Ukifungulia redio siku hizi utakumbana na aina mbalimbali za
muziki ambao washiriki wake ni Watanzania, utasikia taarab, bongofleva, rumba,
rege, muziki wa asili na muziki wa kisasa wenye vionjo vya kiasili na
kadhalika. Je hapo mwanzo ilikuwaje? Kupata picha italazimu turudi nyuma kabla ya kuanzishwa kwa ukoloni wa
Kijerumani. Watu wa nchi hii waliishi kwa makundi ya kikabila na hivyo kila
kundi kuendeleza utamaduni wake na sanaa zake ikiwemo ‘muziki’.
Saturday, April 14, 2018
Saturday, January 6, 2018
TASNIA YA MUZIKI 2017 KWA UFUPI
Kuanzia
mwaka 2012 nimekuwa nikimaliza mwaka kwa kuandika makala ya mtizamo wangu
kuhusu hali ya muziki katika mwaka uliokwisha. Na mwaka 2017 ndio huoo
umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Kama
ilivyokuwa kwa miaka mingi sasa, anga za muziki wa nchi yetu zilitawaliwa na
muziki wa Bongoflava. Muziki ambao kwa asilimia kubwa hutengenezwa studio,
hakuna shaka watu wengi nchini na nchi
jirani wametokea kuupenda sana muziki huu. Katika mkutano ulifanyika wiki
chache zilizopita, kiongozi mmoja wa mambo ya Hakimiliki kutoka Kenya alisema asilimia kubwa ya muziki
unaopigwa kwenye vyombo vyao vya utangazaji ni wa kutoka Tanzania. Imefika
mahali mpaka wasanii wa huko wameanza kudai muziki wa Tanzania upunguzwe ili
wao waweze kupata nafasi zaidi katika redio na luninga zao. Inachekesha kuwa
kilio kama hichohicho kinasikika kwa wanamuziki wa aina tofauti nchini
kuhusiana na ‘kufunikwa’ na Bongofleva. Wasanii wa Bongofleva wameendelea
kupata tuzo kutoka kwa taasisi mbalimbali za Kimataifa, na hata wengine kuingia
mikataba na kampuni kubwa za kimataifa za usambazaji, na kwa picha hii
Bongoflava itaendelea kutawala anga za muziki hata mwaka ujao. Muziki ambao
tunaweza kusema chanzo chake ni muziki wa mchiriku wenye asili ya ngoma za
Kizaramo, maarufu kama muziki wa singeli nao ulikuja juu sana kwa miezi
michache ya mwaka huu, japokuwa ule moto wake unapungua, inawezekana muziki huo
unajimaliza wenyewe kutokana na mashahiri yanayotumika katika nyimbo hizo, na
hata video zinazo ambatana nazo, lakini hakika muziki huu ni ubunifu unaoweza
kuitwa muziki wa asili ya Kitanzania bila shaka yoyote. Hakukuwa na mambo ya
kushtua sana katika muziki wa Taarab hali hiyohiyo pia ilionekana katika muziki
wa dansi. Bendi kadhaa na vikundi vya taarab vilitangaza kuanzishwa lakini havikuja
na kitu kipya cha kuweza kuleta mshtuko katika tasnia, kifupi hakukuwa na jambo
lolote chanya la kukumbukwa kutoka upande huo kwa mwaka 2017. Pamoja na kuwa
haukuonekana kuwa umeshuka lakini pia hakukuwa na dalili za kupanda kwa muziki
wa Enjili, kwenye sanaa usipopanda ujue umeshuka. Muziki wa kwaya ulianza
kujitokeza zaidi hasa kwenye kutoa elimu ya mambo mbalimbali ya kijamii na pia
kurudia nafasi yake ya zamani ya kusifia viongozi mbalimbali, kazi ambayo kwaya
ilikuwa ikifanya toka miaka ya mwanzoni baada ya Uhuru. Kwaya kadhaa ziliweza
kutengeneza video ambazo zimekuwa zikionekana kwenye luninga, japo ni wazi
hazikutengenezwa kwa ajili ya biashara. Kuna kundi la wanamuziki ambao wao husema
huwa hawana nia kabisa ya kusikika kwenye vyombo vya utangazaji vya hapa
nchini, wao hutengeneza muziki kwa ajili ya maonyesho ya nje ya nchi.
Wanamuziki hawa wameendelea kuwa na safari za kwenda nje kupiga muziki wao
katika matamasha ya kimataifa bila kuhangaika kutambulisha kazi zao hapa
nchini, sababu kubwa ambayo wamekuwa wakitoa ni urasimu wa taratibu za muziki
kusikika katika vyombo vyetu vya utangazaji.
