Marehemu Ramadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System
ni mzaliwa Ujiji, Kigoma. Alikuwa mtu aliyependa sana utani na ucheshi.
Bendi yake ya kwanza aliyojiunga mwaka 1977, ilikuwa Super
Kibisa iliyokuwa na makao yake makuu Kigoma. Super Kibisa ni bendi iliyoanzishwa mwaka 1968 pale
Kigoma. Mwaka 1977 kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye
alikuwa ni binamu yake Ramadhani Kinguti, na
hivyo ikawa rahisi kwake kujiunga
na bendi ile. Super Kibisa ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna
Mahepe, na Maulidi. Katika bendi ya Super Kibisa, kipaji cha utunzi cha Kinguti
kilianza kujitokeza mapema na aliweza
kutunga nyimbo kadhaa kama vile Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina.
Miaka miwili baadae, 1979, Kinguti alichukuliwa na Ahmed
Sululu ambae alikua Katibu wa bendi ya
Dodoma International na kuhamia Dodoma. Dodoma International ilimchukua
Kinguti ili kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama bendi hiyo na
kuhamia JUWATA.
Alipofika Dodoma international , Kinguti alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa
mahiri marehemu Kassim Rashid. Kinguti aliiacha Dodoma International Orchestra
na kujiunga na Orchestra Makassy ambapo
wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Radi, mwimbaji Mkongo ambaye alifariki kwa kukanyagwa na
daladala maeneo ya Kinondoni Mbuyuni. Baadhi ya wanamuziki wengine ambao
Kinguti alikuwa nao alipokuwa Orchestra Makassy walikuwa marehemu Remmy Ongala, marehemu Andy Swebe, Keppy
Kiombile, John Kitime, marehemu Issa Nundu, marehemu Kyanga Songa, Choyo
Godjero na wengineo, pia alikuweko marehemu Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim
Mganga (babake wa mwanamuziki wa Bongo flava Kassim Mganga-Milionea wa Mahaba)
kwenye rhythm, na wengine wengi. Kwa
kipindi fulani muda huu Kinguti akiwa na wenzake chini ya Mzee Makassy
wakafanya ziara ndefu nchini Kenya, kati ya waliokuwepo katika safari hiyo ni
Nico Makoli, Keppy Kiombile, Andy Swebe,
Mzee Aimala Mbutu, Mzee Liston na wengine wengi akiwemo Mzee makassy mwenyewe.
1986 alijiunga Afrisongoma chini ya Lovy Longomba, hapa
alitunga nyimbo kadhaa kama Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe,
waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, marehemu Lovy Longomba na Anania Ngoliga, kwenye solo alikuweko
marehemu Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge. Kwa muda mfupi alikuwa DDC
Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba,
ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua, Hussein Jumbe na Benno Villa.
Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Stars Band akiwa na
Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao
kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya
kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection,
alikaa bendi hii iliyokuwa chini ya Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha
kuanzisha bendi akiwa na Hassan Shaw, bendi iliyoitwa The Jambo Survivors
ambayo wengi hapa Tanzania wataikumbuka kwa kibao cha Maproso. Bendi ya Jambo
Survivors ikiwa bado na Ramadhan Kinguti na Hassan Shaw, kwa miaka kadhaa
ikahamia Thailand. Baada ya kurudi Thailand afya ya Kinguti ilikuwa na migogoro
mingi hivyo hakurudi tena kwenye muziki na muda mwingi alikuwa Dar es Salaam
kisha Kigoma.
Ramadhani Kinguti amefariki tarehe 21 Disemba 2022 katika
hospitali ya Maweni Kigoma, na mazishi ni tarehe 22 Disemba 2022 hapohapo
Kigoma
Mungu amlaze Pema.
RIP Ramadhani Kinguti System Tulikupenda lakini Mwenyezi Mungu amekupenda zaidi
ReplyDeleteKingugi system mkongwe wa muziki wa dansi hapa Tanzania tunamwombea mwanga wa milele Mungu amwangazie na akawasalimie Sana hakina shabani Dede, Eddy sheggy na wengi wengineo
ReplyDelete🙏🏾Pumzika kwa amani Ramadhan Kinguti.Amina.
ReplyDeleteSafari yetu sote.😞