Saturday, April 14, 2018

MUZIKI WETU UMETOKA SAFARI NDEFU part 1


Ukifungulia redio siku hizi utakumbana na aina mbalimbali za muziki ambao washiriki wake ni Watanzania, utasikia taarab, bongofleva, rumba, rege, muziki wa asili na muziki wa kisasa wenye vionjo vya kiasili na kadhalika. Je hapo mwanzo ilikuwaje? Kupata picha italazimu turudi  nyuma kabla ya kuanzishwa kwa ukoloni wa Kijerumani. Watu wa nchi hii waliishi kwa makundi ya kikabila na hivyo kila kundi kuendeleza utamaduni wake na sanaa zake ikiwemo ‘muziki’. 

Nimeweka neno muziki katika parandesi kwa kuwa neno muziki si la asili ya hapa kwetu, ni neno lililoletwa na Wajerumani. Inajulikana wazi kitu kama hakipo katika utamaduni wa jamii fulani hakiwezi kuwa na jina.  Sijapata kukutana na jamii ya Kibantu yenye neno lenye kutafsiri neno muziki, hivyo hapo kuleta swali,  Je, ina maana kabla ya Wajerumani hakukuweko muziki? Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa muziki haukuwepo kwa mtizamo uliopo sasa. Kuna uchambuzi kuwa jamii zetu zilikuwa na muziki lakini ulikuwa na maana tofauti na muziki tunaoufahamu sasa. Kwanza kulikuwa na ngoma, ngoma ni chombo cha muziki, ngoma ni shughuli, mfano ngoma ya mavuno, au tambiko au msiba. Hivyo basi wimbo kutoka ngoma ya msiba haukuimbwa kwenye harusi, wala wimbo wa ngoma za tambiko haukuwa kwa ajili ya kuimba kwa kujiburudisha, wimbo wa ngoma za shughuli kama jando na unyago zilibaki kutumika katika shughuli hizo tu na si vinginevyo. Ujio wa Wajerumani ukaleta maana mpya baada ya wao kuja na vyombo vyao vya muziki na taratibu zao na mtizamo wao kuhusu muziki. Ujio wa Wajerumani ulianzisha kuzaliwa na kuongezeka kwa miji, na hivyo kuanza kukusanya watu wa makabila mbalimbali kuanza kuishi pamoja. Kati ya mambo makubwa waliyoingiza Wajerumani ni shughuli za kijeshi, jeshi liliokuwa linavaa sare, na kutembea kwa paredi na hivyo kutembea sare wakisindikizwa na muziki wa bendi za kijeshi, ulikuwa utamaduni mpya katika macho ya wenyeji. Huo ukawa kati ya njia za mwanzo za muziki kutoka nje kuingia katika hisia za babu zetu.  Wajerumani wenyewe walianzisha bendi za vijana ambazo si za kijeshi mojawapo ilikuwa  ni Bagamoyo Native Band iliyokuweko kwenye mwaka 1910
Bagamoyo Native Band

 Vijana waliokuwa wametoka katika makabila mbalimbali wakakusanyika na kuanza kubuni muziki wao wakiigiza watawala wao. Hivyo kuanzisha ngoma iliyokuwa ikiiga uaskari kwa kucheza kwa ‘step’ mbalimbali kama vile askari, pia vijana hawa walitengeza vifaa vyao vilivyoweza kulia kuigiza sauti za vyombo vya kupuliza vya kijeshi, na hivyo ukazaliwa muziki ulioitwa Beni. 
Muziki wa Beni unasemekana ulienea katika pwani yote ya Afrika ya Mashariki. Ulikuwa na muziki maarufu ambao ulifikia hata hatua ya vikundi vya Beni kutoka mji mmoja kwenda kushindana na vikundi vya miji mingine.  Muziki huu ulisaidia sana pia kukua kwa Kiswahili kwani ndio ilikuwa lugha iliyowezesha vijana kuwasiliana. Katika kuenea kwake muziki wa Beni ulichukuliwa na makabila mbalimbali na kupendezeshwa kadri walivyoona wao. Siku hizi Beni bado ni maarufu sana Malawi, ambako washiriki wake bado wanaendeleza utamaduni wa kuvaa kama askari wakati wakicheza ngoma hii. Video hapa chini


Na hapa kwetu uchezaji wa ngoma za aina ya  Mganda ambazo wachezaji huvaa sare kama makarani wa enzi za  mkoloni, yaani shati jeupe, suruali nyeupe, soksi ndefu, tai, na viatu safi ni muendelezo wa muziki wa Beni.


