Thursday, March 17, 2022

MARK MANJI WA ORCHESTRA MKWAWA wana Ligija

 

Waliochuchumaa na magitaa kushoto ni Simon Sewando, kulia John Mkamwa.Aliyesimama wa kwanza kulia Mark Manji.

Mark Manji alianza kupenda sana kusikiliza  wapigaji wa magitaa makavu(accoustic) maarufu kama magalaton,  waliokuwa kijiji kwao Chitare, Musoma. Upigaji wa magitaa makavu ulikuwa maarufu katika maeneo mengi ya Musoma labda kutokana na gitaa kuwa na kufanana na Ritungu au kwa kuwa Musoma ilikuwa jirani na Kenya ambako kulikuwa na wapiga magitaa maarufu kama akina George Mukabi, John Mwale na kadhalika. Mark alinambia kuwa anakumbuka toka yuko darasa la tatu alianza kuwa  na  hamu sana ya kuwa mwanamuziki. Hamu hii iliongezeka alipoingia kidato cha kwanza Alliance Secondary pale Musoma  ambako kila Jumamosi alianza kwenda kuchungulia wakati  bendi mbalimbali zikipiga  Musoma mjini. Bendi aliyokuwa maarufu wakati huo ilikuwa inaitwa Eleven Stars Band, pamoja na kuwa bendi ilikuwa na watu sita iliitwa Eleven Stars kwa kuwa mwenye bendi pia alikuwa anaendesha club ya mpira iliyokuwa na jina hilo. Bendi hiyo iliyokuwa na mpiga solo kutoka Kigoma, mpiga bezi Mkongo, mwimbaji Mkongo na Watanzania wengine wawili, mmoja wa waimbaji alikuwa akiitwa Dode ambaye kwake ndiko vyombo  vya bendi vilikuwa vinatunzwa.  Huyu Dode, ambaye baadae sana Mark aligundua ni kifupi cha Deusdedit alikuwa akiishi karibu na kaka yake mmoja, hivyo akaomba kujifunza gitaa na taratibu akajifunza gitaa la rhythm. Hizi juhudi zake za kujifunza muziki ziliwahi hata kusababisha kufukuzwa shule wakati akiwa form II, lakini hatimae kwa mbinde alimaliza kidato cha nne.
Mwaka 1970  akawa amechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Mkwawa,  katika kumbukumbu zake hakuwahi kusikia kuwa Iringa kulikuwa na bendi kwa hiyo alikataa kwenda kuendelea na shule kwa kuwa alitaka kuwa mwanamuziki. Akawa na ndoto za aidha kwenda kusoma Tanga, Morogoro, au Tabora maana huko alijua kulikuwa na bendi kubwa na maarufu. Pamoja na baba yake kujitahidi kumshawishi kwenda kusoma Mkwawa alikataa katakata akitaka kujiunga  na muziki au aende kusoma kwenye mji wenye bendi. Alijitahidi hata kubadilishana na mwenzie aliyechaguliwa kusoma Galanos Tanga lakini ikashindikana. Baada ya kama wiki tatu toka shule zimefunguliwa akakutana na mtu aliyemshangaa kwanini hajaenda shule, na alipomwambia kuwa hana mpango wa kwenda Iringa kwa kuwa hakuna bendi, yule mtu alimtaarifu kuwa katika shule ya Mkwawa kuna bendi, na tena ndio inayopiga Iringa mjini. Baada ya kusikia hayo moja kwa moja akaenda kwa baba yake na kumwambia kuwa ameamua kwenda shule, tena kesho yake. Baba yake hakuongeza neno, akampa fedha haraka sana nae  haraka akenda ofisi  za wilaya na kupewa warrant ya kwenda kusafiri kuelekea Iringa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kusafiri nje ya Musoma, lakini alifanikisha safari yake ndefu ya meli hadi Mwanza, kisha kupanda treni Mwanza mpaka Dodoma na kumalizia safari kwa basi toka Dodoma hadi Iringa. Alifika shuleni Mkwawa kama saa kumi na moja jioni, akakuta taratibu ziko nzuri maana akakuta orodha iliyoeleza bweni na chumba alichokuwa kapangiwa kuishi, alikuwa kapangiwa bweni la Magembe West. Haraka akaweka mizigo tu kwenye chumba alichopangiwa na kuulizia bendi iko wapi, akaelekezwa na kukuta mazoezi yanaendelea, akakaa hapo kwa saa nzima na kujua kweli amefika alipotaka.
Pamoja na masomo akaendelea na bendi ambayo kweli iliendelea kupiga Iringa mjini kila wikiendi katika dansi lililojulikana kama bugi, dansi ambalo lilianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Bendi ilijulikana kwa jina la Orchestra Mkwawa na mtindo wao ulikuwa Ligija. Baadhi ya wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Mark Manji na Masanja wakiwa wapiga gitaa la rhythm, Simon Sewando na Kakonko gitaa la solo, Tanganyika mpuliza Sax, John Mkamwa kwenye bass, Danford Mpumilwa na Semboni waimbaji, Zacharia Kakobe kwenye conga na Norman Hiza pia kwenye bezi.
 Mwaka 1972 baada ya kumaliza mitihani ya mwisho bendi ilisafiri hadi Dar es salaam kwenda kurekodi nyimbo zao,bendi ya  Vijana Jazz ndio walikuwa wenyeji wao na wakawaazima hata vyombo walivyoenda kurekodia.
Baada ya kumaliza shule ya Mkwawa kama ilivyokuwa ada wakati huo akaenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, mwaka 1973 baada ya kumaliza JKT akaingia Dar es Salaam akiwa na nia ya kujiunga aidha na Dar es Salaam Jazz au Western Jazz bendi alizozipenda sana, lakini anasema hali ya maisha duni ya wanamuziki aliyoikuta ilimkatisha tamaa kuwa mwanamuziki na kuamua kuendelea na masomo, na kufanya muziki kuwa ni shughuli yake ya ziada, jambo ambalo ameweza kulifanya na wakati huu ambapo amekwisha staafu kazi ameanzisha kituo kikubwa cha kufundisha taaluma mbalimbali za muziki, kule Tabata.
 Mark Manji nae alikuja kuanzisha bendi aliyoiita Chikoike Sound, jina hilo la bendi lilitokana na kufupisha majina ya watoto wake. Simon Sewando , ambaye mpaka sasa ni mwalimu chuo kikuu cha Dar es Salaa idara ya electronics nae alianzisha bendi iliyoitwa TZ Brothers. Muimbaji Danford Mpumilwa nae alikuja kuanzisha bendi iliyokuwa maarufu pale Arusha iliyoitwa Serengeti Band.
Kati ya bendi ambazo Orchestra Mkwawa iliwahi kupiga nazo katika jukwaa moja ni miaka hiyo ni Cuban Marimba ya  Kilaza, Butiama Jazz Band, STC Jazz Band wakati huo ikiwa na wanamuziki akina Marijani Rajabu, Raphael Sabuni, Belino, Ally Rahman na wengineo.

