye makundi ya Whatsapp, vikiambatana na sifa kuhusu ubora wa bendi hizi. Ndio namna ya zama hizi kufurahia muziki.
 Hakika kuna nyimbo ambazo wapenzi huchangamkia  kwa kucheza sana, lakini ukiangalia kila mtu anacheza akili inavyomtuma, hakuna tena mpangilio wa kucheza staili maalumu ya muziki. Ile staili ya wapenzi kukumbatiana kwa hisia wakati wa kucheza rumba imepotea, si ajabu kabisa kumkuta mtu anacheza na mpenzi wake, kila mtu na staili yake na wakati huohuo kila mmoja anatuma meseji kwenye simu. kweli zama zimebadilika mno.

Mwisho nimalizie na sentensi ya hali ninayoiona  katika muziki wa dansi, 'ZAMANI WATU WALIKWENDA DANSINI NA KUKUTA POMBE, SIKU HIZI WATU WANAENDA KWENYE POMBE NA KUKUTA DANSI'


 

Tuesday, July 12, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 3

 

SAFARI  yetu ya kuzikumbuka bendi mbalimbali nchini, wiki hii inatuingiza mkoa wa Iringa, lakini kati ya Iringa na Dodoma kuna wilaya inaitwa Mpwapwa. Hapa kulikuwa pia na bendi moja matata sana iliyoitwa  Mpwapwa Jazz Band. Bendi hii haikuwa ndogo kwani iliweza kurekodi nyimbo kadhaa ambazo zilipata umaarufu wa Kitaifa wakati wa uhai wake, ikiwemo wimbo Nilikuwa sina kazi, wimbo ambao unazungumzia hadithi ya kudumu ya kukimbiwa na mpenzi kutokana na kutokuwa na kipato.
Mji wa Iringa ulianza kama  ngome ya Wajerumani walipokuwa katika harakati za kumsaka Mutwa Mkwawa baada ya kuangusha ngome yake kule Kalenga. Hata jina Iringa limetokana na neno la Kihehe 'Lilinga' yaani ngome. Jeshi la Wajerumani likiwa na maafisa wachache wa Kijerumani, lilikuwa  na askari wengi wa Kiafrika kutoka pande mbalimbali za Afrika ya Mashariki na kati. Kulikuwa na askari wa Kinubi, askari wa Kimanyema, askari wa Kizaramo, askari wa Kinyamwezi na makabila mengine kadha wa kadha. Askari hawa wakaanza kuishi na familia zao maeneo yanayojulikana kama Miyomboni, jirani na kituo kikuu cha polisi ambapo haswa ndipo yalikuwa makao makuu ya jeshi la Wajerumani. 
Watoto na wajukuu wa askari hawa  walikuwa wakijitambulisha kuwa wao ndio wenyeji halali wa mji wa Iringa. Hivyo walikuwa na timu ya mpira iliyoitwa Boni kifupi cha Born Town, wakiwa wanamaananisha kuwa wao ndio wazawa haswa wa pale mjini. Na wakati huohuo wakaanzisha pia bendi iliyoitwa Born Jazz band, pengine kati ya bendi za awali za mji huu. Kama  ilivyokuwa Dodoma kuwa na bendi inaitwa Sextet Jazz band, Iringa kulikuwa na bendi inaitwa Habanero Jazz Band. Sextet na Habanero yalikuwa majina ya bendi mbili za huko Cuba. Katika zama hizo bendi za hapa nchini zilikuwa zikiiga muziki kutoka Cuba, si Congo. Bendi ya Iringa iliyokuja kupata umaarufu mkubwa ilikuwa Highland Stars Band. Mpiga gitaa Abel Balthazar ni moja ya wapigaji maarufu waliowahi kupitia bendi hii. Nyumbani kwa  mpiga solo maarufu wa Msondo Ngoma Ridhwani Abdul Pangamawe, ndipo yalipokuwa yakifanyika mazoezi ya Highland Stars Band. Mzee Abdul Pangamawe na mama Ridhwani wote walikuwa wakijua kupiga magitaa, si ajabu kabisa nyumba hiyo kutoa mpiga gitaa  na kinanda mahiri anayetingisha nchi mpaka leo. Moja ya wimbo wao maarufu wa Highland Stars ulikuwa ni Sitasita Mpenzi.

