Thursday, April 23, 2015

MWANAMUZIKI MKONGWE MUTOMBO LUFUNGULA AUDAX HATUNAE TENA

AUDAX(kushoto) akiwa na Kasongo Mpinda
Mwanamuziki muimbaji na mtunzi mashuhuri wa bendi ya Maquis Original Mutombo Lufungula Audax, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, huko Kimara Michungwani. Mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa Mwananyamala Hospitali. Audax alikuwa ndie mmoja wa wanamuziki asili wa kundi la Maquis Du Zaire. Kundi la Maquis lilianza katika mji wa Kamina, jimbo la Shaba, huko Kongo. Awali kundi lilianza kwa kuitwa Super Teo, kisha kubadili jina na kuitwa Rocken, ......INAENDELEA

Tuesday, April 21, 2015

MWANAMUZIKI WA SIKU NYINGI PAUL GAMA AFARIKI DUNIA

KWA MASIKITIKO MAKUBWA TUMETAARIFIWA KUWA MWANAMUZIKI WA ZAMANI PAUL GAMA AMEFARIKI DUNIA HUKO DODOMA TAREHE 16.4.2015 MUDA WA SAA NNE ASUBUHI. NARUDIA MAKALA HII YA HISTORIA YA PAUL GAMA KADRI ALIVYOTUELEZA MWENYEWE

Paul Daniel Gama
Paul Daniel Gama alizaliwa Barabara ya 11 Dodoma (1947). Baba yake alikuwa ni mwanajeshi wa KAR mwenye asili ya Songea na mama yake alikuwa na asili ya Usangu alikuwa anafanya kazi  katika 
Spokes Mashiyane na filimbi yake
hospitali ya Mirembe ambayo wakati huo ilikuwa ni hospitali kubwa ya majeruhi wa vita ya pili ya dunia. Aliingia shule na alipofika darasa la nne alijikuta akiwa na kipaji kukubwa cha kupiga filimbi, wakati huo wapiga filimbi walipenda sana kumuiga mpiga filimbi maarufu kutoka Africa ya Kusini Spokes Mashiyane. Akiwa na wenzie walianzisha kikundi ambacho kilikuwa na maskani eneo la Mji Mpya pale Dodoma. Vijana hao pia walikuwa wakiiga  nyimbo za wanamuziki maarufu wa wakati huo, kama Salum Abdallah na  Cuban Marimba, pia Salum Zahor na Kiko Kids. Katika kufanya fani yao hiyo kama kitu cha kujipa burudani waliligusa sikio la  aliyekuwa mwalimu wa Elimu ya Watu Wazima katika Community Center ya pale Dodoma. Mwalimu huyu aliwasaidia kuwaazimia amplifaya moja kutoka kwenye bendi nyingine ilikuweko Dodoma wakati huo, The Jolly Sextet Band. Band iliyokuwa ikimilikiwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa East African Postal and Telecommunication Services, huyu bwana alikuja na vyombo vingi akaanzisha bendi ambayo mmoja wa wapigaji wake alikuwa Mzee Mnenge ambaye hatimaye alitua NUTA Jazz Band.
Bongos
Hiki kikundi cha Gama na wenzie kilikuwa katika mfumo wa Jazz Band za zamani ambapo walikuwa na ngoma na filimbi tu,ikisindikizwa na kuimba, lakini waliweza kukonga nyoyo hata za wanamuziki wengine, na Gama akawa anasakwa na bendi kubwa iliyokuweko wakati ule Central Jazz band. Alipomaliza darasa la saba tu ndugu yake aliyeitwa Titus Olaf Gama alimshawishi aingie Central Jazz lakini hakuwa tena mpiga filimbi bali mpiga Bongos, fani aliyoiweza sana hata  kuipenda na hasa baada ya kuwaona wanamuziki wa NUTA akiwemo Muhidin Gurumo  ambaye wakati huo alikuwa akipiga Bongos na kuimba. Bongos no ngoma ndogo zilizokuwa muhimu katika kundi wakati huo ambapo hakukuweko na drums wala tumba. Taratibu akaanza kupata hamu ya kupiga bass, wanamuziki wenzie walimkatisha sana tamaa kwa kuambiwa kuwa vidole vyake vilifaa sana kwa kupiga bongos na si kupiga gitaa.

