Thursday, July 21, 2022

KAMIKI WIMBO WA MIAKA YA SABINI UNAOKUMBUKWA NA WAZEE MPAKA LEO

Kamiki yeye motema aaa, Kamiki yeye motema oooo. Wapenzi wa muziki wa kavasha wa miaka ya 70 na 80, hawakosi kuanza kutabasamu, mistari hiyo niliyoanzia habari hii ilikuwa ni maneno ya mwanzo ya wimbo maarufu enzi hizo, wimbo ulioitwa Kamiki. Wimbo huu ulipigwa na bendi  iliyoitwa Orchestra Kiam kutoka Kongo. Bendi hii ilikuwa na nyimbo nyingi sana zilizopendwa sana karibu Afrika nzima. Wakati huo ulikuwa ndio wakati ambapo vijana waliojiona wa kisasa Afrika nzima walikuwa wakivaa suruali pana zilizoitwa Bugaluu na viatu vyenye soli ndefu ambavyo vilifahamika kama platform. Shati zilikuwa ni zenye kubana sana na siliitwa ‘slimfit’, huku kichwani kila kijana mjanja alikuwa nafuga nywele ndefu zilizokuwa zikichanwa kwa mtindo wa Afro. Vijana wa kiume walikuwa wakitumia sana chanuo za chuma ambazo zilipashwa moto kisha kunyoosha nywele ili ziwe ndefu. Lakini turudi kwa Orchestra Kiam, historia ya kundi hili ilianza baada ya Papa Noel, mwanamuziki mkongwe wa Kongo aliyepigia bendi nyingi maarufu za Kongo ikiwemo TP OK Jazz, kuwa na taratibu za kusaidia vijana waliotaka kujiendeleza kimuziki waliokuwa wakiishi jirani na kwake, hivyo basi  alitengeneza bendi iliyoitwa Orchestra Bamboula, bendi hii haikuwa na vyombo, vijana walifanya mazoezi kwa magitaa makavu nyumbani kwa mkongwe huyu na walipo bahatika kupata sehemu za kufanya  onyesho, Papa Noel alikuwa akikodi vyombo na bendi kuweza kupiga, lakini kwa mtindo huu mara nyingi hawakupata malipo mazuri, lakini nia yao ilikuwa kupiga muziki na si kusaka fedha.
Siku moja Papa Noel alisafiri na TP OK Jazz kwenda kufanya onyesho nchini Algeria aliporudi alikuta vijana wake wamesambaratika, basi akatafuta vijana wengine na kuunda kundi jipya lililofanya mazoezi miezi sita. Baada ya muda huo Papa Noel alienda kwenye studio ya mkongwe mwingine wa muziki  wa Kongo ,Verckys, na kulipia gharama za kurekodi, kundi la Bamboula  likaingia studio na kurekodi na chini ya fundi mitambo wa studio hiyo Kidiata M’Pole, bendi hiyo ikarekodi  nyimbo nne katika muda wa masaa machache, kama ilivyokuwa taratibu miaka hiyo.
Ilikuwa ni kawaida ya Verckys kusikiliza nyimbo  zilizorekodiwa katika studio yake, na aliposikia nyimbo hizo mpya akamtuma meneja wake kuwatafuta vijana waliopiga muziki  huo. Meneja wake aliyekuwa anamfahamu Frank Muzola Ngunga, akaanza msako. Muzola alipopatikana alisema wana nyimbo nyingine pia ambazo hawajazirekodi, wakaalikwa kuzirekodi zote, Muzola akasita kurekodi nyimbo hizo kwani alihisiki atakuwa anamsaliti Papa Noel, wenzie wakamshinikiza hatimae akakubali. Wakati huo Papa Noel alikuwa akitafuta fedha za kukamilisha malipo ya kuweza kutengeneza santuri ya nyimbo nne zilizorekodiwa na pia kumlipa fundi mitambo aliyezirekodi. Kesho yake Papa Noel alikwenda studio kukamilisha malipo alishangaa kukuta kundi lake likiwa studio linarekodi likiwa linasikilizwa na Verckys, ugomvi mkubwa ukaanza hapohapo, lakini hatimae Verckys alimzidi kete Papa Noel kwa kumtaka aonyeshe mkataba wake na wana muziki hao. Papa Noel aliondoka kwa hasira hakuna anaejua alizipeleka wapi nyimbo zile nne zilizorekodiwa kwani hata yeye alipoulizwa miaka mingi baadae alisema hakumbuki.
Verckys aliamua kuliita kundi lake jipya,  Orchestra Kiam, Kiam ikiwa kifupi cha Kiamwangana jina halisi la Verckys. Wanamuziki waanzilishi wa kundi hili walikuwa Frank Muzola Ngunga, Bakolo Keta, Jeannot Botuli Ilonge na Mboyo Bola Eddie waimbaji, wapiga gitaa la solo walikuwa  Guyno na Souza Vangu (Souza alijiunga miezi michache baadae), wapiga gitaa la  rhythm walikuwa  Lélé Nsundi na Djo Morena, kwenye gitaa la bezi alikuweko Vieux Kody na mpiga drums  Suké Ngonge. Wanamuziki hawa wakaingia mkataba na Verkcys akampa kila mmoja wao fungu la bonas ya kujiunga na bendi na kisha wakawa wanalipwa mshahara, shilingi alfu thelathini katikati ya mwezi na shilingi alfu sabini mwisho wa mwezi, na wengine pia wakanunuliwa samani kwa ajili ya vyumba vyao, hakika walijiona wamepata mfadhili wa kweli ukikumbuka kuwa kwa Papa Noel, walikuwa wakiishi kwa kubahatisha. Walikabidhiwa vyombo vipya wakawa wanafanya mazoezi siku tatu kwa wiki na siku za wikiendi wakawa wanapiga katika kumbi mbalimbali ambazo zilikuwa zimeingia mkataba na Verckys. Verckys aliendeleza utaratibu huu wa kuwa na bendi alizozilipa mshahara mdogo na kupata mapato makubwa kutokana na kuzikodisha kwenye kumbi na pia kuuza santuri za bendi zilizokuwa chini yake.
Mwaka 1974 Orchestra Kiam waliingia studio na kurekodi wimbo wa Nina, wimbo wao wa kwanza kupendwa sana, ulikuwa utunzi wa  Bakolo Keta, utunzi mwingine wa Bokolo ulioitwa  Baya-Baya ulisaidia sana umaarufu wa bendi hii. Umaarufu wa Kiam ukaanza kuwapa uchu matajiri wengine kuimiliki bendi hii. Mfanya biashara mmoja Mbuta Suka alianzisha label yake aliyoiita Mabele Productions, na  mwanzoni mwa mwaka 1975 aliwashawishi wanamuziki kadhaa wa Kiam kuja kurekodi kwa kutumia label yake  kwa kutumia utaratibu  ulioitwa zong zing, yaani kurekodi nje ya bendi. Kundi kubwa la Kiam lilishiriki kazi hii na kurekodi nyimbo nne. Mbuta Nsuka alianza kusambaza santuri za nyimbo hizo na kuzitambulisha kuwa zimepigwa na Orchestra Baya-Baya, Verckys alipozisikia nyimbo hizo alijua ni bendi yake akawasimamisha kazi wanamuziki wote walioshiriki. Mbuta Nsuka akatumia fursa hiyo kuwashawishi wanamuziki hao waachane na Verckys, na ndipo rasmi ikaundwa bendi ya Orchestra Baya- Baya.

