Thursday, August 18, 2022

KIKI, PROMO, PROPAGANDA, WATOTO WA BABA MMOJA

 


Kiki ni neno ambalo limekuwa maarufu zama hizi za Bongofleva. Kiki ni neno lilitokana na neno la Kiingereza, ‘kick’ yaani teke. Hivyo kiki maana yake katika ulimwengu wa wasanii ni kutafuta tukio ambalo litashtua jamii na kupaisha sifa yao au ya kazi yao. Ni kama vile ambavyo ukimpiga teke chura ndio unamsaidia kuruka. Hivyo wasanii wa zama hizi hutafuta kiki za aina mbalimbali ili kupaisha sifa za kazi zao, wengine hujitangaza kuwa wamefariki, wengine utakasikia wamefumaniwa, au wengine wameachana au wengine kutangaza wamerudiana au wameoana, au mara nyingine kueneza taarifa kuwa wimbo wao umeibiwa studio, na imefikia hata wazazi wa wasanii wengine kuingia kikamilifu katika shughuli za kiki kwa kutoa matamshi tata kuhusu kazi za watoto wao ili tu watu waelekeze masikio na macho yao kwenye kazi mpya. Pamoja na neno kiki kuwa jipya lakini hakika kutafuta kiki hakukuanza na Bongofleva. Makampuni yenye kutaka kutangaza bidhaa mpya sokoni, yamekuwa yakifanya matukio mengi makubwa kutafuta kiki. Makampuni hupitisha magari yenye maspika makubwa mitaani na kutangaza bidhaa zao, au hufanya matamasha makubwa, au huanzisha hata misemo tata ili tu kupata kiki ya bidhaa zao. Lakini hapa haiitwi kiki inaitwa promosheni. Wanasiasa nao hakika ni mabingwa wa kiki,wakati wa kutafuta kura, kila aina ya vituko hufanyika. Tumeshaona wanasiasa wanapiga magoti kuomba kura, wengine hata kugaragara chini wakiomba kura, hao wanaoamua kucheza ngoma za kiasili au dansi jukwaani ni kawaida sana.  Na wakifungua mdomo kueleza sifa walizonazo na watakachokifanya vyote ni kujinadi ili kuonekana bora, ila huku haiitwi kiki inaitwa siasa, au wengine huiita propaganda. Zama hizi hata viongozi wa dini nao wamo katika kutafuta kiki, utasikia wakishusha sifa za uwezo wao kama katika vyombo mbalimbali vya matangazo, wengine wamefikia mpaka kuingilia matatizo ya wasanii maarufu ili nao wajulikane kuwa wapo. Kutokana na malezi duni ya baadhi ya wasanii, kiki hizi zimekuwa zikichukua sura mpya siku hadi siku. Kwa sasa zimefikia hata kuongea, kutangaza au kuonyesha vitu vya faragha hadharani, ikiwa kama njia ya kutafuta kiki, na hapo ndipo ugomvi na watu wenye busara zao unapoanza.

Kama nilivyosema mwanzo neno kiki ni geni lakini shughuli zake si ngeni kabisa. Bendi za zamani zilikuwa na njia kuu moja tu ya kupata pesa nayo ilikuwa kwa  kiingilio mlangoni, gate collection, na hakika kulilazimika kuweko na mbinu za kujitangaza, au kutafuta kiki. Kulikuwa na njia kuu tatu za kutangaza onyesho,  kwanza ni kupitia redioni na pili kupitia magazeti, na tatu kwa kubandika matangazo kwenye kuta na nguzo za umeme. Magazeti yaliyokuwa yakishughulika na muziki yalikuwa ni magazeti ya serikali, magazeti ya Chama Cha Mapinduzi na magazeti ya chama cha wafanyakazi, NUTA na baadae JUWATA.  Vyombo hivi havikuwa na maadili ya kuruhusu ‘kiki’ za maisha binafsi ya wanamuziki, matangazo yalilazimika kuwa yanayohusu muziki tu.  Hivyo ubunifu ulikuweko, bendi zilijinadi kwa staili zake zenye mvuto ili kutafuta kiki. Kulikuweko staili kama  Katakata mwendo wa jongoo vumbi nyuma, Bomoa tutajenga kesho, Super mnyanyuo, Sikinde ngoma ya ukae, Mahepe ngoma ya wajanja, Dunda dunda, Bayankata, Kokakoka balaa  na majina mengine mengi. Matangazo kwenye magazeti yaliwekwa picha za wanamuziki au kuchorwa picha za kujinadi kwa njia moja au nyingine. Maswala ya kuachana, kupendana, kuhongana, kufumaniana hayakuhusika kabisa katika kutangaza kazi ya muziki. Nikifikiria sana nadhani vitu ambavyo wasanii wa sasa hufanya katika kutafuta kiki, vingefanywa na wasanii wa miaka ile na kutangazwa kama ilivyo sasa ingekuwa ndio mwisho wa msanii huyo, jamii ingemtema.

Nadhani moja ya sababu ya kuweko kwa kiki za ajabu katika zama hizi, ni kujaribu kujazia mapungufu yaliyomo kwenye sanaa husika. Msanii anakuwa anajua hata yeye kuwa kazi yake ni duni,  hivyo anazua kitu kisichohusika kabisa na kazi yake ya sanaa ili kuweza kuwafanya wateja japo wasikilize kazi yake kwa muda.

Taratibu za kurekodi siku hizi nazo zinafanya msanii asiwe na uhakika wa mpokeo ya wimbo wake hivyo kulazimisha vituko ili kujulikana kama ana kazi mpya. Msanii wa kizazi cha sasa anaweza kutunga wimbo asubuhi akaingia studio na kukamilisha wimbo na jioni wimbo uko tayari youtube na umeanza kurushwa kwenye vyombo ya utangazaji mbalimbali,

Hali haikuwa hivyo zamani, ukiwa na wazo la wimbo unalipeleka kwenye bendi yako yenye watu zaidi ya saba, wao wanakusikiliza na kuamua kama uchukuliwe na bendi au la, wakikubali ndipo mnaanza kuujenga wimbo, magitaa, ngoma. vyombo vya upulizaji, kila mtu anatoa wazo lake. Wimbo ulichukua japo siku mbili kukamilika, ingawa kuna nyimbo zilichukua hata zaidi ya wiki kuwa tayari. Bendi ikiridhika , wimbo ulianza kupigwa kwenye maonyesho, na hapa ndipo wapenzi wa bendi walikuwa wakiingia na kutoa maoni yao, mkikubaliana ndipo unaenda kurekodiwa. Mara nyingi bendi zilikuwa zinajua kabla hata ya kwenda kurekodi wimbo gani utakuwa maarufu kutokana na maoni ya wapenzi. Kwa taratibu hizo kiki za kujidhalilisha zilikuwa hazina nafasi, kazi ilikuwa inajiuza yenyewe.

No comments:

Post a Comment