Sunday, July 10, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 2

 


Wiki iliyopita safari yetu ilitupitisha Singida enzi Mzee Mose Nnauye alipokuwa Mkuu wa mkoa huo na mchango wake katika kuanzisha bendi maarufu ya mji wa Singida iliyoitwa Ujamaa Jazz band. Leo tuingie Dodoma, mji huu mkongwe ulio katikati ya nchi yetu na tuzikumbuke baadhi ya bendi za mji huo na vituko vya kukumbukwa vilivyowahi kutokea katika enzi za uhai wa bendi hizo.
Tuanze na bendi iliyoitwa Jolly Sextet Band. Bendi hii ilianzishwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa Shirika la posta la Afrika ya Mashariki, wakati huo likijulikana kama East African Posts and Telecommunications Corporation. Mkenya huyu alikuja na vyombo vyake vya muziki na kati ya watu walikuja kuwa maarufu waliotokea bendi hiyo ni mpiga saksafoni maarufu Mnenge Ramadhani. Mnenge alijiunga na bendi hii akitokea bendi nyingine ya Dodoma iliyoitwa Central Jazz Band. Mnenge hatimae alitoka Jolly Sextet Band na kujiunga na NUTA Jazz Band alikopata umaarufu kwa upigaji wa saksafon.
 Mwaka 1948 Uingereza iliigawa nchi katika majimbo ya kiutawala manane, Dodoma ikawa katika jimbo lililoitwa Central Province, na pia Dodoma iko katikati ya nchi hivyo basi wanamuziki kadhaa walianzisha bendi iliyoitwa Central Jazz band. Hii bendi ilitoa wanamuziki wengi sana waliokuja kutikisa anga za muziki Tanzania, wakiwemo akina Mnenge Ramadhani, Juma Ubao, maarufu kwa jina King Makusa, Patrick Balisdya, Ally Rahmani huyu alikuwa mpiga gitaa mahiri, enzi za STC  wote ni mazao ya Central Jazz

Mfanya biashara mmoja, Mohamed Omar Badwel, aliyekuwa na gereji na studio ya kupiga picha alinunua vyombo na kuanzisha bendi iliyokuja kuitwa Dodoma Jazz Band. Bendi hii ilikuwa na wanamuziki wazuri sana na ilitoa nyimbo zilizokuja kufahamika nchi nzima, wimbo wao uliokuwa maarufu sana miaka ya sitini ulikuwa Zaina Njoo.
Mmoja kati ya wapiga solo wa kwanza wa bendi hii alikuwa Hassan Mursali kwa asili alikuwa Mnyasa, huyu pia alikuwa anakitwa Hassan Kiziwi kwani pamoja na kuwa mahiri katika upigaji wa gitaa la solo alikuwa na tatizo la kusikia vizuri. Hassan aliwahi kujiunga na Kilwa Jazz band na wimbo ambao alipiga gitaa la solo ni ule  wenye maneno  Dunia Njema kukaa wawili. Hatimae alikuja kuacha muziki na kuwa fundi saa.
Dodoma Jazz Band ilikuwa ikisafiri sana katika kila wilaya nchi nzima, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilikuwa na lengo la kwenda kumchukua mpiga solo wa bendi ya Kilosa Jazz Band, si mwingine ila ni Abel Balthazar. Bendi ilifanikiwa kumchukua Abel na kurudi nae Dodoma. Siku chache baadae wazee waliotumwa na uongozi wa  Kilosa Jazz Band walifika kwa kiongozi wa Dodoma Jazz wakiwa na barua na kumuomba aifungue na kuisoma mbele yao kabla hawajaondoka. Ndani ya barua ile kulikuwa na maagizo kuwa Abel asiporudi Kilosa, basi kuna mwanamuziki mmoja wa Dodoma Jazz band atafariki. Pamoja na Abel kuwa keshashonewa suti mpya ya sare na Dodoma Jazz alirudishwa Kilosa mara moja kuepusha janga.
Mwanamuziki mwengine aliyewahi kupitia Dodoma Jazz Band ni Rashid Hanzuruni, mpiga gitaa marufu ambaye moja kati ya nyimbo zake alizopiga solo ambazo ni maarufu mpaka leo ni ule wimbo wa Kilwa Jazz Band ambao wengi wanaujua kama Lau Nafasi. Hanzuruni alijikuta katika bendi hii akiwa safarini akitokea Tabora ambako alikuwa amekorofishana na wanamuziki wenzie wa Tabora Jazz Band, alikuwa akielekea Dar es Salaam kujiunga na NUTA Jazz band, lakini akakatishwa safari hiyo na meneja wa Dodoma Jazz Band aliyemshawishi ajiunge na Dodoma Jazz Band. Hanzuruni hakukaa sana Dodoma, akaondoka na kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya ndoto yake ya kujiunga na NUTA Jazz Band, hata hivyo ndoto hiyo haikutimia kwani wakati huo NUTA Jazz Band ilikuwa na mpiga solo mahiri sana aliyeitwa Hamisi Franco, Hanzuruni akaishia kujiunga na Western Jazz Band.

Central Jazz band ilikuja kuwa chanzo cha Afro70 Band ya Patrick Balisdya, kwani ndiko Patrick na wenzie walikopata vyombo vya kwanza vya kuanzishia bendi yao hiyo maarufu.

Dodoma International Orchestra 1978


Bendi nyingine maarufu iliyowahi kuweko Dodoma ni Dodoma International Orchestra, hii ilikuwa mali ya Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa wa Dodoma. Dodoma International kwa kipindi ilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki mkongwe mpuliza saksafon Sheddy Mbotoni. Dodoma International Orchestra ilipitisha wanamuziki wengi sana waliokuja kuwa maarufu katika anga za muziki nchini, waimbaji kama Shaaban Dede, Ahamadi Sululu, Athumani Soso, Saburi Athumani, wapiga magitaa akina Charles Kasembe, Kassim Rashidi, Mohamed Ikunji, na wanamuziki wengine wengi maarufu wote walipitia bendi hii mahiri. Dodoma International ilijitambulisha kwa mitindo kadha wa kadha kama ‘perekete’, mafuriko ya jasho’, ‘zunguluke’ na mingineyo mingi iliyobadilika kutokana na wanamuziki kubadilika katika kuingia na kutoka. Bendi nyingine ya Dodoma ilikuwa ni mali ya fundi redio maarufu Mzee Alphonse Materu, na bendi aliipa jina lake ikaitwa Materu Stars. Materu Stars nayo ilipitisha wanamuziki wengi sana akiwemo aliyekuwa kiongozi wa bendi maarufu ya Butiama Jazz Band, mzee Alphonce Makelo, ambaye kwa sasa maepoteza uwezo wake wa kuona. Bendi nyingine iliyokuwa Dodoma na kupewa jina la mwenye bendi ni bendi ambayo bado ipo hai na  inaitwa Saki Stars. Saki lilikuwa ni kifupi cha  jina Salome Kiwaya, mwanamuziki wa kike aliyeiongoza bendi yake mpaka umauti wake uliotokana na ajali ya gari. Wiki ijayo tutaendelea na safari yetu ya bendi za Tanzania.

 

 

No comments:

Post a Comment