Shule ya Mkwawa ilikuwa na bendi mbili, bendi ya pili walijiita The Midnight Movers, bendi hii ilikuwa ikipiga muziki  wa  kizungu, wakati huo muziki ulioigwa sana na bendi za aina hiyo  ulikuwa ni wa soul, na blues. Hivyo bendi hii ya pili ilipiga muziki wa akina James Brown, Wilson Picket, Otis Redding, Jimi Hendrix na kadhalika, baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika bendi hii walikuwa ni Kafumba, Martin Mhando, Eddie Hans Poppe, Bijoux, Deo Ishengoma na Shaba katika drums. Deo aliyekuwa mwimbaji mmoja wapo alikuwa na mvuto wa pekee kutokana na Afro yake kubwa na uvaaji wa suruali pana za mtindo wa bugaluu ziliomfanya ajulikane mji mzima wa Iringa.   

2 comments:

  1. Deo ishengoma : wimbo aliopenda kuimba wa nafikiri wa Wilson Picket " i am gonna wait till tbe midnight hour.."

    ReplyDelete
  2. mbunifu wa mtindo wa ligija uliokuwa unatumiwa na bendi ya mkwawa ulibuniwa na Jumanne Zegege ambaye hata kwenye nyimbo zao jina la Zegege linatajwa

    ReplyDelete