Bendi nyingine mjini Iringa ilikuwa ni Iringa Jazz Band, hii ilikuwa mali ya TANU Youth  League. Miji mingi sana ilikuwa na bendi za TANU Youth League katika miaka ya 60 na 70. 
Mkwawa High School, ambayo awali ilikuwa shule ya ‘Wazungu’ na iliyokuwa ikiitwa St George and St Michael European School, ilikuja kuwa na bendi nzuri sana ya wanafunzi iliyoitwa Orchestra Mkwawa. Wakiwa na mtindo wao waliouita Ligija walitoa burudani kila mwisho wa wiki katika ukumbi wa Welfare Center, katika utaratibu wa madansi ya mchana maarufu kama Buggy, wao kama wanafunzi hawakuwa na ruksa ya kuwa katika kumbi za dansi usiku, hivyo waliweza kupiga muziki huo mchana tu. Pia katika shule hiyo hiyo kulikuwa na bendi nyuingine iliyokuwa ikipiga muziki wa Kizungu na iliitwa Midnight Movers. Marehemu Eddy Hanspoppe, Deo Ishengoma, Martin Mhando walikuwa kati ya wanamuziki wa bendi hii. Vyombo walivyotumia vilikuwa ni vile ambavyo vilikuwa vikitumiwa na bendi iliyokuwa ya TANU Youth League. Magitaa ya bendi hii hatimae yalikuja kuchukuliwa na vijana wachache walioanzisha bendi iliyokuwa ikijulikana kama Chikwalachikwala. Chikwalachikwala ikajigawa na kukapatikana bendi iliyoitwa BOSE Ngoma, jina lililotokana na aina ya speaker walizokuwa nazo.

                                                    Chikwalachikwala Jukwaani Kijiji cha Mgama, 

Mwaka 1987 ikazaliwa Tancut Almasi Orchestra  bendi nyingine kubwa iliyowahi kutokea Iringa, bendi hii ilikuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Diamond Cutting Company kilichokuwa pale Iringa. Majina ya wanamuziki maarufu waliopitia bendi hii ni mengi sana kati hao walikuweko mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Banza Tax, Mafumu Bilali, Kawelee Mutimwana, Shaban Yohana Wanted, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe na wengine wengi akiwemo mwandishi wa makala hii.

TANCUT ALMASI ORCHESTRA JUKWAANI


Bendi nyingine iliyowahi kuweko Iringa  mjini ni Ruaha International Orchestra , iliyokuwa mali ya mfanya biashara mmoja aliyeitwa Mtandi. Bendi hii ilikuwa chini ya uongozi wa muimbaji marehemu Kalala Mbwebwe na wimbo wake Lutadila  ni kumbukumbu kubwa kwa wapenzi wa bendi hii. Bendi nyingine zilizowahi kuwa Iringa, zilikuwa ni VICO Stars iliyokuwa mali ya kanisa Katoliki, Living Light Band iliyokuwa mali ya hoteli ya Living Light.
Kumaliza mkoa huu bila kutaja bendi maarufu ya JKT Mafinga haitakuwa sawa. Bendi hii ilikuwa maarufu kwa jina la Kimulimuli, jina hili lilitokana na taa za disco zilizokuwa zinafungwa wakati bendi hii inapiga. Vyombo maarufu vya muziki aina ya Ranger FBT ambavyo vilikuwa vikitumika na bendi nyingi miaka ya 80 vilikuwa vinakuja na taa za disco, na wenyeji wa Mafinga walikuwa wakisema kwa Kihehe ‘Twibita kukina kimulimuli’ yaani tunaenda kucheza Kimulimuli, na hakika jina hilo ndilo likawa utambulisho wa bendi hiyo,  na hata bendi yenyewe ilitunga nyimbo kusifia jina lao la Kimulimuli.  Kati ya wanamuziki maarufu waliowahi kupitia bendi hii ni Zahiri Ally Zorro na Zakaria Daniel Mabula Tendawema ambaye niliandika alipata jina la Tendawema kutokana na kutunga wimbo ulioitwa Tenda wema nenda zako alipokuwa Shinyanga Jazz band. Safari inaendelea….

