THE JETS

THE JETS
THE JETS

PAKUA HII

Jumatatu, 21 Mei 2018

WAPENZI WA MUZIKI WA MIAKA YA SITINI NA SABINI WAWEKA KUMBUKUMBU ZAO, na wewe wakaribishwa

The Flaming Stars wakiwa Arnatougro, ukumbi huu umetekwa na kuwa ukumbi wa mikutano ya madiwani

Siku moja niliuliza swali hili……Katika miaka ya 60 hadi katikati ya 70 kulikuwa na bendi nyingi za vijana ambazo unaweza kulinganisha na wanamuziki wa sasa wanaojulikana kama kizazi kipya. Katika jiji la Dar es Salaam, kulikuweko na bendi nyingi kama vile The Sparks, The Comets, The Flames, The Jets, Crimson Rage, The Lovebugs, Trippers Imagination, Safari Trippers, Afro 70. je unakumbuka nyingine ?
Majibu……………………
  Patrick Tsere said...
Yeah kulikuwa na Flaming Stars wengi wao wakiwa wanafunzi wa Minaki miongoni mwao akiwemo Michael Mhuto, Cuthbert Sabuni na mdogo wake John Sabuni, Peter Kondowe (Peko). Hao waliwaka sana mwaka 1966 to 1968. Wimbo wao mmoja ninaokumbuka ni "Mpenzi Maria sisahau x2 Hata nyota nazo, pia mbalamwezi haziwezi kusahau Maria. Usikuu huwa nalia usiku huu huwa naota Maaamaria". Baadaye wakaenda Mombasa and then they split.

Walikuwepo Hot Five ambayo ilikuwa kali sana miaka hiyo ya 1966 hadi 1969 ilipovunjika ikazaliwa Sparks na Tonics. Ilipokuwa the Hot 5 kiongozi wao alikuwa Michael Jackson na akina Jerry Mwakipesile na Lameck Ubwe. Kwenye drums alikuwa Adam Salumu aka Addy Sally. Ubwe alibakia na Sparks na akina Jackson na Sweet Francis na mdogo wake Green Jackson wakaanzisha Tonics ambayo ilifanya makao yake Arusha wakipiga muziki CAMEO Bar karibu na Msikiti mkuu wa arusha.

When I was in Zambia from 1984 to 1996 nilikutana na Michael Jackson akiwa kwao alikuwa ameugua kichaa wa kuzurura jijini Lusaka amebeba makopo na usingeweza kuamini kwamba ndiye yule aliekuwa star. It was a sad scene I must say.

Kipindi hicho wengine walikuwa the Rifters chini ya Adam Kinguyi, Kijana wa Ilala.

Na hao uliowataja. Of course walikuwepo wakongo kama akina Pascal Onema wakipiga New Palace Hotel ambayo sasa ni Mbowe. Akina Papa Micky na Nova Success. Freddy Supreme (Ndala Kasheba) na Fauvete

  Anonymous said...
Kuna bendi ya BAR KEYS ya upanga (kama sijakosea ni 4 flats upanga)sikumbuki wapigaji nilikuwa mdogo sana mpaka leo kuna instumental lao naweza kulipiga kwenye kinanda

  Anonymous said...
Brian Shaka and the Oshekas walikuwa Mtaa wa Undali, Upanga.
  Anonymous said...
Napenda kuwakumbusha groupe moja ya vijana wa Kigoa iliyokuwa ikiburudisha Kilimanjaro Hotel,George De Souza pia kundi lingine ambalo lilitamba sana na nikiwa mpenzi wao,The Sunburst.Mengine mengi tutakumbushana siku za mbele.


