Tuesday, April 12, 2022
MWAKA 1973 YALIFANYIKA MASHINDANO YA BENDI BORA TANZANIA UNAJUA MSDHINDI ALIKUWA NANI?
Sunday, March 27, 2022
TUMETIMIZA MIAKA 16 TOKA KIFO CHA TX MOSHI WILLIAM, SAUTI YAKE INAENDELEA KUSIKIKA
Msondo wakiwa mazoezini katika ukumbi wa Amana |
Moshi William alizaliwa mwaka 1958 Hale Mwakinyumbi Korogwe. Hale alikuwepo mwanamuziki maarufu aliyekuwa akiitwa Mzee Masongi, yeye alikuwa na bendi, na bendi hii ilikuwa chanzo cha wanamuziki wengi maarufu akiwemo Moshi William. Jina halisi la Moshi William lilikuwa Shaaban Ally Mhoja lakini alikuja kubadili na kuitwa Moshi William kutokana na kuja kulelewa na baba mwingine. Bendi ambazo TX Moshi William aliwahi kupitia baada ya kutoka Hale zilikuwa ni Safari Trippers wana Sokomoko, UDA Jazz Band wana Bayankata, na Polisi Jazz Band wana Vangavanga, na hatimae JUWATA Jazz Band wana Msondo Ngoma, bendi aliyodumu nayo mpaka kifo. Kati ya nyimbo zake za kwanza mara baada ya kujiunga na JUWATA zilikuwa Ajuza, Ashibaye na Asha Mwanaseif, wimbo huu wa tatu alimtungia mkewe, baada ya hapo alitunga nyimbo nyingi sana na kwa ujumla alirekodi album karibu 13. Sifa ya Moshi kuanza kuitwa TX ilitungwa na marehemu Julius Nyaisanga aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam. Zama hizo, serikali ilikuwa imeweka sheria kuwa magari ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi nchini yawekwe namba ambazo zilianzia na TX kuonyesha ni ya Kimataifa, hivyo TX ikageuka kuwa nembo ya sifa ya kuwa na hadhi ya Kimataifa. Kutokana na umahiri wa Moshi katika kutunga na kuimba, Nyaisanga akampachika kisifa cha TX. Na hakika umahiri wake ulijidhihirisha kwani kwa miaka mitatu mfululizo kati ya mwaka 2003 mpaka 2005, TX Moshi William alitunukiwa tuzo za utunzi bora na Kilimanjaro Music Awards. Pamoja na Msondo, Moshi aliwahi kurekodi nyimbo nyingi akiwa na wanamuziki wenzake nje ya Msondo, kwa utaratibu ulikuwa maarufu kwa jina la zing zong au wengine waliita zozing. Moshi alifariki siku ya tarehe 29 March 2006 katika wodi ya Sewa Haji baada ya operesheni ya kuondoa chuma katika mguu wake uliovunjika kwenye ajali. Alifariki saa tatu kasoro robo asubuhi na kuzikwa siku hiyohiyo katika makaburi ya Keko Machungwa.
Mungu Amlaze Pema Shaaban Ally Mhoja Kishiwa - TX Moshi William
Saturday, March 26, 2022
DR UFUTA MPIGA SOLO WACUBAN MARIMBA NA TK LUMPOPO AFARIKI DUNIA
Dr Ufuta uzeeni |
Ufuta alizaliwa Utuu Misheni Mahenge karibu miaka 70 iliyopita, alianzisha bendi yake ya kwanza mwaka 1966, bendi yake aliyoiita Taifa Jazz, bendi hii iliyokuwa na waimbaji wanne, ilikuwa haina hata chombo kimoja kilichotumia umeme. Kati ya mwaka 1966 na 1968 hiyo ndiyo ikawa bendi moja maarufu pale Mahenge. Mbunge wa jimbo la Mahenge wakati huo Mheshimiwa Ilanga, aliwanunulia vyombo vichache vijana hawa na hii ikawa bendi rasmi iliyokuwa ikisindikizana na Mbunge huyo katika kampeni zake mbalimbali.
