SAFARI yetu ya kuzikumbuka bendi mbalimbali nchini, wiki hii inatuingiza mkoa wa Iringa, lakini kati ya Iringa na Dodoma kuna wilaya inaitwa Mpwapwa. Hapa kulikuwa pia na bendi moja matata sana iliyoitwa Mpwapwa Jazz Band. Bendi hii haikuwa ndogo kwani
iliweza kurekodi nyimbo kadhaa ambazo zilipata umaarufu wa Kitaifa wakati wa
uhai wake, ikiwemo wimbo Nilikuwa sina
kazi, wimbo ambao unazungumzia hadithi ya kudumu ya kukimbiwa na mpenzi kutokana na kutokuwa na kipato.
Mji wa Iringa ulianza kama ngome ya Wajerumani walipokuwa
katika harakati za kumsaka Mutwa Mkwawa baada ya kuangusha ngome yake kule
Kalenga. Hata jina Iringa limetokana na neno la Kihehe 'Lilinga' yaani ngome. Jeshi la Wajerumani likiwa na maafisa wachache wa Kijerumani,
lilikuwa na askari wengi wa Kiafrika
kutoka pande mbalimbali za Afrika ya Mashariki na kati. Kulikuwa na askari wa
Kinubi, askari wa Kimanyema, askari wa Kizaramo, askari wa Kinyamwezi na
makabila mengine kadha wa kadha. Askari hawa wakaanza kuishi na familia zao
maeneo yanayojulikana kama Miyomboni, jirani na kituo kikuu cha polisi ambapo
haswa ndipo yalikuwa makao makuu ya jeshi la Wajerumani. Watoto na
wajukuu wa askari hawa walikuwa
wakijitambulisha kuwa wao ndio wenyeji halali wa mji wa Iringa. Hivyo walikuwa
na timu ya mpira iliyoitwa Boni kifupi cha Born Town, wakiwa wanamaananisha
kuwa wao ndio wazawa haswa wa pale mjini. Na wakati huohuo wakaanzisha pia
bendi iliyoitwa Born Jazz band, pengine kati ya bendi za awali za mji huu.
Kama ilivyokuwa Dodoma kuwa na bendi
inaitwa Sextet Jazz band, Iringa kulikuwa na bendi inaitwa Habanero Jazz Band.
Sextet na Habanero yalikuwa majina ya bendi mbili za huko Cuba. Katika zama
hizo bendi za hapa nchini zilikuwa zikiiga muziki kutoka Cuba, si Congo. Bendi
ya Iringa iliyokuja kupata umaarufu mkubwa ilikuwa Highland Stars Band. Mpiga
gitaa Abel Balthazar ni moja ya wapigaji maarufu waliowahi kupitia bendi hii.
Nyumbani kwa mpiga solo maarufu wa
Msondo Ngoma Ridhwani Abdul Pangamawe, ndipo yalipokuwa yakifanyika mazoezi ya
Highland Stars Band. Mzee Abdul Pangamawe na mama Ridhwani wote walikuwa wakijua
kupiga magitaa, si ajabu kabisa nyumba hiyo kutoa mpiga gitaa na kinanda mahiri anayetingisha nchi mpaka
leo. Moja ya wimbo wao maarufu wa Highland Stars ulikuwa ni Sitasita Mpenzi.
Bendi nyingine mjini Iringa ilikuwa ni Iringa Jazz Band, hii ilikuwa mali
ya TANU Youth League. Miji mingi sana
ilikuwa na bendi za TANU Youth League katika miaka ya 60 na 70.
