Thursday, July 14, 2022

ZAMANI WATU WALIENDA DANSINI WAKAKUTA POMBE, SIKU HIZI WANAENDA KWENYE POMBE WANAKUTA DANSI

 

Kumbukumbu zangu huwa zinanirudisha Iringa nilipokuwa na umri wa miaka sita au saba hivi. Nadhani ndipo nilipoanza kutambua kuwa watu huwa wanaenda dansini. Maana mara kwa mara wazazi wangu walikuwa wanajitayarisha wanavaa nguo nzuri halafu wanatuaga ‘Haya laleni sisi tunaenda dansini’.
Moja ya dansi nakumbuka lilikuwa limepigwa na Cuban Marimba wakiongozwa na Salum Abdallah, nakumbuka kwa sababu kesho yake Mwalimu Nyerere alikuja kuhutubia watu wa Iringa kwenye uwanja ambapo upo sasa ni uwanja wa Samora. Wakati huo ulikuwa ni uwanja wa mpira wa shule ya Mshindo Middle School, na baba yangu alikuwa Headmaster wa shule ile. Nyumba yetu ilikuwa pembeni tu ya uwanja huo wa mpira. Siku hiyo alipokuja kuhutubia Mwalimu Nyerere, wimbo uliokuwa ukisikika kwenye spika ukirudia rudia, ulikuwa wimbo wa Cuban Marimba na baadhi ya  maneno yake yalikuwa ‘ Tutie jembe mpini, twendeni tukalime’, lazima ilikuwa baada ya Uhuru maana ndio nyimbo baada ya Uhuru zilivyokuwa na ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujenga nchi mkoloni kisha ondoka.
 Wakati wimbo huo ukiimba, mama yangu akatuambia na wadogo zangu kuwa wimbo huo walikuwa wameucheza jana yake dansini. 

Kwa kweli toka nikiwa mtoto, dansi kwangu ni neno la furaha  kwenye maisha yangu. Nikiwa mdogo  wazazi wangu walikuwa wakituonyesha namna ya kucheza aina mbalimbali za dansi, zikiwemo tap dancing, aina ya dansi ambayo visigino vya viatu lazima uvigonge kwa nguvu sakafuni wakati wa kucheza kufuatia mapigo ya muziki, hivyo basi vinatoa beat fulani kufuatana na wimbo, dansi moja ngumu kuicheza maana inachosha baada ya dakika moja tu. Tulifundishwa kucheza  chachacha, waltz, foxtrot na aina nyingine za dansi ambazo sijapata hata  kujua majina yake.

Nyakati hizo na miaka mingi baadae, mtu akiaga anakwenda dansini, jambo la muhimu atakalolifanya huko ni kucheza nyimbo nyingi kadri atavyoweza. Kesho yake mazungumzo kuhusu dansini ni kuulizana nyimbo ngapi zilichezesha. Mpenzi wa muziki kurudi nyumbani akiwa kachoka kwa kucheza ilikuwa ndio dalili ya kufurahia kwa usiku ule.

Miaka mingi baadae hatimae nikaja kuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi.  Hii aina ya muziki  uliokuja kuitwa muziki wa dansi, ulipewa jina hili kuanzia mwaka 1986 baada ya mkutano mkubwa wa wanamuziki ulioitishwa na Baraza la Muziki Tanzania kuja na wazo la kuwa na vyama vya muziki, ili kutofautisha na muziki wa Taarab, ndipo kikaundwa Chama cha Muziki wa Dansi na dhana ya muziki wa bendi ambao nia yake ilikuwa kucheza ukaitwa 'muziki wa dansi'.

Muziki wa bendi ambao sasa unaitwa muziki wa dansi, ulitungwa na hatimae kupigwa kwa vifaa vya kisasa na lengo kubwa ni kuwa wapenzi wa muziki huo watacheza.  Katika miaka ya hamsini na mwanzoni mwa miaka ya sitini, bendi zilikuwa zikitangaza aina muziki itakaoupiga, kwa mfano kiongozi wa bendi aliweza kutoa maelezo yafuatayo kabla ya kupiga wimbo. ‘Muziki ufuatao unaitwa Dada Adija, umepigwa katika mtindo wa Cha Cha’. Basi muziki ukianza wapenzi wa muziki wangeingia uwanjani na kucheza ChaCha. Na hivyo hivyo kama wimbo ni Twist, Bolelo, Charanga na kadhalika, hata kucheza kulikuwa na mpangilio unaoeleweka.

Tungo za zamani zilikamilishwa kwa muungano wa mawazo kutoka kwa wanamuziki mbalimbali katika bendi. Mtunzi wa awali aliweza kuleta  mashahiri, mara nyingine yakiambatana na melodia na kuwaimbia wenzie ambao walianza kutunga vipande vyao kupitia  vyombo mbalimbali wanavyovipiga. Tungo nyingi za awali zilianza kwa rumba, na ilipofika katikati mwendo ulibadilika na kuingia katika kile tulichokuwa tukikiita ‘chemka’.
 Chemka mara nyingi ilianza kwa kuimba na kisha kuingia kipande cha gitaa la solo. Hapa ndipo wapiga solo walikuwa wakipimwa kwa umahiri wao wa kutunga na kupiga vipande vya solo ambavyo vingeweza kuwateka akili wasikilizaji na kuwafanya wacheze dansi.



Katika bendi nilizopitia kama vile TANCUT Almasi na Vijana Jazz Band, baada ya bendi kukamilisha kuufanyia mazoezi wimbo, wimbo huo ulianza kupigwa katika maonyesho mbalimbali, lakini jambo la muhimu ambalo wanamuziki wote tulikuwa tukiliangalia lilikuwa ni Je, watu wanaucheza wimbo mpya? Ikionekana wimbo  umekosa hamasa ya kuwasimamisha  wachezaji, wimbo huo ulirudishwa mazoezini na kubadilisha vitu tulivyohisi vinafanya watu wasipende kucheza wimbo ule. Na mara nyingine wimbo huo ulitupwa pembeni moja kwa moja, mamia ya nyimbo  katika bendi mbalimbali ziliishia kupigwa kwenye kumbi mara moja tu na hazikurudiwa tena, kwa kuwa tu watu hawakuchangamkia kuzicheza.
Siku hizi mambo yako tofauti kabisa, unaweza kuingia kwenye onyesho la muziki wa Taarab, muziki ambao zamani ulikuwa ukisifika kwa kuwa muziki wa kusikiliza tu, ukakuta wapenzi wakitiririka jasho kwa kucheza nyimbo mbalimbali za Taarab. Na ukaingia katika onyesho la ‘muziki wa dansi’, ukakuta waimbaji wakitoka mishipa ya shingo, solo likapigwa kwa ufasaha, vyombo vingine vikachangia lakini hakuna anaeshughulika kucheza dansi hilo. Kama ingekuwa  zamani, hiyo ni dalili ya moja kwa moja kuwa muziki huo hauwafurahishi wapenzi. Lakini hizi ni zama nyingine.

Katika zama hizi, bendi huwa na wacheza show wake au hata waimbaji wa bendi nao wakatengeneza show yao, kisha wakawa wanapiga muziki na kucheza wao wenyewe. Ni kama nilinganishe na msemo maarufu wa  'kujitekenya halafu kucheka mwenyewe'. Wimbo ukiisha  wanamuziki huanza wimbo mwingine bila  kuhisi kuwa kuna tatizo.
Teknolojia imeleta aina nyingine ya kuonyesha upenzi na unazi wa muziki. Wapenzi wa muziki siku hizi huonyesha upenzi wao wa muziki kwa kuchukua simu na kurekodi  bendi ikiimba na kucheza, hawachezi wala kutikisika, kazi yao ni kunyanyua simu na kurekodi. Vipande hivi vya video husambazwa kwenye makundi ya Whatsapp, vikiambatana na sifa kuhusu ubora wa bendi hizi. Ndio namna ya zama hizi kufurahia muziki.
 Hakika kuna nyimbo ambazo wapenzi huchangamkia  kwa kucheza sana, lakini ukiangalia kila mtu anacheza akili inavyomtuma, hakuna tena mpangilio wa kucheza staili maalumu ya muziki. Ile staili ya wapenzi kukumbatiana kwa hisia wakati wa kucheza rumba imepotea, si ajabu kabisa kumkuta mtu anacheza na mpenzi wake, kila mtu na staili yake na wakati huohuo kila mmoja anatuma meseji kwenye simu. kweli zama zimebadilika mno.