Anon said…..
 Umetaja akina Sabuni ni muhimu usimsahau Raphael Sabuni ambae mara ya mwisho nilimuona live akiwa na STC jazz, wakiwa na Marijani Rajab, na nyimbo zao kama , Ulikuwa usiku wa manane, Rafiki si mtu mwema. 
Top Life Bar Kinondoni bado ni bar, ukiangalia unashangaa kuwa palikuwa pakubwa kiasi cha bendi kupafanya ndo mahala pake, nadhani utakumbuka wimbo wa Papa Micky akisifu Top Life Bar Kinondoni

Jumamosi, 19 Mei 2018

VIDEO- THOMAS RUFUS FUNKY PENGUIN LIVE KATIKA TAMASHA LA WATTSTAX

VIDEO- ISAAC HAYES --THEME FROM SHAFT LIVE

SALIM JAMES WILLIS MWANAMUZIKI WA AFRO 70


The Dynamites..Salim walio kaa Salim Willis,Khamis, Abdallah Doger. Waliosimama ni Kheri Salah, Bashir Fahani na Mohamed Mnyika

ENZI ZA MABROTHER MAN, PARTY KILA WIKIENDI

Mabrothermen, usafi ilikuwa lazima na picha za Jimi Hendrix ukutani ilikuwa ni muhimu

Hapa namuona  Mheshimiwa Balozi mstaafu ambaye pia alikuwa muimbaji mzuri sana wa nyimbo za James Brown (Picha kwa hisani ya Bro Dimando)

Kila zama katika miji kuna vijana wa aina mbalimbali wanaotokana na aina ya malezi wanayolelewa, mitaa wanayokulia, shule wanazosomea, sanaa wanazopenda na kadhalika. HUko nyuma kwenye miaka ya 60 yalikuweko na makundi ya vijana wakiitwa Mabrotherman, kutokana na kuiga utamaduni wa vijana  Wamarikani weusi. Mabrotherman, kwanza walikuwa wanatokana na kundi la vijana ambao walikuwa wamepitia sekondari, walikuwa wakipenda kusoma, kati ya stori muhimu katika vikao vya mabrotherman ni matukio toka kwenye vitabu vya hadithi zilizoandikwa na Ian Fleming (James Bond) na James Hadley Chase, na sinema ambazo zilitikisa kama vile Saturday Night Fever, au filamu zote za Shaft, ama filamu zenye waigizaji weusi. Pia kusoma magazeti kama Drum na Ebony. Mabrotherman walikuwa wasafi wenye kujipenda ambao Pamoja na yote vijana walipenda sana kuparty, kwa kila kisingizio ilitengenezwa party kulikuwa na party kila week end. Vijana walichanga pesa na kukutana kwenye nyumba mbalimbali, kuna wazazi walioruhusu vijana wao wafanye party katika maeneo ya nyumba zao, wengine hata kuruhusu kutumia vifaa vya gharama wakati huo kama music systems. Mavazi yakiwa suruali za Bellbottoms au mara nyingine ziliitwa Pecos, kutokana na jina la filamu ya ma Cowboy iliyoitwa My name is Pecos ambapo muigizaji mkuu Robert Woods alikuwa kavaa suruali iliyotanuka sana chini. Shati zilikuwa za kubana na ziliitwa  na slim fit.

Ijumaa, 18 Mei 2018

UNAWAKUMBUKA SUNBURST?Hawa ndio Sunburst bendi iliyofanya vizuri sana mwanzoni mwa miaka ya 70,mwaka 1973 ikashinda mashindano ya Bendi Bora Dar es Salaam na kuwa ya kwanza. Toka kushoto Toby John Ejuama (saxophone) huyu alikuwa Mnaijeria kutoka Biafra, kama mnakumbuka Tanzania tulimuunga mkono  Ojukwu.!!!! Anaefuata ni Flory mpiga gitaa aliyekuwaMkongo, kisha mkongwe Johnny Rocks kwenye (drums), huyu alikuwa pia anapiga na George Di Souza pale Margot.  James Mpungo (lead vocals) kijana wa Mbeya ambaye hatimae alijiunga na Mangelepa. Anafuatia Kassim Rajabu Magati (organ/lead vocals, kwenye gitaa la bezi ni Bashir Idd Fahani. 

SUNBURST iliposhinda zawadi ya bendi bora 1973


Kundi la Sunburst lilianzishwa mwaka 1970 na mwanamuziki Mkongo Hembi Flory, Aliwakusanya mpiga drum Jphhny Rocks Fernandes, mpiga bass Bashir Idd Farhani, na mpiga keyboards Kassim Magati. Kisha ndipo akajiunga James Mpungwe.