Mwaka 1968 kaka yake Lucas Simon alimshawishi aachane na bendi
yake ya Taifa Jazz na kujiunga na Cuban Marimba wakati huo ikiwa chini ya Juma
Kilaza. Na bendi ya Cuban aliweza kufika mpaka Nairobi ambako wakati wa
kurekodi fundi mitambo mmoja pale studio alianza kumuita Dokta kutokana na upigaji wake
mahiri na cheo hicho amebaki nacho mpaka umauti wake.
Picha hii ilikuwa ni ganda la moja ya santuri ya nyimbo za Cuban Marimba. Dr Ufuta ni aliyevaa miwani . Wa kwanza kulia waliosimama ni Juma Kilaza. |
Mwaka 1974 kuliktokea kutokuelewana kati ya wanamuziki wa
Cubana Marimba na wamiliki wa bendi hiyo ambao walikuwa warithi wa marehemu Salum
Abdallah, mtiti huo ukasababisha Juma Kilaza, Joakim Ufuta, Juma Sangula, Ally Said na Hemedi Maneti kuihama bendi hiyo na kuunda TK Lumpopo, na hapo walitoa nyimbo nyingi za kukumbukwa, wimbo wao wa kwanza ulikuwa Maisha ya
Sasa. Katika bendi hii pia kukatokea kutokuelewana kwa ajili ya maslahi, Hemedi
Maneti akatimka na kujiunga na Vijana
Jazz Band, Dr Ufuta akarudi tena Cuban Marimba. Baada ya muda kama ilivyokuwa kawaida miaka ile, bendi ilianza ziara ya mikoa mbalimbali Kenya. Wakiwa Naivasha kukatokea kukorofishana tena, wenzie
wakarudi Tanzania yeye akabaki akitafuta maisha nchini Kenya.
Monday, March 21, 2022
MANENO UVURUGE AENDELEA NA SAFARI ZAKE ZA MUZIKI
Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo |
Wakati huohuo katika ukumbi wa Lango la Chuma Mabibo makao makuu ya bendi ya Mambo Bado, mambo yalikuwa magumu, bendi hiyo ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, waimbaji Lodji Mselewa na Nana Njige nao wakaenda kujiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana, kiongozi wa Mambo Bado Tchimanga Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa ikaingia katika hali mbaya zaidi kwani Assossa aliiacha tena Mambo Bado ikafa rasmi.
Saturday, March 19, 2022
MJUE ALLY OMARY JAMWAKA
Ally Omary Jamwaka |
Toka kushoto Ally Jamwaka, fundi mitambo wa Biashara Jazz band, kushoto Chamchu mpiga drum wa Biashara Jazz Band, wakiwa wamesimama kwenye uwanja wa Samora Iringa mwaka 1975 |
Wengi wa wanamuziki waliokuwa STC Jazz Band walikuwa wasomi kwa hiyo waliacha muziki na kuingia katika kazi nyingine tofauti za kiofisi katika mashirika mbalimbali ya BIT. Ally Jamwaka alikaa katika Biashara Jazz Band iliyokuwa chini ya uongozi wa Juma Ubao aka King Makusa hadi mwaka 1977 alipoamua kujiunga na Tanzania Stars. Bendi hii ilikuwa na makao yake katika ukumbi maarufu miaka hiyo iliyoitwa Margot ambayo ilikuwa katikati ya Jiji pembeni ya barabara ya Samora. Ukumbi huu ulikuwa maarufu sana kwani kulikuwa na muziki kila siku ya wiki mpaka usiku wa manane, mabaharia walikuwa wakisha kutia nanga Dar es Salaam ,walielekea Margot ambapo palikuwa ni mahala penye starehe za kila aina, hapo ndipo pia kilikuwa kituo kikubwa cha 'machangudoa' ambao walikuwa wakitega nyavu zao kuwasubiri wateja. Kufika kwake bendi hiyo alipishana na wanamuziki maarufu ambao wote ni marehemu, Haruna Lwali mpiga tumba na Joseph Mulenga mpiga gitaa wakahamia bendi iliyokuwa ikipiga ukumbi jirani wa Gateways ambapo kulikuwa na bendi maarufu ya Orchestra Santa Fe.
