Saturday, March 19, 2022

MJUE ALLY OMARY JAMWAKA

Ally Omary Jamwaka

Ally Omary Jamwaka alizaliwa katika kijiji cha Malui tarehe 1 Machi 1953, akajiunga na shule ya msingi ya kijijini kwake kuanzia 1960 na kusoma hapo mpaka darasa la saba. Mwaka 1969 akaingia katka jiji la Dar es Salaam kuanza kusaka maisha. Kazi aliyoipenda ilikuwa ni usanii, pengine kwa kuwa  kaka yake Shaaban Omary  alikuwa mpiga drums.  Jamwaka alianza safari yake ya usanii kwa kujiunga na kikundi cha sanaa kilichokuwa na maskani pale Buguruni kikiwa chini ya Mzee Mindu. Wakati yuko huko akakutana na rafiki yake aliyeitwa Adam Bakari, huyu baadae sana alikuja kuwa muimbaji maarufu na kupewa jina la Sauti ya Zege, kwa pamoja wakatengeneza kundi lao waliloliita The Hippies. Kundi hili la muziki wa vijana lilikuwa kazi yake kubwa kwenda kwenye madansi ya bendi kubwa na kuomba 'kijiko'. Huu ulikuwa mtindo ulioenea nchi nzima wakati huo, bendi ndogo zilikuwa zikipita zinapopiga bendi kubwa na kuomba 'kijiko' na hivyo kuruhusiwa kupiga nyimbo kadhaa kwa kutumia vyombo  vya bendi kubwa, wakati bendi hiyo inapumzika,  hii iliwapa wadogo uzoefu na wale waliokuwa wazuri waliweza hata kupata ajira papo hapo. The Hippies makao yao makuu yalikuwa mtaa wa Somali maeneo ya Kariakoo, walikuwa wakipiga muziki wa kukopi bendi za nje zilizotamba wakati huo, hasa zile za Ulaya na Marekani. Jamwaka wakati huo alikuwa tayari akipiga tumba na drums.
 Mwaka 1971 alijiunga na Biashara Jazz iliyokuwa bado mpya kabisa baada ya kubadili jina kutoka STC Jazz. Hii ilikuwa ni bendi iliyokuwa chini ya miliki ya Board of Internal Trade (BIT) ambayo chini yake kulikuwa na mashirika ya umma kama RTC, DABCO, HOSCO, GEFCO na kadhalika. Katika bendi hii aliwakuta akina Raphael Sabuni, Belino, Muddy, na kaka yake Shaaban Omary Jamwaka ambaye alikuwa mpiga drum wa bendi hiyo wakati huo.
Toka kushoto Ally Jamwaka, fundi mitambo wa Biashara Jazz band, kushoto Chamchu mpiga drum wa Biashara Jazz Band, wakiwa wamesimama kwenye uwanja wa Samora Iringa mwaka 1975