Mwisho nimalizie na sentensi ya hali ninayoiona  katika muziki wa dansi, 'ZAMANI WATU WALIKWENDA DANSINI NA KUKUTA POMBE, SIKU HIZI WATU WANAENDA KWENYE POMBE NA KUKUTA DANSI'


 

Tuesday, July 12, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 3

 

SAFARI  yetu ya kuzikumbuka bendi mbalimbali nchini, wiki hii inatuingiza mkoa wa Iringa, lakini kati ya Iringa na Dodoma kuna wilaya inaitwa Mpwapwa. Hapa kulikuwa pia na bendi moja matata sana iliyoitwa  Mpwapwa Jazz Band. Bendi hii haikuwa ndogo kwani iliweza kurekodi nyimbo kadhaa ambazo zilipata umaarufu wa Kitaifa wakati wa uhai wake, ikiwemo wimbo Nilikuwa sina kazi, wimbo ambao unazungumzia hadithi ya kudumu ya kukimbiwa na mpenzi kutokana na kutokuwa na kipato.
Mji wa Iringa ulianza kama  ngome ya Wajerumani walipokuwa katika harakati za kumsaka Mutwa Mkwawa baada ya kuangusha ngome yake kule Kalenga. Hata jina Iringa limetokana na neno la Kihehe 'Lilinga' yaani ngome. Jeshi la Wajerumani likiwa na maafisa wachache wa Kijerumani, lilikuwa  na askari wengi wa Kiafrika kutoka pande mbalimbali za Afrika ya Mashariki na kati. Kulikuwa na askari wa Kinubi, askari wa Kimanyema, askari wa Kizaramo, askari wa Kinyamwezi na makabila mengine kadha wa kadha. Askari hawa wakaanza kuishi na familia zao maeneo yanayojulikana kama Miyomboni, jirani na kituo kikuu cha polisi ambapo haswa ndipo yalikuwa makao makuu ya jeshi la Wajerumani. 
Watoto na wajukuu wa askari hawa  walikuwa wakijitambulisha kuwa wao ndio wenyeji halali wa mji wa Iringa. Hivyo walikuwa na timu ya mpira iliyoitwa Boni kifupi cha Born Town, wakiwa wanamaananisha kuwa wao ndio wazawa haswa wa pale mjini. Na wakati huohuo wakaanzisha pia bendi iliyoitwa Born Jazz band, pengine kati ya bendi za awali za mji huu. Kama  ilivyokuwa Dodoma kuwa na bendi inaitwa Sextet Jazz band, Iringa kulikuwa na bendi inaitwa Habanero Jazz Band. Sextet na Habanero yalikuwa majina ya bendi mbili za huko Cuba. Katika zama hizo bendi za hapa nchini zilikuwa zikiiga muziki kutoka Cuba, si Congo. Bendi ya Iringa iliyokuja kupata umaarufu mkubwa ilikuwa Highland Stars Band. Mpiga gitaa Abel Balthazar ni moja ya wapigaji maarufu waliowahi kupitia bendi hii. Nyumbani kwa  mpiga solo maarufu wa Msondo Ngoma Ridhwani Abdul Pangamawe, ndipo yalipokuwa yakifanyika mazoezi ya Highland Stars Band. Mzee Abdul Pangamawe na mama Ridhwani wote walikuwa wakijua kupiga magitaa, si ajabu kabisa nyumba hiyo kutoa mpiga gitaa  na kinanda mahiri anayetingisha nchi mpaka leo. Moja ya wimbo wao maarufu wa Highland Stars ulikuwa ni Sitasita Mpenzi.

Bendi nyingine mjini Iringa ilikuwa ni Iringa Jazz Band, hii ilikuwa mali ya TANU Youth  League. Miji mingi sana ilikuwa na bendi za TANU Youth League katika miaka ya 60 na 70. 
Mkwawa High School, ambayo awali ilikuwa shule ya ‘Wazungu’ na iliyokuwa ikiitwa St George and St Michael European School, ilikuja kuwa na bendi nzuri sana ya wanafunzi iliyoitwa Orchestra Mkwawa. Wakiwa na mtindo wao waliouita Ligija walitoa burudani kila mwisho wa wiki katika ukumbi wa Welfare Center, katika utaratibu wa madansi ya mchana maarufu kama Buggy, wao kama wanafunzi hawakuwa na ruksa ya kuwa katika kumbi za dansi usiku, hivyo waliweza kupiga muziki huo mchana tu. Pia katika shule hiyo hiyo kulikuwa na bendi nyuingine iliyokuwa ikipiga muziki wa Kizungu na iliitwa Midnight Movers. Marehemu Eddy Hanspoppe, Deo Ishengoma, Martin Mhando walikuwa kati ya wanamuziki wa bendi hii. Vyombo walivyotumia vilikuwa ni vile ambavyo vilikuwa vikitumiwa na bendi iliyokuwa ya TANU Youth League. Magitaa ya bendi hii hatimae yalikuja kuchukuliwa na vijana wachache walioanzisha bendi iliyokuwa ikijulikana kama Chikwalachikwala. Chikwalachikwala ikajigawa na kukapatikana bendi iliyoitwa BOSE Ngoma, jina lililotokana na aina ya speaker walizokuwa nazo.

                                                    Chikwalachikwala Jukwaani Kijiji cha Mgama, 

Mwaka 1987 ikazaliwa Tancut Almasi Orchestra  bendi nyingine kubwa iliyowahi kutokea Iringa, bendi hii ilikuwa mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Diamond Cutting Company kilichokuwa pale Iringa. Majina ya wanamuziki maarufu waliopitia bendi hii ni mengi sana kati hao walikuweko mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Banza Tax, Mafumu Bilali, Kawelee Mutimwana, Shaban Yohana Wanted, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe na wengine wengi akiwemo mwandishi wa makala hii.

TANCUT ALMASI ORCHESTRA JUKWAANI


Bendi nyingine iliyowahi kuweko Iringa  mjini ni Ruaha International Orchestra , iliyokuwa mali ya mfanya biashara mmoja aliyeitwa Mtandi. Bendi hii ilikuwa chini ya uongozi wa muimbaji marehemu Kalala Mbwebwe na wimbo wake Lutadila  ni kumbukumbu kubwa kwa wapenzi wa bendi hii. Bendi nyingine zilizowahi kuwa Iringa, zilikuwa ni VICO Stars iliyokuwa mali ya kanisa Katoliki, Living Light Band iliyokuwa mali ya hoteli ya Living Light.
Kumaliza mkoa huu bila kutaja bendi maarufu ya JKT Mafinga haitakuwa sawa. Bendi hii ilikuwa maarufu kwa jina la Kimulimuli, jina hili lilitokana na taa za disco zilizokuwa zinafungwa wakati bendi hii inapiga. Vyombo maarufu vya muziki aina ya Ranger FBT ambavyo vilikuwa vikitumika na bendi nyingi miaka ya 80 vilikuwa vinakuja na taa za disco, na wenyeji wa Mafinga walikuwa wakisema kwa Kihehe ‘Twibita kukina kimulimuli’ yaani tunaenda kucheza Kimulimuli, na hakika jina hilo ndilo likawa utambulisho wa bendi hiyo,  na hata bendi yenyewe ilitunga nyimbo kusifia jina lao la Kimulimuli.  Kati ya wanamuziki maarufu waliowahi kupitia bendi hii ni Zahiri Ally Zorro na Zakaria Daniel Mabula Tendawema ambaye niliandika alipata jina la Tendawema kutokana na kutunga wimbo ulioitwa Tenda wema nenda zako alipokuwa Shinyanga Jazz band. Safari inaendelea….

