Mwaka 1984 nilikuwa mwanamuziki wa bendi ya
Orchestra Mambo Bado, bendi iliyokuwa inaongozwa na Tchimanga Kalala Assossa.
Bendi ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wa bendi
ulikuwa unajulikana kama Bomoa. Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa
Tutajenga Kesho, wimbo ambao baadae
kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa
Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule, usisike kwenye radio ya Taifa,
redio ambao ilikuwa pekee wakati huo. Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu
ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji,
Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Banza Tax muimbaji, Athumani
Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi, Andre
Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe
wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm.
Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja
na meneja wa bendi. Masikani ya bendi yalikuwa katika ukumbi wa Lango la Chuma,
Mabibo Dar es Salaam
Tarehe 12 April 1984, kundi zima lilitua katika mji
wa Shinyanga baada ya kuwasili hapo kwa treni kutokea Dar es Salaam. Kwa
taratibu za miaka hiyo, pamoja na ratiba ya ziara ya bendi kutangazwa kwenye
gazeti la Uhuru, meneja wa bendi alikuwa akilazimika kutangulia mji ambao dansi
litapigwa kuwahi kufanya mikataba na kumbi ambazo dansi lingepigwa na pia kufuatilia vibali mbalimbali
vya kuruhusu onyesho kufanyika. Mawasiliano yalikuwa magumu na urasimu ulikuwa
mkubwa. Haikuwa kazi rahisi maana miaka hiyo ili bendi isafiri ililazimika
kupata kibali cha Afisa Utamaduni
wa Mkoa ambao ni masikani ya bendi kuruhusu bendi kutoka nje ya Mkoa na kisha
kibali hicho kupelekwa kwa Ofisa Utamaduni wa Mkoa ambao bendi inakwenda, nae
baada ya kuruhusu bendi kuingia mkoani kwake, unaomba kibali cha Afisa Utamaduni
wa Wilaya unakotaka kupiga muziki ili nae akuruhusu kufanya onyesho kwenye
wilaya yake. Baada ya hapo meneja hutafuta na mtu ambaye ana spika ya mkononi,
megaphone kuikodisha na kisha kutafuta mtu wa kutangaza onyesho. Ili kubana
matumizi kuna mara nyingine wanamuziki wenyewe ililazimika wapite mtaani na
spika hiyo kujitangaza. Kulikuwa na mji kama Mpanda wakati huo, ambapo
mtangazaji hakuwa na megaphone, mtu maalumu alipita mtaa kwa mtaa akiwa na
ngoma ambao aliipiga watu wakikusanyika basi anatangaza ujio wa bendi katika
mji wao.
Tarehe 12 April 1984, Orchestra Mambo Bado iliwasili
Shinyanga kwa treni ikitokea Dar es Salaam, kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa.
Wanamuziki tulionyeshwa vyumba vya kulala, mambo yalionekana kuwa yatakuwa
mazuri kwa siku ile, matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye nguzo za umeme
sehemu mbalimbali za mji, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya
ujio wetu ilikuwa dhahiri. Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi ilipotangazwa kuwa
nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki
katika ajali ya gari jirani na Morogoro. Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu
akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa
sana, tulikuwa na nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku
moja tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na
kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake, tukitegemea mapato
mengine makubwa katika maonyesho ya Mwanza wikiendi iliyokuwa inafuata. Hayo
yote tulijua sasa yameharibika, tulirudisha vyumba vyote mara moja na kubaki na
viwili tu kimoja kikiwa cha wasichana waliokuwa kwenye bendi, wengine wote
ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kingine. Baadae tulikaa na Afisa
Utamaduni kutafakari kama dansi lingeweza kulia siku ile, na kama halitalia
nini hatima ya watu hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam? Kama kiasi cha saa
moja jioni, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya
kurudi Dar es Salaam, kwani ilijulikana wazi kitaanza kipindi cha maombolezo
ambacho hakuna mtu alijua kitaisha lini,
hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea na safari kutoka hapo. Vipindi vya
maombolezo huwa ni vipindi ambavyo pamoja na mambo mengine shughuli za muziki
husimamishwa. Kwa wanamuziki na wale wanaotegemea shughuli za muziki na familia
zao, kipindi hiki huwa kigumu sana. Lakini kinaleta ukakasi akilini kwani shughuli
za kupiga muziki kwenye kumbi husimamishwa, madisco hufungwa na vikundi vya
muziki haviruhusiwi kufanya kazi
lakini radio huendelea kupiga muziki uleule ambao umezuiwa kwenye kumbi, sehemu
za starehe kama baa huendelea kupiga muziki na kufanya biashara zao bila tatizo
ila wanamuziki ndio huzuiwa kufanya shughuli zao kwa maelezo kuwa ni kipindi
cha maombolezo. Nakumbuka sana misiba
mikubwa ya viongozi wetu ukiwemo wa Baba wa Taifa kwa sababu kubwa
mbili, kwanza uchungu wa kupoteza kiongozi wetu na njaa iliyofuatia baada ya
hapo.
No comments:
Post a Comment