Thursday, July 28, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 6 -MBEYA

 


Hebu tuendelee na safari ya kukumbuka bendi mbalimbali nchini, leo tuanzie mkoa wa Mbeya, tuanze na wilaya ya Mbeya, wilaya ambayo kabla ya mwaka 1927 ilikuwa ikijulikana kama wilaya ya Igali.
Mbeya ilikuja kuanza kupata umaarufu kutokana na kugundulika kwa dhahabu sehemu mbalimbali za kuzungukia mji huu kuanzia mwaka1906, hali iliyoendelea kwa karibu miaka ishirini baada ya hapo. Mji ukapata wageni kutoka kila kona ya Afrika Mashariki na Kati mpaka visiwa vya Ngazija, watu wakaja Mbeya na miji jirani kutafuta utajiri.

Popote penye vijana wengi, tena wakiwa wanatafuta pesa, hakukosekani burudani na hasa burudani ya muziki. Bahati mbaya si mengi yaliyohusu burudani za wakati huo yaliyowekwa kwenye kumbukumbu,lakini kati ya machache tuanze na historia ya mtu moja aliyekuwa maarufu sana aliyeitwa John Benedict Mugogo Mwakangale, mwenyewe alipendelea kuitwa JBM. John Mwakangale, JBM alikuwa mwanasiasa mashuhuri katika harakati za kupigania Uhuru na baadae katika siasa ya kutafuta umoja wa Afrika. Alifanya kazi kubwa ya kutambuliwa na hatimae alikuweko katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Tanganyika huru chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na akateuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa Kazi, pia alikuwa Mbunge wa Nyanda za juu kusini kwa kipindi kirefu, kabla ya Uhuru na hata baada ya Uhuru. Pamoja na yote hayo JBM pia alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki. Kati ya mwaka 1959 na mwaka 1960 alikwenda Zambia, wakati huo ikiitwa Northern Rhodesia, alikwenda kununua vyombo vya muziki kwa ajili ya bendi yake iliyoitwa Free Mwakangale Jazz. Alipokuwa huko akakutana na vijana kutoka jimbo la Luanshya waliokuwa  na kundi lao      wakipiga vizuri sana muziki, akaongea nao na hatimae wakakubaliana kuondoka kwao na kuingia Tanganyika kujiunga na Free Mwakangale Jazz, mmoja wa vijana hao alikuwa Michael Enoch. Michael Enoch baadae alikuja kuchukuliwa na Dar es Salaam Jazz Band na kuiendeleza kwa miaka mingi akiwa mpiga solo, kisha akahamia Dar es Salaam International akiwa mpiga saksafon  na hatimae Mlimani Park Orchestra alikoendeleza umahiri wake katika saksafon, na kupewa majina mengi ya sifa, King Enoch, na Teacher, Michael alikutwa na mauti  alipokuwa DDC Mlimani Park Orchestra.
Bendi ya Free Mwakangale Jazz makao yake makuu yalikuwa mji uliopewa jina la Neu Langenburg na Wajerumani lakini wote tunaufahamu siku hizi kama Tukuyu, , pamoja na Michael Enoch bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki wengine wanaokumbukwa ni Ben Jack na Saiz Vera.
Kuna hadithi ya kuchekesha na kusikitisha kuhusu kisa kilichofanya Free Mwakangale Jazz ife na Michael Enoch atue Dar es Salaam Jazz Band.
Siku moja  bendi ya Free Mwakangale Jazz ilipata safari ya kwenda Mwanza na baada ya kufika huko ilifanya maonyesho kadhaa, siku moja vijana hawa walikodi gari ili kubeba vyombo vyao, pengine wakati huo kwa ugeni na pengine hata Kiswahili walikuwa hawajakifahamu sawasawa, dreva wa gari akawaomba wamsubiri akaweke mafuta, wakamruhusu, alipoondoka hakuonekana tena ukawa ndio mwisho wa Free Mwakangale Jazz. Wanamuziki wakajikuta wamekwama Mwanza, bahati nzuri baada ya muda mfupi walipata kazi ya kupiga muziki katika bendi moja pale Mwanza, wakiwa katika bendi hiyo, muwakilishi wa Dar es Salaam Jazz Band , marehemu Limi Ally,ambaye alikuwa katika harakati za kumtafuta mpiga gitaa la solo akamuona Michael Enoch, na ndipo wakakubaliana kurudi nae Dar es Salaam kujiunga na Dar es Salaam Jazz Band.

Bendi nyingine ya Mbeya ilikuwa TANU Youth League Jazz Band, bendi iliyokuwa maarufu miaka ya sitini na ilirekodi nyimbo kadhaa RTD, kati ya nyimbo zake zilizokuwa maarufu ni ule ulioitwa Nampenda Firida mwenye macho mazuri. Kulikuwa na bendi nyingine ambayo ilisemekana ilitokana na kufa kwa TANU Youth League Jazz Band ilikuwa ikiitwa  bendi ya Lemi au Remi.

Bendi nyingine iliyokuweko Mbeya ni hiyo iliyoko kwenye picha ambayo iliitwa Azimio Co Bantou Jazz Band. Ukiangalia vizuri picha hiyo, utaona ilipigwa katika kota zilizokuwa za wafanyakazi wa  serikali zilizokaribu na mitaa ya Ghana, pengine hapo ndipo yalikuwa masikani ya bendi hii.

Katika tasnia ya muziki wa bendi kuna utamaduni wa kuigana majina, kwa mfano baada ya kuundwa bendi ya Dar es Salaam International Orchestra, bendi nyingi ziliibuka na kujiita international, zikiwemo Dodoma International Orchestra, Tanga International Orchestra, Ruaha International Orchestra na kadhalika. Kule Sumbawanga ikaundwa bendi iliyoitwa Rukwa International Orchestra, bendi hii ilijitokea sana na kushiriki matukio ya kitaifa. Rukwa International Orchestra ilikuwa mojawapo ya bendi zilizojitokeza kushiriki Mashindano ya Bendi Bora (MASHIBOTA) yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam miaka ya 90.

No comments:

Post a Comment