Kama Franco Luambo Luanzo angekuwa hai mwaka huu angekuwa anatimiza miaka 84 kwani alizaliwa tarehe 6 Julai 1938, lakini kwa mapenzi ya Mungu alifariki tarehe 12 Oktoba 1989 akiwa na umri wa miaka 51 tu. Wakati Franco akiwa na umri wa miaka 6 tu Morogoro Jazz Band ilianzishwa katika mji wa Morogoro. Kuna somo kubwa hapa, kwa bahati mbaya kutokana na Tanzania kutokuandika historia yake ya muziki, watu wengi na hata wanamuziki wengi wa kizazi hiki hudhani kuwa nchi yetu iliiga toka Kongo maswala ya muziki wa bendi, lakini historia inaonyesha kuwa mambo hayakuwa hivyo hata kidogo kama tarehe hizo hapo juu zinavyoashiria wazi, pengine wanamuziki wetu wa zama hizo hawakujua hata kama Kongo kuna wanamuziki.
Leo safari yetu ya kuzikumbuka bendi zetu, imetuleta mkoa wa Morogoro, na kama
unavyoona wakazi wa Morogoro tayari waliakuwa wakifurahia muziki wa bendi kabla
hata ya vita ya piti kumalizika.
Morogoro Jazz band inajulikana na wengi mpaka leo hasa katika kipindi
alichokuwepo Mbaraka Mwinyshehe Mwaluka. Wimbo maarufu wa Jogoo la shamba ni
moja kati ya nyimbo za bendi hiyo ambazo hata watoto wadogo wa kizazi hiki
wanaufahamu, na kuutumia katika kutaniana tena kwa utani unaofanana sana na nia ya kutungwa kwa wimbo huo.
Mwaka 1948
nguli mwingine wa Morogoro, Salum Yazidu Abdallah (SAY), mwanamuziki aliyezaliwa
kutoka kwa baba Mwarabu na mama Mlugulu, alianzisha bendi yake aliyoiita La
Paloma, neno la Kispayola likiwa na maana Njiwa. Wanamuziki na wapenzi wa rumba
miaka hiyo, kwa ujumla walikuwa wakisikiliza santuri z Kispanyola kutoka Cuba. Santuri hizo
zilizokuwa na namba zilizoanzia GV 1 na kuendelea hadi zaidi kidogo ya GV 200
zilikuwa na muziki kutoka bendi mbalimbali za Cuba, wanamuziki wa huku wakawa
wanapiga muziki kuiga huo wa Cuba na hata kuunda bendi zao nazo kuzipa majina
ya bendi zile za kule Cuba, ndio maana tukaziona bendi za Sextet Jazz ya Dodoma
na Habanero Jazz Band ya Iringa.
Salum Abdallah aliwahi kutoroka toka kwao Morogoro na kwenda Mombasa ili azamie meli na kwenda
Cuba kujifunza muziki, bahati mbaya kipindi hicho vita ya dunia ya pili ilikuwa
imepamba moto na hivyo safari yake ikaishia Mombasa, alipata taabu sana Mombasa hatimae Umoja wa Waarabu wa Mombasa walimtaarifu baba yake aliyekuja kumrudisha mwanawe Morogoro.
Aliporudi Morogoro ndipo
akaanzisha bendi yenye jina la ‘La Paloma’ jina lilitokana na wimbo maarufu wa
Cuba ambao mpaka leo bado unapigwa na bendi zetu nyingi kama muziki wa ala
mapema kabla ya kuanza rasmi kwa dansi.
La Paloma Band ilibadili jina na kujiita Cuban Marimba Band mwaka 1952, chini
ya Salum Abdallah bendi ilirekodi nyimbo nyingi ambazo mpaka leo bado
zinapendwa hata na vijana wa leo. Nyimbo kama Wangu Ngaiye, Shemeji Shemeji
wazima taa, Wanawake na kadhalika si
ngeni masikioni mwa wapenzi wa muziki hata leo. Cuban Marimba ilikuwa maarufu
kiasi cha kampuni za kurekodi kutoka Mombasa zilikuwa zikiifuata bendi Morogoro ili kuirekodi. Wimbo maarufu wa
Wanawake Tanzania ulirekodiwa Korogwe, baada ya kampuni ya kurekodi ya Assanand
kuifuata bendi Morogoro na kukuta imesafiri. Baada ya kuitafuta hatimae
wakakutana Korogwe. Wakati Assand akiwa njiani gari lake lilikwama kwenye
matope, na aliomba msaada wa kusukumwa, wanawake wakajitokeza na kulisukuma
gari lile. Asanand alipomuhadithia mkasa ule Salumu Abdallah ndipo ulipotungwa wimbo
maarufu wa Wanawake Tanzania.
Kwa mapenzi ya Mungu Salum Abdallah alifariki katika ajali ya ajabu mwaka 1965.