Baadhi ya wanamuziki waliokuweko katika bendi ya Tanzania Stars wakati huo walikuwa Joseph Emmanuel muimbaji na mpiga gitaa na mtunzi wa wimbo uliotamba wakati wake ulioitwa 'Mawazo', Hussein Sadiki, Yahaya Bushiri nae pia alikuwa mpiga gitaa mzuri sana. Bendi hii ilikuwa inapiga muziki kutoka nchi mbalimbali duniani hasa ukikumbuka kuwa walikuwa na wateja mabaharia kutoka kila kona ya dunia, hivyo ukiingia Margot ungeweza kusikia nyimbo cha Kichina, Kihindi, Kigiriki na kadhalika. Baada ya ukumbi huu kuchukuliwa na Chama Cha Ushirika, bendi pia ikachukuliwa na ndipo ilipozaliwa ile bendi maarufu ya Washirika Tanzania Stars.
Jamwaka aliendelea kupigia Tanzania Stars mpaka mwaka 1979 ambapo bendi ya Mlimani Park ilimfukuza kazi mpiga tumba wake aliyekuwa akiitwa Tanzania One, Haruna Lwali, na hapo Abel Balthazar alimfuata Jamwaka na kumkaribisha Mlimani Park Orchestra. Mlimani Park ilikuwa chini ya TTTS, shirika la umma lililokuwa likiendesha shughuli za usafirishaji na hasa wa taxi. Bendi ilipewa huduma nzuri sana na shirika hili na kufikia kuwa moja ya bendi kubwa nchini, nyimbo zake za wakati ule bado zinaheshimika katika nyanja za muziki hata leo. Ukumbi wa Msasani Beach Club ulikuwa mmoja wa mali za TTTS, na bendi ya Mlimani Park ndio iliyojenga ukumbi huo kwa kutumia mapato ya kila Jumatano kuelekezwa kwenye ujenzi wa ukumbi huo. Baada ya ukumbi huo kukamilika wanamuziki wakiwa na imani ambayo baadae ilikuja kuonekana potofu, waliamua kutumia fedha yao ya kila Jumatano kuanza kujenga ukumbi wa bendi yao uliokuwa Mpakani eneo linalojulikana kama DDC. Ujenzi ulifika mahala ukadorora na kufa kabisa. Hapa kuna maelezo kuwa bendi ilipigwa 'kipapai' na bendi pinzani iliyokuwa jirani ili isikamilishe ujenzi maana ingekuwa bendi ya kwanza Tanzania kuwa na ukumbi wake wa kisasa. Kama ni kweli walipigwa kipapai, basi hilo lilifanikiwa kwani ukumbi haukukamilika mpaka leo . Mwaka 1982 mali za TTTS kama vile bendi na ukumbi wa Mpakani ukahamishiwa Dar es Salaam Development Corporation (DDC), awali kulikuweko na wazo kuwa bendi ihamishwe iwe chini ya ATC maana wakati huo Air Tanzania walikuwa na Club yao nzuri tu, lakini ikaonekana DDC walikuwa na kumbi kama vile DDC Kariako, DDC Magomeni, DDC Keko na hivyo bendi ingefanya kazi kwa ufanisi zaidi huko, bendi na wanamuziki wakauzwa DDC. Mambo yalibadilika sana kwa bendi hii kwani menejiment mpya haikuthamini bendi, na hata matamko ya mara kwa mara toka kwa Meneja Mkuu wa DDC wakati huo yaliudhi sana wanamuziki kwani si mara moja alikuwa akiwatamkia wanamuziki kuwa bendi ikifa hana tatizo maisha yataendelea. Hili lilipunguza sana morali ya wanamuziki, hivyo basi 1985 awamu ya kwanza ya kundi kubwa la wanamuziki liliondoka DDC Mlimani Park Orchestra na kujiunga na Orchestra Safari Sound na kuanzisha kundi la International Orchestra Safari Sound iliyokuwa na mtindo wa Ndekule, ambapo walikuweko Abel Barthazar, Muhidin Maalim Gurumo, Ally Makunguru, Ngosha, Kassim Rashid wakiungana na wenzao akina Skassy Kasambula walianzisha moto mkali uliotikisa nchi. Katika awamu ya pili ya wimbi la wanamuziki wa Sikinde kwenda OSS, Ally Jamwaka pia alikuweko, wakati huo akiwa na Fresh Jumbe, Cosmas Chidumule,Hamis Juma Kinyasi, Bobchipe Chipembele wakasindikizana na Michael Bilali ambaye alirudishwa Sikinde mapema kwa nguvu ya wapenzi wa Sikinde waliochanga fedha na kulipa fedha alizokuwa kachukua toka uongozi wa OSS.