Sunday, July 10, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 2

 


Wiki iliyopita safari yetu ilitupitisha Singida enzi Mzee Mose Nnauye alipokuwa Mkuu wa mkoa huo na mchango wake katika kuanzisha bendi maarufu ya mji wa Singida iliyoitwa Ujamaa Jazz band. Leo tuingie Dodoma, mji huu mkongwe ulio katikati ya nchi yetu na tuzikumbuke baadhi ya bendi za mji huo na vituko vya kukumbukwa vilivyowahi kutokea katika enzi za uhai wa bendi hizo.
Tuanze na bendi iliyoitwa Jolly Sextet Band. Bendi hii ilianzishwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa Shirika la posta la Afrika ya Mashariki, wakati huo likijulikana kama East African Posts and Telecommunications Corporation. Mkenya huyu alikuja na vyombo vyake vya muziki na kati ya watu walikuja kuwa maarufu waliotokea bendi hiyo ni mpiga saksafoni maarufu Mnenge Ramadhani. Mnenge alijiunga na bendi hii akitokea bendi nyingine ya Dodoma iliyoitwa Central Jazz Band. Mnenge hatimae alitoka Jolly Sextet Band na kujiunga na NUTA Jazz Band alikopata umaarufu kwa upigaji wa saksafon.
 Mwaka 1948 Uingereza iliigawa nchi katika majimbo ya kiutawala manane, Dodoma ikawa katika jimbo lililoitwa Central Province, na pia Dodoma iko katikati ya nchi hivyo basi wanamuziki kadhaa walianzisha bendi iliyoitwa Central Jazz band. Hii bendi ilitoa wanamuziki wengi sana waliokuja kutikisa anga za muziki Tanzania, wakiwemo akina Mnenge Ramadhani, Juma Ubao, maarufu kwa jina King Makusa, Patrick Balisdya, Ally Rahmani huyu alikuwa mpiga gitaa mahiri, enzi za STC  wote ni mazao ya Central Jazz

Mfanya biashara mmoja, Mohamed Omar Badwel, aliyekuwa na gereji na studio ya kupiga picha alinunua vyombo na kuanzisha bendi iliyokuja kuitwa Dodoma Jazz Band. Bendi hii ilikuwa na wanamuziki wazuri sana na ilitoa nyimbo zilizokuja kufahamika nchi nzima, wimbo wao uliokuwa maarufu sana miaka ya sitini ulikuwa Zaina Njoo.
Mmoja kati ya wapiga solo wa kwanza wa bendi hii alikuwa Hassan Mursali kwa asili alikuwa Mnyasa, huyu pia alikuwa anakitwa Hassan Kiziwi kwani pamoja na kuwa mahiri katika upigaji wa gitaa la solo alikuwa na tatizo la kusikia vizuri. Hassan aliwahi kujiunga na Kilwa Jazz band na wimbo ambao alipiga gitaa la solo ni ule  wenye maneno  Dunia Njema kukaa wawili. Hatimae alikuja kuacha muziki na kuwa fundi saa.
Dodoma Jazz Band ilikuwa ikisafiri sana katika kila wilaya nchi nzima, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilikuwa na lengo la kwenda kumchukua mpiga solo wa bendi ya Kilosa Jazz Band, si mwingine ila ni Abel Balthazar. Bendi ilifanikiwa kumchukua Abel na kurudi nae Dodoma. Siku chache baadae wazee waliotumwa na uongozi wa  Kilosa Jazz Band walifika kwa kiongozi wa Dodoma Jazz wakiwa na barua na kumuomba aifungue na kuisoma mbele yao kabla hawajaondoka. Ndani ya barua ile kulikuwa na maagizo kuwa Abel asiporudi Kilosa, basi kuna mwanamuziki mmoja wa Dodoma Jazz band atafariki. Pamoja na Abel kuwa keshashonewa suti mpya ya sare na Dodoma Jazz alirudishwa Kilosa mara moja kuepusha janga.
Mwanamuziki mwengine aliyewahi kupitia Dodoma Jazz Band ni Rashid Hanzuruni, mpiga gitaa marufu ambaye moja kati ya nyimbo zake alizopiga solo ambazo ni maarufu mpaka leo ni ule wimbo wa Kilwa Jazz Band ambao wengi wanaujua kama Lau Nafasi. Hanzuruni alijikuta katika bendi hii akiwa safarini akitokea Tabora ambako alikuwa amekorofishana na wanamuziki wenzie wa Tabora Jazz Band, alikuwa akielekea Dar es Salaam kujiunga na NUTA Jazz band, lakini akakatishwa safari hiyo na meneja wa Dodoma Jazz Band aliyemshawishi ajiunge na Dodoma Jazz Band. Hanzuruni hakukaa sana Dodoma, akaondoka na kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya ndoto yake ya kujiunga na NUTA Jazz Band, hata hivyo ndoto hiyo haikutimia kwani wakati huo NUTA Jazz Band ilikuwa na mpiga solo mahiri sana aliyeitwa Hamisi Franco, Hanzuruni akaishia kujiunga na Western Jazz Band.

Central Jazz band ilikuja kuwa chanzo cha Afro70 Band ya Patrick Balisdya, kwani ndiko Patrick na wenzie walikopata vyombo vya kwanza vya kuanzishia bendi yao hiyo maarufu.

Dodoma International Orchestra 1978


Bendi nyingine maarufu iliyowahi kuweko Dodoma ni Dodoma International Orchestra, hii ilikuwa mali ya Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa wa Dodoma. Dodoma International kwa kipindi ilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki mkongwe mpuliza saksafon Sheddy Mbotoni. Dodoma International Orchestra ilipitisha wanamuziki wengi sana waliokuja kuwa maarufu katika anga za muziki nchini, waimbaji kama Shaaban Dede, Ahamadi Sululu, Athumani Soso, Saburi Athumani, wapiga magitaa akina Charles Kasembe, Kassim Rashidi, Mohamed Ikunji, na wanamuziki wengine wengi maarufu wote walipitia bendi hii mahiri. Dodoma International ilijitambulisha kwa mitindo kadha wa kadha kama ‘perekete’, mafuriko ya jasho’, ‘zunguluke’ na mingineyo mingi iliyobadilika kutokana na wanamuziki kubadilika katika kuingia na kutoka. Bendi nyingine ya Dodoma ilikuwa ni mali ya fundi redio maarufu Mzee Alphonse Materu, na bendi aliipa jina lake ikaitwa Materu Stars. Materu Stars nayo ilipitisha wanamuziki wengi sana akiwemo aliyekuwa kiongozi wa bendi maarufu ya Butiama Jazz Band, mzee Alphonce Makelo, ambaye kwa sasa maepoteza uwezo wake wa kuona. Bendi nyingine iliyokuwa Dodoma na kupewa jina la mwenye bendi ni bendi ambayo bado ipo hai na  inaitwa Saki Stars. Saki lilikuwa ni kifupi cha  jina Salome Kiwaya, mwanamuziki wa kike aliyeiongoza bendi yake mpaka umauti wake uliotokana na ajali ya gari. Wiki ijayo tutaendelea na safari yetu ya bendi za Tanzania.

 

 

Saturday, July 9, 2022

UNAKUMBUKA SOCIAL EVENING?

