Akiwa na bendi ya African Fiesta Tabu Ley aliimba wimbo
ulioitwa Mokolo nakokufa, wimbo wa rhumba la taratibu uliotokea kupendwa Afrika
nzima, baadhi ya maneno ya wimbo huo yalikuwa haya;
Mokolo mosusu ngai
nakanisi
Naloti lokola ngai
nakolala aah mama
Mokolo nakokufa
Mokolo nakokufa, nani
akolela ngai ?
Nakoyeba te o tika
namilela.
Liwa ya zamba soki mpe
liwa ya mboka
Liwa ya mpasi soki mpe
liwa ya mai O mama
Mokolo nakokufa
Kwa kifupi maana ya maneno
haya ni;
Siku moja niliona kama
nimeota siku yangu ya kufa,
Siku ya kufa nani
atanililia? Sijui labda nitabiri.
Ntafia porini au
nyumbani?
Kifo changu kitakuwa
cha maumivu au kuzama majini?
Ahh siku yangu ya
kufa.
Wimbo huu ulikuja kuwa
na maana kubwa siku ya tarehe 30 Novemba 2013, siku taarifa ya kifo cha Tabu
Ley ilipotolewa.
Tabu Ley maarufu kwa jina na Rochereau, alizaliwa 13 Novemba, mwaka 1940 huko Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasi ya
Kongo. Alianza maisha akiitwa Pascal Emmanuel Sinamoyi Tabu, jina la Rocherau
lilikuwa ni jina la utani toka shuleni na ndilo alilolitumia alipopeleka nyimbo
zake za kwanza kwa Joseph Kabasele wakati akiomba kujiunga na bendi ya African
Jazz. Tabu Ley alianza maisha yake ya muziki mapema sana na 1954 akiwa na umri
wa miaka 14 tu aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha, ambao
akaurekodi na kundi maarufu la African Jazz lililokuwa chini ya Joseph ‘Grande
Kalle’ Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle). Tabu Ley aliendelea na shule na
hatimae alipomaliza ‘High School’ 1959, akajiunga rasmi na African Jazz. Tabu
Ley alishiriki katika wimbo, ulioitwa Independence Cha Cha, wimbo huu ulipendwa sana
na kugeuka na kuwa wimbo rasmi wa kusherehekea uhuru wa Kongo uliopatikana May
1960. Tabu akapata umaarufu mkubwa kuanzia hapo, na akakaa kwenye
bendi hiyo mpaka mwaka 1963, ambapo yeye na mpiga solo maarufu Nicolaus Kasanda, maarufu kwa jina la Dr Nico,
wakaanzisha kundi lao la African Fiesta. Wapenzi wa muziki wa zamani, wana
kumbukumbu za muunganiko huo wa magwiji hawa, Afrika iliwapokea na kuwakubali. Lakini mwaka 1965, wakati Kongo imewaka moto
kimuziki na ushindani kuwa mkali sana, Tabu akaachana na Dr Nico na kuanzisha kundi
lake la African Fiesta National au mara nyingine likiitwa Africa Fiesta
Flash, wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni kati ya wakongwe
waliowahi kupitia katika kundi hili tishio katika siku zao za mwanzo. Mwaka 1970,
Tabu Ley alianzisha kundi aliloliita Orchestre Afrisa International. Jina hilo
lilitokana na kuunganisha majina ya ‘record labels’ zake mbili , Africa na Editions Isa akapata jina Afrisa. Afrisa
International na TP OK Jazz ndizo zilikuwa bendi maarufu zaidi Afrika katika
kipindi hicho. Afrisa International waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful
Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo na Tabu
Ley aliweza hata kupata tuzo toka serikali za nchi kama Chad iliyompa heshima
ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima
ya Knight of Senegal, na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau.
Katikati ya miaka ya 80 Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja
kutikisa anga za Afrika naye si mwingine ila Mbilia Bel, baadae Tabu alimuoa
Mbilia na wakapata mtoto mmoja. Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha
kipaji gani alikuwa nacho mama huyu aliyekuwa mzuri kwa umbo na sura, aliyejua pia
kucheza na kutawala jukwaa vizuri. 1988 Tabu akamgundua muimbaji wa kike
mwingine Faya Tess. Wakina mama hawa wakaleta mvutano mkubwa katika bendi, Mbilia akaacha bendi
na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake.
Ni wakati wa kipindi
hiki, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya lile rumba
la Afrisa na TPOK Jazz ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa
zikaanza kufifia.
Mwanzoni mwa miaka ya
90 Tabu Ley alihamia Marekani akaishi Kusini mwa California, akabadili muziki
wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la ‘Kimataifa’, akatunga nyimbo
kama Muzina, Exil Ley, Babeti Soukous. 1996 Tabu Ley
alishiriki katika album ya kundi la Africando na kushiriki katika wimbo Paquita wimbo
aliyokuwa ameurekodi miaka ya 60 akiwa na African Fiesta. Tabu alipata cheo cha
Uwaziri katika utawala wa Laurent Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata
baada ya kifo cha Laurent Kabila November 2005 Tabu alipewa cheo cha Vice- Governor wa mambo ya utawala, siasa
na ustawi wa jamii wa jiji la Kinshasa.
Mwaka 2006 Tabu
Ley akashirikiana na rafiki yake wa muda mrefu Maika Munah
na kutoa album yake ya mwisho iliyoitwa Tempelo, katika album hiyo kuna wimbo
ambao ni kama kumbukumbu ya kote alikopita na pia akaimba wimbo mmoja na binti
yake Melodie.
Mwaka 2008 alipata
mshtuko wa moyo na hakika kuanzia hapo afya yake haikutengemaa mpaka kifo
kilipomchukua siku ya Jumamosi Nov 30 2013, katika hospital ya St Luc Brusells
Ubelgiji. Mchanganyiko wa matatizo ya kisukari na moyo ndiyo yaliyosababisha
kifo cha mbuyu huu wa muziki wa rumba. Inasemekana tabu Ley alipata watoto 104
katika uhai wake. Hata yeye mwenyewe alipokuwa hai akiulizwa ana watoto wangapi
alikiri kuwa hana uhakika. Watoto wake wachache walifuata nyayo za baba yao,
akiwemo Melodie, binti aliyezaa na Mbilia Bel ambae sauti yake imo katika album
ya mwisho ya Tabu Ley ‘Tempelo’ aliyoitoa mwaka 2006. Wengine katika muziki ni
Pegguy Tabu,
Abel Tabu, Philemon and Youssoupha Mabiki.
Youssoupha ni rapper
anaeishi Paris, alizaliwa mwaka 1979 , mama yake alikuwa kutoka Senegal. Mwanae
Marc Tabu ni mtangazaji kwenye TV moja huko Paris na ndie aliyetoa taarifa ya
kwanza ya kifo cha baba yake kwenye ukurasa wake wa Facebook Novemba 2013
No comments:
Post a Comment