Katika jitihada zake za kujifunza gitaa la bezi alikuwa kila mara akiwahi mazoezi na kujaribu kujifunza gitaa la bezi. Hilo lilikuwa gumu mpaka pale bendi  ya Lake Jazz Band ilipotembelea Dodoma. Bendi hiyo wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Shem Karenga  akiwa anapiga gitaa la bezi, Mzee alum ambaye alikuwa na ulemavu wa macho, mwanzo alikuwa akipiga gitaa la solo na baadae akahamia kupiga gitaa la rhythm wakati gitaa solo lilikuja kupigwa na jamaa aliyeitwa Kally. Kutokana na simulizi ni wazi kuwa wanamuziki wa kutoka Burundi walikuwa wengi sana nchini wakati huo. Pia katika bendi hiyo alikuweko Mzee Juma Kitambi, mtunzi wa wimbo maarufu wa Rangi ya Chungwa.
Gama alichukua nafasi hii kumfuata Mzee Salum ili aweze kumfundisha gitaa. Kwa kuwa wanamuziki wengine walikuwa wakitoka kwenda kutembea Mzee Salum alibaki nyumbani na hivyo Gama alichukua nafasi hiyo kumnunulia sigara Mzee Salum ana kumsihi amfundishe gitaa nae alifanya hivyo na Gama akatokea kuwa mpiga bezi mahiri.
Katika kipindi hiki akatokea mfanya biashara Mohamed Omar Badwel, huyu alikuwa na gereji na studio ya kupiga picha, aliweza kwenda Mombasa na kurudi na seti ya vyombo na kuanzisha Dodoma Jazz Band. Gama akahama Central Jazz Band na kujiunga na wanamuziki wengine walioanzisha Dodoma Jazz. Band ilianza ikiwa na mpiga solo Hassan Mursali mwanamuziki mweny asili ya Malawi, siku hizo ikiitwa Nyasaland alikuwa ndie mpiga solo, lakini aliwaacha baadae na kujiunga na NUTA Jazz Band, upigaji wake wa solo unaweza kuusikia katika kusikiliza kibao kimoja maarufu cha NUTA, kilichoitwa Dunia Njema Kukaa Wawili.
Hasan alikuwa mtu wa kuhama hama hatimae alipoteza uwezo wa kusikia jambo ambalo lilihusishwa na kuhamham kwake kwani ushirikina ulitawala sana wakati huo, kama maelezo yanayofuata yanavyoonyesha. Dodoma Jazz ilikuwa pia inafanya ziara katika sehemu nyingi , kama vile Iringa, Mbeya ,Tabora, Dar es Salaam na kadhalika, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilifanyika ikiwa na lengo la kumfuata Abel Barthazal aliyekuwa akipiga katika bendi ya Kilosa Jazz. Bendi  ilipokelewa vizuri na wakafanya maonyesho yao Kilosa na hatimae kuondoka na Abel. Siku chache baade wakati huo Mzee  Mohamed Omar, mwenye bendi alikuwa kasha mnunulia suti kadhaa Abel, ukaja ugeni toka Kilosa wakiwa na barua yenye maelezo kuwa ikiwa Abel Hatarudi Kilosa, mmoja wa wanamuziki wa Dodoma Jazz atafariki, na barua hii ililetwa kwa mkono na mjumbe ambae alisisitiza wakishaisoma mbele yake ndio anaondoka. Abel alirudishwa Kilosa mara moja.
Baada ya hapo aliyekuwa meneja wa bendi Ramadhan Waziri alitumwa Burundi kwenda kutafuta wapigaji, siku alipokuwa anarudi na wapigaji wapya akakutana kwenye treni na Rashid Hanzuruni, mpiga solo mahiri sana ambaye upigaji wake husikika katika wimbo  Napenda nipate lau nafasi
Hanzuruni alikuwa kaiacha Tabora Jazz baada ya  kutokea ugomvi mkubwa ambapo alipoteza meno kadhaa, hivyo alikuwa kwenye hilo treni akielekea Dar es Salaam kumfuata mpigaji mwenzie Samba ambae alikuwa NUTA Jazz. Ramadhani aliweza kumshawishi hanzuruni akabaki Dodoma Jazz ambako alikaa kwa muda na hatimae akaja kuchukuliwa na Sama ili aingie NUTA Jazz, ndoto hiyo haikufanikiwa kwana NUTA alikuweko mpigaji mahiri  Hamisi Franco, hii ndiyo ilipelekea Hanzuruni kwenda Western Jazz Band