Sunday, July 10, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 2

 


Wiki iliyopita safari yetu ilitupitisha Singida enzi Mzee Mose Nnauye alipokuwa Mkuu wa mkoa huo na mchango wake katika kuanzisha bendi maarufu ya mji wa Singida iliyoitwa Ujamaa Jazz band. Leo tuingie Dodoma, mji huu mkongwe ulio katikati ya nchi yetu na tuzikumbuke baadhi ya bendi za mji huo na vituko vya kukumbukwa vilivyowahi kutokea katika enzi za uhai wa bendi hizo.
Tuanze na bendi iliyoitwa Jolly Sextet Band. Bendi hii ilianzishwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa Shirika la posta la Afrika ya Mashariki, wakati huo likijulikana kama East African Posts and Telecommunications Corporation. Mkenya huyu alikuja na vyombo vyake vya muziki na kati ya watu walikuja kuwa maarufu waliotokea bendi hiyo ni mpiga saksafoni maarufu Mnenge Ramadhani. Mnenge alijiunga na bendi hii akitokea bendi nyingine ya Dodoma iliyoitwa Central Jazz Band. Mnenge hatimae alitoka Jolly Sextet Band na kujiunga na NUTA Jazz Band alikopata umaarufu kwa upigaji wa saksafon.
 Mwaka 1948 Uingereza iliigawa nchi katika majimbo ya kiutawala manane, Dodoma ikawa katika jimbo lililoitwa Central Province, na pia Dodoma iko katikati ya nchi hivyo basi wanamuziki kadhaa walianzisha bendi iliyoitwa Central Jazz band. Hii bendi ilitoa wanamuziki wengi sana waliokuja kutikisa anga za muziki Tanzania, wakiwemo akina Mnenge Ramadhani, Juma Ubao, maarufu kwa jina King Makusa, Patrick Balisdya, Ally Rahmani huyu alikuwa mpiga gitaa mahiri, enzi za STC  wote ni mazao ya Central Jazz

Mfanya biashara mmoja, Mohamed Omar Badwel, aliyekuwa na gereji na studio ya kupiga picha alinunua vyombo na kuanzisha bendi iliyokuja kuitwa Dodoma Jazz Band. Bendi hii ilikuwa na wanamuziki wazuri sana na ilitoa nyimbo zilizokuja kufahamika nchi nzima, wimbo wao uliokuwa maarufu sana miaka ya sitini ulikuwa Zaina Njoo.
Mmoja kati ya wapiga solo wa kwanza wa bendi hii alikuwa Hassan Mursali kwa asili alikuwa Mnyasa, huyu pia alikuwa anakitwa Hassan Kiziwi kwani pamoja na kuwa mahiri katika upigaji wa gitaa la solo alikuwa na tatizo la kusikia vizuri. Hassan aliwahi kujiunga na Kilwa Jazz band na wimbo ambao alipiga gitaa la solo ni ule  wenye maneno  Dunia Njema kukaa wawili. Hatimae alikuja kuacha muziki na kuwa fundi saa.
Dodoma Jazz Band ilikuwa ikisafiri sana katika kila wilaya nchi nzima, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilikuwa na lengo la kwenda kumchukua mpiga solo wa bendi ya Kilosa Jazz Band, si mwingine ila ni Abel Balthazar. Bendi ilifanikiwa kumchukua Abel na kurudi nae Dodoma. Siku chache baadae wazee waliotumwa na uongozi wa  Kilosa Jazz Band walifika kwa kiongozi wa Dodoma Jazz wakiwa na barua na kumuomba aifungue na kuisoma mbele yao kabla hawajaondoka. Ndani ya barua ile kulikuwa na maagizo kuwa Abel asiporudi Kilosa, basi kuna mwanamuziki mmoja wa Dodoma Jazz band atafariki. Pamoja na Abel kuwa keshashonewa suti mpya ya sare na Dodoma Jazz alirudishwa Kilosa mara moja kuepusha janga.
Mwanamuziki mwengine aliyewahi kupitia Dodoma Jazz Band ni Rashid Hanzuruni, mpiga gitaa marufu ambaye moja kati ya nyimbo zake alizopiga solo ambazo ni maarufu mpaka leo ni ule wimbo wa Kilwa Jazz Band ambao wengi wanaujua kama Lau Nafasi. Hanzuruni alijikuta katika bendi hii akiwa safarini akitokea Tabora ambako alikuwa amekorofishana na wanamuziki wenzie wa Tabora Jazz Band, alikuwa akielekea Dar es Salaam kujiunga na NUTA Jazz band, lakini akakatishwa safari hiyo na meneja wa Dodoma Jazz Band aliyemshawishi ajiunge na Dodoma Jazz Band. Hanzuruni hakukaa sana Dodoma, akaondoka na kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya ndoto yake ya kujiunga na NUTA Jazz Band, hata hivyo ndoto hiyo haikutimia kwani wakati huo NUTA Jazz Band ilikuwa na mpiga solo mahiri sana aliyeitwa Hamisi Franco, Hanzuruni akaishia kujiunga na Western Jazz Band.