Mkwawa High School, ambayo awali ilikuwa shule ya ‘Wazungu’ na iliyokuwa
ikiitwa St George and St Michael European School, ilikuja kuwa na bendi nzuri
sana ya wanafunzi iliyoitwa Orchestra Mkwawa. Wakiwa na mtindo wao waliouita
Ligija walitoa burudani kila mwisho wa wiki katika ukumbi wa Welfare Center,
katika utaratibu wa madansi ya mchana maarufu kama Buggy, wao kama wanafunzi
hawakuwa na ruksa ya kuwa katika kumbi za dansi usiku, hivyo waliweza kupiga
muziki huo mchana tu. Pia katika shule hiyo hiyo kulikuwa na bendi nyuingine
iliyokuwa ikipiga muziki wa Kizungu na iliitwa Midnight Movers. Marehemu Eddy
Hanspoppe, Deo Ishengoma, Martin Mhando walikuwa kati ya wanamuziki wa bendi
hii. Vyombo walivyotumia vilikuwa ni vile ambavyo vilikuwa vikitumiwa na bendi
iliyokuwa ya TANU Youth League. Magitaa ya bendi hii hatimae yalikuja
kuchukuliwa na vijana wachache walioanzisha bendi iliyokuwa ikijulikana kama
Chikwalachikwala. Chikwalachikwala ikajigawa na kukapatikana bendi iliyoitwa
BOSE Ngoma, jina lililotokana na aina ya speaker walizokuwa nazo.
Chikwalachikwala Jukwaani Kijiji cha Mgama,
Mwaka 1987 ikazaliwa Tancut Almasi Orchestra bendi nyingine kubwa iliyowahi kutokea Iringa, bendi hii ilikuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Diamond Cutting Company kilichokuwa pale Iringa. Majina ya wanamuziki maarufu waliopitia bendi hii ni mengi sana kati hao walikuweko mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Banza Tax, Mafumu Bilali, Kawelee Mutimwana, Shaban Yohana Wanted, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe na wengine wengi akiwemo mwandishi wa makala hii.
TANCUT ALMASI ORCHESTRA JUKWAANI
Bendi nyingine iliyowahi kuweko Iringa
mjini ni Ruaha International Orchestra , iliyokuwa mali ya mfanya
biashara mmoja aliyeitwa Mtandi. Bendi hii ilikuwa chini ya uongozi wa muimbaji
marehemu Kalala Mbwebwe na wimbo wake Lutadila
ni kumbukumbu kubwa kwa wapenzi wa bendi hii. Bendi nyingine zilizowahi
kuwa Iringa, zilikuwa ni VICO Stars iliyokuwa mali ya kanisa Katoliki, Living
Light Band iliyokuwa mali ya hoteli ya Living Light.
Kumaliza mkoa huu bila kutaja bendi maarufu ya JKT Mafinga haitakuwa sawa.
Bendi hii ilikuwa maarufu kwa jina la Kimulimuli, jina hili lilitokana na taa
za disco zilizokuwa zinafungwa wakati bendi hii inapiga. Vyombo maarufu vya
muziki aina ya Ranger FBT ambavyo vilikuwa vikitumika na bendi nyingi miaka ya
80 vilikuwa vinakuja na taa za disco, na wenyeji wa Mafinga walikuwa wakisema
kwa Kihehe ‘Twibita kukina kimulimuli’ yaani tunaenda kucheza Kimulimuli, na
hakika jina hilo ndilo likawa utambulisho wa bendi hiyo, na hata bendi yenyewe ilitunga nyimbo kusifia
jina lao la Kimulimuli. Kati ya
wanamuziki maarufu waliowahi kupitia bendi hii ni Zahiri Ally Zorro na Zakaria
Daniel Mabula Tendawema ambaye niliandika alipata jina la Tendawema kutokana na
kutunga wimbo ulioitwa Tenda wema nenda
zako alipokuwa Shinyanga Jazz band. Safari inaendelea….
Ni kweli kabisa eneo la miomboni ndiko kulikuwa na timu ya Born kama ulivyoeleze.
ReplyDeleteUkiizungumzia Ruaha Intenational namkumbuka mpiga gitaa Juma Msosi huyu Bwana alikuwa mtumishi wa Serikali akifanya kazi pale Regional Bloc