Friday, January 16, 2015

IMETIMIA MIAKA 36 TOKA KIFO CHA MBARAKA MWINSHEHE, MUZIKI WAKE BADO UKO HEWANI

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro Juni 27, 1944. Siku ya Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikiska kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha mwanamuziki huyo, mpiga gitaa muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga karibu kila wilaya ya nchi hii. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia katika hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari...........ENDELEA HUKU

Tuesday, December 16, 2014

HATIMAE SHEM IBRAHIM KARENGA AZIKWA

HATIMAE  mwanamuziki mkongwe mpiga gitaa muimbaji na mtunzi mahiri Shem Ibrahim Karenga amezikwa katika makaburi  ya Kisutu jioni ya leo. Shughuli hiyo ilianza kwa utata baada ya kuwa makaburini hapo kulikuwa na misiba minne hivyo kila lilipokuja jeneza wanamuziki, ndugu na wapenzi wa muziki walijikuta wakisindikiza jeneza na..........INAENDELEA HUKU

Monday, December 15, 2014

BURIANI SHEM IBRAHIM KARENGA

LEO Jumatatu tarehe 15 Desemba 2014, majira ya saa nne asubuhi taarifa zilianza kusambaa kuwa mwamba mwingine wa muziki wa dansi Tanzania umedondoka. Mzee Shem Karenga hatunae tena,kwa vyovyote waliohudhuria dansi alilopiga Ijumaa na Jumamosi iliyopita pale Mwembeyanga watakuwa hawaamini, lakini imekuwa mapenzi ya Mungu, kwamba asubuhi ya leo aliamka hajisikii vizuri na alipelekwa hospitali ya Amana lakini hakukuweza kufanyika kitu Mzee akarudi kwa Muumba wake. Mungu aipokee roho yake. Miezi michache iliyopita tulipata muda mrefu wa kuongea na Mzee Shem Karenga ili kujua alikotokea na mawazo yake kwa sasa mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo;................................. ENDELEA HUKU

Monday, November 10, 2014

LEO NIMEKUMBUKA KIBAO MASAFA MAREFU CHA TANCUT ALMASI...angalia video


Kasaloo Kyanga ndie mtunzi wa kibao hiki maarufu, kilirekodiwa RTD Dar es Salaam katika awamu ya pili ya recording za Tancut Almasi. Recording hii ilitaka kuvunja bendi kwa kuwa wakati bendi ikiwa studio, Said Mabela alipita studio na Katibu wa bendi akamuuliza kwa siri anausikiaje muziki? Sijui kwa sababu gani lakini Mabela alijibu, "Hapa hakuna kitu nasikia solo tupu". Katibu wa bendi ambaye pia wakati huo alikuwa Katibu wa tawi la JUWATA la Tancut, akatujia juu wanamuziki wa Tancut kuwa tunapiga solo tupu na hivyo tuache kurekodi na bendi irudi Iringa kwa mazoezi zaidi. Ulikuwa ugomvi mkubwa, wakati huo Mabela amekwisha ondoka hata kumuuliza alikuwa ana maana gani haikuwezekana. Fundi wa RTD James Muhilu ndie aliyemtuliza Katibu huyo kwa kumueleza kuwa nae haelewi maana ya maneno ya Mabela na recording ikaendelea na dunia ikapata bahati ya kusikia kibao hiki. Nakumbuka katika awamu ya kwanza ya kurekodi Sidi Morris alikuja studio na kupiga tumba katika vibao kadhaa kikiwemo Wifi utunzi wa mwenye blog hii John Kitime. Hili lilileta mzozo Maquis ambako Sidi alikuwa akifanyia kazi na hivyo akasimamishwa bendi kwa kushiriki kurekodi