Central Jazz band ilikuja kuwa chanzo cha Afro70 Band ya Patrick Balisdya, kwani ndiko Patrick na wenzie walikopata vyombo vya kwanza vya kuanzishia bendi yao hiyo maarufu.

Dodoma International Orchestra 1978


Bendi nyingine maarufu iliyowahi kuweko Dodoma ni Dodoma International Orchestra, hii ilikuwa mali ya Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa wa Dodoma. Dodoma International kwa kipindi ilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki mkongwe mpuliza saksafon Sheddy Mbotoni. Dodoma International Orchestra ilipitisha wanamuziki wengi sana waliokuja kuwa maarufu katika anga za muziki nchini, waimbaji kama Shaaban Dede, Ahamadi Sululu, Athumani Soso, Saburi Athumani, wapiga magitaa akina Charles Kasembe, Kassim Rashidi, Mohamed Ikunji, na wanamuziki wengine wengi maarufu wote walipitia bendi hii mahiri. Dodoma International ilijitambulisha kwa mitindo kadha wa kadha kama ‘perekete’, mafuriko ya jasho’, ‘zunguluke’ na mingineyo mingi iliyobadilika kutokana na wanamuziki kubadilika katika kuingia na kutoka. Bendi nyingine ya Dodoma ilikuwa ni mali ya fundi redio maarufu Mzee Alphonse Materu, na bendi aliipa jina lake ikaitwa Materu Stars. Materu Stars nayo ilipitisha wanamuziki wengi sana akiwemo aliyekuwa kiongozi wa bendi maarufu ya Butiama Jazz Band, mzee Alphonce Makelo, ambaye kwa sasa maepoteza uwezo wake wa kuona. Bendi nyingine iliyokuwa Dodoma na kupewa jina la mwenye bendi ni bendi ambayo bado ipo hai na  inaitwa Saki Stars. Saki lilikuwa ni kifupi cha  jina Salome Kiwaya, mwanamuziki wa kike aliyeiongoza bendi yake mpaka umauti wake uliotokana na ajali ya gari. Wiki ijayo tutaendelea na safari yetu ya bendi za Tanzania.

 

 

Saturday, July 9, 2022

UNAKUMBUKA SOCIAL EVENING?