Huku Orchestra Kiam kikawa kilio maana waliobaki walikuwa ni muimbaji Frank Muzola Ngunga, mpiga bezi  Vieux Kody na mpiga rhythm Djo Morena. Muzola Ngunga akapewa kazi ya kutafuta wanamuziki wengine kufufua bendi.  Baada ya kama mwezi kundi likafufuka na waimbaji Germain Kanza, Adoly Bamweniko na Otis Mbuta, kwenye magitaa akapatikana mpiga solo Adamo Lewis na  Djuké, kwenye gitaa la rhythm akaweko Antoine Denewadé. Baada ya mazoezi ya miezi michache Kiam wakarudi tena studio. Hapo ndipo vikatoka vibao maarufu kama Memi, Yanga Yanga na Kobondela .

Wakati huo Orchestra Baya-Baya walianza safari ya kuzunguka kupiga muziki miji mbalimbali, muda si mrefu bendi ikakwama  katika mji wa Bandaka kutokana  na kukosekana mapato.  Ukawa mwisho wa Orchestra Baya- Baya, Lélé Nsundi ,Bakolo Keta na Suké Ngonge wakarudi Orchestre Kiam. Huyu Lélé Nsundi alikuwa mpangaji mzuri sana wa muziki hivyo ilianza kazi  nzuri sana ya  nyimbo mpya ikianzia na wimbo maarufu wa Kamiki , wimbo huu ulitungwa na Muzola Ngunga kumsifia mwanamke aliye kuwa akiishi nae wakati huo. Wimbo huo ulipendwa Afrika nzima wakati huo na hata leo. Mpaka mwaka 1977 Kiam waliendelea kutoa vibao motomoto kama Ifantu, Bomoto, Ya Yona, Mbale, Bakule, Masumu na kadhalika. Mwezi Agosti mwaka 1978, Kiam walirekodi wimbo ulioitwa Exode  wakiwa na muimbaji mualikwa kutoka Gabon alieitwa Mack Joss. Mark akawazindua kuhusu hakimiliki na jinsi Verkcys alivyokuwa akiwadhulumu haki zao hizo, kwa kuwapa mshara tu bila kuwapa mirabaha iliyotokana na mauzo ya santuri walizotunga na kushiriki. Elimu hii ikawafanya  Bakolo Keta , Lélé Nsundi na Adoly Bamweniko, kuondoka Kiam mara moja. Lilikuwa pigo kubwa kwa Kiam kwani baada ya hapo hawakuweza kutoa tena nyimbo za kutikisa wapenzi wao.

Verckys alijitahidi sana kulitambulisha kundi la Kiam Afrika ya Mashariki na Afrika ya Magharibi, jambo ambalo lilifanya kundi hili kukumbukwa zaidi katika maeneo haya kuliko Kinshasa kwenyewe mpaka leo. Lakini hatimae mwaka 1983, Muzola Ngunga na Verckys waliamua kulivunja rasmi kundi la Orchestra Kiam.

 

No comments:

Post a Comment