KWA MASIKITIKO MAKUBWA TUMETAARIFIWA KUWA MWANAMUZIKI WA ZAMANI PAUL GAMA AMEFARIKI DUNIA HUKO DODOMA TAREHE 16.4.2015 MUDA WA SAA NNE ASUBUHI. NARUDIA MAKALA HII YA HISTORIA YA PAUL GAMA KADRI ALIVYOTUELEZA MWENYEWE
Paul Daniel Gama |
Paul
Daniel Gama alizaliwa Barabara ya 11 Dodoma (1947). Baba yake alikuwa ni
mwanajeshi wa KAR mwenye asili ya Songea na mama yake alikuwa na asili ya
Usangu alikuwa anafanya kazi
katika
Spokes Mashiyane na filimbi yake |
hospitali ya Mirembe ambayo wakati huo ilikuwa ni hospitali kubwa
ya majeruhi wa vita ya pili ya dunia. Aliingia shule na alipofika darasa la
nne alijikuta akiwa na kipaji kukubwa cha kupiga filimbi, wakati huo wapiga
filimbi walipenda sana kumuiga mpiga filimbi maarufu kutoka Africa ya Kusini
Spokes Mashiyane. Akiwa na wenzie walianzisha kikundi ambacho kilikuwa na
maskani eneo la Mji Mpya pale Dodoma. Vijana hao pia walikuwa wakiiga nyimbo za wanamuziki maarufu wa wakati
huo, kama Salum Abdallah na Cuban
Marimba, pia Salum Zahor na Kiko Kids. Katika kufanya fani yao hiyo kama kitu
cha kujipa burudani waliligusa sikio la
aliyekuwa mwalimu wa Elimu ya Watu Wazima katika Community Center ya
pale Dodoma. Mwalimu huyu aliwasaidia kuwaazimia amplifaya moja kutoka kwenye
bendi nyingine ilikuweko Dodoma wakati huo, The Jolly Sextet Band. Band
iliyokuwa ikimilikiwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa
East African Postal and Telecommunication Services, huyu bwana alikuja na vyombo vingi akaanzisha
bendi ambayo mmoja wa wapigaji wake alikuwa Mzee Mnenge ambaye hatimaye alitua
NUTA Jazz Band.
Bongos |
Hiki
kikundi cha Gama na wenzie kilikuwa katika mfumo wa Jazz Band za zamani
ambapo walikuwa na ngoma na filimbi tu,ikisindikizwa na kuimba, lakini waliweza
kukonga nyoyo hata za wanamuziki wengine, na Gama akawa anasakwa na bendi
kubwa iliyokuweko wakati ule Central Jazz band. Alipomaliza darasa la saba tu
ndugu yake aliyeitwa Titus Olaf Gama alimshawishi aingie Central Jazz lakini
hakuwa tena mpiga filimbi bali mpiga Bongos, fani aliyoiweza sana hata kuipenda na hasa baada ya kuwaona
wanamuziki wa NUTA akiwemo Muhidin Gurumo
ambaye wakati huo alikuwa akipiga Bongos na kuimba. Bongos no ngoma
ndogo zilizokuwa muhimu katika kundi wakati huo ambapo hakukuweko na drums wala
tumba. Taratibu akaanza kupata hamu ya kupiga bass, wanamuziki wenzie
walimkatisha sana tamaa kwa kuambiwa kuwa vidole vyake vilifaa sana kwa kupiga
bongos na si kupiga gitaa.
Katika
jitihada zake za kujifunza gitaa la bezi alikuwa kila mara akiwahi mazoezi na
kujaribu kujifunza gitaa la bezi. Hilo lilikuwa gumu mpaka pale bendi ya Lake Jazz Band ilipotembelea Dodoma.