SIKILIZA HAPA WIMBO WA SIMBA ANGURUMA

KUTOKA LOVE BUGS HADI KILIMANJARO BAND

Baadhi ya wanamuziki wa The Revolutions wakiwa wamejipumzisha juu ya hoteli ya Kilimanjaro, mahala ambapo umejengwa ukumbi wa 'Summit' siku hizi. Kutoka kushoto Mohammed 'Moddy'Mrisho, Hemedi Chuky (marehemu), Vuli Yeni, Ibrahim'Boss'  Mtumwa  na Joe "Ball" Rebello.

Alhamisi, 17 Mei 2018

HILI NDILO KUNDI ZIMA ZA SAFARI TRIPPERS 'SOKOMOKO NDANI YA NYUMBA'

Christian Kazinduki, Kiringo, Ali, David Musa Gordon, Vuli Yeni aliyeshika sax,  Marijani Rajabu aliyesimama juu ya kiti ameshika gitaa. Wenye kuwatambua wengine tafadhali  tunaomba majina

Jumatano, 16 Mei 2018

THE RIFTERS BENDI ILIYOANZIA ILALA

Toka kushoto mstari wa nyuma Mlima, Adam Kingui, Dokta, Mbele kushoto, Nassoro 'Mick Jagger' Fadhil, Khalid Mosty

Bendi ya The Rifters ilikuwa ni bendi ya vijana wadogo ambayo ilianzishwa na Adam Kingui na James Mwinga huko Ilala Dar Es Salaam mwaka 1966. Ni bendi ambayo ilipitia mabadiliko mengi sana kwani katika miaka hiyo wanamuziki walikuwa wengi na kwa ujumla muziki kwa kundi kama hili haukuwa unalipa bali ilikuwa ni kwa upenzi wa muziki na pia wanamuziki wengi walikuwa pia shule. Adam alidumu kwenye bendi mpaka pale ilipokuja kufutika. 

Jumamosi, 12 Mei 2018

JE WANAMUZIKI WA ZAMANI WALIKUWA WAZALENDO ZAIDI?


