Thursday, July 14, 2022

ZAMANI WATU WALIENDA DANSINI WAKAKUTA POMBE, SIKU HIZI WANAENDA KWENYE POMBE WANAKUTA DANSI

 

Kumbukumbu zangu huwa zinanirudisha Iringa nilipokuwa na umri wa miaka sita au saba hivi. Nadhani ndipo nilipoanza kutambua kuwa watu huwa wanaenda dansini. Maana mara kwa mara wazazi wangu walikuwa wanajitayarisha wanavaa nguo nzuri halafu wanatuaga ‘Haya laleni sisi tunaenda dansini’.
Moja ya dansi nakumbuka lilikuwa limepigwa na Cuban Marimba wakiongozwa na Salum Abdallah, nakumbuka kwa sababu kesho yake Mwalimu Nyerere alikuja kuhutubia watu wa Iringa kwenye uwanja ambapo upo sasa ni uwanja wa Samora. Wakati huo ulikuwa ni uwanja wa mpira wa shule ya Mshindo Middle School, na baba yangu alikuwa Headmaster wa shule ile. Nyumba yetu ilikuwa pembeni tu ya uwanja huo wa mpira. Siku hiyo alipokuja kuhutubia Mwalimu Nyerere, wimbo uliokuwa ukisikika kwenye spika ukirudia rudia, ulikuwa wimbo wa Cuban Marimba na baadhi ya  maneno yake yalikuwa ‘ Tutie jembe mpini, twendeni tukalime’, lazima ilikuwa baada ya Uhuru maana ndio nyimbo baada ya Uhuru zilivyokuwa na ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujenga nchi mkoloni kisha ondoka.
 Wakati wimbo huo ukiimba, mama yangu akatuambia na wadogo zangu kuwa wimbo huo walikuwa wameucheza jana yake dansini. 

Kwa kweli toka nikiwa mtoto, dansi kwangu ni neno la furaha  kwenye maisha yangu. Nikiwa mdogo  wazazi wangu walikuwa wakituonyesha namna ya kucheza aina mbalimbali za dansi, zikiwemo tap dancing, aina ya dansi ambayo visigino vya viatu lazima uvigonge kwa nguvu sakafuni wakati wa kucheza kufuatia mapigo ya muziki, hivyo basi vinatoa beat fulani kufuatana na wimbo, dansi moja ngumu kuicheza maana inachosha baada ya dakika moja tu. Tulifundishwa kucheza  chachacha, waltz, foxtrot na aina nyingine za dansi ambazo sijapata hata  kujua majina yake.

Nyakati hizo na miaka mingi baadae, mtu akiaga anakwenda dansini, jambo la muhimu atakalolifanya huko ni kucheza nyimbo nyingi kadri atavyoweza. Kesho yake mazungumzo kuhusu dansini ni kuulizana nyimbo ngapi zilichezesha. Mpenzi wa muziki kurudi nyumbani akiwa kachoka kwa kucheza ilikuwa ndio dalili ya kufurahia kwa usiku ule.

Miaka mingi baadae hatimae nikaja kuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi.  Hii aina ya muziki  uliokuja kuitwa muziki wa dansi, ulipewa jina hili kuanzia mwaka 1986 baada ya mkutano mkubwa wa wanamuziki ulioitishwa na Baraza la Muziki Tanzania kuja na wazo la kuwa na vyama vya muziki, ili kutofautisha na muziki wa Taarab, ndipo kikaundwa Chama cha Muziki wa Dansi na dhana ya muziki wa bendi ambao nia yake ilikuwa kucheza ukaitwa 'muziki wa dansi'.

Muziki wa bendi ambao sasa unaitwa muziki wa dansi, ulitungwa na hatimae kupigwa kwa vifaa vya kisasa na lengo kubwa ni kuwa wapenzi wa muziki huo watacheza.  Katika miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini, bendi zilikuwa zikitangaza aina muziki itakaoupiga, kwa mfano kiongozi wa bendi aliweza kutoa maelezo yafuatayo kabla ya kupiga wimbo. ‘Muziki ufuatao unaitwa Dada Adija, umepigwa katika mtindo wa Cha Cha’. Basi muziki ukianza wapenzi wa muziki wangeingia uwanjani na kucheza ChaCha. Na hivyo hivyo kama wimbo ni Twist, Bolelo, Charanga na kadhalika, hata kucheza kulikuwa na mpangilio unaoeleweka.

