Wednesday, August 10, 2022

WANAMUZIKI WA SASA WANAKUBALI KUKOSOLEWA?

 

Top Ten Show 1989

Jana nilikuwa naangalia maktaba yangu ya kanda za video za zamani, nikaiona kanda moja iliyonirudisha miaka mingi sana nyuma. Ilikuwa ni kanda ya video ya onyesho moja la bendi ya Tancut Almasi Orchestra lililofanyika katika ukumbi wa klabu ya bendi hiyo eneo la Sabasaba pale Iringa.
Mwaka 1989 yalianza kufanyika mashindano ya bendi yaliyoitwa Top Ten Show, mashindano haya yalifikia kilele mwaka 1990. Yalikuwa ni mashindano makubwa sana ya muziki wa dansi na mpaka leo hayajawahi kufanyika mashindano ya bendi yenye ukubwa ule. Mashindano haya yaliyotayarishwa kwa ushirikiano wa CHAMUDATA, Radio Tanzania na Umoja wa Vijana wa CCM, yalianza tarehe 29 Julai 1989 na kufikia kilele tarehe 25 November 1989. Bendi zilizoshiriki zilikuwa 50 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Arusha , Kilimanjaro, Tanga, Iringa,  Mbeya,  Morogoro, Rukwa , Kigoma na Pwani. Hii ilikuwa maendeleo kwani Top Ten Show ya mwaka 1988 ilikuwa na bendi 27 tu. Wafanyakazi wa Radio Tanzania Dar es Salaam  walizunguka katika mikoa mbalimbali na bendi za huko zilifanya maonyesho ambayo yaliyorushwa ‘live’  redioni na hivyo kuwapa wasikilizaji nchi nzima nafasi ya kusikiliza na kufuatilia mashindano hayo katika hatua zote.  Mwaka huo nilishiriki mashindano haya wakati nikiwa mmoja wa wanamuziki wa bendi ya TANCUT Almasi Orchestra iliyokuwa na masikani yake mjini Iringa.  Masharti ya mashindano tulipewa mapema sana. Kila bendi ilitakiwa ijitayarishe kwa nyimbo tatu, mmoja uwe unaitwa Nakulilia Afrika, wimbo wa pili ulikuwa lazima utokane na wimbo wa tuni ya asili ya kabila mojawapo la Tanzania na wimbo wa tatu uwe wimbo wowote ambao bendi ilipendelea kuupiga. Tulianza kufanya mazoezi makali  ya nyimbo hizo. Marehemu Kasaloo Kyanga na pacha wake Kyanga Songa wakaja na tungo yao ya wimbo Afrika Nakulilia, na mimi nikatoa mchango wa wimbo wa asili ya Kihehe ulioitwa Lung’ulye, kwa pamoja tukaamua kuwa wimbo wetu wa tatu uwe Ngoma za Afrika uliokuwa utunzi wa Kalala Mbwebwe.
Baada ya mazoezi makali tuliamua kufanya onyesho lisilo la kiingilio na kuwakaribisha wapenzi wa muziki wa dansi pale Iringa kuja kutoa maoni yao kuhusu matayarisho yetu hayo.  Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati huo, Mama Mary Chipungahelo alikuwa mgeni rasmi  wa onyesho hilo. Kilichofanyika pale siku ile, kilikuwa si kitu ambacho naona kitawezekana kwa urahisi katika zama hizi. Baada ya kupiga nyimbo zile wapenzi walikaribishwa jukwaani  kuongea ukweli kuhusu nyimbo zile, tuliomba waliotaka kutoa sifa wakae nazo, tulichokuwa nania nacho ni mapungufu katika matayarisho hayo. Hakika kulikuweko maneno makali ambayo sidhani wasanii wengi siku hizi wangekubali kukosolewa vile. Kulikuwa na kukosoa kuanzia mavazi, uchezaji na hata tungo zenyewe. Tungo ya Afrika Nakulilia iliyotungwa na akina Kasaloo ilikataliwa kwani ilionekana ilitokana na wimbo wa Pepe Kalle, hivyo muimbaji Kalala Mbwebwe na mpiga gitaa la solo Kawele Mutimwana wakaleta tungo nyingine ambayo ndio ilikuwa moja ya kete zetu katika mashindano yale.



