Thursday, September 8, 2016

WESTERN JAZZ BAND MOJA YA BENDI ILIYOKUWA MAARUFU TANZANIA

Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz. Wanamuziki hao walikuwa
Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye nyimbo ka Rosa na kadhalika.
Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall, ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.

Saturday, August 20, 2016

MAZISHI YA BI SHAKILA , YATAFANYIKA LEO MBAGALA CHARAMBE

Mazishi ya Bi Shakila yatakuwa leo Jumamosi 20 AGOSTI 2016. Mbagala Charambe, saa kumi alasiri Uwanja wa Ninja.
 Namna ya kufika msibani nyumbani kwa marehemu kwa kutumia daladala. Unapanda magari ya Mbagala Rangi Tatu, ukifika mwisho unachukua basi la Nzasa na unashuka Mnara wa Voda hapo unauliza kwa Bi Shakila utaonyeshwa

Thursday, February 25, 2016

MZEE KASSIM MAPILI HATUNAE TENA


Mzee mapili
MZEE Kassim Mapili hatunae tena. Habari ilitufikia jioni hii kuwa Mzee aliingia chumbani kwake Jumanne usiku akitokea kuangalia mechi ya Arsenal na Barcelona, na toka alipoingia hakutoka tena, hivyo jioni ya leo majirani walilazimika kutoa taarifa ambapo polisi walivunja mlango wa chumba cha Mzee na kukuta amefariki. Kutokana na hali ya mwili inaonekana alifariki tangu juzi na hali ya mwili si nzuri. Mzee Mapili alilazwa miezi michache iliyopita Muhimbili kutokan na kuwa na tatizo la moyo, lakini alikusema mwenyewe hata wiki iliyopita kuwa kutokana na kusaidiwa na Salma Moshi, msanii mkongwe anaeishi Marekani kupata Bima ya Afya hali yake imeimarika kwani anapata dawa zote zinazohitajika bila ya matatizo. Siku ya Jumatatu Mzee mapili alishiriki kikamilifu katika kumzika mtangazaji Fred Mosha, na hata kumuimbia marehemu akisikitika kuondoka kwake mapema. MUNGU AMLAZE PEMA MZEE WETU MAPILI

Monday, February 22, 2016

LEO NDIO SIKU YA MAZISHI YA RAFIKI YETU NA NDUGU YETU FRED CAMILLIUS MOSHA


FRED
RIP FRED MOSHA
  LEO NDIO SIKU YA MAZISHI YA RAFIKI YETU NA NDUGU YETU FRED CAMILLIUS MOSHA. FRED ALIKUWA MTANGAZAJI ALIYEKUWA NA MAPENZI MAKUBWA NA MUZIKI WA DANSI. MAPENZI YAKE YALIANZA TOKA AKIWA MDOGO KWANI NAMKUMBUKA AKIJA NA MAMA YAKE KATIKA MADANSI YA MCHANA AMBAYO BENDI YETU YA TANCUT ALMASI ILIKUWA IKIPIGA KWENYE UKUMBI WA OMAX KEKO. UPENZI HUU ULIFIKIA MPAKA KIPINDI ALITAKA KUACHA SHULE NA KUJIUNGA NA BENDI YA DDC MLIMANI PARK, BAHATI NZURI MAMA YAKE ALIIKAMATA BARUA YA MAOMBI YAKE YA KAZI, NA KUZUIA MPANGO HUO WA KUACHA SHULE. FRED HAKIKA ALIKUWA MTANGAZAJI BORA WA HABARI ZA WANAMUZIKI WA MUZIKI WA ZAMANI WA DANSI.
RATIBA YA MAZISHI NI KAMA IFUATAYO;
  • SAA 4-5 MWILI UTAPELEKWA NYUMBANI KWAKE CHAMAZI UKITOKEA MUHIMBILI
  • SAA 7 MWILI KUPELEKWA KANISA LA RC CHANG'OMBE KWA MISA YA MAZISHI
  • BAADA YA HAPO SAFARI ITAANZA YA KUELEKEA MAKABURI YA KINONDONI KWENYE MAKAZI YAKE YA MILELE
  • MUNGU MALAZE PEMA PEPONI FRED MOSHA