Watanzania tuna tatizo kubwa la kutokuwa na kumbukumbu nyingi kimaandishi, hivyo mambo mengi ya zamani yakianza kuelezwa huwa na mapungufu au mambo ya ziada ya kutunga aidha kutokana na kupoteza kumbukumbu au kupendezesha habari kutokana na nani unaemhadithia na kwanini. Nina imani ujio wa teknolojia ya blog ni jambo ambalo litasaidia sana kuweka kumbukumbu sahihi za matukio mbalimbali nchini kwetu. Kwa muda mrefu kumekuwa na hadithi kuwa wanamuziki wa zamani walikuwa wakitunga nyimbo nyingi za kizalendo kutokana na wao kuwa wazalendo. Kuna ukweli fulani kuhusu hilo, walikuweko vijana wengi waliokuwa wazalendo na walitunga nyimbo ambazo mpaka zama hizi bado nyimbo hizo zina hamasisha uzalendo, lakini pia kuna maelezo ya ziada ya kuelezea sababu ya tungo za kizalendo kuwa nyingi miaka hiyo.
BARKEYS....TANZANITES
Wanamuziki wa Tanzania  walitegemea studio za Radio Tanzania (RTD) kurekodi nyimbo zao, lakini kulikuweko na masharti ya kurekodi yaliyokuwa yakibadilika au kuongezwa mara kwa mara na vyombo mbalimbali, vikiwemo Umoja wa Vijana wa TANU ( TYL), uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, na Radio Tanzania yenyewe. Kati ya masharti yaliyokuweko ni yale yaliyoelekeza kuwa nyimbo zote kabla hazijarekodiwa RTD, mashahiri yake ilikuwa lazima yapelekwe kuhakikiwa na kamati ya RTD, na hapo maneno yalichujwa na hatimae nyimbo ambazo ziliruhusiwa kurekodiwa zilipitishwa na zile zenye utata aidha zilikataliwa au wanamuziki walishauriwa kuzifanyia mabadiliko, na ilitokea mara nyingine nyimbo ambazo zilipitia mchujo huu zilikuja kuzuiliwa kurushwa hewani na moja ya vyombo nilivyovitaja hapo juu. Sharti jingine lilihusu bendi za Kikongo, ambazo  zilipewa masharti ya kuanza kurekodi nyimbo zilizotumia lugha ya Kiswahili, kwani wakati huu bendi nyingi za Kikongo zilitunga nyimbo zao kwa lugha ya Kilingala. Sharti  jingine lilikuja kutolewa, ni kuwa kila bendi inapokwenda kurekodi ni lazima kuweko na wimbo mmoja au zaidi wa kisiasa au wenye ujumbe kwa jamii, sharti hilo ndilo lililofanya kuweko na nyimbo nyingi sana za kizalendo. Pia kulikuweko na maazimio, matamko ya serikali, kampeni mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa,  hata matukio makubwa na kwa yote hayo vikundi vya muziki vilihamasishwa kutunga na kurekodi nyimbo, nyimbo ambazo kwa sasa zimekuwa ni kigezo cha kuonyesha kuwa vijana zamani walikuwa watunzi wa nyimbo za kizalendo. Labda nizungumzie nyimbo chache ambazo nilishiriki enzi hizo ambazo huitwa ni za kizalendo. Nianze na wimbo ambao nilitunga na kushiriki kuimba wakati niko katika bendi ya Orchestra Mambo Bado mwaka 1983, wimbo ulioitwa CCM Itashinda, wimbo huu ulitungwa wiki chache kabla ya sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi mwaka huo, wimbo huo ulikuwa ni wa kukamilisha album iliyokuwa na wimbo maarufu wa Bomoa Tujenga Kesho ambao hatimae ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana Mkoa wa Dar es Salaam kuwa usipigwe katika radio. Mwaka 1988 nikiwa katika bendi ya TANCUT Almasi, marehemu Mzee Zacharia Daniel aliyekuwa maarufu kwa jina la Tendawema,  alitunga wimbo ulioitwa Kuwajibika, waimbaji katika wimbo huo walikuwa Mzee Daniel Tendawema, mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Hashim Kasanga na Mohamed Shaweji. katika kipindi hicho bendi zilitakiwa kutunga nyimbo zilizohamisisha wananchi kuwajibika katika sehemu zao za kilimo na kazi, bendi nyingi zilitunga nyimbo zilizoitwa Kuwajiba, ililazimika kuwa na wimbo unao sisitiza ‘Kuwajibika’.  Nilihama kutoka bendi ya TANCUT mwaka 1989  na kwenda Vijana Jazz Band. Kwanza bendi hii ni mali ya Umoja wa Vijana wa CCM hivyo kazi yake moja kubwa ilikuwa kutunga nyimbo za kuhamasisha na kuelimisha shughuli za Chama Cha Mapinduzi na serikali yake, hivyo hakika nilishiriki nyimbo nyingi sana kuimba na kupiga gitaa katika nyimbo hizo. Lakini niongelee wimbo wa Nelson Mandela wimbo huo ulikuwa moja ya nyimbo ambazo bendi za Tanzania zilihamasishwa kutunga kutokana na ziara ambayo Rais Nelson Mandela alikuja kuifanya Tanzania kama shukrani yake kwa Watanzania kwa kuunga mkono mapambano dhidi ya ukaburu. Wimbo huo tulioufanyia mazoezi usiku kucha  na kwenda kuurekodi RTD, ulikuwa ndio wimbo wa mwisho ambao  Hemed Maneti aliurekodi kabla ya kifo chake.   Bendi iliupiga wimbo huo mbele ya Nelson Mandela alipohutubia uwanja wa Jamhuri Dodoma, uwanja wa  Jamhuri Morogoro, na mwisho tulipiga Uwanja wa Taifa tukiwa na bendi ya Washirika Tanzania Stars ambayo nayo ilikuwa na wimbo wa Mandela uliokuwa ukiimbwa na Eddy Sheggy, siku Mandela alipokuja kuhutubia Dar es Salaam.
Nyimbo hizi za kizalendo sio tu zilihamasishwa kutungwa lakini pia radio ilihakikisha kuwa inazipiga hewani hivyo zilikuja kujulikana na kupendwa. Pamoja na kuwa kuna radio nyingi siku hizi, nafasi ya kusikika hewani nyimbo za kizalendo siku hizi ni finyu sana, pengine ndio maana hata wanamuziki hawoni motisha ya kutunga tena
nyimbo hizo.