Hivyo badala ya kupoteza muda kupingana na mfumo, wao wameendelea na
shughuli za kujitambulisha nje, ni nadra habari zao kuonekana kwenye vyombo vya
habari vya nchini japo wanazunguka nchi mbalimbali duniani wakipiga muziki
unaotambulika huko kuwa ni wa Kitanzania.
Muziki wa asili ni kazi ambayo
inaonekana ni kwa ajili ya watalii na shughuli maalumu za kiserikali au sherehe
za kifamilia. Picha hii inadanganya kwani muziki asili unaendelea nchini mijini
na vijijini japo hauonekani kwenye vyombo vya utangazaji, labda pale ambapo ni
kiburudisho cha viongozi. Muziki wa asili uko katika makundi mawili, uko muziki
ambao unafanywa na wasanii ukiwa ni mchanganyiko wa ngoma mbalimbali ili kuweza
kuvutia biashara, na uko muziki asili ambao huchezwa na kuimbwa na wenye kabila
lao kwa upenzi wa utamaduni wao. Kwa kuwa hauonekani wala kuzungumziwa sana
kwenye vyombo vya utangazaji, unaweza ukadhani haupo au haupendwi lakini hilo
si sahihi. Maelfu ya vijana nchi nzima wanacheza na kupiga ngoma za kiasili kwa
ufasaha mkubwa.
Kumekuweko na matamasha kadhaa ya muziki
nchini, kama tamasha la Fiesta, Marahaba, Tulia Traditional Dance Festival, Sauti
za Busara, Karibu Music Festival na kadhalika, lakini matamasha haya ilikuwa ni
nafasi ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanamuziki walioko nchini. Wilaya,
mikoa nayo ingeweza kutayarisha matamasha yake ya utamaduni ingekuwa sehemu
nzuri sana ya kuendeleza utamaduni, wasanii kubadilishana ujuzi, kuibua vipaji
na kuleta burudani kwa wananchi kwa
ujumla. Ufadhili katika shughuli za muziki umekua ukiangalia sana faida za
kibiashara, kumekuwa na kampuni chache ikiwa zipo ambazo zimefadhili matamasha kwa
nia tu ya kuendeleza muziki. Matamasha mengine yamekuwa yakitegemea ufadhili wa
balozi mbalimbali za nje kuwezesha kufanya maonyesho ya muziki wetu. Ni
kichekesho kwa kweli. Hata zile kampuni ambazo ni maarufu nje ya Tanzania kwa
kuunga mkono shughuli za sanaa, kwa namna ya ajabu zikiwa Tanzania ghafla
zinakuwa na msimamo tofauti.
Maeneo ya
kufanya shughuli za muziki yamezidi kupungua, mengine yamevunjwa na maeneo
kuachwa wazi kama vile eneo lilokuwa DDC Magomeni na Mango Kinondoni, mengine
yamekuwa makanisa na kadhalika. Pamoja na kuwa kulikuwa na wimbi la kujenga
kumbi ambazo hutangazwa kuwa ni ‘multi purpose’, kumbi hizi haswa zilijengwa
kwa ajili ya kufanyia shughuli za harusi, kuna mambo kadhaa ambayo si rafiki
kwa muziki katika kumbi hizi, na hata wenye kumbi hukataa kumbi zao kutumika
kwa shughuli za muziki hasa wa dansi.
Katika mwaka 2017 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Dr Harrison Mwakyembe amekuwa na mikutano mingi na wanamuziki, jambo jema
kinachosubiriwa 2018 ni matokeo ya mikutano hii. Ushauri kwa wanamuziki ambao
muziki wao unajikongoja, kuna umuhimu wa kutafuta majibu ya kisayansi kwanini
hali iko hivyo. Majibu mepesi ya kulaumu vyombo vya habari, serikali na wadau
wengine, kamwe hayata saidia katika kuleta mabadiliko.
