Friday, August 5, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU ARUSHA NA MOSHI

 

The Ambassador Band ya AICC

Safari ya kuzikumbuka bendi zetu leo inatufikisha miji ya kaskazini mwa nchi yetu. Jiji la Moshi na jiji la Arusha. 
Tuanze na jiji la Moshi, hakika  ukisikiliza hadithi mtaani za siku hizi unaweza ukadhani Moshi si mji wa kuwepo katika historia ya muziki, lakini kinyume kabisa, huwezi kuongelea historia ya muziki Tanzania bila kutaja Moshi. Kwanza kuna mchango mkubwa wa wanamuziki waliotoka Moshi, na pili kati ya wawekezaji wakubwa katika muziki waliowahi kutokea Tanzania, waliotoka Moshi.
Taja bendi karibu zote zilizokuwa kubwa miaka ya sitini na sabini utaukuta mkono wa muwekezaji toka Moshi.
Wanamuziki wa Moshi walianza kuiweka Tanzania katika ramani ya muziki wa Afrika ya Mashariki kuanzia miaka ya 50. Mabingwa kama Frank Humplick na Dada zake, ambao walikuwa watoto wa  baba muhandisi kutoka Austria na mama Mchaga,  Dr Hosea Macha na mke wake, Dr Hosea alikuwa baba mzazi wa mwandishi na msanii maarufu Freddy Macha,  Kimambo Brothers na wengine wengi waliweza kurekodi nyimbo zao kwa mtindo ule wa kutumia gitaa kavu, yaani gitaa lisilotumia umeme. Frank Humplick alirekodi nyimbo nyingi na wasanii wa Kenya chini ya lebo ya Jambo, ukiwemo wimbo maarufu Mi Francois mi naimba,ambao alifanya ‘kolabo’ na mwanamuziki kutoka Kongo Edward Mazengo, mambo yote hayo kabla ya Uhuru.
Baadhi ya bendi nyingine  zilizokuweko Moshi ni Ringo Jazz, halafu kulikuweko na Black Beatles, hawa walikuwa wakivaa kama wale wanamuziki wa Beatles wa Uingereza, walikuwa na gari lao la Combi ambalo waliliandika maandishi makubwa Black Beatles.  Moshi pia ilikuweko bendi maarufu ya Zaire Success, hii ilikuwa bendi ya vijana wa Kikongo. Kulikuwa na hadithi zamani ikisema hawa walikuwa ni kundi lililovunjika kutoka kutoka kwa kundi la Orchestra Fauvette la akina King Kiki na Ndala Kasheba Supreme, hata lile kundi la bendi ya Wakongo la Mwanza lilioitwa Orchestra Super Veya nayo husemekana ilitokana na mpasuko wa Orchestre Fauvette.
Mara ya mwisho kuingia muziki wa Zaire Success ilikuwa mwaka 1974 walipopiga community center Same, siku ilipofunguliwa Benki ya kwanza mji huo. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bwana Peter Kisumo. Mimi na rafiki zangu tulizuiliwa kuingia kwa kuwa kulikuwa na mgambo mlangoni kazi yake ilikuwa kuangalia waliovaa nguo zisizofaa,  tulikuwa tumevaa suruali zetu zilizokuwa pana chini, maarufu kwa jina la bugaluu. Ikalazimu kwenda kubadili ili kuweza kuingia dansi lile.  Nigusie hapa kuwa kuwa Same pia kulikuwa na bendi iliyoitwa TANU Youth League Jazz Band, kuna Askofu maarufu alikuwa mwanamuziki wa bendi hiyo miaka hiyo ya 70.