Saturday, November 8, 2014

HISTORIA FUPI YA TAARAB

Taarab ina historia ndefu katika muziki wa Tanzania kama ulivyokuwa muziki wa dansi. Wapenzi wa taarbu wa zamani waliiweka taarabu katika vyanzo kama Taarab ya Tanga, Taarab ya Dar es Salaam,Taarab ya Zanzibar na Taarab ya Mombasa. Taarab ya Zanzibar wakati huo........INAENDELEA HUKU

Wednesday, October 22, 2014

MIAKA KUMI YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA NDALA KASHEBA

ndala-kasheba_2255445LEO tunatimiza miaka kumi toka kifo cha mwanamuziki mahiri Freddy Supreme au maarufu kama Ndala Kasheba. Freddy alianza kufundishwa gitaa na baba yake wakati akiwa na umri wa miaka 12. Baba yake alijua kupiga gitaa japo hakufanya kazi ya uanamuziki, alikuwa akipiga gitaa nyumbani baada ya saa za kazi. Moja ya bendi maarufu ambazo zilimtambulisha sana Fredd ilikuwa Orchestra Fauvette, Freddy alieleza kuwa bendi ya Orchestra Fauvette ilianza tarehe 7 mwezi wa sita mwaka 1964 katika jiji la Lubumbashi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Jina hilo Fauvette........ENDELEA HUKU

Saturday, October 11, 2014

ALLY RASHID AZIKWA KEKO

Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kumzika Ally Rashid mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alifariki jana mchana. Mazishi yalifanyika katika makaburi ya Keko Machungwa  kaburi lake likiwa jirani kabisa na la mwanamuziki mwingine nguli Moshi William. Mazishi ya Mzee Alyy yalifanyika muda wa saa nne asubuhi pia na kuhudhuriwa na wanamuziki wengi wa zamani na hata wa sasa akiwemo Mchizi Mox ambaye alikuwa kimwita marehemu baba yake mdogo.
MUNGU AMLAZE PEMA ALLY RASHID KWA PICHA INGIA HAPA

Friday, October 10, 2014

MPIGA SAXAPHONE MKONGWE ALLY RASHID 'SABOSO' AFARIKI DUNIA

Mwanamuziki wa zamani aliyekuwa mpiga saxaphone aliyejulikana pia kama Mzee Saboso, Ally Rashid amefariki dunia leo mchana. Mzee Ally kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Ngoma. Wiki chache zilizopita mtandao wetu ulifanya mahojiano marefu na Mzee Ally hivyo soma hapa historia ndefu ya Mzee huyu. Mpaka muda huu ndugu zake hasa wa Zanzibar ambako ndio kwao walikuwa hawajatoa taarifa ya taratibu za maziko. Mara tutakapopata taarifa zaidi tutawataarifu.
Mungu Amlaze Pema peponi Mzee Ally Rashid