Thursday, June 29, 2017
HATIMAE MWANAMUZIKI MKONGWE BROTHER ZENNO AZIKWA
MWANAMUZIKI na mchambuzi wa muziki wa charanga maarufu kwa jina la Brother Zeno hatimae amezikwa na makaburi jirani na alipokuwa akiishi kule Mbagala Kibondemaji. Zerno ambaye alikuwa muimbaji mzuri atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Dar es Salaam Jazz B, bendi iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya, ambayo ilianza kufanikiwa kwa kasina kuanza kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A, chini ya Michael Enoch, bendi ikavunjwa na wanamuziki wengine wakaingizwa Dar Jazz A, lakini Patrick akakasirika na kutokomea , baadae akaja kuanzisha Afro 70 na kufanya mambo makubwa. Baadae Brother Zeno alijiunga na Shirika la Bima ya Taifa, na baada ya kujiunga kampuni hiyo ndie aliyetoa msukumo wa kuanzishwa kwa bendi katika shirika hilo, Bima Jazz Band na hivyo pia kupewa kazi ya kutafuta wanamuziki wa kujiunga na bendi hiyo na yeye mwenyewe kuwa kati ya wanamuziki waanzilishi wa kundi hilo lililokuja kujizolea umaarufu mkubwa. Kati ya wanamuziki wa kwanza katika bendi hiyo waliobaki hai sasa ni wawili tu baada ya kifo cha Zeno.
Binti pekee wa marehemu akiwa na mumewe wakiweka shada la maua |
Baadhi ya wanamuziki waliohudhuria mazishi ya Brother Zeno |
Aliyekaa ni Abdallah Mbosanga mmoja ya wanamuziki wawili waliobaki hai wa bendi ya Bima Jazz band ya kwanza. Mwingine ni Duncan Ndumbalo |
Tuesday, June 27, 2017
BROTHER ZENNO AFARIKI DUNIA
RIP Brother Zerno |
Hakika siku za karibuni zimekuwa ngumu kwa wapenzi wa muziki wa zamani, mfululizo wa misiba na wanamuziki kuugua kumekuwa ni habari karibu kila siku. Mchambuzi mahiri wa muziki wa Charanga Zerno Andrew Lucas, aliyefahamika zaidi kwa jina Brother Zeno, amefariki dunia asubuhi leo katika hospitali ya Temeke, Brother Zeno aliyekuwa akishirikiana na 'Mzee wa Macharanga' Charles Hillary enzi hizo Radio One, alikuwa na ufahamu mkubwa wa muziki wa kutoka Cuba na hivyo kuwa mpenzi mkubwa wa watu waliopenda muziki huo. Brother Zeno amesumbuliwa karibu mwaka mzima na tatizo la moyo na katika siku zake za chache mwisho alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine, alitegemewa angepata nafuu na kuhamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi lakini Mungu amekuwa na mipango mingine.
Msiba wa Mzee utakuwa nyumbani kwake Mbagala Kibonde Maji na mazishi yatakuwa kesho 28/6/2017 saa kumi hukohuko Mbagala
Friday, June 23, 2017
SHAABAN DEDE ANAUMWA AMELAZWA MWAISELA NO 5
Mwanamuziki mkongwe Shaaban Dede 'Kamchape' amelazwa leo katika hospitali ya Muhimbili wadi ya Mwaisela No 5. Wapenzi wa muziki tumkumbuke katika swala zetu.
Monday, June 5, 2017
MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AFARIKI DUNIA
HALILA TONGOLANGA, mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Muhimbili amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Halila alikuwa amesafirishwa kutokea Ndanda kuja Muhimbili akihisiwa kuwa na matatizo ya figo. Licha ya kuwa alifika Muhimbili juzi Ijumaa usiku, lakini alikuwa hakufanyiwa vipimo vyovyote vikubwa mpaka umauti unamkuta. Jana Jumapili ililazimika kuanza kufanya jitihada za kupata daktari ambaye angemshughulikia kwa karibu zaidi, na daktari alipatikana ambaye aliahidi angeanza kufwatilia swala lake leo asubuhi lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa tofauti. Juzi nilipomuona alinambia kuwa ana mengi anataka kunambia, lakini moja aliloweza kunambia pale ni kuwa yeye anajihisi ana kansa, 'Nilimuuliza anajuaje hilo, kwa vile hajapimwa hakuwa na jibu"
Wengi tutamkumbuka Tongolanga kwa wimbo wake wa Kimakonde aliouimba kwa mara ya kwanza akiwa na Les Mwenge 'Kila Munu Ave Na Kwao"
Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa leo saa tano kuelekea kwao Newala. Habari zaidi zitawafikia kupia hapa
Mungu amlaze Pema peponi Halila Tongolanga
Wengi tutamkumbuka Tongolanga kwa wimbo wake wa Kimakonde aliouimba kwa mara ya kwanza akiwa na Les Mwenge 'Kila Munu Ave Na Kwao"
Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa leo saa tano kuelekea kwao Newala. Habari zaidi zitawafikia kupia hapa
Mungu amlaze Pema peponi Halila Tongolanga
Saturday, June 3, 2017
TONGOLANGA ANASUBIRI VIPIMO
Katibu Mtendaji wa BASATA mwenye kitenge akiwa na Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, walipomtembelea Tongolanga asubuhi ya leo. |
Halila Tongolanga kwa kweli anaumwa. Kwa maelezo ya mdogo wake, ni mwezi wa tatu sasa anaingia na kutoka hospitali mbalimbali. Mpaka jana alikuwa katika hospitali ya Ndanda, na kwa msaada wa Mbunge wa Tandahimba aliweza kupatiwa Ambulance na kufikishwa Muhimbili ambako amelazwa Kibasila No 10. Mpaka jioni ya leo alikuwa anasubiri vipimo.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.