Cuban Marimba ikawa chini ya Juma Kilaza. Kilaza aliendelea na bendi hiyo miaka
kadhaa alipoiacha akaanzisha bendi yake iliyoitwa TK Lumpopo, ambayo mata
nyingine alikuwa akiita TK Lumpopo National. Mbaraka Mwinyshehe nae alikuja
kuicha Morogoro Jazz Band na kuanzisha bendi yake ya Super Volcano.
Kwa kipindi kifupi kwenye mwaka 1985 ilitokea bendi iliyoitwa Les Cuban. Vyombo
vya bendi hii vilikuwa mali ya Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro, na alikabidhiwa Mzee Juma
Kilaza ili kuona uwezekano wa kurudisha hadhi ya muziki Morogoro. Mzee Kilaza
aliwaleta wanamuziki wa bendi ya Orchestra Vina Vina toka Nairobi, vijana
aliyorekodi nao huko na kuwaona wako vizuri sana. Kati ya waliokuja na
Orchestra Vina Vina alikuweko muimbaji mlemavu wa macho Nico Zengekala. Les
Cuban ikawa sasa inajitambulisha kwa
mtindo wa Vina vina, ili kutokupoteza jina lao la awali, walifanya kazi kubwa
ya kukumbukwa, nyimbo kama Kifuko cha Zambarau au Jackie ni wimbo bado maarufu
mpaka leo. Lakini bendi iliingia katika matatizo ya kiutawala na kufa mapema
sana.
Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza wa kwanza kulia
Tukirudi nyuma katika miaka ya sitini na sabini, bendi hizi mbili, Morogoro Jazz Band na Cuban Marimba Band ziliuchangamsha sana mji wa Morogoro kiasi cha kwamba siku za mwisho wa wiki, wapenzi wa muziki walikuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kustarehe. Wakati huo usafiri ulikuwa mgumu kwani sehemu kubwa ya barabara kati ya miji hii miwili ilikuwa ni ya vumbi.
Watu wa mkoa wa Morogoro hupenda sana muziki, kulikuwa na bendi. Inawezekana kabisa kuwa katika miaka ya 70 na 80 mkoa wa Morogoro ndio ulikuwa na bendi nyingi zaidi. Hasa ukizingatia kuwa karibu kila wilaya ilikuwa na bendi na tena zilizokuwa zikifahamika Kitaifa.
Kati ya bendi za Mkoa wa Morogoro zilizokuwa Mahenge ni Mahenge Jazz Band na Taifa Jazz Band, hii bendi ya pili ilianzishwa na Joakim Ufuta ‘Dokta’, huyu alikuja kuwa mpiga gitaa la solo maarufu sana katika bendi ya Cuban Marimba na TK Lumpopo. Mahenge pia kulikuwa na bendi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kwiro, Kwiro Jazz Band. Bendi hii ilirekodi mara kadhaa RTD, na wanamuziki wa bendi hiyo si mara moja walilalamika kuwa Morogoro Jazz Band iliwaibia mtindo wao wa Mahoka. Mpiga solo wa bendi ya shule ya sekondari ya Mkwawa, Orchestra Mkwawa, Simon Sewando alikuwa fundi mitambo wa bendi ya Kwiro kabla hajahamia shule ya Mkwawa. Alijulikana kwa jina ya ‘The mad scientist’ kutokana na kufumua fumua na kutengeneza amplifaya za bendi hiyo. Sewando amestaafu akiwa mwalimu wa electronics Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kulikuwa na Kilosa Jazz band ambako alitokea Abel Balthazar na mkasa wake wa kuhamia Dodoma Jazz band niliuandikia katika makala kuhusu bendi za mkoa wa Dodoma. Kulikuweko na Ifakara Jazz Band pia Sukari Jazz band bendi iliyokuwa mali ya kiwanda cha Sukari cha Kilombelo, kulikuweko na Ulanga Jazz band toka Ulanga na bila kusahau Njohole Jazz Band. Njohole Jazz Band walikuwa na nyimbo zao nyingi maarufu Afrika ya Mashariki nzima, kwa sababu walikuwa wakienda Nairobi kurekodi santuri za nyimbo zao. Lakini bendi hii ilikufa kutokana na mkasa wa kusikitisha sana. Walikuwa wakisafiri katika lori ambalo ndani yake pia kulikuwa na mzigo wa vinywaji, gari lile likapinduka na wanamuziki wote wakafa palepale, akabaki kiongozi wao tu aliyekuwa ametangulia kwa usafiri mwingine. Mungu awalaze pema…..Safari Iendelee.
Anko Kitime andika kitabu
ReplyDeleteKwa kweli hapa tumevuna madini, tena dhahabu tupu. Moja la kutazama ni hilo la kuwapo na bendi nyingi mkoa wa Morogoro kuliko Dar es Salaam.
ReplyDeleteTuangalie hiĺo kwa makini, linaweza kutufungulia kitu.
Ahsante Kitime. Tukizungumzia legacy basi yako ndio hii unayoijenga na kutuachia.