   HISTORIA YA ALLY RASHID KHAMIS ‘SABOSO’ ISOME HAPA

Thursday, September 11, 2014

Saturday, August 30, 2014

IFAHAMU HISTORIA YA MAFUMU BILALI BOMBENGA =SUPER SAX

HAPA AKIPIGA TUMBA SIKU YA MKESHA WA MAZISHI YA REMMY ONGALA


AKIWA NA MPULIZA SAX MWENZIE JOSEPH BERNARD
African Beat ilianzishwa mwaka 1998, baada ya Mafumu Bilali Bombenga kujiengua kutoka katika bendi ya African Stars ambayo nayo ilianzishwa mnamo mwaka 1994 kwenye Hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam, huku yeye akiwa ndiye  muanzilishi.
Bombenga anakumbuka kuwa, wakati akiwa na African Stars ambayo hata jina lake alilibuni yeye, walitamba na vibao kama ‘Sakatu Sakatu’, ‘Mayanga’, ‘Maya’, ‘Afrika’ na ‘Dance Dance’.
Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi hilo la African Stars linalojulikana zaidi hivi sasa kama ‘Twanga Pepeta’, ni Bob Gady, Andy Swebe, Alfa Nyuki, Palmena Mahalu, Pamela pamoja na Kayumbu ‘Amigolas’.
“Historia yangu kimuziki, inaanzia mwaka 1972 nilipojiunga na bendi ya Morogoro Jazz, wakati huo nikitokea jeshini Makutupola,” anasema Bombenga.
Mwaka 1973 aliingia na Western Jazz alioshiriki nao kupiga Saxophone, kwenye vibao kadhaa vya bendi hiyo, vikiwamo ‘Hakika’, ‘Kazi ni Kazi’ na ‘Sadaka’, kabla ya mwaka 1978 kutimkia Dar International.
Pamoja na kupuliza kiustadi Saxophone pamoja na kuimba kwenye nyimbo kemkemu, zikiwamo ‘Mayasa’ na ‘Zuena’, lakini pia Bombenga alishiriki kucharaza gitaa la Solo katika kibao ‘Vick’.
Mwaka 1979 alibeba mabegi na kutua Vijana Jazz Band alikotunga kibao ‘Taabu’ na pia kushiriki kukiimba, huku kadhalika akipuliza Saxophone kwenye vibao kama ‘Chiku’ na ‘Matata Ndani ya Nyumba’.
Mwaka 1980 alihamia Maquis ambapo alitesa kwa kupuliza Saxophone kwenye vibao viiingi, baadhi yake ni ‘Zoa’, ‘Sina Ndugu’, ‘Noel’ pamoja na ‘Maige’.
“Nilikaa Maquis hadi mwaka 1984 nilipochomoka tena na kuhamia Bima Lee nilikokutana na wakali kama Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Shaaban Dede ‘Super Motisha’, ‘Joseph Mulenga ‘Spoiller’,” anasema Bombenga.
Mwaka 1985 Bombenga alikuwa mwanzilishi wa bendi ya MK Group ‘Ngoma za Maghorofani’, kabla ya mwaka 1986 kuwa tena mmoja wa waanzilishi wa Tancut Almas ya Iringa.
Mwaka 1987 alirejea tena MK Group ambapo nyimbo yake ya kwanza kupuliza Saxophone awamu hii ya pili ilikuwa ni ‘Utakuja Kuanguka Kwenye Matope’.
Mwaka 1989, kaka yake Adam Kinguti alirudi nchini akitokea Sudan alipokuwa akifanyakazi kwenye ofisi za ubalozi, wakaanzisha Bicco Stars na yeye kushiriki kupuliza Saxophone kwenye vibao kadhaa kama vile; ‘Magret Mage’, ‘Wapangaji’ na Kisamvu’.