Thursday, March 17, 2022
MANENO Uvuruge mwanamuziki toka familia ya wapiga magitaa
Maneno Uvuruge |
Kuna familia nyingine hutokea kuwa na wanamuziki wengi tu,
mfano ni familia ya maarufu ya mwanamuziki marehemu Michael Jackson. Watoto
wote wa familia hiyo walikuja kuwa wanamuziki maarufu, wavulana wakaweza
kuanzisha kundi la The Jackson 5, baadae hata dada zao Latoya na Janet Jackson
nao wakaja kujitokeza kuwa wanamuziki waliokuja kujipatia mafanikio makubwa
katika fani hii. Kuna familia kadhaa zenye sifa hizo hata hapa Tanzania, kuna
familia ya Kanuti, Muumba na Uvuruge ni mifano ya jambo hili. Leo tumzungumzie
Maneno Uvuruge kutoka familia ya akina Uvuruge.
Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika
familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka
ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa
bendi Tanzania.
Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka kutoka baamoja na kwenda nyingine na gitaa lake na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji. Hayakuwa maisha rahisi
Jumanne Uvuruge mtunzi wa wimbo maarufu wa Georgina uliopigwa na Safari TRppers na kuimbwa na Marijani Rajabu |
Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne
alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa kaka yake Stamili alifundishwa na
Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka
yake waliefuatana kuzaliwa..
Stamili Uvuruge hapa akiwa jukwaani wakati akiwa bendi ya Bima Lee |
Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, kila baba yao alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake
Maneno Kushoto akiwa na kaka yake Huluka |
Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Generation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Mwanamuziki muimbaji marehemu Freddy Benjamin ndie aliyemshauri Maneno kujiunga na bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia, ambako Maneno alijaribiwa kama ilivyokuwa kawaida wakati ule kwa mwanamuziki mgeni, lakini pamoja na kuweza kupiga gitaa vizuri alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi hiyo wakati huo. Baada ya hapo Freddy alimuombea kazi katika bendi ya Super Rainbow, bendi ambayo iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na katika bendi hiyo Maneno akakutana na wanamuziki wakubwa wakati huo kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky na Mzee Bebe. Wakati huu Eddy Sheggy ambaye alikuja kuipaisha bendi hiyo kwa wimbo wa Milima ya Kwetu alikuwa hajajiunga na bendi hii wakati huo. Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga. Katika kipindi hichohicho bendi iliyokuwa ikiongozwa na Tchimanga Assossa, Orchestra Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige nao pia wakaja kujiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi..
Huluka Uvuruge akiwa jukwaani Msondo Music Group |
Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Marehemu Mzee Juma Mrisho maarufu pia kama Ngulimba wa Ngulimba, wakati huo Urafiki Jazz Band nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri marehemu Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waimbaji Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe nao pia wakajiunga na bendi hiyo. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa wa kupiga gitaa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis Original, alichukuliwa na bendi hii ili awe mpiga gitaa la rhythm, alijiunga na wapiga rhythm wawili mahiri Mbwana Cox na Omari Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba. Siku moja mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole aliyekuwa mmiliki wa bendi ya Afriso na wakamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge, Kiniki Kieto (mwimbaji), Comson Mkomwa (saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwisha pokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba kwanza alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu bendi hiyo, kwani Mzee Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoaManeno Maquis kwa mara ya pili na kuhamia nae Afrisongoma. Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate huko Uingereza waweze kutengeneza kundi la muziki huko, lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda lakini rafiki zake akiwemo Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa......itaendelea
MARK MANJI WA ORCHESTRA MKWAWA wana Ligija
Waliochuchumaa na magitaa kushoto ni Simon Sewando, kulia John Mkamwa.Aliyesimama wa kwanza kulia Mark Manji.
