Marehemu Omary Kungubaya |
Rajabu Kungubaya |
Rajabu
Omary Kungubaya, mtoto wa marehemu Omary Kungubaya, mwanamuziki ambaye alipata
umaarufu kutokana na wimbo wake wa ‘ Salamu za wagonjwa’ uliokuwa wimbo wa
kufungua na kufunga kipindi cha salamu za wagonjwa kilichokuwa kikirushwa na
Radio Tanzania, leo amepokea mguu wa bandia ili kumsaidia kutokana na mguu wake
wa kulia kuwa umekatwa kutokana na ajali ya bodaboda. Wanamuziki John Kitime na
Mjusi Shemboza walimuona Rajabu kwa mara ya kwanza siku walipoenda kumzika Mzee
Kungubaya na kuona umuhimu wa kumsaidia Rajabu kutokana na hali yake ya kutegemea magongo wakati
wa kutembea. Kwa kutumia kundi a Whatsapp la ZAMA ZILE, (kundi la wapenzi wa muziki wa zamani wanaosikiliza kipindi cha ZAMA ZILE kinachoendeshwa na John Kitime kupitia EFM 93.7fm kila Jumapili kuanzia saa 2-5 usiku), wanakikundi waliweza kuchanga fedha zilizowezesha kijana huyu kupata mguu wa bandia.
Rajabu ni mchangamfu anaeonekana kupendwa na kila mtu, kutokana na
majirani zake wote kumuunga mkono ikiwemo serikali ya mtaa wake. Mwenyekiti wa
serikali ya mtaa akiwa na wajumbe wengine wa serikali ya mtaa wake wote
walimsifu kwa tabia yake ambayo walisema ilikuwa ni mfano hasa kwa jitihada
zake za kutunza familia yake. Mke wa marehemu Mzee Kungubaya, ambaye ni mama mzazi wa Rajabu
alisema yeye alikuwa anategemea kuishi kwa kufanya kazi za kibarua katika
sehemu ambazo kuna ujenzi unaendelea, hufanya kazi kama kubeba maji na zege kuwasaidia wajenzi. Marehemu Kungubaya ameacha watoto wakiwemo wadogo
ambao mmoja yuko shule ya chekechekea na mwingine darasa la 6, wote hawa
wanamtegemea sasa kaka yao ambae ana mguu mmoja. Rajabu alikatika mguu kutokana
na gari kuovertake na kumfuata upande wake na kumgonga wakati akiwa kwenye
bodaboda, aliyemgonga, jina na namba ya simu ipo aliahidi kumsaidia lakini hajatimiza ahadi zake kwa kijaa huyu aliyempa ulemavu wa maisha.
No comments:
Post a Comment