Bendi hiyo wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Shem Karenga akiwa anapiga gitaa la bezi, Mzee alum
ambaye alikuwa na ulemavu wa macho, mwanzo alikuwa akipiga gitaa la solo na
baadae akahamia kupiga gitaa la rhythm wakati gitaa solo lilikuja kupigwa na
jamaa aliyeitwa Kally. Kutokana na simulizi ni wazi kuwa wanamuziki wa kutoka
Burundi walikuwa wengi sana nchini wakati huo. Pia katika bendi hiyo alikuweko
Mzee Juma Kitambi, mtunzi wa wimbo maarufu wa Rangi ya Chungwa.
Gama
alichukua nafasi hii kumfuata Mzee Salum ili aweze kumfundisha gitaa. Kwa kuwa
wanamuziki wengine walikuwa wakitoka kwenda kutembea Mzee Salum alibaki
nyumbani na hivyo Gama alichukua nafasi hiyo kumnunulia sigara Mzee Salum ana
kumsihi amfundishe gitaa nae alifanya hivyo na Gama akatokea kuwa mpiga bezi
mahiri.
Katika
kipindi hiki akatokea mfanya biashara Mohamed Omar Badwel, huyu alikuwa na
gereji na studio ya kupiga picha, aliweza kwenda Mombasa na kurudi na seti ya
vyombo na kuanzisha Dodoma Jazz Band. Gama akahama Central Jazz Band na
kujiunga na wanamuziki wengine walioanzisha Dodoma Jazz. Band ilianza ikiwa na
mpiga solo Hassan Mursali mwanamuziki mweny asili ya Malawi, siku hizo ikiitwa
Nyasaland alikuwa ndie mpiga solo, lakini aliwaacha baadae na kujiunga na NUTA
Jazz Band, upigaji wake wa solo unaweza kuusikia katika kusikiliza kibao kimoja
maarufu cha NUTA, kilichoitwa Dunia Njema
Kukaa Wawili.
Hasan
alikuwa mtu wa kuhama hama hatimae alipoteza uwezo wa kusikia jambo ambalo
lilihusishwa na kuhamham kwake kwani ushirikina ulitawala sana wakati huo, kama
maelezo yanayofuata yanavyoonyesha. Dodoma Jazz ilikuwa pia inafanya ziara
katika sehemu nyingi , kama vile Iringa, Mbeya ,Tabora, Dar es Salaam na
kadhalika, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilifanyika ikiwa na lengo la
kumfuata Abel Barthazal aliyekuwa akipiga katika bendi ya Kilosa Jazz.
Bendi ilipokelewa vizuri na wakafanya
maonyesho yao Kilosa na hatimae kuondoka na Abel. Siku chache baade wakati huo
Mzee Mohamed Omar, mwenye bendi
alikuwa kasha mnunulia suti kadhaa Abel, ukaja ugeni toka Kilosa wakiwa na
barua yenye maelezo kuwa ikiwa Abel Hatarudi Kilosa, mmoja wa wanamuziki wa
Dodoma Jazz atafariki, na barua hii ililetwa kwa mkono na mjumbe ambae
alisisitiza wakishaisoma mbele yake ndio anaondoka. Abel alirudishwa Kilosa
mara moja.
Baada
ya hapo aliyekuwa meneja wa bendi Ramadhan Waziri alitumwa Burundi kwenda
kutafuta wapigaji, siku alipokuwa anarudi na wapigaji wapya akakutana kwenye
treni na Rashid Hanzuruni, mpiga solo mahiri sana ambaye upigaji wake husikika
katika wimbo Napenda nipate lau nafasi
Hanzuruni
alikuwa kaiacha Tabora Jazz baada ya
kutokea ugomvi mkubwa ambapo alipoteza meno kadhaa, hivyo alikuwa kwenye
hilo treni akielekea Dar es Salaam kumfuata mpigaji mwenzie Samba ambae alikuwa
NUTA Jazz. Ramadhani aliweza kumshawishi hanzuruni akabaki Dodoma Jazz ambako
alikaa kwa muda na hatimae akaja kuchukuliwa na Sama ili aingie NUTA Jazz,
ndoto hiyo haikufanikiwa kwana NUTA alikuweko mpigaji mahiri Hamisi Franco, hii ndiyo ilipelekea
Hanzuruni kwenda Western Jazz Band
No comments:
Post a Comment