Mzee Juma Mrisho aka Ngulimba wa Ngulimba liyekuwa Kiongozi wa Urafiki Jazz Band |
Bendi ya Urafiki (Urafiki Jazz Band), ilianzishwa mwaka 1970 na kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichopo Ubungo. Jina rasmi la kiwanda lilikuwa ni FRIENDSHIP TEXTILE MILL. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiki kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kilitex, na kadhalika
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue – Dar Es Salaam.
Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha Nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara.. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za Urafiki Jazz Band zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.
Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Michael Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu – Besi, Abassi Saidi Nyanga – Tenor Saxophone na Fida Saidi, Alto Saxophone. Ngulimba yeye akawa Muimbaji na pia Kiongozi wa Bendi.
Wanamuziki wengine wa mwanzo ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa – Juma Ramadhani Lidenge – Second Solo, Mohamed Bakari Churchil – gitaa la kati (rhythm), Ezekiel Mazanda – rhythm, Abassi Lulela – Besi, Hamisi Nguru – Muimbaji, Mussa Kitumbo – Muimbaji, Cleaver Ulanda – Muimbaji, Maarifa Ramadhani – Tumba, Juma Saidi – Manyanga (maraccass) na Hamisi Mashala – mpiga drums.
Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’
Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga na kundi akiwa mpigaji wa Saxophone.
Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi baadhi wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz wengine wakiwemo Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu – Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.
Pia waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta, hao walikuja 1973 na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Urafiki Jazz imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k..
Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja – D’Salaam na kushika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.
No comments:
Post a Comment