HAPA AKIPIGA TUMBA SIKU YA MKESHA WA MAZISHI YA REMMY ONGALA |
AKIWA NA MPULIZA SAX MWENZIE JOSEPH BERNARD |
Bombenga anakumbuka kuwa, wakati akiwa na African Stars ambayo hata jina lake alilibuni yeye, walitamba na vibao kama ‘Sakatu Sakatu’, ‘Mayanga’, ‘Maya’, ‘Afrika’ na ‘Dance Dance’.
Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi hilo la African Stars linalojulikana zaidi hivi sasa kama ‘Twanga Pepeta’, ni Bob Gady, Andy Swebe, Alfa Nyuki, Palmena Mahalu, Pamela pamoja na Kayumbu ‘Amigolas’.
“Historia yangu kimuziki, inaanzia mwaka 1972 nilipojiunga na bendi ya Morogoro Jazz, wakati huo nikitokea jeshini Makutupola,” anasema Bombenga.
Mwaka 1973 aliingia na Western Jazz alioshiriki nao kupiga Saxophone, kwenye vibao kadhaa vya bendi hiyo, vikiwamo ‘Hakika’, ‘Kazi ni Kazi’ na ‘Sadaka’, kabla ya mwaka 1978 kutimkia Dar International.
Pamoja na kupuliza kiustadi Saxophone pamoja na kuimba kwenye nyimbo kemkemu, zikiwamo ‘Mayasa’ na ‘Zuena’, lakini pia Bombenga alishiriki kucharaza gitaa la Solo katika kibao ‘Vick’.
Mwaka 1979 alibeba mabegi na kutua Vijana Jazz Band alikotunga kibao ‘Taabu’ na pia kushiriki kukiimba, huku kadhalika akipuliza Saxophone kwenye vibao kama ‘Chiku’ na ‘Matata Ndani ya Nyumba’.
Mwaka 1980 alihamia Maquis ambapo alitesa kwa kupuliza Saxophone kwenye vibao viiingi, baadhi yake ni ‘Zoa’, ‘Sina Ndugu’, ‘Noel’ pamoja na ‘Maige’.
“Nilikaa Maquis hadi mwaka 1984 nilipochomoka tena na kuhamia Bima Lee nilikokutana na wakali kama Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Shaaban Dede ‘Super Motisha’, ‘Joseph Mulenga ‘Spoiller’,” anasema Bombenga.
Mwaka 1985 Bombenga alikuwa mwanzilishi wa bendi ya MK Group ‘Ngoma za Maghorofani’, kabla ya mwaka 1986 kuwa tena mmoja wa waanzilishi wa Tancut Almas ya Iringa.
Mwaka 1987 alirejea tena MK Group ambapo nyimbo yake ya kwanza kupuliza Saxophone awamu hii ya pili ilikuwa ni ‘Utakuja Kuanguka Kwenye Matope’.
Mwaka 1989, kaka yake Adam Kinguti alirudi nchini akitokea Sudan alipokuwa akifanyakazi kwenye ofisi za ubalozi, wakaanzisha Bicco Stars na yeye kushiriki kupuliza Saxophone kwenye vibao kadhaa kama vile; ‘Magret Mage’, ‘Wapangaji’ na Kisamvu’.
Mwaka 1991 alitoka Bicco akiwa na mpapasaji kinanda mahiri wa kike ambaye kwa sasa ni marehemu, Asia Daruweshi, baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na Kinguti, wakaanzisha Zanzibar Sound.
“Tukiwa na Zanzibar Sound, tulipata mkataba katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha na mwaka mmoja baadaye mwanamuziki mwenzetu kwenye bendi hiyo, Kanku Kerry alipata mkataba Japan tukaondoka naye kwa sharti la sasa kujiita Kilimanjaro Connection,” anasema Bombenga.
Walizunguka nchi nyingi za bara la Asia wakiwa na Kilimanjaro Connection, waliporudi mwaka 1994 alijitoa na baadaye kidogo Asia naye alijitoa na kurudisha upya bendi yake ya Zanzibar Sound na kurejea mkataba wake Bahari Beach Hotel.
Bombenga wakati huu akabaki bila bendi, ambapo muda si muda Asia alipata kazi nchini Bahrain na kumuachia Bombenga mkataba wa Bahari Beach.
Baada ya kuona ameachiwa mkataba wakati hana bendi, Bombenga ndipo alipomfuata Baraka Msirwa na kumuomba vyombo vya muziki ambapo alimpa kwavile havikuwa na kazi kutokana na kufa kwa bendi za MK Group, MK Beat na MK Sound zilizokuwa zikivitumia.
“Hicho ndio kilikuwa chanzo cha bendi ya African Stars niliyoibuni mwenyewe hadi jina, iliyoniletea uhasama mkubwa na dada yangu Asha Baraka baada ya kujitoa,” anasema Bombenga.
Kwa upande wa warithi, Bombenga ana wanawe wawili wanaoonekana kufuata vema nyayo zake, ambao ni Feruzi (22) anayepapasa kinanda na Aziza (19) ambaye ni mwimbaji.
Bombenga mwenye miaka 40 katika muziki na aliyejifunza mengi kupitia sanaa hiyo, anavutiwa na waimbaji; Isha Mashauzi, Nasseeb Abdul ‘Diamond’, Flora Mbasha na Hassan Bitchuka.
Anatoa ushauri kwa wanamuziki wa Dansi kuketi na vyombo vya habari na kuzungumza, ili kuangalia namna ya kuurejesha kwenye chati muziki wao ambao umekuwa ukiporomoka kila uchao.
Mikakati ya baadaye ya Bombenga ni kustaafu muziki na kujihusisha na ujasiriamali, baada ya kwenda nchini Kinshasa na kufanya maonesho na baadhi ya mastaa wa huko.
“Mimi ni mtoto wa tano katika familia ya mzee Bilali Mafumu, niliyepata elimu yangu ya msingi katika shule ya H.H Agakhan, Kigoma nilikofaulu na kujiunga na shule ya sekondari Kazima, Tabora nilikosoma hadi kidato cha nne,” anasema Bombenga.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Bombenga aliyesoma shule moja ya sekondari na mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage, anasema kuwa 1972 alijiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ya enzi hizo, alikojifunza kuimba na kupuliza Saxophone.
Anaishi Vingunguti, jijini Dar es Salaam na familia yake ambayo ni mkewe na watoto saba, huku akitamani kuongeza wake wengine hadi wawe watatu.
No comments:
Post a Comment