Mwaka 1991 alitoka Bicco akiwa na mpapasaji kinanda mahiri wa kike ambaye kwa sasa ni marehemu, Asia Daruweshi, baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na Kinguti, wakaanzisha Zanzibar Sound.
“Tukiwa na Zanzibar Sound, tulipata mkataba katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha na mwaka mmoja baadaye mwanamuziki mwenzetu kwenye bendi hiyo, Kanku Kerry alipata mkataba Japan tukaondoka naye kwa sharti la sasa kujiita Kilimanjaro Connection,” anasema Bombenga.
Walizunguka nchi nyingi za bara la Asia wakiwa na Kilimanjaro Connection, waliporudi mwaka 1994 alijitoa na baadaye kidogo Asia naye alijitoa na kurudisha upya bendi yake ya Zanzibar Sound na kurejea mkataba wake Bahari Beach Hotel.
Bombenga wakati huu akabaki bila bendi, ambapo muda si muda Asia alipata kazi nchini Bahrain na kumuachia Bombenga mkataba wa Bahari Beach.
Baada ya kuona ameachiwa mkataba wakati hana bendi, Bombenga ndipo alipomfuata Baraka Msirwa na kumuomba vyombo vya muziki ambapo alimpa kwavile havikuwa na kazi kutokana na kufa kwa bendi za MK Group, MK Beat na MK Sound zilizokuwa zikivitumia.
“Hicho ndio kilikuwa chanzo cha bendi ya African Stars niliyoibuni mwenyewe hadi jina, iliyoniletea uhasama mkubwa na dada yangu Asha Baraka baada ya kujitoa,” anasema Bombenga.
Kwa upande wa warithi, Bombenga ana wanawe wawili wanaoonekana kufuata vema nyayo zake, ambao ni Feruzi (22) anayepapasa kinanda na Aziza (19) ambaye ni mwimbaji.  
Bombenga mwenye miaka 40 katika muziki na aliyejifunza mengi kupitia sanaa hiyo, anavutiwa na waimbaji; Isha Mashauzi, Nasseeb Abdul ‘Diamond’, Flora Mbasha na Hassan Bitchuka.
Anatoa ushauri kwa wanamuziki wa Dansi kuketi na vyombo vya habari na kuzungumza, ili kuangalia namna ya kuurejesha kwenye chati muziki wao ambao umekuwa ukiporomoka kila uchao.
Mikakati ya baadaye ya Bombenga ni kustaafu muziki na kujihusisha na ujasiriamali, baada ya kwenda nchini Kinshasa na kufanya maonesho na baadhi ya mastaa wa huko.
“Mimi ni mtoto wa tano katika familia ya mzee Bilali Mafumu, niliyepata elimu yangu ya msingi katika shule ya H.H Agakhan, Kigoma nilikofaulu na kujiunga na shule ya sekondari Kazima, Tabora nilikosoma hadi kidato cha nne,” anasema Bombenga.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Bombenga aliyesoma shule moja ya sekondari na mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage, anasema kuwa 1972 alijiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ya enzi hizo, alikojifunza kuimba na kupuliza Saxophone.
Anaishi Vingunguti, jijini Dar es Salaam na familia yake ambayo ni mkewe na watoto saba, huku akitamani kuongeza wake wengine hadi wawe watatu.





