Msondo wakiwa mazoezini katika ukumbi wa Amana |
Moshi William alizaliwa mwaka 1958 Hale Mwakinyumbi Korogwe. Hale alikuwepo mwanamuziki maarufu aliyekuwa akiitwa Mzee Masongi, yeye alikuwa na bendi, na bendi hii ilikuwa chanzo cha wanamuziki wengi maarufu akiwemo Moshi William. Jina halisi la Moshi William lilikuwa Shaaban Ally Mhoja lakini alikuja kubadili na kuitwa Moshi William kutokana na kuja kulelewa na baba mwingine. Bendi ambazo TX Moshi William aliwahi kupitia baada ya kutoka Hale zilikuwa ni Safari Trippers wana Sokomoko, UDA Jazz Band wana Bayankata, na Polisi Jazz Band wana Vangavanga, na hatimae JUWATA Jazz Band wana Msondo Ngoma, bendi aliyodumu nayo mpaka kifo. Kati ya nyimbo zake za kwanza mara baada ya kujiunga na JUWATA zilikuwa Ajuza, Ashibaye na Asha Mwanaseif, wimbo huu wa tatu alimtungia mkewe, baada ya hapo alitunga nyimbo nyingi sana na kwa ujumla alirekodi album karibu 13. Sifa ya Moshi kuanza kuitwa TX ilitungwa na marehemu Julius Nyaisanga aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam. Zama hizo, serikali ilikuwa imeweka sheria kuwa magari ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi nchini yawekwe namba ambazo zilianzia na TX kuonyesha ni ya Kimataifa, hivyo TX ikageuka kuwa nembo ya sifa ya kuwa na hadhi ya Kimataifa. Kutokana na umahiri wa Moshi katika kutunga na kuimba, Nyaisanga akampachika kisifa cha TX. Na hakika umahiri wake ulijidhihirisha kwani kwa miaka mitatu mfululizo kati ya mwaka 2003 mpaka 2005, TX Moshi William alitunukiwa tuzo za utunzi bora na Kilimanjaro Music Awards. Pamoja na Msondo, Moshi aliwahi kurekodi nyimbo nyingi akiwa na wanamuziki wenzake nje ya Msondo, kwa utaratibu ulikuwa maarufu kwa jina la zing zong au wengine waliita zozing. Moshi alifariki siku ya tarehe 29 March 2006 katika wodi ya Sewa Haji baada ya operesheni ya kuondoa chuma katika mguu wake uliovunjika kwenye ajali. Alifariki saa tatu kasoro robo asubuhi na kuzikwa siku hiyohiyo katika makaburi ya Keko Machungwa.
Mungu Amlaze Pema Shaaban Ally Mhoja Kishiwa - TX Moshi William
No comments:
Post a Comment