Kuanzia
mwaka 2012 nimekuwa nikimaliza mwaka kwa kuandika makala ya mtizamo wangu
kuhusu hali ya muziki katika mwaka uliokwisha. Na mwaka 2017 ndio huoo
umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Kama
ilivyokuwa kwa miaka mingi sasa, anga za muziki wa nchi yetu zilitawaliwa na
muziki wa Bongoflava. Muziki ambao kwa asilimia kubwa hutengenezwa studio,
hakuna shaka watu wengi nchini na nchi
jirani wametokea kuupenda sana muziki huu. Katika mkutano ulifanyika wiki
chache zilizopita, kiongozi mmoja wa mambo ya Hakimiliki kutoka Kenya alisema asilimia kubwa ya muziki
unaopigwa kwenye vyombo vyao vya utangazaji ni wa kutoka Tanzania. Imefika
mahali mpaka wasanii wa huko wameanza kudai muziki wa Tanzania upunguzwe ili
wao waweze kupata nafasi zaidi katika redio na luninga zao. Inachekesha kuwa
kilio kama hichohicho kinasikika kwa wanamuziki wa aina tofauti nchini
kuhusiana na ‘kufunikwa’ na Bongofleva. Wasanii wa Bongofleva wameendelea
kupata tuzo kutoka kwa taasisi mbalimbali za Kimataifa, na hata wengine kuingia
mikataba na kampuni kubwa za kimataifa za usambazaji, na kwa picha hii
Bongoflava itaendelea kutawala anga za muziki hata mwaka ujao. Muziki ambao
tunaweza kusema chanzo chake ni muziki wa mchiriku wenye asili ya ngoma za
Kizaramo, maarufu kama muziki wa singeli nao ulikuja juu sana kwa miezi
michache ya mwaka huu, japokuwa ule moto wake unapungua, inawezekana muziki huo
unajimaliza wenyewe kutokana na mashahiri yanayotumika katika nyimbo hizo, na
hata video zinazo ambatana nazo, lakini hakika muziki huu ni ubunifu unaoweza
kuitwa muziki wa asili ya Kitanzania bila shaka yoyote. Hakukuwa na mambo ya
kushtua sana katika muziki wa Taarab hali hiyohiyo pia ilionekana katika muziki
wa dansi. Bendi kadhaa na vikundi vya taarab vilitangaza kuanzishwa lakini havikuja
na kitu kipya cha kuweza kuleta mshtuko katika tasnia, kifupi hakukuwa na jambo
lolote chanya la kukumbukwa kutoka upande huo kwa mwaka 2017. Pamoja na kuwa
haukuonekana kuwa umeshuka lakini pia hakukuwa na dalili za kupanda kwa muziki
wa Enjili, kwenye sanaa usipopanda ujue umeshuka. Muziki wa kwaya ulianza
kujitokeza zaidi hasa kwenye kutoa elimu ya mambo mbalimbali ya kijamii na pia
kurudia nafasi yake ya zamani ya kusifia viongozi mbalimbali, kazi ambayo kwaya
ilikuwa ikifanya toka miaka ya mwanzoni baada ya Uhuru. Kwaya kadhaa ziliweza
kutengeneza video ambazo zimekuwa zikionekana kwenye luninga, japo ni wazi
hazikutengenezwa kwa ajili ya biashara. Kuna kundi la wanamuziki ambao wao husema
huwa hawana nia kabisa ya kusikika kwenye vyombo vya utangazaji vya hapa
nchini, wao hutengeneza muziki kwa ajili ya maonyesho ya nje ya nchi.
Wanamuziki hawa wameendelea kuwa na safari za kwenda nje kupiga muziki wao
katika matamasha ya kimataifa bila kuhangaika kutambulisha kazi zao hapa
nchini, sababu kubwa ambayo wamekuwa wakitoa ni urasimu wa taratibu za muziki
kusikika katika vyombo vyetu vya utangazaji.
