Saturday, March 26, 2022

DR UFUTA MPIGA SOLO WACUBAN MARIMBA NA TK LUMPOPO AFARIKI DUNIA

 

Dr Ufuta uzeeni
J
OAKIM UFUTA, mpiga gitaa la solo aliyekuwa maarufu kwa wapenzi wa muziki enzi za Cuban Marimba ya Juma Kilaza, na bendi za Juma Kilaza zilizofuatia amefariki dunia. 
Dr Ufuta ambaye maisha yake ya uzeeni yalikuwa magumu kiasi cha kuwa mlinzi wa wa usiku wa sehemu mbalimbali pale Morogoro, na pia alikuwa fundi baiskeli,  amefariki Ifakara siku ya tarehe 18 March na kuzikwa kesho yake 19 March 2022 hukohuko Ifakara. 

Ufuta alizaliwa  Utuu Misheni Mahenge karibu miaka 70 iliyopita, alianzisha bendi yake ya kwanza mwaka 1966,  bendi yake aliyoiita Taifa Jazz, bendi hii iliyokuwa na waimbaji wanne, ilikuwa haina hata chombo kimoja kilichotumia umeme. Kati ya mwaka 1966 na 1968 hiyo ndiyo ikawa bendi moja maarufu  pale Mahenge. Mbunge wa jimbo la Mahenge wakati huo Mheshimiwa Ilanga, aliwanunulia vyombo vichache vijana hawa na hii ikawa bendi rasmi iliyokuwa ikisindikizana na Mbunge huyo katika kampeni zake mbalimbali.

 Mwaka 1968 kaka yake Lucas Simon alimshawishi aachane na bendi yake ya Taifa Jazz na kujiunga na Cuban Marimba wakati huo ikiwa chini ya Juma Kilaza. Na bendi ya Cuban aliweza kufika mpaka Nairobi ambako wakati wa kurekodi fundi mitambo mmoja pale studio alianza kumuita Dokta kutokana na upigaji wake mahiri na cheo hicho amebaki nacho mpaka umauti wake.

Picha hii ilikuwa ni ganda la moja ya santuri ya nyimbo za Cuban Marimba. Dr Ufuta ni aliyevaa miwani . Wa kwanza kulia waliosimama ni Juma Kilaza.

 Mwaka 1974 kuliktokea kutokuelewana kati ya wanamuziki wa Cubana Marimba na wamiliki wa bendi hiyo ambao walikuwa warithi wa marehemu  Salum Abdallah, mtiti huo ukasababisha Juma Kilaza, Joakim Ufuta, Juma Sangula, Ally Said na Hemedi Maneti kuihama bendi hiyo na kuunda TK Lumpopo, na hapo walitoa nyimbo nyingi za  kukumbukwa, wimbo wao wa kwanza ulikuwa Maisha ya Sasa. Katika bendi hii pia kukatokea kutokuelewana kwa ajili ya maslahi, Hemedi Maneti akatimka  na kujiunga na Vijana Jazz Band, Dr Ufuta akarudi tena Cuban Marimba. Baada ya muda kama ilivyokuwa kawaida miaka ile, bendi ilianza ziara ya  mikoa mbalimbali Kenya. Wakiwa Naivasha kukatokea kukorofishana tena,  wenzie wakarudi Tanzania yeye akabaki akitafuta maisha nchini Kenya.


Ufuta akitengeneza 


Mungu Amlaze pema peponi Joakim Ufuta

Monday, March 21, 2022

MANENO UVURUGE AENDELEA NA SAFARI ZAKE ZA MUZIKI

Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo

Wakati Maneno Uvuruge akiwa katika bendi ya  Super Rainbow, ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu. Muimbaji Banza Tax nae akajiunga  na bendi hiyo wakati huohuo.
Wakati huohuo katika ukumbi wa Lango la Chuma Mabibo makao makuu ya bendi ya Mambo Bado, mambo yalikuwa magumu, bendi hiyo ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, waimbaji Lodji Mselewa na Nana Njige nao wakaenda kujiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana, kiongozi wa Mambo Bado Tchimanga Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa ikaingia katika hali mbaya zaidi kwani Assossa aliiacha tena Mambo Bado ikafa rasmi.
 
Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo Maneno akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Mzee Juma Mrisho, lakini bendi ya  Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho, wanamuziki waimbaji Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe, nao wakajiunga na bendi hiyo. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.
Mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo Msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa.