Mark Manji alianza
kupenda sana kusikiliza wapigaji wa magitaa makavu(accoustic)
maarufu kama magalaton, waliokuwa kijiji kwao Chitare,
Musoma. Upigaji wa magitaa makavu ulikuwa maarufu katika maeneo mengi ya Musoma labda kutokana na gitaa kuwa na kufanana na Ritungu au kwa kuwa Musoma ilikuwa jirani na Kenya ambako kulikuwa na wapiga magitaa maarufu kama
akina George Mukabi, John Mwale na kadhalika. Mark alinambia kuwa anakumbuka toka yuko darasa la tatu alianza
kuwa na hamu sana ya kuwa mwanamuziki. Hamu hii iliongezeka
alipoingia kidato cha kwanza Alliance Secondary pale Musoma ambako kila
Jumamosi alianza kwenda kuchungulia wakati bendi mbalimbali zikipiga
Musoma mjini. Bendi aliyokuwa maarufu wakati huo ilikuwa inaitwa Eleven Stars
Band, pamoja na kuwa bendi ilikuwa na watu sita iliitwa Eleven Stars kwa kuwa
mwenye bendi pia alikuwa anaendesha club ya mpira iliyokuwa na jina hilo. Bendi
hiyo iliyokuwa na mpiga solo kutoka Kigoma, mpiga bezi Mkongo, mwimbaji Mkongo
na Watanzania wengine wawili, mmoja wa waimbaji alikuwa akiitwa Dode ambaye
kwake ndiko vyombo vya bendi vilikuwa vinatunzwa. Huyu
Dode, ambaye baadae sana Mark aligundua ni kifupi cha Deusdedit alikuwa akiishi
karibu na kaka yake mmoja, hivyo akaomba kujifunza gitaa na taratibu akajifunza
gitaa la rhythm. Hizi juhudi zake za kujifunza muziki ziliwahi hata kusababisha
kufukuzwa shule wakati akiwa form II, lakini hatimae kwa mbinde alimaliza kidato cha nne.
Mwaka 1970 akawa amechaguliwa kujiunga na shule ya
sekondari ya Mkwawa, katika kumbukumbu zake hakuwahi kusikia kuwa
Iringa kulikuwa na bendi kwa hiyo alikataa kwenda kuendelea na shule kwa kuwa
alitaka kuwa mwanamuziki. Akawa na ndoto za aidha kwenda kusoma Tanga,
Morogoro, au Tabora maana huko alijua kulikuwa na bendi kubwa na maarufu. Pamoja na baba yake
kujitahidi kumshawishi kwenda kusoma Mkwawa alikataa katakata akitaka
kujiunga na muziki au aende kusoma kwenye mji wenye bendi.
Alijitahidi hata kubadilishana na mwenzie aliyechaguliwa kusoma Galanos Tanga
lakini ikashindikana. Baada ya kama wiki tatu toka shule zimefunguliwa
akakutana na mtu aliyemshangaa kwanini hajaenda shule, na alipomwambia kuwa
hana mpango wa kwenda Iringa kwa kuwa hakuna bendi, yule mtu alimtaarifu kuwa
katika shule ya Mkwawa kuna bendi, na tena ndio inayopiga Iringa mjini. Baada
ya kusikia hayo moja kwa moja akaenda kwa baba yake na kumwambia kuwa ameamua
kwenda shule, tena kesho yake. Baba yake hakuongeza neno, akampa fedha haraka
sana nae haraka akenda ofisi za wilaya na kupewa warrant
ya kwenda kusafiri kuelekea Iringa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kusafiri nje ya
Musoma, lakini alifanikisha safari yake ndefu ya meli hadi Mwanza, kisha kupanda treni Mwanza
mpaka Dodoma na kumalizia safari kwa basi toka Dodoma hadi Iringa. Alifika shuleni Mkwawa kama saa kumi na
moja jioni, akakuta taratibu ziko nzuri maana akakuta orodha iliyoeleza bweni
na chumba alichokuwa kapangiwa kuishi, alikuwa kapangiwa bweni la Magembe West. Haraka akaweka
mizigo tu kwenye chumba alichopangiwa na kuulizia bendi iko wapi, akaelekezwa
na kukuta mazoezi yanaendelea, akakaa hapo kwa saa nzima na kujua kweli amefika
alipotaka.