Friday, April 28, 2017
SI KWELI KUWA HARRISON SATCHMO SIWALE ALIFIA GEREZANI,
Mar. Harrison Siwale-Satchmo |
......................
SIKILIZA HAPA GUITAR LA MZEE SIWALE...................
Tarehe 8 September 2013, niliandika katika blog hii habari niliyoipa kichwa cha habari, Harrison Siwale aliishia wapi? Ni habari ya kusikitisha.
Tarehe 8 September 2013, niliandika katika blog hii habari niliyoipa kichwa cha habari, Harrison Siwale aliishia wapi? Ni habari ya kusikitisha.
Niliandika hivi-----Nimetoka
kuongea na Mzee mmoja ambaye nilimuomba anitafutie habari za Harrison
Siwale aka ‘Satchmo’, ambaye alikuwa
mpiga rhythm mahiri na maarufu sana katika miaka ya sabini, Harrison alikuwa na
staili ya pekee ya upigaji wa gitaa wa kudokoa nyuzi na kupata aina ya pekee ya
mlio wa gitaa. Kati ya nyimbo ambazo upigaji huu unasikika ni katika nyimbo za
Jamhuri Jazz Band kama vile Mganga 1
na 2, Blandina na kadhalika. Pamoja na bendi nyingine Harisson aliwahi
kupigia Atomic na Jamhuri Jazz Band zote za Tanga, na kisha kuvuka mpaka na
kuwa na makazi Mombasa kwa muda mrefu ambako aliendelea na muziki. Kwa kadri ya
maelezo niliyopewa leo na huyu Mzee niliyemuomba anitafutie habari ili nijue yu
wapi huyu mwanamuziki siku hizi? Haya ndio aliyonambia.
'Baada
ya kufa kwa yale makundi ya Simba wa Nyika na Les Wanyika, Harrison Siwale
alianza kupiga muziki wa Injili katika eneo la Kilifi. Akawemo katika kundi
lililokuwa likifanya maonyesho yake katika miji mingi ikiwemo Mombasa na
Nairobi. Umahiri wake wa kazi ukamfanya mwenye vyombo vya hilo kundi
alilokuwemo Harrison kumuamini sana na kumuachia awe kiongozi wa kundi hilo na
kuwa huru kuzunguka sehemu mbalimbali. Inasemekana Harrison akapata tamaa ya
kuingia mitini na vyombo vile, hivyo ghafla akapotea. Taarifa zikamfikia mwenye
vyombo kuwa vyombo vyake viko njiani kuvushwa kungia Tanzania kupitia mji wa
Lungalunga. Mwenye vyombo akaweka mtego hapo na Harrison akakamatwa hapo akiwa
na vyombo hivyo, kesi ilifika mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka
mitatu'. Baada ya hapa kuna hadithi mbili, moja ikisema alifia gerezani Shimo la
Tewa, na nyingine ikisema alifariki baada ya kumaliza kifungo chake.
Je,
nini hasa kilitokea? Najaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kupata hadithi
zaidi kuhusu mwanamuziki huyu.
HATIMAE (2017 APRIL).... Kwa bahati sana nimeweza
kuanza kuwasiliana na mtoto wa Harrison Satchmo Siwale, ambae tuliweza
kukutana kupitia facebook. Kijana huyu ambaye jina lake ni Salehe Siwale aliweza
kunambia kuwa baba yake alimuoa mama yao na walizaliwa vijana wawili yeye na
kaka yake.
Na
niliweza kupata taarifa za ziada baada ya kuniunganisha na mama yake ambaye
ndie alikuwa mke wa Mzee Siwale nikaweza kuongea nae mubashara kupitia video call ya whatsapp. Kwanza kabisa mama huyo ansema kuwa katika
kipindi alichoishi na Mzee Siwale hakuwahi kufungwa wala kuzungumzia kuwa
aliwahi kufungwa. Na Mzee Siwale alifariki katika Kitongoji cha Rongai huko Nakuru na kuzikwa tarehe
31/3/2013. Ukiangalia kuwa taarifa ya awali niliyopewa ilikuwa katika miezi michache baada ya kifo chake, niwazi si kweli kuwa alifia Gerezani na kama angekuwa aliwahi kufungwa hakika
mkewe angekuwa anajua.