Saturday, March 19, 2022

MJUE ALLY OMARY JAMWAKA

Ally Omary Jamwaka

Ally Omary Jamwaka alizaliwa katika kijiji cha Malui tarehe 1 Machi 1953, akajiunga na shule ya msingi ya kijijini kwake kuanzia 1960 na kusoma hapo mpaka darasa la saba. Mwaka 1969 akaingia katka jiji la Dar es Salaam kuanza kusaka maisha. Kazi aliyoipenda ilikuwa ni usanii, pengine kwa kuwa  kaka yake Shaaban Omary  alikuwa mpiga drums.  Jamwaka alianza safari yake ya usanii kwa kujiunga na kikundi cha sanaa kilichokuwa na maskani pale Buguruni kikiwa chini ya Mzee Mindu. Wakati yuko huko akakutana na rafiki yake aliyeitwa Adam Bakari, huyu baadae sana alikuja kuwa muimbaji maarufu na kupewa jina la Sauti ya Zege, kwa pamoja wakatengeneza kundi lao waliloliita The Hippies. Kundi hili la muziki wa vijana lilikuwa kazi yake kubwa kwenda kwenye madansi ya bendi kubwa na kuomba 'kijiko'. Huu ulikuwa mtindo ulioenea nchi nzima wakati huo, bendi ndogo zilikuwa zikipita zinapopiga bendi kubwa na kuomba 'kijiko' na hivyo kuruhusiwa kupiga nyimbo kadhaa kwa kutumia vyombo  vya bendi kubwa, wakati bendi hiyo inapumzika,  hii iliwapa wadogo uzoefu na wale waliokuwa wazuri waliweza hata kupata ajira papo hapo. The Hippies makao yao makuu yalikuwa mtaa wa Somali maeneo ya Kariakoo, walikuwa wakipiga muziki wa kukopi bendi za nje zilizotamba wakati huo, hasa zile za Ulaya na Marekani. Jamwaka wakati huo alikuwa tayari akipiga tumba na drums.
 Mwaka 1971 alijiunga na Biashara Jazz iliyokuwa bado mpya kabisa baada ya kubadili jina kutoka STC Jazz. Hii ilikuwa ni bendi iliyokuwa chini ya miliki ya Board of Internal Trade (BIT) ambayo chini yake kulikuwa na mashirika ya umma kama RTC, DABCO, HOSCO, GEFCO na kadhalika. Katika bendi hii aliwakuta akina Raphael Sabuni, Belino, Muddy, na kaka yake Shaaban Omary Jamwaka ambaye alikuwa mpiga drum wa bendi hiyo wakati huo.
Toka kushoto Ally Jamwaka, fundi mitambo wa Biashara Jazz band, kushoto Chamchu mpiga drum wa Biashara Jazz Band, wakiwa wamesimama kwenye uwanja wa Samora Iringa mwaka 1975