Hivyo badala ya kupoteza muda kupingana na mfumo, wao wameendelea na
shughuli za kujitambulisha nje, ni nadra habari zao kuonekana kwenye vyombo vya
habari vya nchini japo wanazunguka nchi mbalimbali duniani wakipiga muziki
unaotambulika huko kuwa ni wa Kitanzania.
Muziki wa asili ni kazi ambayo
inaonekana ni kwa ajili ya watalii na shughuli maalumu za kiserikali au sherehe
za kifamilia. Picha hii inadanganya kwani muziki asili unaendelea nchini mijini
na vijijini japo hauonekani kwenye vyombo vya utangazaji, labda pale ambapo ni
kiburudisho cha viongozi. Muziki wa asili uko katika makundi mawili, uko muziki
ambao unafanywa na wasanii ukiwa ni mchanganyiko wa ngoma mbalimbali ili kuweza
kuvutia biashara, na uko muziki asili ambao huchezwa na kuimbwa na wenye kabila
lao kwa upenzi wa utamaduni wao. Kwa kuwa hauonekani wala kuzungumziwa sana
kwenye vyombo vya utangazaji, unaweza ukadhani haupo au haupendwi lakini hilo
si sahihi. Maelfu ya vijana nchi nzima wanacheza na kupiga ngoma za kiasili kwa
ufasaha mkubwa.
Kumekuweko na matamasha kadhaa ya muziki
nchini, kama tamasha la Fiesta, Marahaba, Tulia Traditional Dance Festival, Sauti
za Busara, Karibu Music Festival na kadhalika, lakini matamasha haya ilikuwa ni
nafasi ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanamuziki walioko nchini. Wilaya,
mikoa nayo ingeweza kutayarisha matamasha yake ya utamaduni ingekuwa sehemu
nzuri sana ya kuendeleza utamaduni, wasanii kubadilishana ujuzi, kuibua vipaji
na kuleta burudani kwa wananchi kwa
ujumla. Ufadhili katika shughuli za muziki umekua ukiangalia sana faida za
kibiashara, kumekuwa na kampuni chache ikiwa zipo ambazo zimefadhili matamasha kwa
nia tu ya kuendeleza muziki. Matamasha mengine yamekuwa yakitegemea ufadhili wa
balozi mbalimbali za nje kuwezesha kufanya maonyesho ya muziki wetu. Ni
kichekesho kwa kweli. Hata zile kampuni ambazo ni maarufu nje ya Tanzania kwa
kuunga mkono shughuli za sanaa, kwa namna ya ajabu zikiwa Tanzania ghafla
zinakuwa na msimamo tofauti.
Maeneo ya
kufanya shughuli za muziki yamezidi kupungua, mengine yamevunjwa na maeneo
kuachwa wazi kama vile eneo lilokuwa DDC Magomeni na Mango Kinondoni, mengine
yamekuwa makanisa na kadhalika. Pamoja na kuwa kulikuwa na wimbi la kujenga
kumbi ambazo hutangazwa kuwa ni ‘multi purpose’, kumbi hizi haswa zilijengwa
kwa ajili ya kufanyia shughuli za harusi, kuna mambo kadhaa ambayo si rafiki
kwa muziki katika kumbi hizi, na hata wenye kumbi hukataa kumbi zao kutumika
kwa shughuli za muziki hasa wa dansi.
Katika mwaka 2017 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Dr Harrison Mwakyembe amekuwa na mikutano mingi na wanamuziki, jambo jema
kinachosubiriwa 2018 ni matokeo ya mikutano hii. Ushauri kwa wanamuziki ambao
muziki wao unajikongoja, kuna umuhimu wa kutafuta majibu ya kisayansi kwanini
hali iko hivyo. Majibu mepesi ya kulaumu vyombo vya habari, serikali na wadau
wengine, kamwe hayata saidia katika kuleta mabadiliko.
No comments:
Post a Comment