Ma soul brothers wakiwa kwenye party
KWA wengi waliokuwa wakisoma sekondari miaka ya 60 na 70, moja ya siku zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu ilikuwa siku ya ‘Social Evening’. Siku hii ilikuwa ndio siku ambayo wanafunzi walipata nafasi kusakata dansi na kupata marafiki wapya, na mara nyingine hata kuachwa na marafiki wa zamani. Mara nyingi dansi hili liliambatana na kualika wanafunzi kutoka shule nyingine za jirani. Na kawaida ilikuwa shule ya wavulana kualika wanafunzi kutoka shule ya wasichana na shule ya wasichana kualika wanafunzi kutoka shule ya wavulana. Matayarisho yalikuwa yanaanza mapema kwa waalikaji kuandika barua kwa Mwalimu Mkuu au mwalimu wa ‘Social’ wa shule wanayotaka kuialika. Baada ya hapo kazi kubwa ni kukusanya michango kutoka kwa wanafunzi wanaotaka kushiriki siku hiyo. Michango hii kazi yake ilikuwa kununua viburudisho kwa wageni; soda, biskuti au hata maandazi, na pia kununua betri za ‘player’ ya kupigia muziki. Umeme ulikuwa nadra kwenye shule nyingi. Kamati ya starehe ilikuwa ‘busy’ kutafuta santuri mpya, kwa kuazima popote pale, na kama kuna mwalimu ana record player ilikuwa jambo la heri sana.  Ukumbi ulipigwa deki vizuri ili wageni wakifika wasije wakawadharau. Hatimae siku huwadia, social evening mara nyingi zilikuwa Jumamosi kuanzia saa nane mchana na kuisha kati ya saa moja mpaka mbili usiku. Wageni hukaribishwa na burudani huanza. Baada ya hotuba na kugawa vinywaji, wenyeji huleta burudani kama vile kucheza jiving, baada ya hapo ‘Dada mkuu’ au mwenyekiti wa kamati ya social wa shule moja hufungua dansi na mwenzie kaka mkuu au mwenyekiti wa kamati ya social wa upande wa pili. Na ndipo wengine mnajitosa kusaka mapatna. Kawaida ya miaka hiyo mwanaume unamfuata msichana kisha unainama kidogo kumuomba ucheze nae, anaweza akakubali au kukataa. Katika shughuli hizi waalimu wa kuangalia nidhamu walikuwa wakishiriki kuangalia kuwa maadili yanafuatwa. Wakati mnacheza mwalimu anapitapita kuangalia kama ‘hamsogeleani ‘ sana.  Kama nilivyosema hapo juu, muziki ulitoka kwenye record player ambayo ilikuwa na spika moja ndogo hivyo haikuwa na sauti kubwa. Ukiona ukubwa wa maspika siku hizi, unabaki kushangaa, tuliwezaje wanafunzi 200 hadi 300 kucheza muziki na kuusikia vizuri kwa kutumia spika moja  ya player yenye betri 6. Spika ambayo ili itoe bezi ililazimika kuwekwa juu ya pipa. Kulikuwa na nidhamu kubwa sana katika uchezaji, kulikuwa hakuna kupiga kelele, unasikia viatu tu vikisaga chini kwa kufuata mdundo wa muziki. Swala la kuwa pombe haikuhusika katika burudani hizi ni moja ya sababu ya kuwezekana kwa nidhamu hii. Mazungumzo yalikuwa ya chini chini mara nyingi yakihusu masomo.
Katika miaka ya 60 santuri za nyimbo kutoka Congo ndizo zilikuwa maarufu, magwiji wa muziki kama akina Franco, Johhny Bokelo, Dr Nico, Bavon Marie Marie na bendi zao maarufu, Ok Jazz, Negro Success, Co Bantuo, Bantou de La Capital, na miaka ya 70 kukatawaliwa na bendi zilizokuwa zikipiga mtindo wa Cavacha, Lipua Lipua, Kiam, Veve, Kamale na nyingine nyingi. Muziki wa soul ulikuwa na mabingwa wake akina Otis Redding, James Brown, Clarence Carter, Wilson Pickett na wengine wengi. 
 Kutoka  Marekani wanamuziki wa muziki wa country kama Skeeter Davis, Jim Reeves, Connie Francis ndio walitawala social evenings.
Wimbo wa Isaac Hayes wa Do your thing maana ulikuwa wimbo wa taratibu ambao ulikuwa mrefu, hivyo kila mtu alikuwa akimkimbilia mtu wake mara tu ukiaanza wimbo huo, maana ndio wimbo wa kukumbatyia kwa muda mreeffuuuuuu, ulikuwa na urefu wa dakika 19.
 Wavulana kwa wasichana walishiriki kuandika maneno ya nyimbo hizo kwenye madaftari yao na kubadilishana madaftari. Nyimbo maarufu katika madaftari ya wavulana zilikuwa ni nyimbo za Kikongo. Tambola na Mokili wa Johhny Bokelo na Conga Success na Bougie ya Motema wa Dr Nico na African Fiesta zilikuwa hazikosekana kwenye madaftari ya wavulana, wakati akina dada walipendelea sana kuandika maneno ya nyimbo za Skeeter Davis na Dark City Sisters kutoka Afrika ya Kusini. Kama nilivyosema hapo juu, umeme tu ulikuwa tatizo kweye shule nyingi, hivyo swala la kuwaona na kuwajua wanamuziki waliokuwa wakiporomosha muziki huo lilikuwa nadra sana. Magazeti yalikuwa machache, vyombo ambavyo siku hizi vinaonekana ni kawaida kabisa kama radio na TV navyo vilikuwa nadra sana. Lakini kwa njia ya ajabu vijana walikuwa wanajua namna ya kucheza staili za muziki mbalimbali!! Chacha, pachanga, charanga, baadae soul, bumping na kadhalika. Kwenye shule mbalimbali kulikuwa na wanafunzi ambao walikuwa wanapata bahati kuwa na ndugu au marafiki ambao walikuwa wakibahatisha kuwafundisha uchezaji mbalimbali wakati wa likizo, basi mwanafunzi wa aina hiyo anakuwa maarufu sana mara arudipo shule akiwa na staili mpya ya uchezaji, watu wote wanaanza kumuiga  uchezaji ili kujitayarisha kwa social evening. Ilikuwa si ajabu ukija na staili mpya ukapata hata mpenzi mpya.

Friday, July 8, 2022

TUZIKUMBUKE BENDI ZETU 1


 Kuanzia miaka ya 1920 kuna taarifa za maandishi za kuwepo kwa vikundi vya muziki Tanzania. Tanzania Bara ikiwa na bendi nyingi za muziki wa dansi, wakati Tanzania visiwani Taarab ikitawala. Leo nataka niwazungushe mikoa mbalimbali ambako kulikuwa na bendi. Bendi nyingine zilikuwa maarufu mpaka kujulikana nje ya nchi yetu na nyingine hazikuwa maarufu au hazikudumu sana, lakini kuna wasanii wengi walitoka huko na kuja kuwa maarufu nchini na hata duniani.
Nianze na Kigoma, huu si mji ambao siku hizi unatajwa wakati ukiongelea muziki wa dansi lakini kulikuwa na bendi kadhaa kutoka mji huo zilizokuja kujitokeza, tuanze na Lake Tanganyika Jazz Band, hii ndiyo bendi alikotokea mpiga solo, mtunzi na muimbaji Shem Karenga, ambaye alianza huko akiwa mpiga gitaa la bezi na hatimae kuhamia Tabora jazz band ambako nyota yake ilianzia kung’ara hapo. Kigoma kulikuweko na bendi iliyoitwa Super Kibisa Jazz  Band, bendi hii ilikuwa na waimbaji wazuri na wapigaji wazuri sana, mmoja wa wapiga magitaa wa bendi hiyo Mzee Simba, hatimae alikuja kujiunga na JKT Kimbunga, bendi aliyokaa nayo mpaka alipostaafu. Pia kulikuweko na bendi iliyochukua jina la mji huo na kuitwa Kigoma jazz band, bendi nyingine iliyokuweko Kigoma iliitwa Kasababo Jazz Band, hii ndiyo ilikuwa bendi ya awali kabisa ya marehemu Shaaban Dede.
Mkoa jirani wa Mara ulikuwa na bendi nyingi pia, bila shaka ni vizuri kuanza na bendi ya Mara Jazz Band, hii ilipata umaarufu mkubwa ikiwa na mtindo wake wa Sensera. Lakini pia kulikuwa na bendi iliyochukua jina la mji wa Musoma, bendi iliyoitwa Musoma Jazz Band hii ilijitambulisha kwa mtindo wake wa Segese. Bendi nyingine kutoka mkoa huu ilikuwa Special Baruti Band, hii ndiyo bendi ya awali ya muimbaji maarufu Jerry Nashon kabla hajaingia jiji la Dar es Salaam. Musoma kulikuwa na bendi iliyokuwa mali ya Kanisa Katoliki iliyoitwa Juja Jazz band, hata kule Iringa kulikuwa na bendi nyingine mali ya Kanisa katoliki iliyoitwa VICO Stars ikiwa ni kifupi cha Vijana Consolata Stars. Bendi nyingine kutoka mkoa wa Mara ilikuwa ni Eleven Stars Band, japo ilijiita jina hilo, bendi ilikuwa na wanamuziki sita tu.