Mungu
Amlaze Pema Mchungaji Harrison ‘Satchmo’ Siwale
Saturday, April 22, 2017
KIFO CHA SOKOINE KILIIKUTA ORCHESTRA MAMBO BADO IKO SHINYANGA
Mwaka 1984 nilikuwa mwanamuziki wa bendi ya
Orchestra Mambo Bado, bendi iliyokuwa inaongozwa na Tchimanga Kalala Assossa.
Bendi ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wa bendi
ulikuwa unajulikana kama Bomoa. Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa
Tutajenga Kesho, wimbo ambao baadae
kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa
Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule, usisike kwenye radio ya Taifa,
redio ambao ilikuwa pekee wakati huo. Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu
ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji,
Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Banza Tax muimbaji, Athumani
Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi, Andre
Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe
wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm.
Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja
na meneja wa bendi. Masikani ya bendi yalikuwa katika ukumbi wa Lango la Chuma,
Mabibo Dar es Salaam
Tarehe 12 April 1984, kundi zima lilitua katika mji
wa Shinyanga baada ya kuwasili hapo kwa treni kutokea Dar es Salaam. Kwa
taratibu za miaka hiyo, pamoja na ratiba ya ziara ya bendi kutangazwa kwenye
gazeti la Uhuru, meneja wa bendi alikuwa akilazimika kutangulia mji ambao dansi
litapigwa kuwahi kufanya mikataba na kumbi ambazo dansi lingepigwa na pia kufuatilia vibali mbalimbali
vya kuruhusu onyesho kufanyika. Mawasiliano yalikuwa magumu na urasimu ulikuwa
mkubwa. Haikuwa kazi rahisi maana miaka hiyo ili bendi isafiri ililazimika
kupata kibali cha Afisa Utamaduni
wa Mkoa ambao ni masikani ya bendi kuruhusu bendi kutoka nje ya Mkoa na kisha
kibali hicho kupelekwa kwa Ofisa Utamaduni wa Mkoa ambao bendi inakwenda, nae
baada ya kuruhusu bendi kuingia mkoani kwake, unaomba kibali cha Afisa Utamaduni
wa Wilaya unakotaka kupiga muziki ili nae akuruhusu kufanya onyesho kwenye
wilaya yake. Baada ya hapo meneja hutafuta na mtu ambaye ana spika ya mkononi,
megaphone kuikodisha na kisha kutafuta mtu wa kutangaza onyesho. Ili kubana
matumizi kuna mara nyingine wanamuziki wenyewe ililazimika wapite mtaani na
spika hiyo kujitangaza. Kulikuwa na mji kama Mpanda wakati huo, ambapo
mtangazaji hakuwa na megaphone, mtu maalumu alipita mtaa kwa mtaa akiwa na
ngoma ambao aliipiga watu wakikusanyika basi anatangaza ujio wa bendi katika
mji wao.
Tarehe 12 April 1984, Orchestra Mambo Bado iliwasili
Shinyanga kwa treni ikitokea Dar es Salaam, kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa.
Wanamuziki tulionyeshwa vyumba vya kulala, mambo yalionekana kuwa yatakuwa
mazuri kwa siku ile, matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye nguzo za umeme
sehemu mbalimbali za mji, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya
ujio wetu ilikuwa dhahiri. Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi ilipotangazwa kuwa
nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki
katika ajali ya gari jirani na Morogoro. Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu
akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa
sana, tulikuwa na nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku
moja tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na
kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake, tukitegemea mapato
mengine makubwa katika maonyesho ya Mwanza wikiendi iliyokuwa inafuata. Hayo
yote tulijua sasa yameharibika, tulirudisha vyumba vyote mara moja na kubaki na
viwili tu kimoja kikiwa cha wasichana waliokuwa kwenye bendi, wengine wote
ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kingine. Baadae tulikaa na Afisa
Utamaduni kutafakari kama dansi lingeweza kulia siku ile, na kama halitalia
nini hatima ya watu hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam? Kama kiasi cha saa
moja jioni, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya
kurudi Dar es Salaam, kwani ilijulikana wazi kitaanza kipindi cha maombolezo
ambacho hakuna mtu alijua kitaisha lini,
hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea na safari kutoka hapo. Vipindi vya
maombolezo huwa ni vipindi ambavyo pamoja na mambo mengine shughuli za muziki
husimamishwa. Kwa wanamuziki na wale wanaotegemea shughuli za muziki na familia
zao, kipindi hiki huwa kigumu sana. Lakini kinaleta ukakasi akilini kwani shughuli
za kupiga muziki kwenye kumbi husimamishwa, madisco hufungwa na vikundi vya
muziki haviruhusiwi kufanya kazi
lakini radio huendelea kupiga muziki uleule ambao umezuiwa kwenye kumbi, sehemu
za starehe kama baa huendelea kupiga muziki na kufanya biashara zao bila tatizo
ila wanamuziki ndio huzuiwa kufanya shughuli zao kwa maelezo kuwa ni kipindi
cha maombolezo. Nakumbuka sana misiba
mikubwa ya viongozi wetu ukiwemo wa Baba wa Taifa kwa sababu kubwa
mbili, kwanza uchungu wa kupoteza kiongozi wetu na njaa iliyofuatia baada ya
hapo.