 Wengi wa wanamuziki waliokuwa STC Jazz Band walikuwa wasomi kwa hiyo waliacha muziki na kuingia katika kazi nyingine tofauti za kiofisi katika mashirika mbalimbali ya BIT. Ally Jamwaka alikaa katika Biashara Jazz Band iliyokuwa chini ya uongozi wa Juma Ubao aka King Makusa hadi mwaka 1977 alipoamua kujiunga na Tanzania Stars. Bendi hii ilikuwa na makao yake katika ukumbi maarufu miaka hiyo iliyoitwa Margot ambayo ilikuwa katikati ya Jiji pembeni ya barabara ya Samora. Ukumbi huu ulikuwa maarufu sana kwani kulikuwa na muziki kila siku ya wiki mpaka usiku wa manane, mabaharia walikuwa wakisha kutia nanga Dar es Salaam ,walielekea Margot ambapo palikuwa ni mahala penye starehe za kila aina, hapo ndipo pia kilikuwa kituo kikubwa cha 'machangudoa' ambao walikuwa wakitega nyavu zao kuwasubiri wateja.  Kufika kwake bendi hiyo alipishana na wanamuziki maarufu ambao wote ni marehemu, Haruna Lwali mpiga tumba na Joseph Mulenga mpiga gitaa wakahamia bendi iliyokuwa ikipiga ukumbi jirani wa Gateways ambapo kulikuwa na bendi maarufu ya Orchestra Santa Fe.
Baadhi ya wanamuziki waliokuweko katika bendi ya Tanzania Stars wakati huo walikuwa Joseph Emmanuel muimbaji na mpiga gitaa na mtunzi wa wimbo uliotamba wakati wake ulioitwa 'Mawazo', Hussein Sadiki, Yahaya Bushiri nae pia alikuwa mpiga gitaa mzuri sana. Bendi hii ilikuwa inapiga muziki kutoka nchi mbalimbali duniani hasa ukikumbuka kuwa walikuwa na wateja mabaharia kutoka kila kona ya dunia, hivyo ukiingia Margot ungeweza kusikia nyimbo cha Kichina, Kihindi, Kigiriki na kadhalika. Baada ya ukumbi huu kuchukuliwa na Chama Cha Ushirika, bendi pia ikachukuliwa na ndipo ilipozaliwa ile bendi maarufu ya Washirika Tanzania Stars.
 Jamwaka aliendelea kupigia Tanzania Stars mpaka mwaka 1979 ambapo bendi ya Mlimani Park ilimfukuza kazi mpiga tumba wake aliyekuwa akiitwa Tanzania One, Haruna Lwali, na hapo Abel Balthazar alimfuata Jamwaka na kumkaribisha Mlimani Park Orchestra. Mlimani Park  ilikuwa chini ya TTTS, shirika la umma lililokuwa likiendesha shughuli za usafirishaji na hasa wa taxi. Bendi ilipewa huduma nzuri sana na shirika hili na kufikia kuwa moja ya bendi kubwa nchini, nyimbo zake za wakati ule bado zinaheshimika katika nyanja za muziki hata leo. Ukumbi wa Msasani Beach Club ulikuwa mmoja wa mali za TTTS, na bendi ya Mlimani Park ndio iliyojenga ukumbi huo kwa kutumia mapato ya kila Jumatano kuelekezwa kwenye ujenzi wa ukumbi huo. Baada ya ukumbi huo kukamilika wanamuziki wakiwa na imani ambayo baadae ilikuja kuonekana potofu, waliamua kutumia fedha yao ya kila Jumatano kuanza kujenga ukumbi wa bendi yao uliokuwa Mpakani eneo linalojulikana kama DDC. Ujenzi ulifika mahala ukadorora na kufa kabisa. Hapa kuna maelezo kuwa  bendi ilipigwa 'kipapai' na bendi pinzani iliyokuwa jirani ili isikamilishe ujenzi maana ingekuwa bendi ya kwanza Tanzania kuwa na ukumbi wake  wa kisasa. Kama ni kweli walipigwa kipapai, basi hilo lilifanikiwa kwani ukumbi haukukamilika mpaka leo . Mwaka 1982 mali za TTTS kama vile bendi na ukumbi wa Mpakani ukahamishiwa Dar es Salaam Development Corporation (DDC), awali kulikuweko na wazo kuwa bendi ihamishwe iwe chini ya ATC maana wakati huo Air Tanzania walikuwa na Club yao nzuri tu, lakini ikaonekana DDC walikuwa na kumbi kama vile DDC Kariako, DDC Magomeni, DDC Keko na hivyo bendi ingefanya kazi kwa ufanisi zaidi huko, bendi na wanamuziki wakauzwa DDC. Mambo yalibadilika sana kwa bendi hii kwani menejiment mpya haikuthamini bendi, na hata matamko ya mara kwa mara toka kwa Meneja Mkuu wa DDC wakati huo yaliudhi sana wanamuziki kwani si mara moja alikuwa akiwatamkia wanamuziki kuwa bendi ikifa hana tatizo maisha yataendelea. Hili lilipunguza sana morali ya wanamuziki, hivyo basi 1985 awamu ya kwanza ya kundi kubwa la wanamuziki liliondoka DDC Mlimani Park Orchestra na kujiunga na Orchestra Safari Sound na kuanzisha kundi la International Orchestra Safari Sound iliyokuwa na mtindo wa Ndekule, ambapo walikuweko Abel Barthazar, Muhidin Maalim Gurumo, Ally Makunguru, Ngosha, Kassim Rashid wakiungana na wenzao akina Skassy Kasambula walianzisha moto mkali uliotikisa nchi. Katika awamu ya pili ya wimbi la wanamuziki wa Sikinde kwenda OSS, Ally Jamwaka pia alikuweko, wakati huo akiwa na Fresh Jumbe, Cosmas Chidumule,Hamis Juma Kinyasi, Bobchipe Chipembele wakasindikizana na Michael Bilali ambaye alirudishwa Sikinde mapema kwa nguvu ya wapenzi wa Sikinde waliochanga fedha na kulipa fedha alizokuwa kachukua toka uongozi wa OSS.  

Thursday, March 17, 2022

MANENO Uvuruge mwanamuziki toka familia ya wapiga magitaa

 

Maneno Uvuruge

Kuna familia nyingine hutokea kuwa na wanamuziki wengi tu, mfano ni familia ya maarufu ya mwanamuziki marehemu Michael Jackson. Watoto wote wa familia hiyo walikuja kuwa wanamuziki maarufu, wavulana wakaweza kuanzisha kundi la The Jackson 5, baadae hata dada zao Latoya na Janet Jackson nao wakaja kujitokeza kuwa wanamuziki waliokuja kujipatia mafanikio makubwa katika fani hii. Kuna familia kadhaa zenye sifa hizo hata hapa Tanzania, kuna familia ya Kanuti, Muumba na Uvuruge ni mifano ya jambo hili. Leo tumzungumzie Maneno Uvuruge kutoka familia ya akina Uvuruge.

Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.

Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka kutoka baamoja na kwenda nyingine na gitaa lake  na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji. Hayakuwa maisha rahisi

Jumanne Uvuruge mtunzi wa wimbo maarufu wa Georgina uliopigwa na Safari TRppers na kuimbwa na Marijani Rajabu

Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa kaka yake Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa..

Stamili Uvuruge hapa akiwa jukwaani wakati akiwa bendi ya Bima Lee

 
Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba  na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, kila baba yao alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake

Maneno Kushoto akiwa na kaka yake Huluka

 
Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Generation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Mwanamuziki muimbaji marehemu Freddy Benjamin ndie aliyemshauri Maneno kujiunga na bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia, ambako Maneno alijaribiwa kama ilivyokuwa kawaida wakati ule kwa mwanamuziki mgeni, lakini pamoja na kuweza kupiga gitaa vizuri alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi hiyo wakati huo. Baada ya hapo Freddy alimuombea kazi katika bendi ya Super Rainbow, bendi ambayo iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na katika bendi hiyo Maneno akakutana na wanamuziki wakubwa wakati huo kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky na Mzee Bebe. Wakati huu Eddy Sheggy ambaye alikuja kuipaisha bendi hiyo kwa wimbo wa Milima ya Kwetu alikuwa hajajiunga  na bendi hii wakati huo. Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga. Katika kipindi hichohicho bendi iliyokuwa ikiongozwa na Tchimanga Assossa, Orchestra Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige nao pia wakaja kujiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi..

Huluka Uvuruge akiwa jukwaani Msondo Music Group


Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Marehemu Mzee Juma Mrisho maarufu pia kama Ngulimba wa Ngulimba, wakati huo Urafiki Jazz Band  nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri marehemu Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waimbaji Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe nao pia wakajiunga na bendi hiyo. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa wa kupiga gitaa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis Original, alichukuliwa na bendi hii ili awe mpiga gitaa la rhythm, alijiunga na wapiga rhythm wawili mahiri Mbwana Cox na Omari Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba. Siku moja mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole aliyekuwa mmiliki wa bendi ya Afriso na wakamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge, Kiniki Kieto (mwimbaji), Comson Mkomwa (saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma.  Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwisha pokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba kwanza alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu bendi hiyo, kwani Mzee Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoaManeno Maquis kwa mara ya pili na kuhamia nae Afrisongoma. Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate huko Uingereza waweze kutengeneza kundi la muziki huko, lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda lakini rafiki zake akiwemo Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa......itaendelea


MARK MANJI WA ORCHESTRA MKWAWA wana Ligija

 

Waliochuchumaa na magitaa kushoto ni Simon Sewando, kulia John Mkamwa.Aliyesimama wa kwanza kulia Mark Manji.

