Katika safari yetu ya kuzikumbuka bendi mbalimbali nchini,
kuna kitu kinaonekana wazi kabisa, katika swala la muziki kwa ujumla tumerudi
nyuma sana. Kulikuwa na bendi binafsi, bendi za serikali , bendi za chama
tawala na karibu kila mji ulikuwa na zaidi ya bendi moja. Watu walikuwa
wachache sana kuliko siku hizi lakini walikuwa na na nafasi za uchaguzi wa
burudani kuliko siku hizi. Sababu ni nyingi lakini si nia ya makala hizi
kuongelea hayo japo baada ya mzunguko wa nchi nzima pengine italazimika kujiuliza
tumefikaje huku tuliko? Kabla ya kuendelea na safari kuna kitu kiko wazi
kinajitokeza, wakati wa awamu tatu za mwanzo za uongozi wa nchi hii, wasanii wa
kila mahala walithaminika, ndio maana unakuta kila mkoa kulikuweko na makundi
ya muziki ambayo hatimae yaliweza kujitokeza na kufahamika nchi nzima. Siku
hizi ni kawaida kabisa viongozi wa juu kuoneka wakisindikizwa na wasanii
‘wakubwa ‘ wa kutoka Dar es Salaam, utadhani huko wanakokwenda hakuna wasanii,
au wanaenda nchi nyingine kutangaza sanaa ya nchi yao.
Safari yetu leo
inatupeleka mikoa ya kusini, mikoa hii haikuwa nyuma kabisa katika mambo ya
dansi, kulikuweko na bendi toka enzi ya mkoloni. Kati ya bendi ambazo nina
kumbukumbu nazo, nianze na White Jazz Band iliyokuwa na masikani yake mjini
Lindi, bendi hii kama zilivyokuwa bendi
nyingine ilipitisha wanamuziki wengi lakini kati ya wanamuziki waliokuja
kung’aa nchini waliopitia bendi hii ni marehemu Mzee Kasim Mapili, yeye alinza
kupiga muziki katika bendi hii mwaka 1958, kuna kila sababu kuamini kuwa
ilikuweko kabla ya mwaka huo. Mwaka 1963 tayari kulikuwa na bendi iliyokuwa
inaitwa Jamhuri Jazz Band mjini Lindi, bendi hii ilikuwa mali ya TANU Youth
League, au Jumuiya ya Vijana wa TANU. Jamhuri Jazz Band hii ya ilikuweko kabla ya Jamhuri Jazz Band ile ya
Tanga, japo tutakapofika mkoa wa Tanga tutapata historia ndefu zaidi ya bendi
hiyo.
Wakati tukiwa bado Lindi, haiwezekani kutoitaja Mitonga Jazz
Band. Bendi hii ilifanya makubwa kwa kutoa mfululizo wa vibao pendwa, kikiwemo
Mariana na Sitaoa tena Mchinga, ambavyo vikipigwa mpaka leo bado wanaovisikia
hata kwa mara ya kwanza huvipenda. Album ya wimbo Mariana ilirekodiwa na
mafundi mitambo wa Radio Tanzania Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Polisi pale
Lindi, lakini ubora wake unazishinda nyimbo nyingi zilizorekodiwa kwenye studio
za kisasa, jambo linaloonyesha umahiri wa wanamuziki wa bendi hiyo, na umahiri
wa mafundi mitambo.
Tukitoka Lindi tuingie mji wa Masasi, mji huu nao ulikuwa na
bendi nyingi na ni mji ambao umewahi kutoa wanamuziki wengi ambao walikuja kuwa
maarufu Afrika ya Mashariki nzima. Tuanze na Masasi Jazz Band, bendi hii ilitoa
wanamuziki maarufu kama Gerald Nangati, wapiga gitaa la rhythm wawili mahiri, Ally Makunguru aliyekuja
kupigia bendi za JKT Kimbunga Stereo, Mlimani Park, International Orchestra
Safari Sound na hatimae kuhamia Kenya ambako pia alipiga muziki katika bendi
kubwa maarufu za huko. Masasi Jazz Band ndiko alikotoka Charles Kasembe ambaye alikuja kupiga na
Mbaraka Mwinshehe, akapitia Dodoma International Orchestra na hatimae akahamia
Kenya alikokuwa na bendi yake ya Les Volcano.
Bendi nyingine iliyokuweko Masasi ilikuwa Umoja Jazz Band,
pia kulikuweko na TANU Youth League Jazz Band katika mji huo, jambo lililokuwa
kawaida katika miji mingi, ni wazi kulikuwa na sera za makusudi za TANU
kuhakikisha kila wilaya kuna kuwa na bendi ya vijana wa TANU. Bendi hii ya TANU
Youth League Jazz Band ndio ilikuwa bendi ya kwanza ya mwanamuziki mwingine
aliyekuja kuwa mpiga solo mahiri sana katika bendi za JKT Kimbunga Stereo na
DDC Mlimani Park Orchestra Mzee Henry Mkanyia.
Kwa mara ya kwanza nilipokutana na Ally Makunguru mwaka
1975, alinambia kuwa alipokuwa Masasi pia alikuwa akipigia bendi iliyokuwa
ikiitwa Kochoko Jazz band, hiyo ni bendi nyingine ya mji huyo. Masasi ulikuwa
mji mdogo sana wakati huo lakini ulikuwa na bendi nyingi kiasi hiki, na hizi
nilizotaja hapa, ni zile zilizoko katika kumbukumbu zangu tu.
Nachingwea nako hakukuwa kimya kulikuwa na bendi iliyoitwa
Mondomondo Jazz band, bendi iliyokuwa ikileta burudani kwa wakazi wa mji huo.
Mtwara ulikuwa mji mwingine wa maraha kule kusini mwa
Tanzania, toka miaka hiyo mpaka leo Mtwara imeendelea kutoa wanamuziki mahiri
ambao wamekuwa waking’aa kitaifa na kimataifa. Kati ya bendi zilizowahi kuweko
Mtwara tuanze na bendi iliyochukua jina la mji huo Mtwara Jazz Band, pia mapema
baada ya Uhuru ilikuweko bendi iliyoitwa Honolulu Jazz Band. Mamlaka ya Bandari
katika miaka ya zamani ilikuwa inajihusisha sana katika michezo na utamaduni,
na hapo Mtwara ikaanzisha bendi ilioyoitwa Bandari Mtwara Jazz Band. Lakini pia
ziliwahi kuweko bendi nyingine zaidi katika mji huu, kulikuwa na Mambo Jazz
Band na bendi nyingine iliyoitwa Bantu Jazz Band… Kwa leo nimalizie kwa kuitaja
bendi iliyokuweko mji ambao hautajwi sana linapokuja swala la bendi nao ni
Kilwa Masoko. Mji huu nao ulikuwa na bendi yake iliyoitwa Lucky Star Jazz Band
No comments:
Post a Comment