Saturday, March 18, 2017
AMRI BILA TAFITI ZINAATHIRI SANA SEKTA YA MUZIKI
KATIKA
shughuli ambazo watu wengi huona ni rahisi kuendesha na kutoa maamuzi bila
utafiti ni soka na muziki. Ukisikiliza mazungumzo baada ya mechi za soka ndipo
utakaposikia watu wanavyotoa ushauri au kukosoa wachezaji, kocha refa, chama
cha mpira wa miguu, hakika ingewezekana watu hawa wakapata mamlaka, maamuzi
yangekuwa ya ajabu sana.
Hali
kadhalika kwenye muziki. Kwa mfano ukiuliza, kwanini muziki
wa bendi hauna umaarufu kama zamani? Hakika ukipita kila mtaa utapata majibu, wengine
watakwambia kosa la vyombo vya utangazaji , wengine watakwambia wanamuziki
wenyewe , wengine watakwambia serikali, na pia utapewa maelekezo mbalimbali ya
nini kifanyike. Bahati nzuri majibu haya ya mtaani hayana madhara kwani huishia
hapo hapo. Lakini bahati mbaya huja pale ambapo viongozi wenye mamlaka nao hugeuka
wataalamu wa muziki na wao kutoa maamuzi kadri ya mtizamo wao, lakini maamuzi
yao huwa amri, na amri inapotolewa bila utafiti wa kutosha madhara yake
yanaweza kuendelea miaka mingi baadae. Ninaloweza kusema kwa uhakika, ni kuwa
muziki wa Tanzania leo ungekuwa katika nafasi ya juu zaidi duniani kama
isingekuwa maamuzi ambayo yalitolewa bila utafiti miaka ya nyuma. Labda nitoe
mifano kadhaa. Mpaka miaka ya 70, wanamuziki wa Tanzania walikuwa wakienda
sambamba na wanamuziki wa nchi nyingine nyingi Afrika, licha ya kutokuwa na
miundo mbinu muhimu katika maendeleo ya muziki kama vile kutokuwa na kampuni za
kurekodi na kutengeneza santuri. Lakini kimuziki, wanamuziki wa kipindi hiki walikuwa
bega kwa bega na wenzao ambao walikuwa na miundo mbinu stahiki. Tanzania tulikuwa
na bendi ambazo zilikuwa zinapiga
muziki wa rumba, nyimbo nyingi za wakati huo mpaka leo bado zinasifika na
kupendwa katika anga za muziki. Pia tulikuwa na wanamuziki vijana ambao wengi wao walikuwa mashuleni,
hawa wakiwa na mtizamo mpana zaidi wa kutambulika duniani, wanamuziki hawa kama
ilivyokuwa sehemu nyingi Afrika walianza kupiga muziki uliojulikana kama Afro
Rock, muziki ambao ulichanganya mahadhi ya muziki asili wa Kitanzania na mapigo
ya kizungu, wakifuatia nyayo za kundi la Osibisa, na wanamuziki kama Ransome
Fela Kuti. Kukawa na makundi kama Afro 70, Trippers, Sun Burst, The Jets na
kadhalika kwa kuyataja machache, makundi ambayo yalianza kuingiza muziki wa
Tanzania kwenye soko kubwa zaidi la Kimataifa, kwa mfano wimbo wa Weekend wa
Afro70 uliingia kwenye Top Ten Nigeria miaka hiyo, wakati huo muziki wa Nigeria
haukuwa na umaarufu wowote nchini kwetu.
