BENDI kongwe iliyokuwa maarufu sana, Maquis Original itauanza mwaka huu kwa kufanya maonyesho mawili makubwa ya kumbukizi ya enzi zake. Maquis Original awali ilikuwa ikiitwa Maquis du Zaire wakati ikiingia nchini Tanzania kwa mara ya kwanza, ilikuwa ikitokea mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati huo nchi hiyo ikiitwa Zaire. Baada ya kuwasili Tanzania, haikupita muda mrefu bendi ikawa moja ya bendi tishio nchini. Nyimbo za bendi hii hata zile ilizo rekodi mwanzoni baada ya kuingia nchini bado ni nyimbo pendwa kwa waliokuweko enzi hizo na hata ambao wamezaliwa miaka mingi baada ya bendi kuwa imepotea katika ulimwengu wa muziki. Uamuzi wa wanamuziki wa bendi hii kujikusanya na kufanya maonyesho yao hakika ni faraja kubwa kwa wapenzi wa bendi hii. Bendi itafanya maonyesho mawili. Onyesho la kwanza litakuwa tarehe 21 Januari 2023 katika ukumbi wa Break Point Makumbusho na tarehe 27 January katika ukumbi wa Royal Village Dodoma
MAMBO MATAMU YAJA
Hebu tukumbuke enzi hizo kwa kuangalia tangazo la dansi la Orchestra Maquis miaka hiyo ambalo nina uhakika litaleta kumbukumbu kwa wapenzi wa Maquis wa enzi hizo za Mtindo wa Telemka Chekecha Scania LBT III, wakati huo gari za Scania ndizo zilikuwa maarufu nchini na Scania LBT III ilikuwa gari yenye saiz kubwa kuliko zote, na ndio yenye kusifika zaidi. Maquis walikuwa na ufadhili wa kampuni hiyo ya magari, ukumbi wa nyumbani wa bendi hii wakati huo ulikuwa ukumbi wa White House uliokuwa Ubungo. Karibuni tena wapenzi wa White House mchangie, mambo yalikuwa mazito chini ya uongozi wa Chinyama Chiyaza ambae alikuwa mpiga Saxophone katika bendi. Wakati huu Maquis ilikuwa na maendeleo makubwa sana ya kuwa na mashamba, magari, matrekta na hata kuwa na Kota zake pale Sinza Palestina. Hebu angalia majina ya wanamuziki waliokuwa kwenye bendi hiyo, wote walikuwa miamba ya muziki.
No comments:
Post a Comment