Kuanzia miaka ya 1920 kuna taarifa za maandishi za kuwepo kwa vikundi vya muziki Tanzania. Tanzania Bara ikiwa na bendi nyingi za muziki wa dansi, wakati Tanzania visiwani Taarab ikitawala. Leo nataka niwazungushe mikoa mbalimbali ambako kulikuwa na bendi. Bendi nyingine zilikuwa maarufu mpaka kujulikana nje ya nchi yetu na nyingine hazikuwa maarufu au hazikudumu sana, lakini kuna wasanii wengi walitoka huko na kuja kuwa maarufu nchini na hata duniani.
Nianze na Kigoma, huu si mji ambao siku hizi unatajwa wakati ukiongelea muziki wa dansi lakini kulikuwa na bendi kadhaa kutoka mji huo zilizokuja kujitokeza, tuanze na Lake Tanganyika Jazz Band, hii ndiyo bendi alikotokea mpiga solo, mtunzi na muimbaji Shem Karenga, ambaye alianza huko akiwa mpiga gitaa la bezi na hatimae kuhamia Tabora jazz band ambako nyota yake ilianzia kung’ara hapo. Kigoma kulikuweko na bendi iliyoitwa Super Kibisa Jazz Band, bendi hii ilikuwa na waimbaji wazuri na wapigaji wazuri sana, mmoja wa wapiga magitaa wa bendi hiyo Mzee Simba, hatimae alikuja kujiunga na JKT Kimbunga, bendi aliyokaa nayo mpaka alipostaafu. Pia kulikuweko na bendi iliyochukua jina la mji huo na kuitwa Kigoma jazz band, bendi nyingine iliyokuweko Kigoma iliitwa Kasababo Jazz Band, hii ndiyo ilikuwa bendi ya awali kabisa ya marehemu Shaaban Dede.
Mkoa jirani wa Mara ulikuwa na bendi nyingi pia, bila shaka ni vizuri kuanza na bendi ya Mara Jazz Band, hii ilipata umaarufu mkubwa ikiwa na mtindo wake wa Sensera. Lakini pia kulikuwa na bendi iliyochukua jina la mji wa Musoma, bendi iliyoitwa Musoma Jazz Band hii ilijitambulisha kwa mtindo wake wa Segese. Bendi nyingine kutoka mkoa huu ilikuwa Special Baruti Band, hii ndiyo bendi ya awali ya muimbaji maarufu Jerry Nashon kabla hajaingia jiji la Dar es Salaam. Musoma kulikuwa na bendi iliyokuwa mali ya Kanisa Katoliki iliyoitwa Juja Jazz band, hata kule Iringa kulikuwa na bendi nyingine mali ya Kanisa katoliki iliyoitwa VICO Stars ikiwa ni kifupi cha Vijana Consolata Stars. Bendi nyingine kutoka mkoa wa Mara ilikuwa ni Eleven Stars Band, japo ilijiita jina hilo, bendi ilikuwa na wanamuziki sita tu.
Tukiingia jiji la Mwanza, jiji lililokuwa likijisifu kwa starehe miaka ya
sitini na sabini, kutokana na almasi, pamba na biashara ya mifugo, kulikuweko
na bendi kadhaa ikiwemo Kimbo Twist Band ambako waliwahi kupita kati ya wapiga
solo mahiri waliowahi kutokea Tanzania, marehemu Rashid Hanzuruni na marehemu Kassim Mponda.
Mwanza pia kulikuwa na bendi ambayo asilimia kubwa walikuwa ni wanamuziki kutoka
Kongo, bendi hiyo iliitwa Orchestra Super Veya, bendi hii ilikuwa na umaarufu
mkubwa kanda ya ziwa na ndiko alikopitia mwanamuziki maarufu Mzee Zahir Ally
Zollo.
Mji wa Shinyanga kulikuwa na bendi maarufu iliyoitwa Shinyanga Jazz Band, bendi
hii ilirekodi nyimbo kadhaa lakini wimbo wao mmoja unakumbukwa na wapenzi wa
muziki wa dansi mpaka leo unaitwa Tenda Wema nenda zako. Wimbo huu ulitungwa na
marehemu Mzee Zacharia Daniel Mabula, na kwa sababu ya wimbo huo mpaka kifo
chake aliitwa Zacharia Tendawema au Mzee Tendawema, licha ya historia yake ya kupitia bendi nyingi
zikiwemo Western Jazz band, JKT Kimulimuli na TANCUT Almasi Orchestra ambako
pia huko alitunga nyimbo nyingi, lakini wimbo huo ulikuwa ndio nembo yake.
Tabora ulikuwa mji uliochangamka sana, kwanza ni moja kati ya miji ya zamani
nchini, pili Tabora ulikuwa mji wenye vijana wengi kutokana na kuwa na
shule na vyuo vilivyokuweko katika mji
ule. Kulikuwa na shule kongwe kama Sekondari ya Tabora Boys na Sekondari ya
Tabora Girls, pia vyuo kama Tabora Secretarial, chuo cha Ualimu cha Tabora, na
chuo kikongwe cha reli, Railway Training
School. Hivyo basi Tabora nayo ilichangamka sana kimuziki, kulikuwa na bendi
maarufu ya Tabora Jazz Band, na bendi yake dada, Nyanyembe Jazz band na pia
ilikuweko bendi kongwe ya Kiko Kids. Wanamuziki wengi sana maarufu walitoka
bendi hizi wakiwemo Shem Karenga , Wema Abdallah, Kassim Kaluona na Salum Zahoro,
majina yaliyokuja kuvuma Afrika ya Mashariki na kati.
Mwaka 1972
Mzee Moses Nnauye aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Singida, kutokana na kupenda
kwake muziki haikuchukua muda mrefu akahakikisha Singida ikapata bendi nzuri iliyoitwa
Ujamaa Jazz Band, bendi iliyokuwa ikipiga kwa mtindo iliyouita King’ita Ngoma.
Wanamuziki kadhaa kama Waziri Ally, Selemani Mwanyiro walipitia bendi hii.
Nikumbushe jambo jingine kuwa Mzee Nnauye alipokuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo
pia alianzisha bendi iliyoitwa Sabasaba Jazz band, mtindo wa bendi hiyo uliitwa
Kizibo. Hamza Kalala alikuwa mpiga solo wa kwanza wa bendi hii, baada ya Mzee
Nyange aliyekuwa mpiga solo wa Cuban Marimba kukataa wito wa kujiunga na bendi
hiyo.
No comments:
Post a Comment