Tungo za zamani zilikamilishwa kwa muungano wa mawazo kutoka kwa wanamuziki mbalimbali katika bendi. Mtunzi wa awali aliweza kuleta  mashahiri, mara nyingine yakiambatana na melodia na kuwaimbia wenzie ambao walianza kutunga vipande vyao kupitia  vyombo mbalimbali wanavyovipiga. Tungo nyingi za awali zilianza kwa rumba, na ilipofika katikati mwendo ulibadilika na kuingia katika kile tulichokuwa tukikiita ‘chemka’.
 Chemka mara nyingi ilianza kwa kuimba na kisha kuingia kipande cha gitaa la solo. Hapa ndipo wapiga solo walikuwa wakipimwa kwa umahiri wao wa kutunga na kupiga vipande vya solo ambavyo vingeweza kuwateka akili wasikilizaji na kuwafanya wacheze dansi.



Katika bendi nilizopitia kama vile TANCUT Almasi na Vijana Jazz Band, baada ya bendi kukamilisha kuufanyia mazoezi wimbo, wimbo huo ulianza kupigwa katika maonyesho mbalimbali, lakini jambo la muhimu ambalo wanamuziki wote tulikuwa tukiliangalia lilikuwa ni Je, watu wanaucheza wimbo mpya? Ikionekana wimbo  umekosa hamasa ya kuwasimamisha  wachezaji, wimbo huo ulirudishwa mazoezini na kubadilisha vitu tulivyohisi vinafanya watu wasipende kucheza wimbo ule. Na mara nyingine wimbo huo ulitupwa pembeni moja kwa moja, mamia ya nyimbo  katika bendi mbalimbali ziliishia kupigwa kwenye kumbi mara moja tu na hazikurudiwa tena, kwa kuwa tu watu hawakuchangamkia kuzicheza.
Siku hizi mambo yako tofauti kabisa, unaweza kuingia kwenye onyesho la muziki wa Taarab, muziki ambao zamani ulikuwa ukisifika kwa kuwa muziki wa kusikiliza tu, ukakuta wapenzi wakitiririka jasho kwa kucheza nyimbo mbalimbali za Taarab. Na ukaingia katika onyesho la ‘muziki wa dansi’, ukakuta waimbaji wakitoka mishipa ya shingo, solo likapigwa kwa ufasaha, vyombo vingine vikachangia lakini hakuna anaeshughulika kucheza dansi hilo. Kama ingekuwa  zamani, hiyo ni dalili ya moja kwa moja kuwa muziki huo hauwafurahishi wapenzi. Lakini hizi ni zama nyingine.

Katika zama hizi, bendi huwa na wacheza show wake au hata waimbaji wa bendi nao wakatengeneza show yao, kisha wakawa wanapiga muziki na kucheza wao wenyewe. Ni kama nilinganishe na msemo maarufu wa  'kujitekenya halafu kucheka mwenyewe'. Wimbo ukiisha  wanamuziki huanza wimbo mwingine bila  kuhisi kuwa kuna tatizo.
Teknolojia imeleta aina nyingine ya kuonyesha upenzi na unazi wa muziki. Wapenzi wa muziki siku hizi huonyesha upenzi wao wa muziki kwa kuchukua simu na kurekodi  bendi ikiimba na kucheza, hawachezi wala kutikisika, kazi yao ni kunyanyua simu na kurekodi. Vipande hivi vya video husambazwa kwenye makundi ya Whatsapp, vikiambatana na sifa kuhusu ubora wa bendi hizi. Ndio namna ya zama hizi kufurahia muziki.
 Hakika kuna nyimbo ambazo wapenzi huchangamkia  kwa kucheza sana, lakini ukiangalia kila mtu anacheza akili inavyomtuma, hakuna tena mpangilio wa kucheza staili maalumu ya muziki. Ile staili ya wapenzi kukumbatiana kwa hisia wakati wa kucheza rumba imepotea, si ajabu kabisa kumkuta mtu anacheza na mpenzi wake, kila mtu na staili yake na wakati huohuo kila mmoja anatuma meseji kwenye simu. kweli zama zimebadilika mno.

Mwisho nimalizie na sentensi ya hali ninayoiona  katika muziki wa dansi, 'ZAMANI WATU WALIKWENDA DANSINI NA KUKUTA POMBE, SIKU HIZI WATU WANAENDA KWENYE POMBE NA KUKUTA DANSI'


 

1 comment:

  1. Ujazungumzia na bendi ya Orch Mambo Bado.
    Hii bendi pia walikuwa na style yao dansi likitaka kuanza zile taa za kawaida uzimwa na kuwashwa taa za marembo na kadri dansi likiendelea Kiongozi Asossa alikuwa anataja lineup ya Wanamuziki wake hii nayo ilikupasa uiweke ikizingatia wewe Kitime ni muhusika

    ReplyDelete