Showing posts with label congo. Show all posts
Showing posts with label congo. Show all posts

Monday, August 22, 2022

TABU LEY, MWANAMUZIKI ALIYEKUWA NA WATOTO ZAIDI YA MIA MOJA

 


 


Akiwa na bendi ya African Fiesta Tabu Ley aliimba wimbo ulioitwa Mokolo nakokufa, wimbo wa rhumba la taratibu uliotokea kupendwa Afrika nzima, baadhi ya maneno ya wimbo huo yalikuwa haya;

Mokolo mosusu ngai nakanisi

Naloti lokola ngai nakolala aah mama

Mokolo nakokufa

Mokolo nakokufa, nani akolela ngai ?

Nakoyeba te o tika namilela.

Liwa ya zamba soki mpe liwa ya mboka

Liwa ya mpasi soki mpe liwa ya mai O mama

Mokolo nakokufa

Kwa kifupi maana ya maneno haya ni;

Siku moja niliona kama nimeota siku yangu ya kufa,

Siku ya kufa nani atanililia? Sijui labda nitabiri.

Ntafia porini au nyumbani?

Kifo changu kitakuwa cha maumivu au kuzama majini?

Ahh siku yangu ya kufa.

Wimbo huu ulikuja kuwa na maana kubwa siku ya tarehe 30 Novemba 2013, siku taarifa ya kifo cha Tabu Ley ilipotolewa.
Tabu Ley maarufu kwa jina na Rochereau, alizaliwa 13 Novemba, mwaka 1940 huko Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo. Alianza maisha akiitwa Pascal Emmanuel Sinamoyi Tabu, jina la Rocherau lilikuwa ni jina la utani toka shuleni na ndilo alilolitumia alipopeleka nyimbo zake za kwanza kwa Joseph Kabasele wakati akiomba kujiunga na bendi ya African Jazz. Tabu Ley alianza maisha yake ya muziki mapema sana na 1954 akiwa na umri wa miaka 14 tu aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao akaurekodi na kundi maarufu la African Jazz lililokuwa chini ya Joseph ‘Grande Kalle’ Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle). Tabu Ley aliendelea na shule na hatimae alipomaliza ‘High School’ 1959, akajiunga rasmi na African Jazz. Tabu Ley alishiriki katika wimbo, ulioitwa Independence Cha Cha, wimbo huu  ulipendwa sana na kugeuka na kuwa wimbo rasmi wa kusherehekea uhuru wa Kongo uliopatikana May 1960. Tabu akapata  umaarufu mkubwa kuanzia hapo, na akakaa kwenye bendi hiyo mpaka mwaka 1963, ambapo yeye na mpiga solo maarufu  Nicolaus Kasanda, maarufu kwa jina la Dr Nico, wakaanzisha kundi lao la African Fiesta. Wapenzi wa muziki wa zamani, wana kumbukumbu za muunganiko huo wa magwiji hawa, Afrika iliwapokea na kuwakubali. Lakini mwaka 1965, wakati Kongo imewaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali sana, Tabu akaachana na Dr Nico na kuanzisha kundi lake la African Fiesta National au mara nyingine likiitwa Africa Fiesta Flash, wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni kati ya wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio katika siku zao za mwanzo. Mwaka 1970, Tabu Ley alianzisha kundi aliloliita Orchestre Afrisa International. Jina hilo lilitokana na kuunganisha majina ya ‘record labels’ zake mbili , Africa na Editions Isa akapata jina Afrisa.  Afrisa International na TP OK Jazz ndizo zilikuwa bendi maarufu zaidi Afrika katika kipindi hicho. Afrisa International waliteremsha vibao kama SorozoKaful MayayAon Aon, na Mose Konzo na  Tabu Ley aliweza hata kupata tuzo toka serikali za nchi kama Chad iliyompa heshima ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima ya Knight of Senegal, na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau. Katikati ya miaka ya 80 Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika naye si mwingine ila Mbilia Bel, baadae Tabu alimuoa Mbilia na wakapata mtoto mmoja. Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho mama huyu aliyekuwa mzuri kwa umbo na sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri. 1988 Tabu akamgundua muimbaji wa kike mwingine Faya Tess. Wakina mama hawa wakaleta mvutano mkubwa katika bendi, Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake.

Ni wakati wa kipindi hiki, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya lile rumba la Afrisa na TPOK Jazz ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.

Mwanzoni mwa miaka ya 90 Tabu Ley alihamia Marekani akaishi Kusini mwa California, akabadili muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la ‘Kimataifa’, akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley, Babeti Soukous. 1996 Tabu Ley alishiriki katika album ya kundi la Africando na kushiriki katika wimbo Paquita wimbo aliyokuwa ameurekodi miaka ya 60 akiwa na African Fiesta. Tabu alipata cheo cha Uwaziri katika utawala wa Laurent Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Laurent Kabila November  2005 Tabu alipewa cheo cha Vice- Governor wa mambo ya utawala, siasa na ustawi wa jamii wa jiji la Kinshasa.