  

Friday, August 29, 2014

MFAHAMU MKONGWE WA SAXOPHONE RASHID PEMBE

RASHID PEMBE


 “TUKIO la kuutumikia Umoja wa Vijana kwa muda wa miaka 18 na kulipwa mafao ya sh. Mil 1.6, baada ya kustaafu, ndilo linalosumbua kichwa changu hadi leo, ambalo kiukweli sitakaa nikalisahau,” ndivyo anavyoanza kueleza Rashid Pembe.
Pembe ni kati ya wanamuziki nguli wa miondoko ya Dansi, aliyetokea mbali hadi sasa ambapo anaonekana amepata mafanikio kiasi kupitia sanaa hiyo.
Mwaka 2005 aliomba kustaafu kuitumikia bendi ya Vijana Jazz aliyokuwa nayo tangu Aprili, 1987, baada ya kuona imeanza kuyumba na kupoteza mwelekeo na kilichomkuta ndio hicho ambacho wakati fulani aliwahi kujutia kuwa mwanamuziki wa Dansi.
Kwa sasa Pembe anamiliki bendi yake binafsi, inayojulikana kama Mark Band, ambayo chanzo cha jina ‘MARK’ ni herufi moja moja za majina ya mwanzo ya wanamuziki wanne wanzilishi wa bendi hiyo.
Wanamuziki hao na nafasi zao kwenye mabano, ni pamoja na Mgazija (Bass), Alex (Solo), Rashid (Saxophone) na Karamazoo (Saxophone).
Mark Band iliasisiwa rasmi mwaka 2006, ambapo baada ya kuiunda, waliamua kuwaongeza wanamuziki wengine kama Said Majivu (Drums), Said Makelele (Tarumbeta) pamoja na Noel Minja na Balusi Kitembo ambao ni waimbaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Pembe anasema kuwa, kama ilivyo kwa bendi nyingine nyingi, walipoanzisha bendi hiyo walikumbana na changamoto kemkemu, ikiwa ni pamoja na kukodi vyombo kwa gharama kubwa.
“Hata hivyo, Mungu alitujalia kwani baadaye tulipata mkataba wa kutumbuiza siku tatu katika wiki, kwenye Hoteli ya See Criff, jijini Dar es Salaam, tukaanza kujipanga kwa ununuzi wa vyombo vyetu wenyewe,” anasema Pembe.
Anamtaja Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Mohammed Seif Khatibu kuwa ni kati ya watu waliochangia kuwakwamua ndani ya Mark Band kwa kuwaombea mkopo wa sh. Mil 3, kwenye Hoteli ya See Criff walioilipa polepole kwa kufanya shoo hapo.
Waliitumia pesa hiyo kwa kuchanganya na nyingine walizipata kupitia maonesho yao mengine na kununua vyombo kidogo kidogo hadi sasa wanapomiliki vyombo vyenye thamani zaidi ya sh. Mil 50.
Mwaka 2010 waliingia mkataba na Kampuni ya Kijerumani iitwayo ‘Mother Africa’ wa kutumbuiza nchi mbalimbali kama vile; Misri, Sweden, na nchi za Amerika ya Kusini kama vile Chile na Peru na pia  Ufaransa pamoja na Ujerumani yenyewe.
“Tumekuwa na maisha ya namna hiyo kwa muda mrefu sasa, ya kutumbuiza nje, huku hapa nchini tukifanya shoo nyakati za likizo zetu tu,” anasema Pembe.
Pembe anasema, tayari kwa upande wa nyimbo, Mark Band imeshafyatua albamu nzima, ambapo ni kibao kimoja tu kiitwacho ‘Matukio’ ndicho walichokisambaza kwenye vituo mbalimbali vya radio na runinga hapa nchini.
Vibao vingine kwenye albamu hiyo waliyoirekodia katika Studio za Bakunde Production, jijini Dar es Salaam, ni ‘The Girl From Tanzania’, ‘Baba Kaleta Panya Remix’, ‘Amani’, ‘Anjela’ na ‘Pombe’.
Pembe anasema, mafanikio ndani ya Mark Band ni kumiliki vyombo vya thamani, kuwa na akaunti nono na kujulikana duniani kote, huku mafanikio kwa upande wake ikiwa ni kuwasomesha wanawe na kuanza kuwanunulia viwanja kila mmoja na chake.
Akielezea namna alivyojifunza muziki, Pembe anasema kuwa mwaka 1981 alijiunga na Jeshi la Polisi kama fundi ujenzi, baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari.