Ijumaa, 11 Mei 2018

BARUA YA SALAMU KWA WAHESHIMIWA WABUNGE KUTOKA KWA MSANII (1)Waheshimiwa Wabunge wangu nawasalimu kwa heshima, nawasalimu wote bila kujali itikadi kwani wote ni Wabunge wangu. Waheshimiwa nimeona niwaandikie waraka huu kwani si rahisi kuonana na nyie waheshimiwa nikapata nafasi ya kuzungumza niliyo nayo moyoni kwani ninyi ni watu mlio na majukumu mengi.
Waheshimiwa safari zangu za kuanza kujaribu kusikilizwa nanyi hazikuanza karibuni kwani nakumbuka kuanza kutafuta nafasi ya namna hiyo kuanzia mwaka 1994. Lakini silalamiki sana kwani ninyi ni watu mlio na majukumu mengi.

JE UASI ULIOSABABISHA PATRICE LUMUMBA AUWAWE USINGEFANYIKA, MUZIKI WA TANZANIA UNGEKUWA NA SURA GANI?


Nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ilipata Uhuru wake tarehe 30 June 1960,  uchaguzi wake wa kwanza ambao ulikuwa wa vyama vingi ulileta kigugumizi cha kwanza cha namna ya kushika madaraka kwani hakukuwa na chama kilichoshinda na kuweza kuendesha nchi peke yake hivyo basi chama cha Alliance de  Bakongo cha Joseph Kasavubu kililazimika kuungana na chama cha  Mouvement national Congolais cha Patrice Lumumba ili kuunda serikali. Joseph Kasavubu akawa Rais, na Patrice Lumumba akawa Waziri Mkuu. Pamoja na muungano huu viongozi hawa wawili walikuwa na mtizamo tofauti kuhusu hatima ya Kongo.
Waziri Mkuu Patrice Lumumba
Haikuchukua hata mwezi baada ya kupata Uhuru kukatokea maasi ya askari yaliyochochewa na Wabelgiji ambayo yalisababisha jimbo la Katanga lililopo kusini mashariki mwa nchi hiyo kujitenga. Mwezi Septemba mwaka huohuo Rais Kasavubu akatangaza kuwa kamfukuza kazi Lumumba, ambaye nae aligoma na yeye pia  kutangaza kumfukuza kazi Rais wake. Hapo ndipo Kanali Joseph Mobutu akamkamata Lumumba na kumkabidhi kwa waasi wa Katanga ambako Lumumba aliuwawa kikatili.
Waziri MkuuPatrice Lumumba akiwa amekamatwa na askari wake