Tukiingia jiji la Mwanza, jiji lililokuwa likijisifu kwa starehe miaka ya sitini na sabini, kutokana na almasi, pamba na biashara ya mifugo, kulikuweko na bendi kadhaa ikiwemo Kimbo Twist Band ambako waliwahi kupita kati ya wapiga solo mahiri waliowahi kutokea Tanzania, marehemu  Rashid Hanzuruni na marehemu Kassim Mponda. Mwanza pia kulikuwa na bendi ambayo asilimia kubwa walikuwa ni wanamuziki kutoka Kongo, bendi hiyo iliitwa Orchestra Super Veya, bendi hii ilikuwa na umaarufu mkubwa kanda ya ziwa na ndiko alikopitia mwanamuziki maarufu Mzee Zahir Ally Zollo.
Mji wa Shinyanga kulikuwa na bendi maarufu iliyoitwa Shinyanga Jazz Band, bendi hii ilirekodi nyimbo kadhaa lakini wimbo wao mmoja unakumbukwa na wapenzi wa muziki wa dansi mpaka leo unaitwa Tenda Wema nenda zako. Wimbo huu ulitungwa na marehemu Mzee Zacharia Daniel Mabula, na kwa sababu ya wimbo huo mpaka kifo chake aliitwa Zacharia Tendawema au Mzee Tendawema, licha ya  historia yake ya kupitia bendi nyingi zikiwemo Western Jazz band, JKT Kimulimuli na TANCUT Almasi Orchestra ambako pia huko alitunga nyimbo nyingi, lakini  wimbo huo ulikuwa ndio nembo yake.
Tabora ulikuwa mji uliochangamka sana, kwanza ni moja kati ya miji ya zamani nchini, pili Tabora ulikuwa mji wenye vijana wengi kutokana na kuwa na shule  na vyuo vilivyokuweko katika mji ule. Kulikuwa na shule kongwe kama  Sekondari ya Tabora Boys na Sekondari ya Tabora Girls, pia vyuo kama Tabora Secretarial, chuo cha Ualimu cha Tabora, na chuo kikongwe cha reli,  Railway Training School. Hivyo basi Tabora nayo ilichangamka sana kimuziki, kulikuwa na bendi maarufu ya Tabora Jazz Band, na bendi yake dada, Nyanyembe Jazz band na pia ilikuweko bendi kongwe ya Kiko Kids. Wanamuziki wengi sana maarufu walitoka bendi hizi wakiwemo Shem Karenga , Wema Abdallah, Kassim Kaluona na Salum Zahoro, majina yaliyokuja kuvuma Afrika ya Mashariki na kati.

Mwaka 1972 Mzee Moses Nnauye aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Singida, kutokana na kupenda kwake muziki haikuchukua muda mrefu akahakikisha Singida ikapata bendi nzuri iliyoitwa Ujamaa Jazz Band, bendi iliyokuwa ikipiga kwa mtindo iliyouita King’ita Ngoma. Wanamuziki kadhaa kama Waziri Ally, Selemani Mwanyiro walipitia bendi hii. Nikumbushe jambo jingine kuwa Mzee Nnauye alipokuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo pia alianzisha bendi iliyoitwa Sabasaba Jazz band, mtindo wa bendi hiyo uliitwa Kizibo. Hamza Kalala alikuwa mpiga solo wa kwanza wa bendi hii, baada ya Mzee Nyange aliyekuwa mpiga solo wa Cuban Marimba kukataa wito wa kujiunga na bendi hiyo.


Tuesday, April 12, 2022

MWAKA 1973 YALIFANYIKA MASHINDANO YA BENDI BORA TANZANIA UNAJUA MSDHINDI ALIKUWA NANI?

 

TANGAZO la mashindano hayo lilitolewa kwenye gazeti na mashindano hayo yalidhaminiwa na NDC.. Shirika la Maendeleo la Taifa.

Mshindi wa kwanza ilikuwa ni bendi ya Sunburst. Picha ya chini kulia, aneonekana amevaa kofia na kushika kikombe ni James Mpungo kiongozi wa Sunburst, bendi ya pili ilikuwa Tonics na Marijani Rajabu akiwakilisha Safari Trippers iliyochukua zawadi ya tatu







Hawa ndio Sunburst bendi iliyoanzishwa mwaka 1970 na mwanamuziki Mkongo Hembi Flory, ilikuwa bendi moto sana mwanzoni mwa miaka ya 70. Mwaka 1973 ikashinda mashindano ya Bendi Bora Dar es Salaam na kuwa ya kwanza. Katika picha hapo juu, toka kushoto Toby John Ejuama (saxophone) huyu alikuwa Mnaijeria kutoka Biafra, kama mnakumbuka Tanzania tulimuunga mkono  Ojukwu, kiongozi aliyekuwa na ndoto za jimbo la Biafra kujitenga na Nigeria, hivyo tukawa kimbilio la watu kutoka huko. Anaefuata ni Flory mpiga gitaa Mkongo, kisha mkongwe Johnny Rocks kwenye (drums), huyu alikuwa pia anapiga na George Di Souza pale Margot.  James Mpungo (lead vocals) kijana wa Mbeya ambaye hatimae alijiunga na Mangelepa. Anafuatia Kassim Rajabu Magati (organ/lead vocals, kwenye gitaa la bezi ni Bashir Idd Fahani. 



Sunday, March 27, 2022

TUMETIMIZA MIAKA 16 TOKA KIFO CHA TX MOSHI WILLIAM, SAUTI YAKE INAENDELEA KUSIKIKA

 


Msondo wakiwa mazoezini katika ukumbi wa Amana

Moshi William alizaliwa mwaka 1958 Hale Mwakinyumbi Korogwe. Hale alikuwepo mwanamuziki maarufu aliyekuwa akiitwa Mzee Masongi, yeye alikuwa na bendi, na bendi hii ilikuwa chanzo cha wanamuziki wengi maarufu akiwemo Moshi William.  Jina halisi la Moshi William lilikuwa Shaaban Ally Mhoja lakini alikuja kubadili na kuitwa Moshi William kutokana na kuja kulelewa na baba mwingine.  Bendi ambazo TX Moshi William aliwahi kupitia baada ya kutoka Hale zilikuwa ni Safari Trippers wana Sokomoko, UDA Jazz Band wana Bayankata, na Polisi Jazz Band wana Vangavanga, na hatimae JUWATA Jazz Band wana Msondo Ngoma, bendi aliyodumu nayo mpaka kifo. Kati ya nyimbo zake za kwanza mara baada ya kujiunga na JUWATA zilikuwa Ajuza, Ashibaye  na Asha Mwanaseif, wimbo huu wa tatu alimtungia mkewe, baada ya hapo alitunga nyimbo nyingi sana na kwa ujumla alirekodi album karibu 13.  Sifa ya Moshi kuanza  kuitwa  TX ilitungwa na marehemu Julius Nyaisanga aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam. Zama hizo, serikali ilikuwa imeweka sheria kuwa magari ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi nchini yawekwe namba ambazo zilianzia na TX kuonyesha ni ya Kimataifa, hivyo TX ikageuka kuwa nembo ya sifa ya kuwa na hadhi ya Kimataifa. Kutokana na umahiri wa Moshi katika kutunga na kuimba, Nyaisanga akampachika kisifa cha TX. Na hakika umahiri wake ulijidhihirisha kwani kwa miaka mitatu mfululizo kati ya mwaka 2003 mpaka 2005, TX Moshi William alitunukiwa tuzo za utunzi bora  na Kilimanjaro Music Awards.  Pamoja na Msondo, Moshi aliwahi kurekodi nyimbo nyingi akiwa na wanamuziki wenzake nje ya Msondo, kwa utaratibu ulikuwa maarufu kwa jina la zing zong au wengine waliita zozing.  Moshi alifariki siku ya tarehe 29 March 2006 katika wodi ya Sewa Haji baada ya operesheni ya kuondoa chuma katika mguu wake uliovunjika kwenye ajali. Alifariki saa tatu kasoro robo asubuhi na kuzikwa siku hiyohiyo katika makaburi ya Keko Machungwa.