Tuesday, February 9, 2016

WAKONGWE WA DANSI TANZANIA KATIKA WIMBO WA PAMOJA- MIAKA 50 YA UHURU

VIDEO HII YA WIMBO HUU MIAKA 50 YA UHURU INA KUMBUKUMBU NYINGI. HAPA WAPO PAMOJA JUKWAANI, KASONGO MPINDA NA KABEYA BADU

Thursday, December 3, 2015

ABOUBAKAR KASONGO MPINDA KUZIKWA LEO KISUTU


MUTOMBO & MPINDA
Marehemu Aboubakar Kasongo Mpinda


MWANAMUZIKI Aboubakar Kasongo Mpinda aliyefariki jana jioni anategemewa kuzikwa leo saa kumi katika makaburi ya Kisutu. Mpinda alifariki jana nyumbani kwake Mwananyamala na mwili wake kwenda kuhifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala.
Mungu amlaze Peponi Pema

Wednesday, December 2, 2015

KASONGO MPINDA CLAYTON HATUNAE TENA


MUTOMBO & MPINDA
Marehemu Mutombo Audax (kushoto), akiwa na marehemu Kasongo Mpinda
HAKIKA siku hii ni ya simanzi, nimetoka makaburi ya Kinondoni ambapo tumemzika mwanamuziki David Musa Gordon wa Safari Trippers, nafika nyumbani taarifa inakuja kuwa mwanamuziki mwingine mkongwe Kasongo Mpinda Clayton amefariki jioni hii nyumbani kwake Mwananyamala na mwili umepelekwa hospitali ya Mwananyamala.
Mungu Amlaze Pema

Saturday, November 28, 2015

DAVID MUSA AFARIKI DUNIA


MWANAMUZIKI mwanzilishi wa kundi la Safari Trippers na aliyekuwa mwalimu wa wanamuziki wengi sana David Musa amefariki usiku wa kuamkia leo. Msiba uko nyumbani kwake Chang'ombe. Habari zaidi tutazileta kadri tutakavyozipata. 
safari trippers
Kushoto mwenye miwani David Musa, wa tatu Marijani Rajabu na kulia mwisho Jumanne Uvuruge mtunzi wa wimbo wa Georgina.
 Mungu amlaze pema

Monday, November 23, 2015

MFAHAMU MBARAKA YUSUPH MWANAMUZIKI WA NATIONAL PANASONIC NA POWER IRANDA

“NIMEACHANA na muziki wa dansi hivi sasa na nimeamua kugeukia sanaa ya filamu, ambapo sababu kubwa ni kupungua kwa kasi yangu ya ucharazaji gitaa, kutokana na kupata mara mbili kwa nyakati tofauti, ugonjwa wa kupooza.”
Hayo ni maneno ya Mbaraka Yusuph, kati ya wacharazaji mahiri wa zamani wa magitaa yote pamoja na Saxophone, aliyewahi kuzitumikia bendi mbalimbali hapa nchini, zikiwamo, The Smashers, National Panasonic, OSS ‘Power Iranda’, Seven Blind Beats na the Big Africa ya Arusha..ENDELEA HUKU

Thursday, April 23, 2015

MWANAMUZIKI MKONGWE MUTOMBO LUFUNGULA AUDAX HATUNAE TENA

AUDAX(kushoto) akiwa na Kasongo Mpinda
Mwanamuziki muimbaji na mtunzi mashuhuri wa bendi ya Maquis Original Mutombo Lufungula Audax, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, huko Kimara Michungwani. Mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa Mwananyamala Hospitali. Audax alikuwa ndie mmoja wa wanamuziki asili wa kundi la Maquis Du Zaire. Kundi la Maquis lilianza katika mji wa Kamina, jimbo la Shaba, huko Kongo. Awali kundi lilianza kwa kuitwa Super Teo, kisha kubadili jina na kuitwa Rocken, ......INAENDELEA