Ma soul brothers wakiwa kwenye party
KWA wengi waliokuwa wakisoma sekondari miaka ya 60 na 70, moja ya siku zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu ilikuwa siku ya ‘Social Evening’. Siku hii ilikuwa ndio siku ambayo wanafunzi walipata nafasi kusakata dansi na kupata marafiki wapya, na mara nyingine hata kuachwa na marafiki wa zamani. Mara nyingi dansi hili liliambatana na kualika wanafunzi kutoka shule nyingine za jirani. Na kawaida ilikuwa shule ya wavulana kualika wanafunzi kutoka shule ya wasichana na shule ya wasichana kualika wanafunzi kutoka shule ya wavulana. Matayarisho yalikuwa yanaanza mapema kwa waalikaji kuandika barua kwa Mwalimu Mkuu au mwalimu wa ‘Social’ wa shule wanayotaka kuialika. Baada ya hapo kazi kubwa ni kukusanya michango kutoka kwa wanafunzi wanaotaka kushiriki siku hiyo. Michango hii kazi yake ilikuwa kununua viburudisho kwa wageni; soda, biskuti au hata maandazi, na pia kununua betri za ‘player’ ya kupigia muziki. Umeme ulikuwa nadra kwenye shule nyingi. Kamati ya starehe ilikuwa ‘busy’ kutafuta santuri mpya, kwa kuazima popote pale, na kama kuna mwalimu ana record player ilikuwa jambo la heri sana.  Ukumbi ulipigwa deki vizuri ili wageni wakifika wasije wakawadharau. Hatimae siku huwadia, social evening mara nyingi zilikuwa Jumamosi kuanzia saa nane mchana na kuisha kati ya saa moja mpaka mbili usiku. Wageni hukaribishwa na burudani huanza. Baada ya hotuba na kugawa vinywaji, wenyeji huleta burudani kama vile kucheza jiving, baada ya hapo ‘Dada mkuu’ au mwenyekiti wa kamati ya social wa shule moja hufungua dansi na mwenzie kaka mkuu au mwenyekiti wa kamati ya social wa upande wa pili. Na ndipo wengine mnajitosa kusaka mapatna. Kawaida ya miaka hiyo mwanaume unamfuata msichana kisha unainama kidogo kumuomba ucheze nae, anaweza akakubali au kukataa. Katika shughuli hizi waalimu wa kuangalia nidhamu walikuwa wakishiriki kuangalia kuwa maadili yanafuatwa. Wakati mnacheza mwalimu anapitapita kuangalia kama ‘hamsogeleani ‘ sana.  Kama nilivyosema hapo juu, muziki ulitoka kwenye record player ambayo ilikuwa na spika moja ndogo hivyo haikuwa na sauti kubwa. Ukiona ukubwa wa maspika siku hizi, unabaki kushangaa, tuliwezaje wanafunzi 200 hadi 300 kucheza muziki na kuusikia vizuri kwa kutumia spika moja  ya player yenye betri 6. Spika ambayo ili itoe bezi ililazimika kuwekwa juu ya pipa. Kulikuwa na nidhamu kubwa sana katika uchezaji, kulikuwa hakuna kupiga kelele, unasikia viatu tu vikisaga chini kwa kufuata mdundo wa muziki. Swala la kuwa pombe haikuhusika katika burudani hizi ni moja ya sababu ya kuwezekana kwa nidhamu hii. Mazungumzo yalikuwa ya chini chini mara nyingi yakihusu masomo.
Katika miaka ya 60 santuri za nyimbo kutoka Congo ndizo zilikuwa maarufu, magwiji wa muziki kama akina Franco, Johhny Bokelo, Dr Nico, Bavon Marie Marie na bendi zao maarufu, Ok Jazz, Negro Success, Co Bantuo, Bantou de La Capital, na miaka ya 70 kukatawaliwa na bendi zilizokuwa zikipiga mtindo wa Cavacha, Lipua Lipua, Kiam, Veve, Kamale na nyingine nyingi. Muziki wa soul ulikuwa na mabingwa wake akina Otis Redding, James Brown, Clarence Carter, Wilson Pickett na wengine wengi. 
 Kutoka  Marekani wanamuziki wa muziki wa country kama Skeeter Davis, Jim Reeves, Connie Francis ndio walitawala social evenings.
Wimbo wa Isaac Hayes wa Do your thing maana ulikuwa wimbo wa taratibu ambao ulikuwa mrefu, hivyo kila mtu alikuwa akimkimbilia mtu wake mara tu ukiaanza wimbo huo, maana ndio wimbo wa kukumbatyia kwa muda mreeffuuuuuu, ulikuwa na urefu wa dakika 19.
 Wavulana kwa wasichana walishiriki kuandika maneno ya nyimbo hizo kwenye madaftari yao na kubadilishana madaftari. Nyimbo maarufu katika madaftari ya wavulana zilikuwa ni nyimbo za Kikongo. Tambola na Mokili wa Johhny Bokelo na Conga Success na Bougie ya Motema wa Dr Nico na African Fiesta zilikuwa hazikosekana kwenye madaftari ya wavulana, wakati akina dada walipendelea sana kuandika maneno ya nyimbo za Skeeter Davis na Dark City Sisters kutoka Afrika ya Kusini. Kama nilivyosema hapo juu, umeme tu ulikuwa tatizo kweye shule nyingi, hivyo swala la kuwaona na kuwajua wanamuziki waliokuwa wakiporomosha muziki huo lilikuwa nadra sana. Magazeti yalikuwa machache, vyombo ambavyo siku hizi vinaonekana ni kawaida kabisa kama radio na TV navyo vilikuwa nadra sana. Lakini kwa njia ya ajabu vijana walikuwa wanajua namna ya kucheza staili za muziki mbalimbali!! Chacha, pachanga, charanga, baadae soul, bumping na kadhalika. Kwenye shule mbalimbali kulikuwa na wanafunzi ambao walikuwa wanapata bahati kuwa na ndugu au marafiki ambao walikuwa wakibahatisha kuwafundisha uchezaji mbalimbali wakati wa likizo, basi mwanafunzi wa aina hiyo anakuwa maarufu sana mara arudipo shule akiwa na staili mpya ya uchezaji, watu wote wanaanza kumuiga  uchezaji ili kujitayarisha kwa social evening. Ilikuwa si ajabu ukija na staili mpya ukapata hata mpenzi mpya.