Beni bado iko kwa namna yake huko Zanzibar ambako vyombo vya kupuliza kama tarumbeta ndivyo vyatawala. Wajerumani hawakuwa na shida zana na muziki huu, lakini nchi ilipokuja kuwa chini ya Muingereza, ngoma hii ilionekana ni tatizo kwani ilikuwa ni kitu kimojawapo kikubwa ambacho kiliunganisha vijana bila ya kujali kabila. Mkoloni yoyote yule anafahamu kuwa ili utawale ni muhimu unao watawala wasiunganike. Muingereza aliipiga marufuku ngoma ya Beni, lakini kuweko kwa masalia ya ngoma hii hadi leo ni dalili tosha kuwa ukoloni haukufanikiwa kuifagia ngoma hii moja kwa moja. Vijana waliokuwa wamesoma au waliotaka kuonekana wameendelea waliazisha klabu zilizoitwa ‘social clubs’. Katika klabu hizo wakawa wanasikiliza na kucheza santuri za muziki mbalimbali wa Kizungu na hatimae kuanzisha ‘Dancing Clubs’ klabu zilizoanza kufanya mashindano ya dansi za kizungu kama ilivyokuwa kwa mashindano ya Beni. Vikundi toka Tanga kama vile New Generation Dancing Club au Coast Dancing Club cha Dar es Salaam, vilifanya safari za mara kwa mara kuja Dar es Salaam na Mombasa kwa ajili ya mashindano ya dansa na klabu za huko. Kwa taarifa tu New Generation tafsiri yake ni kizazi kipya, ni vema ikakumbukwa kuwa kila wakati kuna kizazi kipya. Hakika kila zama na vitabu vyake. Hizi klabu hatimae zikawa ni chanzo cha vikundi vya muziki, kama vile Dar es Salaam Social Orchestra na YMCA Social Orchestra. Kumbuka mambo yote haya yalikuwa katika kipindi cha miaka 1920-1930. Katika miaka hiyo hiyo kulianza kupatikana santuri kutoka Cuba, santuri hizi za muziki kutoka Cuba, pamoja na kutaja majina ya vikundi vilivyopiga muziki huo kama vile Estrellas Habaneras, Sexteto Habanero, Septeto Matamoros na kadhalika, santuri hizo zilikuwa na namba zilizoanza na herufi GV, hivyo kulikuwa na GV1, GV2 na kuendelea, wazee wa zamani walizitambua nyimbo zao kwa kutaja namba tu ya GV.



 Muziki huu uliopigwa kwa mitindo  ya Cha cha cha, Rumba, borelo uliwagusa sana wanamuziki wakati ule. Kwani ulikuwa muziki uliofanana na midundo ya Kiafrika. Wanamuziki wakaanza kuiga midundo hiyo na ndio mbegu ya muziki wa rumba wa leo. Mwanamuziki kama Salumu Abdallah aliwahi kutoroka kwao Morogoro na kuanza safari ya kuelekea Cuba ili tu akajifunze muziki, safari yake iliishia Mombasa kwani alipofika huko vita ya pili ya dunia ilikuwa imeanza. Lakini hatimae aliweza kutimiza ndoto yake kwa namna fulani kwa kuanzisha bendi maarufu ya Cuban Marimba Band, bendi ambayo mpaka leo nyimbo zake watu bado wanazicheza na kuzipenda.   Cuban Marimba ilianza kwanza kama bendi iliyoitwa La Paloma mwaka 1948. Hata jina La paloma limetokana na wimbo wa KiCuba wenye jina hilo maana yake Njiwa usikie hapa chini



No comments:

Post a Comment