 

 


 
Kaburi la TX Moshi William


Mungu Amlaze Pema Shaaban Ally Mhoja Kishiwa - TX Moshi William

 

Saturday, March 26, 2022

DR UFUTA MPIGA SOLO WACUBAN MARIMBA NA TK LUMPOPO AFARIKI DUNIA

 

Dr Ufuta uzeeni
J
OAKIM UFUTA, mpiga gitaa la solo aliyekuwa maarufu kwa wapenzi wa muziki enzi za Cuban Marimba ya Juma Kilaza, na bendi za Juma Kilaza zilizofuatia amefariki dunia. 
Dr Ufuta ambaye maisha yake ya uzeeni yalikuwa magumu kiasi cha kuwa mlinzi wa wa usiku wa sehemu mbalimbali pale Morogoro, na pia alikuwa fundi baiskeli,  amefariki Ifakara siku ya tarehe 18 March na kuzikwa kesho yake 19 March 2022 hukohuko Ifakara. 

Ufuta alizaliwa  Utuu Misheni Mahenge karibu miaka 70 iliyopita, alianzisha bendi yake ya kwanza mwaka 1966,  bendi yake aliyoiita Taifa Jazz, bendi hii iliyokuwa na waimbaji wanne, ilikuwa haina hata chombo kimoja kilichotumia umeme. Kati ya mwaka 1966 na 1968 hiyo ndiyo ikawa bendi moja maarufu  pale Mahenge. Mbunge wa jimbo la Mahenge wakati huo Mheshimiwa Ilanga, aliwanunulia vyombo vichache vijana hawa na hii ikawa bendi rasmi iliyokuwa ikisindikizana na Mbunge huyo katika kampeni zake mbalimbali.

 Mwaka 1968 kaka yake Lucas Simon alimshawishi aachane na bendi yake ya Taifa Jazz na kujiunga na Cuban Marimba wakati huo ikiwa chini ya Juma Kilaza. Na bendi ya Cuban aliweza kufika mpaka Nairobi ambako wakati wa kurekodi fundi mitambo mmoja pale studio alianza kumuita Dokta kutokana na upigaji wake mahiri na cheo hicho amebaki nacho mpaka umauti wake.

Picha hii ilikuwa ni ganda la moja ya santuri ya nyimbo za Cuban Marimba. Dr Ufuta ni aliyevaa miwani . Wa kwanza kulia waliosimama ni Juma Kilaza.

 Mwaka 1974 kuliktokea kutokuelewana kati ya wanamuziki wa Cubana Marimba na wamiliki wa bendi hiyo ambao walikuwa warithi wa marehemu  Salum Abdallah, mtiti huo ukasababisha Juma Kilaza, Joakim Ufuta, Juma Sangula, Ally Said na Hemedi Maneti kuihama bendi hiyo na kuunda TK Lumpopo, na hapo walitoa nyimbo nyingi za  kukumbukwa, wimbo wao wa kwanza ulikuwa Maisha ya Sasa. Katika bendi hii pia kukatokea kutokuelewana kwa ajili ya maslahi, Hemedi Maneti akatimka  na kujiunga na Vijana Jazz Band, Dr Ufuta akarudi tena Cuban Marimba. Baada ya muda kama ilivyokuwa kawaida miaka ile, bendi ilianza ziara ya  mikoa mbalimbali Kenya. Wakiwa Naivasha kukatokea kukorofishana tena,  wenzie wakarudi Tanzania yeye akabaki akitafuta maisha nchini Kenya.


Ufuta akitengeneza 


Mungu Amlaze pema peponi Joakim Ufuta

Monday, March 21, 2022

MANENO UVURUGE AENDELEA NA SAFARI ZAKE ZA MUZIKI

Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo

Wakati Maneno Uvuruge akiwa katika bendi ya  Super Rainbow, ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu. Muimbaji Banza Tax nae akajiunga  na bendi hiyo wakati huohuo.
Wakati huohuo katika ukumbi wa Lango la Chuma Mabibo makao makuu ya bendi ya Mambo Bado, mambo yalikuwa magumu, bendi hiyo ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, waimbaji Lodji Mselewa na Nana Njige nao wakaenda kujiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana, kiongozi wa Mambo Bado Tchimanga Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa ikaingia katika hali mbaya zaidi kwani Assossa aliiacha tena Mambo Bado ikafa rasmi.
 
Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo Maneno akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Mzee Juma Mrisho, lakini bendi ya  Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho, wanamuziki waimbaji Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe, nao wakajiunga na bendi hiyo. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.
Mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo Msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa.

Saturday, March 19, 2022

MJUE ALLY OMARY JAMWAKA

Ally Omary Jamwaka

Ally Omary Jamwaka alizaliwa katika kijiji cha Malui tarehe 1 Machi 1953, akajiunga na shule ya msingi ya kijijini kwake kuanzia 1960 na kusoma hapo mpaka darasa la saba. Mwaka 1969 akaingia katka jiji la Dar es Salaam kuanza kusaka maisha. Kazi aliyoipenda ilikuwa ni usanii, pengine kwa kuwa  kaka yake Shaaban Omary  alikuwa mpiga drums.  Jamwaka alianza safari yake ya usanii kwa kujiunga na kikundi cha sanaa kilichokuwa na maskani pale Buguruni kikiwa chini ya Mzee Mindu. Wakati yuko huko akakutana na rafiki yake aliyeitwa Adam Bakari, huyu baadae sana alikuja kuwa muimbaji maarufu na kupewa jina la Sauti ya Zege, kwa pamoja wakatengeneza kundi lao waliloliita The Hippies. Kundi hili la muziki wa vijana lilikuwa kazi yake kubwa kwenda kwenye madansi ya bendi kubwa na kuomba 'kijiko'. Huu ulikuwa mtindo ulioenea nchi nzima wakati huo, bendi ndogo zilikuwa zikipita zinapopiga bendi kubwa na kuomba 'kijiko' na hivyo kuruhusiwa kupiga nyimbo kadhaa kwa kutumia vyombo  vya bendi kubwa, wakati bendi hiyo inapumzika,  hii iliwapa wadogo uzoefu na wale waliokuwa wazuri waliweza hata kupata ajira papo hapo. The Hippies makao yao makuu yalikuwa mtaa wa Somali maeneo ya Kariakoo, walikuwa wakipiga muziki wa kukopi bendi za nje zilizotamba wakati huo, hasa zile za Ulaya na Marekani. Jamwaka wakati huo alikuwa tayari akipiga tumba na drums.
 Mwaka 1971 alijiunga na Biashara Jazz iliyokuwa bado mpya kabisa baada ya kubadili jina kutoka STC Jazz. Hii ilikuwa ni bendi iliyokuwa chini ya miliki ya Board of Internal Trade (BIT) ambayo chini yake kulikuwa na mashirika ya umma kama RTC, DABCO, HOSCO, GEFCO na kadhalika. Katika bendi hii aliwakuta akina Raphael Sabuni, Belino, Muddy, na kaka yake Shaaban Omary Jamwaka ambaye alikuwa mpiga drum wa bendi hiyo wakati huo.
Toka kushoto Ally Jamwaka, fundi mitambo wa Biashara Jazz band, kushoto Chamchu mpiga drum wa Biashara Jazz Band, wakiwa wamesimama kwenye uwanja wa Samora Iringa mwaka 1975