Baada ya kuvuka kigingi cha wapenzi wetu wa Iringa, tulikuja Dar es Salaam na tulikuwa tumepangiwa katika kituo cha ukumbi wa Silent Inn uliokuwa eneo la Mpakani Dar es Salaam. Katika onyesho hilo, tulikuwa jukwaani pamoja na bendi iliyokuwa ikiitwa Orchestra Linga Linga Stars wakati huo muimbaji wake mahiri alikuwa Karama Regesu ambaye kwa sasa yupo Msondo Music Band. Tancut tukaibuka kuwa katika bendi kumi bora na kuja kushiriki fainali za onyesho lile zilizofanyika uwanja wa Taifa. 
Baadhi ya bendi zilifika kumi bora  zilikuwa, Tancut Almasi, Super Matimila, MK Group, Salna Brothers, Varda Arts, Bima Lee, Kilimanjaro Band na Vijana Jazz Band, hakika Uwanja wa Taifa palipendeza siku ile. Lakini kwangu mimi mambo yalikuwa na utata kidogo kwani siku ya fainali, nilikuwa nimeshamia Vijana Jazz Band, lakini kwa siku hiyo nilirudi bendi yangu ya zamani ya  Tancut Almasi  kwani wakati wa mashindano nilishiriki katika bendi hiyo. Uwanja wa Taifa ulijaa wanamuziki wengi sana, na kwa kuwa bendi zilikuwa na ustaarabu wa kuvaa sare, basi sare za aina mbalimbali zilitawala siku hiyo.

Ushindi wa TANCUT

 Hatimae matokeo yalitangazwa na kila wimbo ulikuwa na mshindi wa kwanza mpaka wa kumi, washindi watatu wa kwanza wakipata zawadi mbalimbali. Wimbo wangu wa asili ya Kihehe, ulishinda zawadi ya kwanza katika nyimbo za kiasili na washiriki wote tulipewa ‘radio cassette’ zilizotolewa na Ubalozi wa Uholanzi. Wimbo Afrika Nakulilia ulishika nafasi ya pili na wimbo uliokuwa chaguo la bendi ulikuwa Ngoma za Kwetu uliokuwa utunzi wa Kalala Mbwebwe ulichukua nafasi ya nne katika kundi lake, Kwa ujumla matokeo yalikuwa mazuri sana kwa bendi ya TANCUT Almasi.
Wanamuziki na viongozi wa TANCUT ALMASI Orchestra wakiwa na zawadi zao


 Art Critic

Katika nchi ambazo sanaa imekuwa, huwa kuna watu wanaoitwa ‘art critics’, hawa kwa kweli ni mabingwa katika fani za sanaa wanazo shughulikia na wao kazi yao moja kubwa ni kukosoa kazi mbalimbali za sanaa na hatimae hata kuzipa grade. Kwa mtizamo wa haraka haraka utaweza kudhani kuwa kukosoa kwao kunaweza kuharibu soko la sanaa husika, lakini kwa kuwa hawa watu huwa wakweli na wenye uzoefu, wasanii huwa wanafuatia sana watu hawa wanasemaje kuhusu kazi zao. Kupasishwa na watu hawa hupandisha thamani ya sanaa husika. Wakosoaji hawa pia huwafanya wasanii wawe makini katika kazi zao na hivyo ubora wa sanaa nzima unapanda.  Kitendo cha bendi ya TANCUT kuruhusu kukosolewa kabla ya kuingia katika mashindano ilikuwa sababu moja wapo ya bendi kupata ushindi mnono katika mashindano yale. Wasanii wa sasa hapa nchini wako tayari kukosolewa?

1 comment:

  1. Dah hiyo Linga linga stars naikumbuka sana maskani yake ilikuwa Tandika Devis corner mazoezi yao wanafanya kwenye ofisi ya CCM uwani mpiga Solo wao alikuwa mtu mmoja tunamuita Maulidi Sharia kwa sasa ni marehem baadae akawa mpiga bass msondo

    ReplyDelete