|
Ma soul brothers wakiwa kwenye party |
KWA wengi waliokuwa wakisoma sekondari miaka ya 60 na 70, moja ya siku zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu ilikuwa siku ya ‘Social Evening’. Siku hii ilikuwa ndio siku ambayo wanafunzi walipata nafasi kusakata dansi na kupata marafiki wapya, na mara nyingine hata kuachwa na marafiki wa zamani. Mara nyingi dansi hili liliambatana na kualika wanafunzi kutoka shule nyingine za jirani. Na kawaida ilikuwa shule ya wavulana kualika wanafunzi kutoka shule ya wasichana na shule ya wasichana kualika wanafunzi kutoka shule ya wavulana. Matayarisho yalikuwa yanaanza mapema kwa waalikaji kuandika barua kwa Mwalimu Mkuu au mwalimu wa ‘Social’ wa shule wanayotaka kuialika. Baada ya hapo kazi kubwa ni kukusanya michango kutoka kwa wanafunzi wanaotaka kushiriki siku hiyo. Michango hii kazi yake ilikuwa kununua viburudisho kwa wageni; soda, biskuti au hata maandazi, na pia kununua betri za ‘player’ ya kupigia muziki. Umeme ulikuwa nadra kwenye shule nyingi. Kamati ya starehe ilikuwa ‘busy’ kutafuta santuri mpya, kwa kuazima popote pale, na kama kuna mwalimu ana record player ilikuwa jambo la heri sana. Ukumbi ulipigwa deki vizuri ili wageni wakifika wasije wakawadharau. Hatimae siku huwadia, social evening mara nyingi zilikuwa Jumamosi kuanzia saa nane mchana na kuisha kati ya saa moja mpaka mbili usiku. Wageni hukaribishwa na burudani huanza. Baada ya hotuba na kugawa vinywaji, wenyeji huleta burudani kama vile kucheza jiving, baada ya hapo ‘Dada mkuu’ au mwenyekiti wa kamati ya social wa shule moja hufungua dansi na mwenzie kaka mkuu au mwenyekiti wa kamati ya social wa upande wa pili. Na ndipo wengine mnajitosa kusaka mapatna. Kawaida ya miaka hiyo mwanaume unamfuata msichana kisha unainama kidogo kumuomba ucheze nae, anaweza akakubali au kukataa. Katika shughuli hizi waalimu wa kuangalia nidhamu walikuwa wakishiriki kuangalia kuwa maadili yanafuatwa. Wakati mnacheza mwalimu anapitapita kuangalia kama ‘hamsogeleani ‘ sana. Kama nilivyosema hapo juu, muziki ulitoka kwenye record player ambayo ilikuwa na spika moja ndogo hivyo haikuwa na sauti kubwa. Ukiona ukubwa wa maspika siku hizi, unabaki kushangaa, tuliwezaje wanafunzi 200 hadi 300 kucheza muziki na kuusikia vizuri kwa kutumia spika moja ya player yenye betri 6. Spika ambayo ili itoe bezi ililazimika kuwekwa juu ya pipa. Kulikuwa na nidhamu kubwa sana katika uchezaji, kulikuwa hakuna kupiga kelele, unasikia viatu tu vikisaga chini kwa kufuata mdundo wa muziki. Swala la kuwa pombe haikuhusika katika burudani hizi ni moja ya sababu ya kuwezekana kwa nidhamu hii. Mazungumzo yalikuwa ya chini chini mara nyingi yakihusu masomo.
Katika miaka ya 60 santuri za nyimbo kutoka Congo ndizo zilikuwa maarufu, magwiji wa muziki kama akina Franco, Johhny Bokelo, Dr Nico, Bavon Marie Marie na bendi zao maarufu, Ok Jazz, Negro Success, Co Bantuo, Bantou de La Capital, na miaka ya 70 kukatawaliwa na bendi zilizokuwa zikipiga mtindo wa Cavacha, Lipua Lipua, Kiam, Veve, Kamale na nyingine nyingi. Muziki wa soul ulikuwa na mabingwa wake akina Otis Redding, James Brown, Clarence Carter, Wilson Pickett na wengine wengi.
Kutoka Marekani wanamuziki wa muziki wa country kama Skeeter Davis, Jim Reeves, Connie Francis ndio walitawala social evenings.Wimbo wa Isaac Hayes wa Do your thing maana ulikuwa wimbo wa taratibu ambao ulikuwa mrefu, hivyo kila mtu alikuwa akimkimbilia mtu wake mara tu ukiaanza wimbo huo, maana ndio wimbo wa kukumbatyia kwa muda mreeffuuuuuu, ulikuwa na urefu wa dakika 19.
Wavulana kwa wasichana walishiriki kuandika maneno ya nyimbo hizo kwenye madaftari yao na kubadilishana madaftari. Nyimbo maarufu katika madaftari ya wavulana zilikuwa ni nyimbo za Kikongo. Tambola na Mokili wa Johhny Bokelo na Conga Success na Bougie ya Motema wa Dr Nico na African Fiesta zilikuwa hazikosekana kwenye madaftari ya wavulana, wakati akina dada walipendelea sana kuandika maneno ya nyimbo za Skeeter Davis na Dark City Sisters kutoka Afrika ya Kusini. Kama nilivyosema hapo juu, umeme tu ulikuwa tatizo kweye shule nyingi, hivyo swala la kuwaona na kuwajua wanamuziki waliokuwa wakiporomosha muziki huo lilikuwa nadra sana. Magazeti yalikuwa machache, vyombo ambavyo siku hizi vinaonekana ni kawaida kabisa kama radio na TV navyo vilikuwa nadra sana. Lakini kwa njia ya ajabu vijana walikuwa wanajua namna ya kucheza staili za muziki mbalimbali!! Chacha, pachanga, charanga, baadae soul, bumping na kadhalika. Kwenye shule mbalimbali kulikuwa na wanafunzi ambao walikuwa wanapata bahati kuwa na ndugu au marafiki ambao walikuwa wakibahatisha kuwafundisha uchezaji mbalimbali wakati wa likizo, basi mwanafunzi wa aina hiyo anakuwa maarufu sana mara arudipo shule akiwa na staili mpya ya uchezaji, watu wote wanaanza kumuiga uchezaji ili kujitayarisha kwa social evening. Ilikuwa si ajabu ukija na staili mpya ukapata hata mpenzi mpya.
No comments:
Post a Comment