Friday, July 8, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 1


 Kuanzia miaka ya 1920 kuna taarifa za maandishi za kuwepo kwa vikundi vya muziki Tanzania. Tanzania Bara ikiwa na bendi nyingi za muziki wa dansi, wakati Tanzania visiwani Taarab ikitawala. Leo nataka niwazungushe mikoa mbalimbali ambako kulikuwa na bendi. Bendi nyingine zilikuwa maarufu mpaka kujulikana nje ya nchi yetu na nyingine hazikuwa maarufu au hazikudumu sana, lakini kuna wasanii wengi walitoka huko na kuja kuwa maarufu nchini na hata duniani.
Nianze na Kigoma, huu si mji ambao siku hizi unatajwa wakati ukiongelea muziki wa dansi lakini kulikuwa na bendi kadhaa kutoka mji huo zilizokuja kujitokeza, tuanze na Lake Tanganyika Jazz Band, hii ndiyo bendi alikotokea mpiga solo, mtunzi na muimbaji Shem Karenga, ambaye alianza huko akiwa mpiga gitaa la bezi na hatimae kuhamia Tabora jazz band ambako nyota yake ilianzia kung’ara hapo. Kigoma kulikuweko na bendi iliyoitwa Super Kibisa Jazz  Band, bendi hii ilikuwa na waimbaji wazuri na wapigaji wazuri sana, mmoja wa wapiga magitaa wa bendi hiyo Mzee Simba, hatimae alikuja kujiunga na JKT Kimbunga, bendi aliyokaa nayo mpaka alipostaafu. Pia kulikuweko na bendi iliyochukua jina la mji huo na kuitwa Kigoma jazz band, bendi nyingine iliyokuweko Kigoma iliitwa Kasababo Jazz Band, hii ndiyo ilikuwa bendi ya awali kabisa ya marehemu Shaaban Dede.
Mkoa jirani wa Mara ulikuwa na bendi nyingi pia, bila shaka ni vizuri kuanza na bendi ya Mara Jazz Band, hii ilipata umaarufu mkubwa ikiwa na mtindo wake wa Sensera. Lakini pia kulikuwa na bendi iliyochukua jina la mji wa Musoma, bendi iliyoitwa Musoma Jazz Band hii ilijitambulisha kwa mtindo wake wa Segese. Bendi nyingine kutoka mkoa huu ilikuwa Special Baruti Band, hii ndiyo bendi ya awali ya muimbaji maarufu Jerry Nashon kabla hajaingia jiji la Dar es Salaam. Musoma kulikuwa na bendi iliyokuwa mali ya Kanisa Katoliki iliyoitwa Juja Jazz band, hata kule Iringa kulikuwa na bendi nyingine mali ya Kanisa katoliki iliyoitwa VICO Stars ikiwa ni kifupi cha Vijana Consolata Stars. Bendi nyingine kutoka mkoa wa Mara ilikuwa ni Eleven Stars Band, japo ilijiita jina hilo, bendi ilikuwa na wanamuziki sita tu.