Mwaka 2006  Tabu Ley  akashirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu Maika Munah na kutoa album yake ya mwisho iliyoitwa Tempelo, katika album hiyo kuna wimbo ambao ni kama kumbukumbu ya kote alikopita na pia akaimba wimbo mmoja na binti yake Melodie.

Mwaka 2008 alipata mshtuko wa moyo na hakika kuanzia hapo afya yake haikutengemaa mpaka kifo kilipomchukua siku ya Jumamosi Nov 30 2013, katika hospital ya St Luc Brusells Ubelgiji. Mchanganyiko wa matatizo ya kisukari na moyo ndiyo yaliyosababisha kifo cha mbuyu huu wa muziki wa rumba. Inasemekana tabu Ley alipata watoto 104 katika uhai wake. Hata yeye mwenyewe alipokuwa hai akiulizwa ana watoto wangapi alikiri kuwa hana uhakika. Watoto wake wachache walifuata nyayo za baba yao, akiwemo Melodie, binti aliyezaa na Mbilia Bel ambae sauti yake imo katika album ya mwisho ya Tabu Ley ‘Tempelo’ aliyoitoa mwaka 2006. Wengine katika muziki ni

 Pegguy Tabu, Abel Tabu, Philemon and Youssoupha Mabiki.

Youssoupha ni rapper anaeishi Paris, alizaliwa mwaka 1979 , mama yake alikuwa kutoka Senegal. Mwanae Marc Tabu ni mtangazaji kwenye TV moja huko Paris na ndie aliyetoa taarifa ya kwanza ya kifo cha baba yake kwenye ukurasa wake wa Facebook Novemba 2013

 

Wednesday, August 17, 2022

MJUE JEAN 'JOHNNY' BOKELO ISENGE

 

 


 Jean ‘Johnny’ Bokelo Isenge alizaliwa mwaka 1939 nchini Kongo, nje kidogo ya jiji la Kinshasa. Familia yake ilikuwa ni ya wanamuziki. Johnny alikuwa mdogo wa Paul Ebengo’Dewayon’ Isenge mwanamuziki mwingine aliyekuwa mkubwa sana nchini Kongo toka mwanzoni mwa miaka ya 50. Huyu Dewayon alikuwa na bendi inaitwa Watam, hapa ndipo Johnny alipoanzia muziki akipiga na mtoto mwingine aliyekuja kutikisa ulimwengu wa muziki Franco Luambo Luanzo, wakati huo Franco akiwa na miaka 12 tu. Johnny Bokelo aliendelea kupiga katika bendi alizoanzisha kaka yake kama vile Conga Jazz na Orchèstre Cobantu, lakini mwaka 1958 Johhn akaanzisha bendi yake, Orchestre Conga Succès, akiwa na mdogo wake Mpia Mongongo maarufu kwa jina la Porthos Bokelo, ambaye alikuwa mpiga gitaa la rhythm mahiri sana. Kaka yao Dewayon, akaja kujiunga na kundi hilo1960 lakini miaka miwili baadae1962 Johnny na kaka yake wakatengana. Bokelo alifanikiwa kulijenga kundi lake kuwa na nguvu na likawa kwa namna fulani linafanana sana na OK Jazz. Hata tungo nyingine zilikuwa ni za kujibu tungo za OK Jazz au kuzungumzia mada ambayo imeanzishwa na OK Jazz. Hii haikuwa kwa ugomvi bali kutokana na ukaribu uliokuwa kati ya Franco na Johnny. Kuna wakati Bokelo alianzisha mtindo wa kutunga nyimbo alizozipa jina la Mwambe, kukawa na Mwambe no 1 na 2 mpaka 5 ambapo alikuwa akiongea na kushangaa jamii inaelekea wapi. Upigaji wa Bokelo Dewayon na Franco ulishabihiana, pengine ni kutokana na wote kuanzia Watam. Mwaka 1968 Johnny Bokelo akabadili jina la kundi lake la Conga succès” na kulita “Conga 68” akaanzisha label yake akaanza kutoa santuri, hii ilimuongezea kipato japo wanamuziki wake walitishia kuachana nae kwani walisema hawakuwa wanapata fedha zozote kutokana na mradi huo. Santuri nyingi wakati huu alikuwa akiziachia kwanza kutoka Ufaransa ili kupata mapato zaidi. Kati ya 1972 mpaka 1974 Bokelo Isengo alikuwa anatumia muda mwingi zaidi akiwa studio, kwenye mwaka 1970, viwanda vya kutengeneza santuri vya Kinshasa vikawa vimechoka hivyo bokelo akaanza kupeleka master zake Kenya ili kutengeneza santuri. Mwaka 1980 Bokelo aliachana sana na shughuli za muziki.

Bokelo alifariki 15 January 1995 baada ya kuugua kwa muda mrefu