Mark Manji alianza kupenda sana kusikiliza  wapigaji wa magitaa makavu(accoustic) maarufu kama magalaton,  waliokuwa kijiji kwao Chitare, Musoma. Upigaji wa magitaa makavu ulikuwa maarufu katika maeneo mengi ya Musoma labda kutokana na gitaa kuwa na kufanana na Ritungu au kwa kuwa Musoma ilikuwa jirani na Kenya ambako kulikuwa na wapiga magitaa maarufu kama akina George Mukabi, John Mwale na kadhalika. Mark alinambia kuwa anakumbuka toka yuko darasa la tatu alianza kuwa  na  hamu sana ya kuwa mwanamuziki. Hamu hii iliongezeka alipoingia kidato cha kwanza Alliance Secondary pale Musoma  ambako kila Jumamosi alianza kwenda kuchungulia wakati  bendi mbalimbali zikipiga  Musoma mjini. Bendi aliyokuwa maarufu wakati huo ilikuwa inaitwa Eleven Stars Band, pamoja na kuwa bendi ilikuwa na watu sita iliitwa Eleven Stars kwa kuwa mwenye bendi pia alikuwa anaendesha club ya mpira iliyokuwa na jina hilo. Bendi hiyo iliyokuwa na mpiga solo kutoka Kigoma, mpiga bezi Mkongo, mwimbaji Mkongo na Watanzania wengine wawili, mmoja wa waimbaji alikuwa akiitwa Dode ambaye kwake ndiko vyombo  vya bendi vilikuwa vinatunzwa.  Huyu Dode, ambaye baadae sana Mark aligundua ni kifupi cha Deusdedit alikuwa akiishi karibu na kaka yake mmoja, hivyo akaomba kujifunza gitaa na taratibu akajifunza gitaa la rhythm. Hizi juhudi zake za kujifunza muziki ziliwahi hata kusababisha kufukuzwa shule wakati akiwa form II, lakini hatimae kwa mbinde alimaliza kidato cha nne.
Mwaka 1970  akawa amechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Mkwawa,  katika kumbukumbu zake hakuwahi kusikia kuwa Iringa kulikuwa na bendi kwa hiyo alikataa kwenda kuendelea na shule kwa kuwa alitaka kuwa mwanamuziki. Akawa na ndoto za aidha kwenda kusoma Tanga, Morogoro, au Tabora maana huko alijua kulikuwa na bendi kubwa na maarufu. Pamoja na baba yake kujitahidi kumshawishi kwenda kusoma Mkwawa alikataa katakata akitaka kujiunga  na muziki au aende kusoma kwenye mji wenye bendi. Alijitahidi hata kubadilishana na mwenzie aliyechaguliwa kusoma Galanos Tanga lakini ikashindikana. Baada ya kama wiki tatu toka shule zimefunguliwa akakutana na mtu aliyemshangaa kwanini hajaenda shule, na alipomwambia kuwa hana mpango wa kwenda Iringa kwa kuwa hakuna bendi, yule mtu alimtaarifu kuwa katika shule ya Mkwawa kuna bendi, na tena ndio inayopiga Iringa mjini. Baada ya kusikia hayo moja kwa moja akaenda kwa baba yake na kumwambia kuwa ameamua kwenda shule, tena kesho yake. Baba yake hakuongeza neno, akampa fedha haraka sana nae  haraka akenda ofisi  za wilaya na kupewa warrant ya kwenda kusafiri kuelekea Iringa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kusafiri nje ya Musoma, lakini alifanikisha safari yake ndefu ya meli hadi Mwanza, kisha kupanda treni Mwanza mpaka Dodoma na kumalizia safari kwa basi toka Dodoma hadi Iringa. Alifika shuleni Mkwawa kama saa kumi na moja jioni, akakuta taratibu ziko nzuri maana akakuta orodha iliyoeleza bweni na chumba alichokuwa kapangiwa kuishi, alikuwa kapangiwa bweni la Magembe West. Haraka akaweka mizigo tu kwenye chumba alichopangiwa na kuulizia bendi iko wapi, akaelekezwa na kukuta mazoezi yanaendelea, akakaa hapo kwa saa nzima na kujua kweli amefika alipotaka.
Pamoja na masomo akaendelea na bendi ambayo kweli iliendelea kupiga Iringa mjini kila wikiendi katika dansi lililojulikana kama bugi, dansi ambalo lilianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Bendi ilijulikana kwa jina la Orchestra Mkwawa na mtindo wao ulikuwa Ligija. Baadhi ya wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Mark Manji na Masanja wakiwa wapiga gitaa la rhythm, Simon Sewando na Kakonko gitaa la solo, Tanganyika mpuliza Sax, John Mkamwa kwenye bass, Danford Mpumilwa na Semboni waimbaji, Zacharia Kakobe kwenye conga na Norman Hiza pia kwenye bezi.
 Mwaka 1972 baada ya kumaliza mitihani ya mwisho bendi ilisafiri hadi Dar es salaam kwenda kurekodi nyimbo zao,bendi ya  Vijana Jazz ndio walikuwa wenyeji wao na wakawaazima hata vyombo walivyoenda kurekodia.
Baada ya kumaliza shule ya Mkwawa kama ilivyokuwa ada wakati huo akaenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, mwaka 1973 baada ya kumaliza JKT akaingia Dar es Salaam akiwa na nia ya kujiunga aidha na Dar es Salaam Jazz au Western Jazz bendi alizozipenda sana, lakini anasema hali ya maisha duni ya wanamuziki aliyoikuta ilimkatisha tamaa kuwa mwanamuziki na kuamua kuendelea na masomo, na kufanya muziki kuwa ni shughuli yake ya ziada, jambo ambalo ameweza kulifanya na wakati huu ambapo amekwisha staafu kazi ameanzisha kituo kikubwa cha kufundisha taaluma mbalimbali za muziki, kule Tabata.
 Mark Manji nae alikuja kuanzisha bendi aliyoiita Chikoike Sound, jina hilo la bendi lilitokana na kufupisha majina ya watoto wake. Simon Sewando , ambaye mpaka sasa ni mwalimu chuo kikuu cha Dar es Salaa idara ya electronics nae alianzisha bendi iliyoitwa TZ Brothers. Muimbaji Danford Mpumilwa nae alikuja kuanzisha bendi iliyokuwa maarufu pale Arusha iliyoitwa Serengeti Band.
Kati ya bendi ambazo Orchestra Mkwawa iliwahi kupiga nazo katika jukwaa moja ni miaka hiyo ni Cuban Marimba ya  Kilaza, Butiama Jazz Band, STC Jazz Band wakati huo ikiwa na wanamuziki akina Marijani Rajabu, Raphael Sabuni, Belino, Ally Rahman na wengineo.