Tukiingia jiji la Mwanza, jiji lililokuwa likijisifu kwa starehe miaka ya sitini na sabini, kutokana na almasi, pamba na biashara ya mifugo, kulikuweko na bendi kadhaa ikiwemo Kimbo Twist Band ambako waliwahi kupita kati ya wapiga solo mahiri waliowahi kutokea Tanzania, marehemu  Rashid Hanzuruni na marehemu Kassim Mponda. Mwanza pia kulikuwa na bendi ambayo asilimia kubwa walikuwa ni wanamuziki kutoka Kongo, bendi hiyo iliitwa Orchestra Super Veya, bendi hii ilikuwa na umaarufu mkubwa kanda ya ziwa na ndiko alikopitia mwanamuziki maarufu Mzee Zahir Ally Zollo.
Mji wa Shinyanga kulikuwa na bendi maarufu iliyoitwa Shinyanga Jazz Band, bendi hii ilirekodi nyimbo kadhaa lakini wimbo wao mmoja unakumbukwa na wapenzi wa muziki wa dansi mpaka leo unaitwa Tenda Wema nenda zako. Wimbo huu ulitungwa na marehemu Mzee Zacharia Daniel Mabula, na kwa sababu ya wimbo huo mpaka kifo chake aliitwa Zacharia Tendawema au Mzee Tendawema, licha ya  historia yake ya kupitia bendi nyingi zikiwemo Western Jazz band, JKT Kimulimuli na TANCUT Almasi Orchestra ambako pia huko alitunga nyimbo nyingi, lakini  wimbo huo ulikuwa ndio nembo yake.
Tabora ulikuwa mji uliochangamka sana, kwanza ni moja kati ya miji ya zamani nchini, pili Tabora ulikuwa mji wenye vijana wengi kutokana na kuwa na shule  na vyuo vilivyokuweko katika mji ule. Kulikuwa na shule kongwe kama  Sekondari ya Tabora Boys na Sekondari ya Tabora Girls, pia vyuo kama Tabora Secretarial, chuo cha Ualimu cha Tabora, na chuo kikongwe cha reli,  Railway Training School. Hivyo basi Tabora nayo ilichangamka sana kimuziki, kulikuwa na bendi maarufu ya Tabora Jazz Band, na bendi yake dada, Nyanyembe Jazz band na pia ilikuweko bendi kongwe ya Kiko Kids. Wanamuziki wengi sana maarufu walitoka bendi hizi wakiwemo Shem Karenga , Wema Abdallah, Kassim Kaluona na Salum Zahoro, majina yaliyokuja kuvuma Afrika ya Mashariki na kati.

Mwaka 1972 Mzee Moses Nnauye aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Singida, kutokana na kupenda kwake muziki haikuchukua muda mrefu akahakikisha Singida ikapata bendi nzuri iliyoitwa Ujamaa Jazz Band, bendi iliyokuwa ikipiga kwa mtindo iliyouita King’ita Ngoma. Wanamuziki kadhaa kama Waziri Ally, Selemani Mwanyiro walipitia bendi hii. Nikumbushe jambo jingine kuwa Mzee Nnauye alipokuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo pia alianzisha bendi iliyoitwa Sabasaba Jazz band, mtindo wa bendi hiyo uliitwa Kizibo. Hamza Kalala alikuwa mpiga solo wa kwanza wa bendi hii, baada ya Mzee Nyange aliyekuwa mpiga solo wa Cuban Marimba kukataa wito wa kujiunga na bendi hiyo.


Tuesday, April 12, 2022

MWAKA 1973 YALIFANYIKA MASHINDANO YA BENDI BORA TANZANIA UNAJUA MSDHINDI ALIKUWA NANI?

 

TANGAZO la mashindano hayo lilitolewa kwenye gazeti na mashindano hayo yalidhaminiwa na NDC.. Shirika la Maendeleo la Taifa.

