Saturday, March 18, 2017

AMRI BILA TAFITI ZINAATHIRI SANA SEKTA YA MUZIKI


KATIKA shughuli ambazo watu wengi huona ni rahisi kuendesha na kutoa maamuzi bila utafiti ni soka na muziki. Ukisikiliza mazungumzo baada ya mechi za soka ndipo utakaposikia watu wanavyotoa ushauri au kukosoa wachezaji, kocha refa, chama cha mpira wa miguu, hakika ingewezekana watu hawa wakapata mamlaka, maamuzi yangekuwa ya ajabu sana.
Hali kadhalika kwenye muziki. Kwa mfano ukiuliza,   kwanini muziki wa bendi hauna umaarufu kama zamani? Hakika ukipita kila mtaa utapata majibu, wengine watakwambia kosa la vyombo vya utangazaji , wengine watakwambia wanamuziki wenyewe , wengine watakwambia serikali, na pia utapewa maelekezo mbalimbali ya nini kifanyike. Bahati nzuri majibu haya ya mtaani hayana madhara kwani huishia hapo hapo. Lakini bahati mbaya huja pale ambapo viongozi wenye mamlaka nao hugeuka wataalamu wa muziki na wao kutoa maamuzi kadri ya mtizamo wao, lakini maamuzi yao huwa amri, na amri inapotolewa bila utafiti wa kutosha madhara yake yanaweza kuendelea miaka mingi baadae. Ninaloweza kusema kwa uhakika, ni kuwa muziki wa Tanzania leo ungekuwa katika nafasi ya juu zaidi duniani kama isingekuwa maamuzi ambayo yalitolewa bila utafiti miaka ya nyuma. Labda nitoe mifano kadhaa. Mpaka miaka ya 70, wanamuziki wa Tanzania walikuwa wakienda sambamba na wanamuziki wa nchi nyingine nyingi Afrika, licha ya kutokuwa na miundo mbinu muhimu katika maendeleo ya muziki kama vile kutokuwa na kampuni za kurekodi na kutengeneza santuri. Lakini kimuziki, wanamuziki wa kipindi hiki walikuwa bega kwa bega na wenzao ambao walikuwa na miundo mbinu stahiki. Tanzania tulikuwa na bendi ambazo zilikuwa  zinapiga muziki wa rumba, nyimbo nyingi za wakati huo mpaka leo bado zinasifika na kupendwa katika anga za muziki. Pia tulikuwa  na wanamuziki vijana ambao wengi wao walikuwa mashuleni, hawa wakiwa na mtizamo mpana zaidi wa kutambulika duniani, wanamuziki hawa kama ilivyokuwa sehemu nyingi Afrika walianza kupiga muziki uliojulikana kama Afro Rock, muziki ambao ulichanganya mahadhi ya muziki asili wa Kitanzania na mapigo ya kizungu, wakifuatia nyayo za kundi la Osibisa, na wanamuziki kama Ransome Fela Kuti. Kukawa na makundi kama Afro 70, Trippers, Sun Burst, The Jets na kadhalika kwa kuyataja machache, makundi ambayo yalianza kuingiza muziki wa Tanzania kwenye soko kubwa zaidi la Kimataifa, kwa mfano wimbo wa Weekend wa Afro70 uliingia kwenye Top Ten Nigeria miaka hiyo, wakati huo muziki wa Nigeria haukuwa na umaarufu wowote nchini kwetu.  Kwa kuwa vijana hawa wengi walikuwa bado shuleni, na kufuatana na maadili ya wakati ule, wanafunzi hawakuruhusiwa  kushiriki madansa ya usiku, hivyo basi kulikuweko na utamaduni wa madansa ya mchana yaliyoitwa Bugi. Hapo vijana walikusanyika kupiga muziki wao kila mwisho wa wiki, shughuli zikianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Lakini siku moja kiongozi mmoja akatokea na kupiga marufuku Bugi, hivyo kuwaondoa wanamuziki vijana wengi kwenye muziki kwani wasingeruhusiwa kushiriki madansi ya usiku.  Wakati vijana hao wanaacha muziki, vijana wengine Afrika waliendelea mbele. Hata majirani zetu Kenya na Zambia wakawa na wanamuziki wengi walioweza kuingia katika soko la Kimataifa, wanamuziki wetu walikosa fursa hiyo. Pengo hili linaendelea kuwepo mpaka leo. Kuziba pengo hilo kunahitaji kutafiti tulipojikwaa na kuangalia tunafanya nini kurekebisha hali iliyopo. Swala la kupiga marufuku kazi za muziki si jambo geni katika historia ya muziki, kulikuwa na maamuzi kadhaa ya kisiasa pia ambayo pia hayakuwa na utafiti hivyo kudhoofisha maendeleo ya muziki Tanzania. Kwa mfano kulishawahi kutolewa amri ya kupiga marufuku wacheza show, wakati huo karibu bendi zote kubwa za muziki wa rumba kote Afrika Mashariki na Kati zilihakikisha kuwa zinakuwa na kundi la wacheza show, na waimbaji maarufu kama Mbilia Bel na Tshala Mwana wote awali walikuwa ni wacheza show. Kwa kipindi kirefu kulikuweko na sinto fahamu ya wacheza show na ikalazimika taaluma hiyo irudi kinyemela kwani makundi yote ya muziki kutoka nje yalipokuja nchini yalisindikizana na wacheza show. Nyimbo kadhaa ziliwahi kupigwa marufuku na hatimae kuja kuonekana ni za muhimu katika jamii, ukiwemo wimbo maarufu wa Super Matimila, Mambo kwa Soksi, ambao ulipigwa marufuku na baade kuonekana ni wimbo muhimu kuhamasisha watu kutumia kinga katika zama hizi za balaa la Ukimwi. Upigaji marufuku wa tungo unakwaza watunzi na kuishia kutunga nyimbo nyepesi ambazo zina uhakika wa kutokupigwa marufuku. Katika miaka ya karibuni kumewahi kufanyika maamuzi kadhaa yasiyokuwa na utafiti kwa mfano,  serikali iliwahi kununua mashine iliyoitwa Mastering Mixer kwa gharama ya shilingi milioni 50, kwa maelezo kuwa ndio itakayowezesha kumaliza wizi wa kazi za muziki. Sio siri wizi uko palepale. Hayo yalikuwa maamuzi bila utafiti, ni vizuri kujua hiyo ‘mixer’  iko wapi ili kutathmini ni matokeo ya uamuzi huu uliogharimiwa na serikali. Uamuzi mwingine ulikuwa ni ule wa kutunga sheria ya kuweka stempu za TRA kwenye kazi za sanaa, kwa maelezo kuwa utamaliza wizi wa kazi za muziki na filamu. Si mara moja taarifa imatolewa kuwa serikali ilitoa milioni 20 kwa mtafiti toka ‘Chuo Kikuu’ kuhakiki kuwa njia hiyo ndio itamaliza wizi wa kazi za sanaa, hakuna ‘mtafiti’ anayejitokeza kuwa alipokea fedha na kufanya utafiti huo, wala hakuna nakala ya utafiti huo, ni aina nyingine ya maamuzi bila utafiti na matokeo yake wizi wa kazi za sanaa umeenea kila kona nchini na mauzo halali ya kazi za muziki yamepotea. Ushauri tu kwa viongozi kuwa muziki si shughuli ya kubahatisha ina misingi yake, ni muhimu kwa manufaa ya Taifa, umefika wakati wa kufanya utafiti kwanza kabla ya kutoa maamuzi.

No comments:

Post a Comment