Shule ya Mkwawa ilikuwa na bendi mbili, bendi ya pili walijiita The Midnight Movers, bendi hii ilikuwa ikipiga muziki  wa  kizungu, wakati huo muziki ulioigwa sana na bendi za aina hiyo  ulikuwa ni wa soul, na blues. Hivyo bendi hii ya pili ilipiga muziki wa akina James Brown, Wilson Picket, Otis Redding, Jimi Hendrix na kadhalika, baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika bendi hii walikuwa ni Kafumba, Martin Mhando, Eddie Hans Poppe, Bijoux, Deo Ishengoma na Shaba katika drums. Deo aliyekuwa mwimbaji mmoja wapo alikuwa na mvuto wa pekee kutokana na Afro yake kubwa na uvaaji wa suruali pana za mtindo wa bugaluu ziliomfanya ajulikane mji mzima wa Iringa.   

Saturday, April 14, 2018

MUZIKI WETU UMETOKA SAFARI NDEFU part 1


Ukifungulia redio siku hizi utakumbana na aina mbalimbali za muziki ambao washiriki wake ni Watanzania, utasikia taarab, bongofleva, rumba, rege, muziki wa asili na muziki wa kisasa wenye vionjo vya kiasili na kadhalika. Je hapo mwanzo ilikuwaje? Kupata picha italazimu turudi  nyuma kabla ya kuanzishwa kwa ukoloni wa Kijerumani. Watu wa nchi hii waliishi kwa makundi ya kikabila na hivyo kila kundi kuendeleza utamaduni wake na sanaa zake ikiwemo ‘muziki’. 