 Wengi wa wanamuziki waliokuwa STC Jazz Band walikuwa wasomi kwa hiyo waliacha muziki na kuingia katika kazi nyingine tofauti za kiofisi katika mashirika mbalimbali ya BIT. Ally Jamwaka alikaa katika Biashara Jazz Band iliyokuwa chini ya uongozi wa Juma Ubao aka King Makusa hadi mwaka 1977 alipoamua kujiunga na Tanzania Stars. Bendi hii ilikuwa na makao yake katika ukumbi maarufu miaka hiyo iliyoitwa Margot ambayo ilikuwa katikati ya Jiji pembeni ya barabara ya Samora. Ukumbi huu ulikuwa maarufu sana kwani kulikuwa na muziki kila siku ya wiki mpaka usiku wa manane, mabaharia walikuwa wakisha kutia nanga Dar es Salaam ,walielekea Margot ambapo palikuwa ni mahala penye starehe za kila aina, hapo ndipo pia kilikuwa kituo kikubwa cha 'machangudoa' ambao walikuwa wakitega nyavu zao kuwasubiri wateja.  Kufika kwake bendi hiyo alipishana na wanamuziki maarufu ambao wote ni marehemu, Haruna Lwali mpiga tumba na Joseph Mulenga mpiga gitaa wakahamia bendi iliyokuwa ikipiga ukumbi jirani wa Gateways ambapo kulikuwa na bendi maarufu ya Orchestra Santa Fe.
Baadhi ya wanamuziki waliokuweko katika bendi ya Tanzania Stars wakati huo walikuwa Joseph Emmanuel muimbaji na mpiga gitaa na mtunzi wa wimbo uliotamba wakati wake ulioitwa 'Mawazo', Hussein Sadiki, Yahaya Bushiri nae pia alikuwa mpiga gitaa mzuri sana. Bendi hii ilikuwa inapiga muziki kutoka nchi mbalimbali duniani hasa ukikumbuka kuwa walikuwa na wateja mabaharia kutoka kila kona ya dunia, hivyo ukiingia Margot ungeweza kusikia nyimbo cha Kichina, Kihindi, Kigiriki na kadhalika. Baada ya ukumbi huu kuchukuliwa na Chama Cha Ushirika, bendi pia ikachukuliwa na ndipo ilipozaliwa ile bendi maarufu ya Washirika Tanzania Stars.
 Jamwaka aliendelea kupigia Tanzania Stars mpaka mwaka 1979 ambapo bendi ya Mlimani Park ilimfukuza kazi mpiga tumba wake aliyekuwa akiitwa Tanzania One, Haruna Lwali, na hapo Abel Balthazar alimfuata Jamwaka na kumkaribisha Mlimani Park Orchestra. Mlimani Park  ilikuwa chini ya TTTS, shirika la umma lililokuwa likiendesha shughuli za usafirishaji na hasa wa taxi. Bendi ilipewa huduma nzuri sana na shirika hili na kufikia kuwa moja ya bendi kubwa nchini, nyimbo zake za wakati ule bado zinaheshimika katika nyanja za muziki hata leo. Ukumbi wa Msasani Beach Club ulikuwa mmoja wa mali za TTTS, na bendi ya Mlimani Park ndio iliyojenga ukumbi huo kwa kutumia mapato ya kila Jumatano kuelekezwa kwenye ujenzi wa ukumbi huo. Baada ya ukumbi huo kukamilika wanamuziki wakiwa na imani ambayo baadae ilikuja kuonekana potofu, waliamua kutumia fedha yao ya kila Jumatano kuanza kujenga ukumbi wa bendi yao uliokuwa Mpakani eneo linalojulikana kama DDC. Ujenzi ulifika mahala ukadorora na kufa kabisa. Hapa kuna maelezo kuwa  bendi ilipigwa 'kipapai' na bendi pinzani iliyokuwa jirani ili isikamilishe ujenzi maana ingekuwa bendi ya kwanza Tanzania kuwa na ukumbi wake  wa kisasa. Kama ni kweli walipigwa kipapai, basi hilo lilifanikiwa kwani ukumbi haukukamilika mpaka leo . Mwaka 1982 mali za TTTS kama vile bendi na ukumbi wa Mpakani ukahamishiwa Dar es Salaam Development Corporation (DDC), awali kulikuweko na wazo kuwa bendi ihamishwe iwe chini ya ATC maana wakati huo Air Tanzania walikuwa na Club yao nzuri tu, lakini ikaonekana DDC walikuwa na kumbi kama vile DDC Kariako, DDC Magomeni, DDC Keko na hivyo bendi ingefanya kazi kwa ufanisi zaidi huko, bendi na wanamuziki wakauzwa DDC. Mambo yalibadilika sana kwa bendi hii kwani menejiment mpya haikuthamini bendi, na hata matamko ya mara kwa mara toka kwa Meneja Mkuu wa DDC wakati huo yaliudhi sana wanamuziki kwani si mara moja alikuwa akiwatamkia wanamuziki kuwa bendi ikifa hana tatizo maisha yataendelea. Hili lilipunguza sana morali ya wanamuziki, hivyo basi 1985 awamu ya kwanza ya kundi kubwa la wanamuziki liliondoka DDC Mlimani Park Orchestra na kujiunga na Orchestra Safari Sound na kuanzisha kundi la International Orchestra Safari Sound iliyokuwa na mtindo wa Ndekule, ambapo walikuweko Abel Barthazar, Muhidin Maalim Gurumo, Ally Makunguru, Ngosha, Kassim Rashid wakiungana na wenzao akina Skassy Kasambula walianzisha moto mkali uliotikisa nchi. Katika awamu ya pili ya wimbi la wanamuziki wa Sikinde kwenda OSS, Ally Jamwaka pia alikuweko, wakati huo akiwa na Fresh Jumbe, Cosmas Chidumule,Hamis Juma Kinyasi, Bobchipe Chipembele wakasindikizana na Michael Bilali ambaye alirudishwa Sikinde mapema kwa nguvu ya wapenzi wa Sikinde waliochanga fedha na kulipa fedha alizokuwa kachukua toka uongozi wa OSS.  

No comments:

Post a Comment