Kasavubu aliendelea kutawala kwa shida sana huku kukiweko na uasi mkubwa katika jimbo la Katanga. Akabadilisha Mawaziri wakuu kadhaa na hatimae akampa madaraka hayo Moise Tshombe ili aweze kuzima uasi Katanga. Miezi michache baadae Kasavubu na Tshombe wakafarakana na ndipo hapo Mobutu akapindua serikali na kutangaza hakuna siasa kwa miaka mitano akitoa sababu kuwa siasa ndiyo iliyoleta machafuko nchini humo.  Fujo  na uasi katika jimbo la Katanga lilisababisha nchi yetu kupokea wimbi kubwa la wageni na wakimbizi kutoka Katanga, jimbo ambalo kwa sasa linaitwa Jimbo la Shaba. Kati ya wageni hao kulikuja na wanamuziki ambao waliona huku kuna amani na wangeweza kufanya kazi zao kwa usalama, huo ukawa mwanzo wa wanamuziki wa Kongo kuingia kwa wingi nchini. Kuna waliokuja mmoja mmoja na kuna waliokuja kama bendi. Bendi maarufu zilizotua hapa ni kama Maquis du Zaire, Fauvette, Tha Jambos, iliyokuja kuitwa Orchestra Makassy baadae,  Super Boca na bendi nyingine nying. Wanamuziki hawa walikuja nchini na kukuta vikundi vingi tu vya muziki hapa, lakini vikundi vya muziki hapa nchini vingi vilikuwa na muundo wa klabu, wanamuziki wakipiga muziki baada ya kutoka kwenye ajira zao nyingine, na hivyo muziki kutokuwa ajira wala biashara yenye uzito wowote.  Wanamuziki kutoka Kongo walikuja na kuanza kufanya kazi ya muziki, wakiishi kwa muziki wao na familia zao. Taratibu hii ilitokana na kuwa kwa muda mrefu katika nchi ya Kongo kulikuwa na kumeshajengeka taratibu za kuendesha muziki kibiashara, kampuni ya kwanza ya kurekodi nchini Kongo, ambayo ilitoa santuri za lebo ya Lonongiza ilianzishwa mwaka 1947, na ndio iliyokuwa chanzo cha wanamuziki waliokuja kupata umaarufu mkubwa kama vile Wendo Kolosoy, Franco, Henri Bowane, Joseph Kabasele na wengine wengi.  Wanamuziki wa Tanzania wakaanza taratibu kuiga mambo mengi kutoka kwa wanamuziki hawa wageni, wakaiga utawala wa bendi, nidhamu ya jukwaani, uvaaji na hata muziki uliokuwa ukipigwa na Wakongo, na kwa miaka mingi Kongo ikawa darasa kwa wanamuziki wa Tanzania. Upenzi huu wa muziki wa Kongo bado uko hai kabisa hata leo. Kama nilivyogusia hapo juu, kulikuweko na wanamuziki wengi tu hapa nchini na bendi kubwa maarufu, kama Morogoro Jazz Band iliyoanzishwa mwaka 1944, au Cuban Marimba ambayo ilikuweko 1952, Western Jazz Band mwaka 1958. Ukisikiliza nyimbo za bendi hizi kabla ya ujio wa Wakongo, utakuta walikuwa wakipiga muziki kwa kuiga midundo ya Cuba, muziki kutoka Afrika ya Kusini, na muziki wa kutoka Ulaya kwa mitindo kama waltz, tango, foxtrot na kadhalika. Ukisikiliza nyimbo mbalimbali za wanamuziki  Frank na Dada Zake unaweza kupata picha ya maelezo hayo hapo juu. Kwa maelezo hayo ninajiuliza,  kama Kongo ingepata Uhuru na kuendelea kuwa nchi ya amani, na kutokana na mali nyingi ambazo nchi hiyo imejaliwa, hakika ingekuwa vigumu wanamuziki wake kuikimbia na kuja kutafuta riziki huku ugenini.  Kwa sababu hizo muziki wa Tanzania ungeendelea katika mkondo mwingine kabisa, kwa kila hali. Je tungekuwa muziki wa aina gani ? Rumba lazima lingekuweko kwani upigaji wa rumba ulikuweko lakini ulikuwa unaigwa kutoka Cuba, bila shaka lingekuwa rumba la aina nyingine tofauti na rumba la Kongo,  kama vile ukisikia rumba kutoka Cameroon au Ivory Coast. Nchi za kusini mwa Afrika ambazo hazikuathiriwa na muziki wa Kikongo nyingi zilifwata mitindo kutoka Afrika ya Kusini, huko kulikuwa na kampuni kongwe ya muziki ya Gallotone iliyoanza kusambaza muziki wa nchi hiyo mwaka 1923, muziki ambao ulifika hata huku kwetu na pia kupendwa na kuwa muziki uliokuwa unapigwa na bendi nyingi kabla ya muziki wa Kongo haujaja. Ingekuwa wazo la kufurahisha wangetokea wanamuziki wachache na kupiga muziki wa nchi hii kabla ya ujio wa muziki wa Kongo pengine wangeanzisha aina nyingine ya muziki