Mshindi wa kwanza ilikuwa ni bendi ya Sunburst. Picha ya chini kulia, aneonekana amevaa kofia na kushika kikombe ni James Mpungo kiongozi wa Sunburst, bendi ya pili ilikuwa Tonics na Marijani Rajabu akiwakilisha Safari Trippers iliyochukua zawadi ya tatu







Hawa ndio Sunburst bendi iliyoanzishwa mwaka 1970 na mwanamuziki Mkongo Hembi Flory, ilikuwa bendi moto sana mwanzoni mwa miaka ya 70. Mwaka 1973 ikashinda mashindano ya Bendi Bora Dar es Salaam na kuwa ya kwanza. Katika picha hapo juu, toka kushoto Toby John Ejuama (saxophone) huyu alikuwa Mnaijeria kutoka Biafra, kama mnakumbuka Tanzania tulimuunga mkono  Ojukwu, kiongozi aliyekuwa na ndoto za jimbo la Biafra kujitenga na Nigeria, hivyo tukawa kimbilio la watu kutoka huko. Anaefuata ni Flory mpiga gitaa Mkongo, kisha mkongwe Johnny Rocks kwenye (drums), huyu alikuwa pia anapiga na George Di Souza pale Margot.  James Mpungo (lead vocals) kijana wa Mbeya ambaye hatimae alijiunga na Mangelepa. Anafuatia Kassim Rajabu Magati (organ/lead vocals, kwenye gitaa la bezi ni Bashir Idd Fahani. 



Sunday, March 27, 2022

TUMETIMIZA MIAKA 16 TOKA KIFO CHA TX MOSHI WILLIAM, SAUTI YAKE INAENDELEA KUSIKIKA

 


Msondo wakiwa mazoezini katika ukumbi wa Amana

Moshi William alizaliwa mwaka 1958 Hale Mwakinyumbi Korogwe. Hale alikuwepo mwanamuziki maarufu aliyekuwa akiitwa Mzee Masongi, yeye alikuwa na bendi, na bendi hii ilikuwa chanzo cha wanamuziki wengi maarufu akiwemo Moshi William.  Jina halisi la Moshi William lilikuwa Shaaban Ally Mhoja lakini alikuja kubadili na kuitwa Moshi William kutokana na kuja kulelewa na baba mwingine.  Bendi ambazo TX Moshi William aliwahi kupitia baada ya kutoka Hale zilikuwa ni Safari Trippers wana Sokomoko, UDA Jazz Band wana Bayankata, na Polisi Jazz Band wana Vangavanga, na hatimae JUWATA Jazz Band wana Msondo Ngoma, bendi aliyodumu nayo mpaka kifo. Kati ya nyimbo zake za kwanza mara baada ya kujiunga na JUWATA zilikuwa Ajuza, Ashibaye  na Asha Mwanaseif, wimbo huu wa tatu alimtungia mkewe, baada ya hapo alitunga nyimbo nyingi sana na kwa ujumla alirekodi album karibu 13.  Sifa ya Moshi kuanza  kuitwa  TX ilitungwa na marehemu Julius Nyaisanga aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam. Zama hizo, serikali ilikuwa imeweka sheria kuwa magari ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi nchini yawekwe namba ambazo zilianzia na TX kuonyesha ni ya Kimataifa, hivyo TX ikageuka kuwa nembo ya sifa ya kuwa na hadhi ya Kimataifa. Kutokana na umahiri wa Moshi katika kutunga na kuimba, Nyaisanga akampachika kisifa cha TX. Na hakika umahiri wake ulijidhihirisha kwani kwa miaka mitatu mfululizo kati ya mwaka 2003 mpaka 2005, TX Moshi William alitunukiwa tuzo za utunzi bora  na Kilimanjaro Music Awards.  Pamoja na Msondo, Moshi aliwahi kurekodi nyimbo nyingi akiwa na wanamuziki wenzake nje ya Msondo, kwa utaratibu ulikuwa maarufu kwa jina la zing zong au wengine waliita zozing.  Moshi alifariki siku ya tarehe 29 March 2006 katika wodi ya Sewa Haji baada ya operesheni ya kuondoa chuma katika mguu wake uliovunjika kwenye ajali. Alifariki saa tatu kasoro robo asubuhi na kuzikwa siku hiyohiyo katika makaburi ya Keko Machungwa.

 

 


 
Kaburi la TX Moshi William


Mungu Amlaze Pema Shaaban Ally Mhoja Kishiwa - TX Moshi William