Tuesday, April 21, 2015

MWANAMUZIKI WA SIKU NYINGI PAUL GAMA AFARIKI DUNIA

KWA MASIKITIKO MAKUBWA TUMETAARIFIWA KUWA MWANAMUZIKI WA ZAMANI PAUL GAMA AMEFARIKI DUNIA HUKO DODOMA TAREHE 16.4.2015 MUDA WA SAA NNE ASUBUHI. NARUDIA MAKALA HII YA HISTORIA YA PAUL GAMA KADRI ALIVYOTUELEZA MWENYEWE

Paul Daniel Gama
Paul Daniel Gama alizaliwa Barabara ya 11 Dodoma (1947). Baba yake alikuwa ni mwanajeshi wa KAR mwenye asili ya Songea na mama yake alikuwa na asili ya Usangu alikuwa anafanya kazi  katika 
Spokes Mashiyane na filimbi yake
hospitali ya Mirembe ambayo wakati huo ilikuwa ni hospitali kubwa ya majeruhi wa vita ya pili ya dunia. Aliingia shule na alipofika darasa la nne alijikuta akiwa na kipaji kukubwa cha kupiga filimbi, wakati huo wapiga filimbi walipenda sana kumuiga mpiga filimbi maarufu kutoka Africa ya Kusini Spokes Mashiyane. Akiwa na wenzie walianzisha kikundi ambacho kilikuwa na maskani eneo la Mji Mpya pale Dodoma. Vijana hao pia walikuwa wakiiga  nyimbo za wanamuziki maarufu wa wakati huo, kama Salum Abdallah na  Cuban Marimba, pia Salum Zahor na Kiko Kids. Katika kufanya fani yao hiyo kama kitu cha kujipa burudani waliligusa sikio la  aliyekuwa mwalimu wa Elimu ya Watu Wazima katika Community Center ya pale Dodoma. Mwalimu huyu aliwasaidia kuwaazimia amplifaya moja kutoka kwenye bendi nyingine ilikuweko Dodoma wakati huo, The Jolly Sextet Band. Band iliyokuwa ikimilikiwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa East African Postal and Telecommunication Services, huyu bwana alikuja na vyombo vingi akaanzisha bendi ambayo mmoja wa wapigaji wake alikuwa Mzee Mnenge ambaye hatimaye alitua NUTA Jazz Band.
Bongos
Hiki kikundi cha Gama na wenzie kilikuwa katika mfumo wa Jazz Band za zamani ambapo walikuwa na ngoma na filimbi tu,ikisindikizwa na kuimba, lakini waliweza kukonga nyoyo hata za wanamuziki wengine, na Gama akawa anasakwa na bendi kubwa iliyokuweko wakati ule Central Jazz band. Alipomaliza darasa la saba tu ndugu yake aliyeitwa Titus Olaf Gama alimshawishi aingie Central Jazz lakini hakuwa tena mpiga filimbi bali mpiga Bongos, fani aliyoiweza sana hata  kuipenda na hasa baada ya kuwaona wanamuziki wa NUTA akiwemo Muhidin Gurumo  ambaye wakati huo alikuwa akipiga Bongos na kuimba. Bongos no ngoma ndogo zilizokuwa muhimu katika kundi wakati huo ambapo hakukuweko na drums wala tumba. Taratibu akaanza kupata hamu ya kupiga bass, wanamuziki wenzie walimkatisha sana tamaa kwa kuambiwa kuwa vidole vyake vilifaa sana kwa kupiga bongos na si kupiga gitaa.