Saturday, January 6, 2018

TASNIA YA MUZIKI 2017 KWA UFUPI

Kuanzia mwaka 2012 nimekuwa nikimaliza mwaka kwa kuandika makala ya mtizamo wangu kuhusu hali ya muziki katika mwaka uliokwisha. Na mwaka 2017 ndio huoo umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Kama ilivyokuwa kwa miaka mingi sasa, anga za muziki wa nchi yetu zilitawaliwa na muziki wa Bongoflava. Muziki ambao kwa asilimia kubwa hutengenezwa studio, hakuna shaka watu wengi  nchini na nchi jirani wametokea kuupenda sana muziki huu. Katika mkutano ulifanyika wiki chache zilizopita, kiongozi mmoja wa mambo ya Hakimiliki kutoka  Kenya alisema asilimia kubwa ya muziki unaopigwa kwenye vyombo vyao vya utangazaji ni wa kutoka Tanzania. Imefika mahali mpaka wasanii wa huko wameanza kudai muziki wa Tanzania upunguzwe ili wao waweze kupata nafasi zaidi katika redio na luninga zao. Inachekesha kuwa kilio kama hichohicho kinasikika kwa wanamuziki wa aina tofauti nchini kuhusiana na ‘kufunikwa’ na Bongofleva. Wasanii wa Bongofleva wameendelea kupata tuzo kutoka kwa taasisi mbalimbali za Kimataifa, na hata wengine kuingia mikataba na kampuni kubwa za kimataifa za usambazaji, na kwa picha hii Bongoflava itaendelea kutawala anga za muziki hata mwaka ujao. Muziki ambao tunaweza kusema chanzo chake ni muziki wa mchiriku wenye asili ya ngoma za Kizaramo, maarufu kama muziki wa singeli nao ulikuja juu sana kwa miezi michache ya mwaka huu, japokuwa ule moto wake unapungua, inawezekana muziki huo unajimaliza wenyewe kutokana na mashahiri yanayotumika katika nyimbo hizo, na hata video zinazo ambatana nazo, lakini hakika muziki huu ni ubunifu unaoweza kuitwa muziki wa asili ya Kitanzania bila shaka yoyote. Hakukuwa na mambo ya kushtua sana katika muziki wa Taarab hali hiyohiyo pia ilionekana katika muziki wa dansi. Bendi kadhaa na vikundi vya taarab vilitangaza kuanzishwa lakini havikuja na kitu kipya cha kuweza kuleta mshtuko katika tasnia, kifupi hakukuwa na jambo lolote chanya la kukumbukwa kutoka upande huo kwa mwaka 2017. Pamoja na kuwa haukuonekana kuwa umeshuka lakini pia hakukuwa na dalili za kupanda kwa muziki wa Enjili, kwenye sanaa usipopanda ujue umeshuka. Muziki wa kwaya ulianza kujitokeza zaidi hasa kwenye kutoa elimu ya mambo mbalimbali ya kijamii na pia kurudia nafasi yake ya zamani ya kusifia viongozi mbalimbali, kazi ambayo kwaya ilikuwa ikifanya toka miaka ya mwanzoni baada ya Uhuru. Kwaya kadhaa ziliweza kutengeneza video ambazo zimekuwa zikionekana kwenye luninga, japo ni wazi hazikutengenezwa kwa ajili ya biashara. Kuna kundi la wanamuziki ambao wao husema huwa hawana nia kabisa ya kusikika kwenye vyombo vya utangazaji vya hapa nchini, wao hutengeneza muziki kwa ajili ya maonyesho ya nje ya nchi. Wanamuziki hawa wameendelea kuwa na safari za kwenda nje kupiga muziki wao katika matamasha ya kimataifa bila kuhangaika kutambulisha kazi zao hapa nchini, sababu kubwa ambayo wamekuwa wakitoa ni urasimu wa taratibu za muziki kusikika katika vyombo vyetu vya utangazaji.  Hivyo badala ya kupoteza muda kupingana na mfumo, wao wameendelea na shughuli za kujitambulisha nje, ni nadra habari zao kuonekana kwenye vyombo vya habari vya nchini japo wanazunguka nchi mbalimbali duniani wakipiga muziki unaotambulika huko kuwa ni wa Kitanzania.  Muziki wa asili  ni kazi ambayo inaonekana ni kwa ajili ya watalii na shughuli maalumu za kiserikali au sherehe za kifamilia. Picha hii inadanganya kwani muziki asili unaendelea nchini mijini na vijijini japo hauonekani kwenye vyombo vya utangazaji, labda pale ambapo ni kiburudisho cha viongozi. Muziki wa asili uko katika makundi mawili, uko muziki ambao unafanywa na wasanii ukiwa ni mchanganyiko wa ngoma mbalimbali ili kuweza kuvutia biashara, na uko muziki asili ambao huchezwa na kuimbwa na wenye kabila lao kwa upenzi wa utamaduni wao. Kwa kuwa hauonekani wala kuzungumziwa sana kwenye vyombo vya utangazaji, unaweza ukadhani haupo au haupendwi lakini hilo si sahihi. Maelfu ya vijana nchi nzima wanacheza na kupiga ngoma za kiasili kwa ufasaha mkubwa.
 Kumekuweko na matamasha kadhaa ya muziki nchini, kama tamasha la Fiesta, Marahaba, Tulia Traditional Dance Festival, Sauti za Busara, Karibu Music Festival na kadhalika, lakini matamasha haya ilikuwa ni nafasi ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanamuziki walioko nchini. Wilaya, mikoa nayo ingeweza kutayarisha matamasha yake ya utamaduni ingekuwa sehemu nzuri sana ya kuendeleza utamaduni, wasanii kubadilishana ujuzi, kuibua vipaji na kuleta burudani kwa wananchi  kwa ujumla. Ufadhili katika shughuli za muziki umekua ukiangalia sana faida za kibiashara, kumekuwa na kampuni chache ikiwa zipo ambazo zimefadhili matamasha kwa nia tu ya kuendeleza muziki. Matamasha mengine yamekuwa yakitegemea ufadhili wa balozi mbalimbali za nje kuwezesha kufanya maonyesho ya muziki wetu. Ni kichekesho kwa kweli. Hata zile kampuni ambazo ni maarufu nje ya Tanzania kwa kuunga mkono shughuli za sanaa, kwa namna ya ajabu zikiwa Tanzania ghafla zinakuwa na msimamo tofauti.
Maeneo ya kufanya shughuli za muziki yamezidi kupungua, mengine yamevunjwa na maeneo kuachwa wazi kama vile eneo lilokuwa DDC Magomeni na Mango Kinondoni, mengine yamekuwa makanisa na kadhalika. Pamoja na kuwa kulikuwa na wimbi la kujenga kumbi ambazo hutangazwa kuwa ni ‘multi purpose’, kumbi hizi haswa zilijengwa kwa ajili ya kufanyia shughuli za harusi, kuna mambo kadhaa ambayo si rafiki kwa muziki katika kumbi hizi, na hata wenye kumbi hukataa kumbi zao kutumika kwa shughuli za muziki hasa wa dansi.
 Katika mwaka 2017  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dr Harrison Mwakyembe amekuwa na mikutano mingi na wanamuziki, jambo jema kinachosubiriwa 2018 ni matokeo ya mikutano hii. Ushauri kwa wanamuziki ambao muziki wao unajikongoja, kuna umuhimu wa kutafuta majibu ya kisayansi kwanini hali iko hivyo. Majibu mepesi ya kulaumu vyombo vya habari, serikali na wadau wengine, kamwe hayata saidia katika kuleta mabadiliko.