Kwa kuwa vijana hawa wengi walikuwa bado shuleni, na kufuatana na
maadili ya wakati ule, wanafunzi hawakuruhusiwa kushiriki madansa ya usiku, hivyo basi kulikuweko na
utamaduni wa madansa ya mchana yaliyoitwa Bugi. Hapo vijana walikusanyika
kupiga muziki wao kila mwisho wa wiki, shughuli zikianza saa nane mchana na
kuisha saa kumi na mbili jioni. Lakini siku moja kiongozi mmoja akatokea na
kupiga marufuku Bugi, hivyo kuwaondoa wanamuziki vijana wengi kwenye muziki kwani
wasingeruhusiwa kushiriki madansi ya usiku. Wakati vijana hao wanaacha muziki, vijana wengine Afrika
waliendelea mbele. Hata majirani zetu Kenya na Zambia wakawa na wanamuziki
wengi walioweza kuingia katika soko la Kimataifa, wanamuziki wetu walikosa
fursa hiyo. Pengo hili linaendelea kuwepo mpaka leo. Kuziba pengo hilo
kunahitaji kutafiti tulipojikwaa na kuangalia tunafanya nini kurekebisha hali
iliyopo. Swala la kupiga marufuku kazi za muziki si jambo geni katika historia
ya muziki, kulikuwa na maamuzi kadhaa ya kisiasa pia ambayo pia hayakuwa na
utafiti hivyo kudhoofisha maendeleo ya muziki Tanzania. Kwa mfano kulishawahi
kutolewa amri ya kupiga marufuku wacheza show, wakati huo karibu bendi zote
kubwa za muziki wa rumba kote Afrika Mashariki na Kati zilihakikisha kuwa
zinakuwa na kundi la wacheza show, na waimbaji maarufu kama Mbilia Bel na
Tshala Mwana wote awali walikuwa ni wacheza show. Kwa kipindi kirefu kulikuweko
na sinto fahamu ya wacheza show na ikalazimika taaluma hiyo irudi kinyemela
kwani makundi yote ya muziki kutoka nje yalipokuja nchini yalisindikizana na
wacheza show. Nyimbo kadhaa ziliwahi kupigwa marufuku na hatimae kuja kuonekana
ni za muhimu katika jamii, ukiwemo wimbo maarufu wa Super Matimila, Mambo kwa
Soksi, ambao ulipigwa marufuku na baade kuonekana ni wimbo muhimu kuhamasisha
watu kutumia kinga katika zama hizi za balaa la Ukimwi. Upigaji marufuku wa
tungo unakwaza watunzi na kuishia kutunga nyimbo nyepesi ambazo zina uhakika wa
kutokupigwa marufuku. Katika miaka ya karibuni kumewahi kufanyika maamuzi
kadhaa yasiyokuwa na utafiti kwa mfano, serikali iliwahi kununua mashine iliyoitwa Mastering Mixer
kwa gharama ya shilingi milioni 50, kwa maelezo kuwa ndio itakayowezesha
kumaliza wizi wa kazi za muziki. Sio siri wizi uko palepale. Hayo yalikuwa
maamuzi bila utafiti, ni vizuri kujua hiyo ‘mixer’ iko wapi ili kutathmini ni matokeo ya uamuzi huu
uliogharimiwa na serikali. Uamuzi mwingine ulikuwa ni ule wa kutunga sheria ya kuweka
stempu za TRA kwenye kazi za sanaa, kwa maelezo kuwa utamaliza wizi wa kazi za
muziki na filamu. Si mara moja taarifa imatolewa kuwa serikali ilitoa milioni
20 kwa mtafiti toka ‘Chuo Kikuu’ kuhakiki kuwa njia hiyo ndio itamaliza wizi wa
kazi za sanaa, hakuna ‘mtafiti’ anayejitokeza kuwa alipokea fedha na kufanya
utafiti huo, wala hakuna nakala ya utafiti huo, ni aina nyingine ya maamuzi
bila utafiti na matokeo yake wizi wa kazi za sanaa umeenea kila kona nchini na
mauzo halali ya kazi za muziki yamepotea. Ushauri tu kwa viongozi kuwa muziki
si shughuli ya kubahatisha ina misingi yake, ni muhimu kwa manufaa ya Taifa, umefika
wakati wa kufanya utafiti kwanza kabla ya kutoa maamuzi.
Tuesday, January 31, 2017
URAFIKI JAZZ BAND
Mzee Juma Mrisho aka Ngulimba wa Ngulimba liyekuwa Kiongozi wa Urafiki Jazz Band |
Bendi ya Urafiki (Urafiki Jazz Band), ilianzishwa mwaka 1970 na kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichopo Ubungo. Jina rasmi la kiwanda lilikuwa ni FRIENDSHIP TEXTILE MILL. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiki kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kilitex, na kadhalika
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue – Dar Es Salaam.
Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha Nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara.. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za Urafiki Jazz Band zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.
Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Michael Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu – Besi, Abassi Saidi Nyanga – Tenor Saxophone na Fida Saidi, Alto Saxophone. Ngulimba yeye akawa Muimbaji na pia Kiongozi wa Bendi.
Wanamuziki wengine wa mwanzo ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa – Juma Ramadhani Lidenge – Second Solo, Mohamed Bakari Churchil – gitaa la kati (rhythm), Ezekiel Mazanda – rhythm, Abassi Lulela – Besi, Hamisi Nguru – Muimbaji, Mussa Kitumbo – Muimbaji, Cleaver Ulanda – Muimbaji, Maarifa Ramadhani – Tumba, Juma Saidi – Manyanga (maraccass) na Hamisi Mashala – mpiga drums.
Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’
Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga na kundi akiwa mpigaji wa Saxophone.
Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi baadhi wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz wengine wakiwemo Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu – Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.
Pia waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta, hao walikuja 1973 na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Urafiki Jazz imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k..
Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja – D’Salaam na kushika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.
Saturday, November 12, 2016
RAJABU OMARY KUNGUBAYA APATA MGUU WA BANDIA KUTOKA KWA WAPENZI WA MUZIKI WA ZAMANI
Marehemu Omary Kungubaya |
Rajabu Kungubaya |
Rajabu
Omary Kungubaya, mtoto wa marehemu Omary Kungubaya, mwanamuziki ambaye alipata
umaarufu kutokana na wimbo wake wa ‘ Salamu za wagonjwa’ uliokuwa wimbo wa
kufungua na kufunga kipindi cha salamu za wagonjwa kilichokuwa kikirushwa na
Radio Tanzania, leo amepokea mguu wa bandia ili kumsaidia kutokana na mguu wake
wa kulia kuwa umekatwa kutokana na ajali ya bodaboda. Wanamuziki John Kitime na
Mjusi Shemboza walimuona Rajabu kwa mara ya kwanza siku walipoenda kumzika Mzee
Kungubaya na kuona umuhimu wa kumsaidia Rajabu kutokana na hali yake ya kutegemea magongo wakati
wa kutembea. Kwa kutumia kundi a Whatsapp la ZAMA ZILE, (kundi la wapenzi wa muziki wa zamani wanaosikiliza kipindi cha ZAMA ZILE kinachoendeshwa na John Kitime kupitia EFM 93.7fm kila Jumapili kuanzia saa 2-5 usiku), wanakikundi waliweza kuchanga fedha zilizowezesha kijana huyu kupata mguu wa bandia.
Rajabu ni mchangamfu anaeonekana kupendwa na kila mtu, kutokana na
majirani zake wote kumuunga mkono ikiwemo serikali ya mtaa wake. Mwenyekiti wa
serikali ya mtaa akiwa na wajumbe wengine wa serikali ya mtaa wake wote
walimsifu kwa tabia yake ambayo walisema ilikuwa ni mfano hasa kwa jitihada
zake za kutunza familia yake. Mke wa marehemu Mzee Kungubaya, ambaye ni mama mzazi wa Rajabu
alisema yeye alikuwa anategemea kuishi kwa kufanya kazi za kibarua katika
sehemu ambazo kuna ujenzi unaendelea, hufanya kazi kama kubeba maji na zege kuwasaidia wajenzi. Marehemu Kungubaya ameacha watoto wakiwemo wadogo
ambao mmoja yuko shule ya chekechekea na mwingine darasa la 6, wote hawa
wanamtegemea sasa kaka yao ambae ana mguu mmoja. Rajabu alikatika mguu kutokana
na gari kuovertake na kumfuata upande wake na kumgonga wakati akiwa kwenye
bodaboda, aliyemgonga, jina na namba ya simu ipo aliahidi kumsaidia lakini hajatimiza ahadi zake kwa kijaa huyu aliyempa ulemavu wa maisha.
Saturday, October 29, 2016
EXCLUSIVE- ANGALIA PAMBAMOTO LILIVYOKUWA LIKICHEZWA MIAKA YA 90 -VIDEO
Jukwaani wapiga magitaa
Miraji Shakashia- solo
John Kitime- Rythm
Manitu Musa - Bass
Drums- Juma Choka
Sax Rashid Pembe na Said Mohamed Ndula
Trumpet- Mawazo Hunja na Tuba
Uimbaji
Jerry Nashon, Mohamed Gotagota, na Abdallah Mgonahazelu
TOA MAONI
Subscribe to:
Posts (Atom)