Kiki ni neno
ambalo limekuwa maarufu zama hizi za Bongofleva. Kiki ni neno lilitokana na
neno la Kiingereza, ‘kick’ yaani teke. Hivyo kiki maana yake katika ulimwengu
wa wasanii ni kutafuta tukio ambalo litashtua jamii na kupaisha sifa yao au ya
kazi yao. Ni kama vile ambavyo ukimpiga teke chura ndio unamsaidia kuruka.
Hivyo wasanii wa zama hizi hutafuta kiki za aina mbalimbali ili kupaisha sifa
za kazi zao, wengine hujitangaza kuwa wamefariki, wengine utakasikia
wamefumaniwa, au wengine wameachana au wengine kutangaza wamerudiana au
wameoana, au mara nyingine kueneza taarifa kuwa wimbo wao umeibiwa studio, na imefikia
hata wazazi wa wasanii wengine kuingia kikamilifu katika shughuli za kiki kwa
kutoa matamshi tata kuhusu kazi za watoto wao ili tu watu waelekeze masikio na
macho yao kwenye kazi mpya. Pamoja na neno kiki kuwa jipya lakini hakika
kutafuta kiki hakukuanza na Bongofleva. Makampuni yenye kutaka kutangaza bidhaa
mpya sokoni, yamekuwa yakifanya matukio mengi makubwa kutafuta kiki. Makampuni
hupitisha magari yenye maspika makubwa mitaani na kutangaza bidhaa zao, au
hufanya matamasha makubwa, au huanzisha hata misemo tata ili tu kupata kiki ya
bidhaa zao. Lakini hapa haiitwi kiki inaitwa promosheni. Wanasiasa nao hakika
ni mabingwa wa kiki,wakati wa kutafuta kura, kila aina ya vituko hufanyika.
Tumeshaona wanasiasa wanapiga magoti kuomba kura, wengine hata kugaragara chini
wakiomba kura, hao wanaoamua kucheza ngoma za kiasili au dansi jukwaani ni
kawaida sana. Na wakifungua mdomo
kueleza sifa walizonazo na watakachokifanya vyote ni kujinadi ili kuonekana
bora, ila huku haiitwi kiki inaitwa siasa, au wengine huiita propaganda. Zama
hizi hata viongozi wa dini nao wamo katika kutafuta kiki, utasikia wakishusha
sifa za uwezo wao kama katika vyombo mbalimbali vya matangazo, wengine
wamefikia mpaka kuingilia matatizo ya wasanii maarufu ili nao wajulikane kuwa
wapo. Kutokana na malezi duni ya baadhi ya wasanii, kiki hizi zimekuwa
zikichukua sura mpya siku hadi siku. Kwa sasa zimefikia hata kuongea, kutangaza
au kuonyesha vitu vya faragha hadharani, ikiwa kama njia ya kutafuta kiki, na
hapo ndipo ugomvi na watu wenye busara zao unapoanza.
Kama
nilivyosema mwanzo neno kiki ni geni lakini shughuli zake si ngeni kabisa.
Bendi za zamani zilikuwa na njia kuu moja tu ya kupata pesa nayo ilikuwa
kwa kiingilio mlangoni, gate collection,
na hakika kulilazimika kuweko na mbinu za kujitangaza, au kutafuta kiki.
Kulikuwa na njia kuu tatu za kutangaza onyesho, kwanza ni kupitia redioni na pili kupitia
magazeti, na tatu kwa kubandika matangazo kwenye kuta na nguzo za umeme. Magazeti
yaliyokuwa yakishughulika na muziki yalikuwa ni magazeti ya serikali, magazeti
ya Chama Cha Mapinduzi na magazeti ya chama cha wafanyakazi, NUTA na baadae
JUWATA. Vyombo hivi havikuwa na maadili
ya kuruhusu ‘kiki’ za maisha binafsi ya wanamuziki, matangazo yalilazimika kuwa
yanayohusu muziki tu. Hivyo ubunifu
ulikuweko, bendi zilijinadi kwa staili zake zenye mvuto ili kutafuta kiki.
Kulikuweko staili kama Katakata mwendo
wa jongoo vumbi nyuma, Bomoa tutajenga kesho, Super mnyanyuo, Sikinde ngoma ya
ukae, Mahepe ngoma ya wajanja, Dunda dunda, Bayankata, Kokakoka balaa na majina mengine mengi. Matangazo kwenye
magazeti yaliwekwa picha za wanamuziki au kuchorwa picha za kujinadi kwa njia
moja au nyingine. Maswala ya kuachana, kupendana, kuhongana, kufumaniana
hayakuhusika kabisa katika kutangaza kazi ya muziki. Nikifikiria sana nadhani
vitu ambavyo wasanii wa sasa hufanya katika kutafuta kiki, vingefanywa na
wasanii wa miaka ile na kutangazwa kama ilivyo sasa ingekuwa ndio mwisho wa
msanii huyo, jamii ingemtema.
Nadhani moja
ya sababu ya kuweko kwa kiki za ajabu katika zama hizi, ni kujaribu kujazia
mapungufu yaliyomo kwenye sanaa husika. Msanii anakuwa anajua hata yeye kuwa
kazi yake ni duni, hivyo anazua kitu
kisichohusika kabisa na kazi yake ya sanaa ili kuweza kuwafanya wateja japo
wasikilize kazi yake kwa muda.
Taratibu za
kurekodi siku hizi nazo zinafanya msanii asiwe na uhakika wa mpokeo ya wimbo
wake hivyo kulazimisha vituko ili kujulikana kama ana kazi mpya. Msanii wa
kizazi cha sasa anaweza kutunga wimbo asubuhi akaingia studio na kukamilisha
wimbo na jioni wimbo uko tayari youtube na umeanza kurushwa kwenye vyombo ya
utangazaji mbalimbali,
Hali haikuwa
hivyo zamani, ukiwa na wazo la wimbo unalipeleka kwenye bendi yako yenye watu
zaidi ya saba, wao wanakusikiliza na kuamua kama uchukuliwe na bendi au la,
wakikubali ndipo mnaanza kuujenga wimbo, magitaa, ngoma. vyombo vya upulizaji,
kila mtu anatoa wazo lake. Wimbo ulichukua japo siku mbili kukamilika, ingawa
kuna nyimbo zilichukua hata zaidi ya wiki kuwa tayari. Bendi ikiridhika , wimbo
ulianza kupigwa kwenye maonyesho, na hapa ndipo wapenzi wa bendi walikuwa
wakiingia na kutoa maoni yao, mkikubaliana ndipo unaenda kurekodiwa. Mara
nyingi bendi zilikuwa zinajua kabla hata ya kwenda kurekodi wimbo gani utakuwa
maarufu kutokana na maoni ya wapenzi. Kwa taratibu hizo kiki za kujidhalilisha
zilikuwa hazina nafasi, kazi ilikuwa inajiuza yenyewe.