 Wengi wa wanamuziki waliokuwa STC Jazz Band walikuwa wasomi kwa hiyo waliacha muziki na kuingia katika kazi nyingine tofauti za kiofisi katika mashirika mbalimbali ya BIT. Ally Jamwaka alikaa katika Biashara Jazz Band iliyokuwa chini ya uongozi wa Juma Ubao aka King Makusa hadi mwaka 1977 alipoamua kujiunga na Tanzania Stars. Bendi hii ilikuwa na makao yake katika ukumbi maarufu miaka hiyo iliyoitwa Margot ambayo ilikuwa katikati ya Jiji pembeni ya barabara ya Samora. Ukumbi huu ulikuwa maarufu sana kwani kulikuwa na muziki kila siku ya wiki mpaka usiku wa manane, mabaharia walikuwa wakisha kutia nanga Dar es Salaam ,walielekea Margot ambapo palikuwa ni mahala penye starehe za kila aina, hapo ndipo pia kilikuwa kituo kikubwa cha 'machangudoa' ambao walikuwa wakitega nyavu zao kuwasubiri wateja.  Kufika kwake bendi hiyo alipishana na wanamuziki maarufu ambao wote ni marehemu, Haruna Lwali mpiga tumba na Joseph Mulenga mpiga gitaa wakahamia bendi iliyokuwa ikipiga ukumbi jirani wa Gateways ambapo kulikuwa na bendi maarufu ya Orchestra Santa Fe.
Baadhi ya wanamuziki waliokuweko katika bendi ya Tanzania Stars wakati huo walikuwa Joseph Emmanuel muimbaji na mpiga gitaa na mtunzi wa wimbo uliotamba wakati wake ulioitwa 'Mawazo', Hussein Sadiki, Yahaya Bushiri nae pia alikuwa mpiga gitaa mzuri sana. Bendi hii ilikuwa inapiga muziki kutoka nchi mbalimbali duniani hasa ukikumbuka kuwa walikuwa na wateja mabaharia kutoka kila kona ya dunia, hivyo ukiingia Margot ungeweza kusikia nyimbo cha Kichina, Kihindi, Kigiriki na kadhalika. Baada ya ukumbi huu kuchukuliwa na Chama Cha Ushirika, bendi pia ikachukuliwa na ndipo ilipozaliwa ile bendi maarufu ya Washirika Tanzania Stars.
 Jamwaka aliendelea kupigia Tanzania Stars mpaka mwaka 1979 ambapo bendi ya Mlimani Park ilimfukuza kazi mpiga tumba wake aliyekuwa akiitwa Tanzania One, Haruna Lwali, na hapo Abel Balthazar alimfuata Jamwaka na kumkaribisha Mlimani Park Orchestra. Mlimani Park  ilikuwa chini ya TTTS, shirika la umma lililokuwa likiendesha shughuli za usafirishaji na hasa wa taxi. Bendi ilipewa huduma nzuri sana na shirika hili na kufikia kuwa moja ya bendi kubwa nchini, nyimbo zake za wakati ule bado zinaheshimika katika nyanja za muziki hata leo. Ukumbi wa Msasani Beach Club ulikuwa mmoja wa mali za TTTS, na bendi ya Mlimani Park ndio iliyojenga ukumbi huo kwa kutumia mapato ya kila Jumatano kuelekezwa kwenye ujenzi wa ukumbi huo. Baada ya ukumbi huo kukamilika wanamuziki wakiwa na imani ambayo baadae ilikuja kuonekana potofu, waliamua kutumia fedha yao ya kila Jumatano kuanza kujenga ukumbi wa bendi yao uliokuwa Mpakani eneo linalojulikana kama DDC. Ujenzi ulifika mahala ukadorora na kufa kabisa. Hapa kuna maelezo kuwa  bendi ilipigwa 'kipapai' na bendi pinzani iliyokuwa jirani ili isikamilishe ujenzi maana ingekuwa bendi ya kwanza Tanzania kuwa na ukumbi wake  wa kisasa. Kama ni kweli walipigwa kipapai, basi hilo lilifanikiwa kwani ukumbi haukukamilika mpaka leo . Mwaka 1982 mali za TTTS kama vile bendi na ukumbi wa Mpakani ukahamishiwa Dar es Salaam Development Corporation (DDC), awali kulikuweko na wazo kuwa bendi ihamishwe iwe chini ya ATC maana wakati huo Air Tanzania walikuwa na Club yao nzuri tu, lakini ikaonekana DDC walikuwa na kumbi kama vile DDC Kariako, DDC Magomeni, DDC Keko na hivyo bendi ingefanya kazi kwa ufanisi zaidi huko, bendi na wanamuziki wakauzwa DDC. Mambo yalibadilika sana kwa bendi hii kwani menejiment mpya haikuthamini bendi, na hata matamko ya mara kwa mara toka kwa Meneja Mkuu wa DDC wakati huo yaliudhi sana wanamuziki kwani si mara moja alikuwa akiwatamkia wanamuziki kuwa bendi ikifa hana tatizo maisha yataendelea. Hili lilipunguza sana morali ya wanamuziki, hivyo basi 1985 awamu ya kwanza ya kundi kubwa la wanamuziki liliondoka DDC Mlimani Park Orchestra na kujiunga na Orchestra Safari Sound na kuanzisha kundi la International Orchestra Safari Sound iliyokuwa na mtindo wa Ndekule, ambapo walikuweko Abel Barthazar, Muhidin Maalim Gurumo, Ally Makunguru, Ngosha, Kassim Rashid wakiungana na wenzao akina Skassy Kasambula walianzisha moto mkali uliotikisa nchi. Katika awamu ya pili ya wimbi la wanamuziki wa Sikinde kwenda OSS, Ally Jamwaka pia alikuweko, wakati huo akiwa na Fresh Jumbe, Cosmas Chidumule,Hamis Juma Kinyasi, Bobchipe Chipembele wakasindikizana na Michael Bilali ambaye alirudishwa Sikinde mapema kwa nguvu ya wapenzi wa Sikinde waliochanga fedha na kulipa fedha alizokuwa kachukua toka uongozi wa OSS.  

Thursday, March 17, 2022

MANENO Uvuruge mwanamuziki toka familia ya wapiga magitaa

 

Maneno Uvuruge

Kuna familia nyingine hutokea kuwa na wanamuziki wengi tu, mfano ni familia ya maarufu ya mwanamuziki marehemu Michael Jackson. Watoto wote wa familia hiyo walikuja kuwa wanamuziki maarufu, wavulana wakaweza kuanzisha kundi la The Jackson 5, baadae hata dada zao Latoya na Janet Jackson nao wakaja kujitokeza kuwa wanamuziki waliokuja kujipatia mafanikio makubwa katika fani hii. Kuna familia kadhaa zenye sifa hizo hata hapa Tanzania, kuna familia ya Kanuti, Muumba na Uvuruge ni mifano ya jambo hili. Leo tumzungumzie Maneno Uvuruge kutoka familia ya akina Uvuruge.

Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.

Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka kutoka baamoja na kwenda nyingine na gitaa lake  na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji. Hayakuwa maisha rahisi

Jumanne Uvuruge mtunzi wa wimbo maarufu wa Georgina uliopigwa na Safari TRppers na kuimbwa na Marijani Rajabu

Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa kaka yake Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa..

Stamili Uvuruge hapa akiwa jukwaani wakati akiwa bendi ya Bima Lee

 
Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba  na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, kila baba yao alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake

Maneno Kushoto akiwa na kaka yake Huluka

 
Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Generation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Mwanamuziki muimbaji marehemu Freddy Benjamin ndie aliyemshauri Maneno kujiunga na bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia, ambako Maneno alijaribiwa kama ilivyokuwa kawaida wakati ule kwa mwanamuziki mgeni, lakini pamoja na kuweza kupiga gitaa vizuri alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi hiyo wakati huo. Baada ya hapo Freddy alimuombea kazi katika bendi ya Super Rainbow, bendi ambayo iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na katika bendi hiyo Maneno akakutana na wanamuziki wakubwa wakati huo kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky na Mzee Bebe. Wakati huu Eddy Sheggy ambaye alikuja kuipaisha bendi hiyo kwa wimbo wa Milima ya Kwetu alikuwa hajajiunga  na bendi hii wakati huo. Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga. Katika kipindi hichohicho bendi iliyokuwa ikiongozwa na Tchimanga Assossa, Orchestra Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige nao pia wakaja kujiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi..

Huluka Uvuruge akiwa jukwaani Msondo Music Group


Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Marehemu Mzee Juma Mrisho maarufu pia kama Ngulimba wa Ngulimba, wakati huo Urafiki Jazz Band  nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri marehemu Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waimbaji Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe nao pia wakajiunga na bendi hiyo. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa wa kupiga gitaa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis Original, alichukuliwa na bendi hii ili awe mpiga gitaa la rhythm, alijiunga na wapiga rhythm wawili mahiri Mbwana Cox na Omari Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba. Siku moja mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole aliyekuwa mmiliki wa bendi ya Afriso na wakamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge, Kiniki Kieto (mwimbaji), Comson Mkomwa (saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma.  Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwisha pokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba kwanza alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu bendi hiyo, kwani Mzee Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoaManeno Maquis kwa mara ya pili na kuhamia nae Afrisongoma. Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate huko Uingereza waweze kutengeneza kundi la muziki huko, lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda lakini rafiki zake akiwemo Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa......itaendelea


MARK MANJI WA ORCHESTRA MKWAWA wana Ligija

 

Waliochuchumaa na magitaa kushoto ni Simon Sewando, kulia John Mkamwa.Aliyesimama wa kwanza kulia Mark Manji.