Chuo cha Polisi cha Moshi maarufu kwama Police Training School, PTS, kwa miaka mingi ilikuwa na bendi moja nzuri iliyokuwa ikitumbuiza mjini Moshi mara kwa mara. Moshi pia kulikuwa na bendi iliyokuwa inaitwa Bana Afrika Kituli, awali ilikuwa bendi kubwa ikaapoteza umaarufu mpaka ikawa inapiga kwenye vilabu vya mbege. Mmoja wa wanamuziki wa bendi hii niliwahi kumkuta Tanga akiwa amebadili taaluma na kuwa mganga wa kienyeji. Ni jambo la ajabu kidogo lakini kuna wanamuziki wengi sana ambao walikuja kuacha muziki na mkuwa waganga wa kienyeji.
Shule ya sekondari ya Old Moshi na hata Shule ya Ufundi ya Moshi ( Moshi Tech), zote zilikuwa na bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki kwa umahiri wa hali ya juu. Bendi ya shule ya Old Moshi walijiita Orchestra Mosesco. Baadhi ya wanamuziki wa bendi hii walikuwa Joseph Mkwawa, Pelegrin, Mwakibete, Tamba, Kufakunoga  na kadhalika.
Tuhamie Arusha, mji ambao katika miaka ya mwanzo ya sabini ulikuwa umechangamka sana kutokana na kuwa na wafanyakazi wengi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, halafu ukijumlisha na  biashara ya utalii, hakika mji ulikuwa na burudani nyingi. Hoteli za kitalii zilizokuwa chini ya Shirika la utalii Tanzania, karibu zote zilikuwa zikishindana kuwa na bendi bora hotelini, bendi kama The Revolutions, ambayo baade iliitwa Kilimanjaro Band, The Bar Keys ambayo ikaja kuitwa Tanzanites ni baadhi ya bendi ambazo zilitamba sana kwenye mahoteli ya Arusha. Bendi chache nyingine zilizokuwa zikipiga mahotelini ni Juju Masai ya akina Sabuni, hawa walikuwa ndugu waliokuwa mahiri sana katika muziki,  Crimson Rage, Ambassadors akina Andy Swebe na Likisi matola (wanaoonekana pichani), Tonics ya David Marama  na kadhalika.

Kwenye uwanja wa muziki wa Rumba kulikuwa na bendi kama Orchestra National, bendi ambayo ndio aliyoanzia muimbaji mahiri sana Hassan Bitchuka kabla ya kuonekana na NUTA Jazz Band. Kulikuwana Arusha Jazz Band, bendi iliyokuwa ya akina Wilson Peter na wenzie baada ya kuihama Jamhuri Jazz Band ya Tanga. Arusha Jazz Band ilihamia Mombasa na ndipo ikabadili jina na kujiita Simba wa Nyika, umaarufu wa bendi hiyo unafahamika kwa wapenzi wote wa muziki wa zamani. Arusha pia kulikuwa na bendi ya Chuo Cha Jeshi Monduli, bendi iliyoitwa Les Mwenge, bendi iliyokuja kupata umaarufu mkubwa kutokana na album ya wimbo Kila munu ave na kwao wa Halila Tongolanga.

Ukurugenzi wa Mkoa wa Arusha  ulianzisha bendi, nadhani ulikuwa ukurugenzi wa kwanza kufanya hivyo baadae mikoa mingine ikafuatisha. Bendi hiyo  iliundwa na  wanamuziki wa bendi ya Orchestra Lombelombe, bendi iliyokuwa ni matokeo ya mpasuko wa Morogoro Jazz band. Bendi hiyo mpya ikaitwa Kurugenzi Arusha. Kurugenzi Arusha ilitunga nyimbo kadhaa zilizotikisa anga ya muziki nchini, nyimbo  kama vile Wivu na Ujamaa mpaka leo bado zina wapenzi lukuki. Mwisho huwezi kuongelea bendi za Arusha bila kuitaja  Serengeti Band, bendi iliyoanzishwa na mmoja ya wanamuziki wa Orchestra Mkwawa iliyokuwa bendi ya shule ya Mkwawa, mwandishi mkongwe Danford Mpumilwa, hakika bendi hii nayo ilichangamsha jiji la Arusha.

No comments:

Post a Comment