Katika jitihada zake za kujifunza gitaa la bezi alikuwa kila mara akiwahi mazoezi na kujaribu kujifunza gitaa la bezi. Hilo lilikuwa gumu mpaka pale bendi  ya Lake Jazz Band ilipotembelea Dodoma. Bendi hiyo wakati huo ikiwa na wanamuziki kama Shem Karenga  akiwa anapiga gitaa la bezi, Mzee alum ambaye alikuwa na ulemavu wa macho, mwanzo alikuwa akipiga gitaa la solo na baadae akahamia kupiga gitaa la rhythm wakati gitaa solo lilikuja kupigwa na jamaa aliyeitwa Kally. Kutokana na simulizi ni wazi kuwa wanamuziki wa kutoka Burundi walikuwa wengi sana nchini wakati huo. Pia katika bendi hiyo alikuweko Mzee Juma Kitambi, mtunzi wa wimbo maarufu wa Rangi ya Chungwa.
Gama alichukua nafasi hii kumfuata Mzee Salum ili aweze kumfundisha gitaa. Kwa kuwa wanamuziki wengine walikuwa wakitoka kwenda kutembea Mzee Salum alibaki nyumbani na hivyo Gama alichukua nafasi hiyo kumnunulia sigara Mzee Salum ana kumsihi amfundishe gitaa nae alifanya hivyo na Gama akatokea kuwa mpiga bezi mahiri.
Katika kipindi hiki akatokea mfanya biashara Mohamed Omar Badwel, huyu alikuwa na gereji na studio ya kupiga picha, aliweza kwenda Mombasa na kurudi na seti ya vyombo na kuanzisha Dodoma Jazz Band. Gama akahama Central Jazz Band na kujiunga na wanamuziki wengine walioanzisha Dodoma Jazz. Band ilianza ikiwa na mpiga solo Hassan Mursali mwanamuziki mweny asili ya Malawi, siku hizo ikiitwa Nyasaland alikuwa ndie mpiga solo, lakini aliwaacha baadae na kujiunga na NUTA Jazz Band, upigaji wake wa solo unaweza kuusikia katika kusikiliza kibao kimoja maarufu cha NUTA, kilichoitwa Dunia Njema Kukaa Wawili.
Hasan alikuwa mtu wa kuhama hama hatimae alipoteza uwezo wa kusikia jambo ambalo lilihusishwa na kuhamham kwake kwani ushirikina ulitawala sana wakati huo, kama maelezo yanayofuata yanavyoonyesha. Dodoma Jazz ilikuwa pia inafanya ziara katika sehemu nyingi , kama vile Iringa, Mbeya ,Tabora, Dar es Salaam na kadhalika, lakini safari moja ya kwenda Kilosa ilifanyika ikiwa na lengo la kumfuata Abel Barthazal aliyekuwa akipiga katika bendi ya Kilosa Jazz. Bendi  ilipokelewa vizuri na wakafanya maonyesho yao Kilosa na hatimae kuondoka na Abel. Siku chache baade wakati huo Mzee  Mohamed Omar, mwenye bendi alikuwa kasha mnunulia suti kadhaa Abel, ukaja ugeni toka Kilosa wakiwa na barua yenye maelezo kuwa ikiwa Abel Hatarudi Kilosa, mmoja wa wanamuziki wa Dodoma Jazz atafariki, na barua hii ililetwa kwa mkono na mjumbe ambae alisisitiza wakishaisoma mbele yake ndio anaondoka. Abel alirudishwa Kilosa mara moja.
Baada ya hapo aliyekuwa meneja wa bendi Ramadhan Waziri alitumwa Burundi kwenda kutafuta wapigaji, siku alipokuwa anarudi na wapigaji wapya akakutana kwenye treni na Rashid Hanzuruni, mpiga solo mahiri sana ambaye upigaji wake husikika katika wimbo  Napenda nipate lau nafasi
Hanzuruni alikuwa kaiacha Tabora Jazz baada ya  kutokea ugomvi mkubwa ambapo alipoteza meno kadhaa, hivyo alikuwa kwenye hilo treni akielekea Dar es Salaam kumfuata mpigaji mwenzie Samba ambae alikuwa NUTA Jazz. Ramadhani aliweza kumshawishi hanzuruni akabaki Dodoma Jazz ambako alikaa kwa muda na hatimae akaja kuchukuliwa na Sama ili aingie NUTA Jazz, ndoto hiyo haikufanikiwa kwana NUTA alikuweko mpigaji mahiri  Hamisi Franco, hii ndiyo ilipelekea Hanzuruni kwenda Western Jazz Band



Friday, January 16, 2015

IMETIMIA MIAKA 36 TOKA KIFO CHA MBARAKA MWINSHEHE, MUZIKI WAKE BADO UKO HEWANI

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro Juni 27, 1944. Siku ya Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikiska kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha mwanamuziki huyo, mpiga gitaa muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga karibu kila wilaya ya nchi hii. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia katika hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari...........ENDELEA HUKU