Pamoja na masomo akaendelea na bendi ambayo kweli iliendelea kupiga
Iringa mjini kila wikiendi katika dansi lililojulikana kama bugi, dansi ambalo lilianza saa
nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Bendi ilijulikana kwa jina la Orchestra Mkwawa na mtindo wao ulikuwa Ligija. Baadhi ya wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Mark Manji na Masanja wakiwa wapiga gitaa la rhythm, Simon Sewando na Kakonko gitaa la solo, Tanganyika mpuliza Sax, John
Mkamwa kwenye bass, Danford Mpumilwa
na Semboni waimbaji, Zacharia Kakobe kwenye conga na Norman Hiza pia kwenye bezi.
Mwaka 1972 baada ya kumaliza
mitihani ya mwisho bendi ilisafiri hadi Dar es salaam kwenda kurekodi nyimbo zao,bendi
ya Vijana Jazz ndio walikuwa wenyeji wao na wakawaazima hata vyombo
walivyoenda kurekodia.
Baada ya kumaliza shule ya Mkwawa kama ilivyokuwa ada
wakati huo akaenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, mwaka 1973 baada ya
kumaliza JKT akaingia Dar es Salaam akiwa na nia ya kujiunga aidha na Dar es
Salaam Jazz au Western Jazz bendi alizozipenda sana, lakini anasema hali ya maisha duni ya wanamuziki aliyoikuta ilimkatisha tamaa kuwa mwanamuziki na kuamua kuendelea na
masomo, na kufanya muziki kuwa ni shughuli yake ya ziada, jambo ambalo ameweza
kulifanya na wakati huu ambapo amekwisha staafu kazi ameanzisha kituo kikubwa
cha kufundisha taaluma mbalimbali za muziki, kule Tabata.
Mark Manji nae alikuja kuanzisha bendi aliyoiita Chikoike Sound, jina hilo la bendi lilitokana na kufupisha majina ya watoto wake. Simon Sewando , ambaye mpaka sasa ni mwalimu chuo kikuu cha Dar es Salaa idara ya electronics nae alianzisha bendi iliyoitwa TZ Brothers. Muimbaji Danford Mpumilwa nae alikuja kuanzisha bendi iliyokuwa maarufu pale Arusha iliyoitwa Serengeti Band.
Kati ya bendi ambazo Orchestra
Mkwawa iliwahi kupiga nazo katika jukwaa moja ni miaka hiyo ni Cuban Marimba ya Kilaza,
Butiama Jazz Band, STC Jazz Band wakati huo ikiwa na wanamuziki akina Marijani Rajabu, Raphael Sabuni, Belino, Ally Rahman na wengineo.
Shule ya Mkwawa ilikuwa na
bendi mbili, bendi ya pili walijiita The Midnight Movers, bendi hii ilikuwa ikipiga muziki wa kizungu,
wakati huo muziki ulioigwa sana na bendi za aina hiyo ulikuwa ni wa soul,
na blues. Hivyo bendi hii ya pili ilipiga muziki wa akina James Brown, Wilson
Picket, Otis Redding, Jimi Hendrix na kadhalika, baadhi ya wanamuziki
waliokuwemo katika bendi hii walikuwa ni Kafumba, Martin Mhando, Eddie Hans Poppe, Bijoux, Deo Ishengoma na Shaba katika
drums. Deo aliyekuwa mwimbaji mmoja wapo alikuwa na mvuto wa pekee kutokana na
Afro yake kubwa na uvaaji wa suruali pana za mtindo wa bugaluu ziliomfanya ajulikane mji mzima wa
Iringa.
Monday, April 30, 2018
Saturday, April 14, 2018
MUZIKI WETU UMETOKA SAFARI NDEFU part 1
Saturday, January 6, 2018
TASNIA YA MUZIKI 2017 KWA UFUPI
Thursday, June 29, 2017
HATIMAE MWANAMUZIKI MKONGWE BROTHER ZENNO AZIKWA
Binti pekee wa marehemu akiwa na mumewe wakiweka shada la maua |
Baadhi ya wanamuziki waliohudhuria mazishi ya Brother Zeno |
Aliyekaa ni Abdallah Mbosanga mmoja ya wanamuziki wawili waliobaki hai wa bendi ya Bima Jazz band ya kwanza. Mwingine ni Duncan Ndumbalo |
Tuesday, June 27, 2017
BROTHER ZENNO AFARIKI DUNIA
RIP Brother Zerno |