Mark Manji alianza kupenda sana kusikiliza  wapigaji wa magitaa makavu(accoustic) maarufu kama magalaton,  waliokuwa kijiji kwao Chitare, Musoma. Upigaji wa magitaa makavu ulikuwa maarufu katika maeneo mengi ya Musoma labda kutokana na gitaa kuwa na kufanana na Ritungu au kwa kuwa Musoma ilikuwa jirani na Kenya ambako kulikuwa na wapiga magitaa maarufu kama akina George Mukabi, John Mwale na kadhalika. Mark alinambia kuwa anakumbuka toka yuko darasa la tatu alianza kuwa  na  hamu sana ya kuwa mwanamuziki. Hamu hii iliongezeka alipoingia kidato cha kwanza Alliance Secondary pale Musoma  ambako kila Jumamosi alianza kwenda kuchungulia wakati  bendi mbalimbali zikipiga  Musoma mjini. Bendi aliyokuwa maarufu wakati huo ilikuwa inaitwa Eleven Stars Band, pamoja na kuwa bendi ilikuwa na watu sita iliitwa Eleven Stars kwa kuwa mwenye bendi pia alikuwa anaendesha club ya mpira iliyokuwa na jina hilo. Bendi hiyo iliyokuwa na mpiga solo kutoka Kigoma, mpiga bezi Mkongo, mwimbaji Mkongo na Watanzania wengine wawili, mmoja wa waimbaji alikuwa akiitwa Dode ambaye kwake ndiko vyombo  vya bendi vilikuwa vinatunzwa.  Huyu Dode, ambaye baadae sana Mark aligundua ni kifupi cha Deusdedit alikuwa akiishi karibu na kaka yake mmoja, hivyo akaomba kujifunza gitaa na taratibu akajifunza gitaa la rhythm. Hizi juhudi zake za kujifunza muziki ziliwahi hata kusababisha kufukuzwa shule wakati akiwa form II, lakini hatimae kwa mbinde alimaliza kidato cha nne.
Mwaka 1970  akawa amechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Mkwawa,  katika kumbukumbu zake hakuwahi kusikia kuwa Iringa kulikuwa na bendi kwa hiyo alikataa kwenda kuendelea na shule kwa kuwa alitaka kuwa mwanamuziki. Akawa na ndoto za aidha kwenda kusoma Tanga, Morogoro, au Tabora maana huko alijua kulikuwa na bendi kubwa na maarufu. Pamoja na baba yake kujitahidi kumshawishi kwenda kusoma Mkwawa alikataa katakata akitaka kujiunga  na muziki au aende kusoma kwenye mji wenye bendi. Alijitahidi hata kubadilishana na mwenzie aliyechaguliwa kusoma Galanos Tanga lakini ikashindikana. Baada ya kama wiki tatu toka shule zimefunguliwa akakutana na mtu aliyemshangaa kwanini hajaenda shule, na alipomwambia kuwa hana mpango wa kwenda Iringa kwa kuwa hakuna bendi, yule mtu alimtaarifu kuwa katika shule ya Mkwawa kuna bendi, na tena ndio inayopiga Iringa mjini. Baada ya kusikia hayo moja kwa moja akaenda kwa baba yake na kumwambia kuwa ameamua kwenda shule, tena kesho yake. Baba yake hakuongeza neno, akampa fedha haraka sana nae  haraka akenda ofisi  za wilaya na kupewa warrant ya kwenda kusafiri kuelekea Iringa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kusafiri nje ya Musoma, lakini alifanikisha safari yake ndefu ya meli hadi Mwanza, kisha kupanda treni Mwanza mpaka Dodoma na kumalizia safari kwa basi toka Dodoma hadi Iringa. Alifika shuleni Mkwawa kama saa kumi na moja jioni, akakuta taratibu ziko nzuri maana akakuta orodha iliyoeleza bweni na chumba alichokuwa kapangiwa kuishi, alikuwa kapangiwa bweni la Magembe West. Haraka akaweka mizigo tu kwenye chumba alichopangiwa na kuulizia bendi iko wapi, akaelekezwa na kukuta mazoezi yanaendelea, akakaa hapo kwa saa nzima na kujua kweli amefika alipotaka.
Pamoja na masomo akaendelea na bendi ambayo kweli iliendelea kupiga Iringa mjini kila wikiendi katika dansi lililojulikana kama bugi, dansi ambalo lilianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Bendi ilijulikana kwa jina la Orchestra Mkwawa na mtindo wao ulikuwa Ligija. Baadhi ya wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Mark Manji na Masanja wakiwa wapiga gitaa la rhythm, Simon Sewando na Kakonko gitaa la solo, Tanganyika mpuliza Sax, John Mkamwa kwenye bass, Danford Mpumilwa na Semboni waimbaji, Zacharia Kakobe kwenye conga na Norman Hiza pia kwenye bezi.
 Mwaka 1972 baada ya kumaliza mitihani ya mwisho bendi ilisafiri hadi Dar es salaam kwenda kurekodi nyimbo zao,bendi ya  Vijana Jazz ndio walikuwa wenyeji wao na wakawaazima hata vyombo walivyoenda kurekodia.
Baada ya kumaliza shule ya Mkwawa kama ilivyokuwa ada wakati huo akaenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, mwaka 1973 baada ya kumaliza JKT akaingia Dar es Salaam akiwa na nia ya kujiunga aidha na Dar es Salaam Jazz au Western Jazz bendi alizozipenda sana, lakini anasema hali ya maisha duni ya wanamuziki aliyoikuta ilimkatisha tamaa kuwa mwanamuziki na kuamua kuendelea na masomo, na kufanya muziki kuwa ni shughuli yake ya ziada, jambo ambalo ameweza kulifanya na wakati huu ambapo amekwisha staafu kazi ameanzisha kituo kikubwa cha kufundisha taaluma mbalimbali za muziki, kule Tabata.
 Mark Manji nae alikuja kuanzisha bendi aliyoiita Chikoike Sound, jina hilo la bendi lilitokana na kufupisha majina ya watoto wake. Simon Sewando , ambaye mpaka sasa ni mwalimu chuo kikuu cha Dar es Salaa idara ya electronics nae alianzisha bendi iliyoitwa TZ Brothers. Muimbaji Danford Mpumilwa nae alikuja kuanzisha bendi iliyokuwa maarufu pale Arusha iliyoitwa Serengeti Band.
Kati ya bendi ambazo Orchestra Mkwawa iliwahi kupiga nazo katika jukwaa moja ni miaka hiyo ni Cuban Marimba ya  Kilaza, Butiama Jazz Band, STC Jazz Band wakati huo ikiwa na wanamuziki akina Marijani Rajabu, Raphael Sabuni, Belino, Ally Rahman na wengineo.

Shule ya Mkwawa ilikuwa na bendi mbili, bendi ya pili walijiita The Midnight Movers, bendi hii ilikuwa ikipiga muziki  wa  kizungu, wakati huo muziki ulioigwa sana na bendi za aina hiyo  ulikuwa ni wa soul, na blues. Hivyo bendi hii ya pili ilipiga muziki wa akina James Brown, Wilson Picket, Otis Redding, Jimi Hendrix na kadhalika, baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika bendi hii walikuwa ni Kafumba, Martin Mhando, Eddie Hans Poppe, Bijoux, Deo Ishengoma na Shaba katika drums. Deo aliyekuwa mwimbaji mmoja wapo alikuwa na mvuto wa pekee kutokana na Afro yake kubwa na uvaaji wa suruali pana za mtindo wa bugaluu ziliomfanya ajulikane mji mzima wa Iringa.