Thursday, June 29, 2017

HATIMAE MWANAMUZIKI MKONGWE BROTHER ZENNO AZIKWA

MWANAMUZIKI  na mchambuzi wa muziki wa charanga maarufu kwa jina la Brother Zeno hatimae amezikwa na makaburi jirani na alipokuwa akiishi kule Mbagala Kibondemaji. Zerno ambaye alikuwa muimbaji mzuri atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Dar es Salaam Jazz B, bendi iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya, ambayo ilianza kufanikiwa kwa kasina kuanza kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A, chini ya Michael Enoch, bendi ikavunjwa na wanamuziki wengine wakaingizwa Dar Jazz A, lakini Patrick akakasirika na kutokomea , baadae akaja kuanzisha Afro 70 na kufanya mambo makubwa. Baadae Brother Zeno alijiunga na Shirika la Bima ya Taifa, na baada ya kujiunga kampuni hiyo ndie aliyetoa msukumo wa kuanzishwa kwa bendi katika shirika hilo, Bima Jazz Band na hivyo pia kupewa kazi ya kutafuta wanamuziki wa kujiunga na bendi hiyo na yeye mwenyewe kuwa kati ya wanamuziki waanzilishi wa kundi hilo lililokuja kujizolea umaarufu mkubwa. Kati ya wanamuziki wa kwanza katika bendi hiyo waliobaki hai sasa ni wawili tu baada ya kifo cha Zeno. 







Binti pekee wa marehemu akiwa na mumewe wakiweka shada la maua







Baadhi ya wanamuziki waliohudhuria mazishi ya Brother Zeno


Aliyekaa ni Abdallah Mbosanga mmoja ya wanamuziki wawili waliobaki hai wa bendi ya Bima Jazz band ya kwanza. Mwingine ni Duncan Ndumbalo

Tuesday, June 27, 2017

BROTHER ZENNO AFARIKI DUNIA

RIP Brother Zerno
Hakika siku za karibuni zimekuwa ngumu kwa wapenzi wa muziki wa zamani, mfululizo wa misiba na wanamuziki kuugua kumekuwa ni habari karibu kila siku. Mchambuzi mahiri wa muziki wa Charanga Zerno Andrew Lucas, aliyefahamika zaidi kwa jina Brother Zeno, amefariki dunia asubuhi leo katika hospitali ya Temeke,  Brother Zeno  aliyekuwa akishirikiana na 'Mzee wa Macharanga' Charles Hillary enzi hizo Radio One, alikuwa na ufahamu mkubwa wa muziki wa kutoka Cuba na hivyo kuwa mpenzi mkubwa wa watu waliopenda muziki huo. Brother Zeno amesumbuliwa karibu mwaka mzima na tatizo la moyo na katika siku zake za chache mwisho alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine, alitegemewa angepata nafuu na kuhamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi lakini Mungu amekuwa na mipango mingine.
Msiba wa Mzee utakuwa nyumbani kwake Mbagala Kibonde Maji na mazishi yatakuwa kesho 28/6/2017 saa kumi hukohuko Mbagala

Friday, June 23, 2017

SHAABAN DEDE ANAUMWA AMELAZWA MWAISELA NO 5

Mwanamuziki mkongwe Shaaban Dede 'Kamchape' amelazwa leo katika hospitali ya Muhimbili wadi ya Mwaisela No 5. Wapenzi wa muziki tumkumbuke katika swala zetu.

Monday, June 5, 2017

MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AFARIKI DUNIA

HALILA TONGOLANGA, mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Muhimbili amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Halila alikuwa amesafirishwa kutokea Ndanda kuja Muhimbili akihisiwa kuwa na matatizo ya figo. Licha ya kuwa alifika Muhimbili juzi Ijumaa usiku, lakini alikuwa hakufanyiwa vipimo vyovyote vikubwa mpaka umauti unamkuta. Jana Jumapili ililazimika kuanza kufanya jitihada za kupata daktari ambaye angemshughulikia kwa karibu zaidi, na daktari alipatikana ambaye aliahidi angeanza kufwatilia swala lake leo asubuhi lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa tofauti. Juzi nilipomuona alinambia kuwa ana mengi anataka kunambia, lakini moja aliloweza kunambia pale ni kuwa yeye anajihisi ana kansa, 'Nilimuuliza anajuaje hilo, kwa vile hajapimwa hakuwa na jibu"
Wengi tutamkumbuka Tongolanga kwa wimbo wake wa Kimakonde aliouimba kwa mara ya kwanza akiwa na Les Mwenge 'Kila Munu Ave Na Kwao"
 Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa leo saa tano kuelekea kwao Newala. Habari zaidi  zitawafikia kupia hapa
Mungu amlaze Pema peponi Halila Tongolanga


Saturday, June 3, 2017

TONGOLANGA ANASUBIRI VIPIMO

Katibu Mtendaji wa BASATA mwenye kitenge akiwa na Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, walipomtembelea Tongolanga asubuhi ya leo.
Halila Tongolanga kwa kweli anaumwa. Kwa maelezo ya mdogo wake, ni mwezi wa tatu sasa anaingia na kutoka hospitali mbalimbali. Mpaka jana alikuwa katika hospitali ya Ndanda, na kwa msaada wa Mbunge wa Tandahimba aliweza kupatiwa Ambulance na kufikishwa Muhimbili ambako amelazwa Kibasila No 10. Mpaka jioni ya leo alikuwa anasubiri vipimo.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.