“Nikiwa Polisi, wakati najiandaa kupelekwa chuo cha ufundi, Marehemu Tx Moshi William aliyekuwa kwenye bendi ya jeshi hilo wakati huo, alinishauri kuachana na ufundi na kujiunga na kitengo cha Bendi,” anafahamisha Pembe.
Pembe anasema, Tx Moshi alimshauri hivyo kwasababu waliishi mtaa mmoja kabla hawajawa polisi, ambapo alikuwa akimuona namna alivyokuwa ‘mtundu’ kwenye gitaa la Solo.
Kiongozi wa polisi wakati huo, Mzee Mayagilo akamuombea Pembe uhamisho, lakini pia wakati anasubiri kwenda kuendelezwa ujuzi wa kupiga gitaa, mpigaji Saxophone wao, Abdul Mwalugembe akastaafu.
“Tukio hilo lilimfanya Mayagilo kunibadilisha na nikaanza kusomea upulizaji Saxophone, ambapo nilisoma nadharia mwezi mmoja na nusu na vitendo pia muda kama huo, nikawa fiti kabisa,” anasema Pembe.
Anasema kuwa, alirekodi nyimbo nyingi Polisi Jazz, baada ya zile zilizoambatana na ‘Mwaka wa Watoto’, ambazo hata hivyo hazikuchukua chati.
Mwaka 1987 alistaafu ligwaride akiwa askari mwenye cheo cha Koplo, kwa kununua mkataba, baada ya kuvunjika ghafla kwa ahadi aliyopewa na Jeshi, ya kupelekwa nchini Korea kuendelezwa kimasomo, kwa sababu alihisi ndoto zake za kufika mbali kielimu zilishagonga ukuta wa zege.
Akiwa na Vijana Jazz aliyojiunga nayo wakati imetoka kuipua vibao kama ‘Mari Maria’, ‘Ambha’ na ‘Bujumbura’, Pembe anasema kuwa, kibao chake cha kwanza kurekodi kilikuwa ni kile kinachokwenda kwa jina la ‘Miaka 10 ya Umoja wa Vijana’.
“Hadi nafungasha virago Vijana Jazz, niliyoitumikia na kushika nyadhifa mbalimbali za Kiuongozi, nilikuwa nimetunga vibao vinne ambavyo ni ‘Siri ya Ndani’, ‘Baba Sammy’, ‘Mwanamke Salo’ na ‘Dar es Salaam’,” anasema Pembe.
Pembe asiyependa kuona bendi haina maendeleo na ambaye katika muziki anawakubali King Enock na Elias Nyoni, anasema hajapata mafanikio wakati wa Vijana Jazz, zaidi ya kusafiri nchini Zambia pekee.
Kwa mtazamo wake, Pembe anaona biashara huria na udhamini katika vipindi, kwenye vituo mbalimbali vya radio na runinga ndivyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa kuliua Dansi.
Anasema mfumuko wa vituo vingi vya radio na runinga umefanya kuwapo na upendeleo binafsi kwa badhi ya mitindo ya muziki, huku mingine ikididimizwa kwa makusudi kwa manufaa ya watu wachache kama si mtu mmoja.
“Watoto wangu wanaoonekana kufuata kwa karibu zaidi nyayo zangu baba yao, ni Omary (21) ambaye yuko Kisiwani Zanzibar hivi sasa akijishughulisha na muziki wa Hoteli na Mwajuma (15), ambaye bado ni mwanafunzi wa darasa la saba,” anasema Pembe.
Tayari Pembe aliye mbioni kufungua chuo cha Saxophone, ameshawaambukiza wengi kipaji cha upulizaji chombo hicho, badhi yao wakiwa ni wanamuziki wa Dansi, Injili pamoja na miondoko mingine.
Aidha, badhi ya wasanii wa miondoko ya muziki wa Bongofleva waliomshirikisha kupuliza Saxophone kwenye vibao vyao, ni pamoja na Q Chillah, Kikosi cha Mizinga na Cindi katika nyimbo ya pamoja na Ommy Dimpoz.
Huyo ndiye Rashid Pembe, baba wa familia mwenye mke na watoto sita ambao ni Rehema, Pembe, Amina, Omary, Khalid na Mwajuma.
Alizaliwa mwaka 1957, Kisarawe Pwani na kupata elimu ya msingi katika shule nne tofauti ambazo ni Kisarawe, Vikindu, Sotele na Kisiju zote za mkoani Pwani, kuanzia mwaka 1966 hadi mwaka 1972