Showing posts with label buggy. Show all posts
Showing posts with label buggy. Show all posts

Thursday, August 18, 2022

TUMETIMIZA MIAKA 18 BILA PATRICK BALISIDYA

Patrick Balisidya, nyuma yake Salim Willis

Mwaka 1974 mwezi wa sita, ulikuwa mwezi wa furaha kwangu na wenzangu wa Operesheni Ukombozi pale Ruvu JKT.

Tulikuwa tumemaliza miezi sita ya kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa ‘kwa mujibu wa sheria’. Mafunzo ya miezi sita yaliyoanzia kambi ya Mafuleta kule Handeni na kukakamilika katika kambi kubwa ya Ruvu, mkoa wa Pwani. Miezi sita iliyojaa visa na vituko  vingi vya ujana, marafiki wapya, na shughuli nyingi za kujenga ukakamavu,  kama vile mchakamchaka kila asubuhi, paredi, route march na mazoezi mbalimbali ya kivita na  kazi mbalimbali zikiwemo kilimo cha mpunga, ufugaji wa kuku na ng’ombe, hakika hakukuweko muda uliokosa shughuli. Hatimae siku ya mwisho ilifika tukafanya paredi kubwa ya kumaliza mafunzo, chini ya Mkuu wa Kambi Marehemu Meja Jenerali Rashid Makame. 

Baada ya paredi ya 'Pass Out', kulikuwa na shamra shamra nyingi za kumaliza mafunzo  zilizoishia na dansi lililoporomoshwa na bendi ya Afro 70.
Pamoja na kuwa nilikuwa nafahamu habari za bendi hii na pia nilishaanza kununua santuri zao toka mwaka 1973, siku hiyo ilikuwa siku ya kwanza kuiona bendi hiyo ikiwa jukwaani. Ilikuwa furaha juu ya furaha. Furaha ya kumaliza muda wa kulitumikia Jeshi la Kujenga Taifa juu yake furaha ya kuiona Afro70, bendi tuliyozowea kuiita Afrosa, kutokana na jina la mtindo wa muziki wake.
Dansi lilianza kama saa tatu usiku hivi baada ya chakula cha jioni, Afro 70 hawakutuangusha, na nyimbo zao zilizokuwa maarufu ziliporomoshwa usiku kucha, Dirishani, Weekend, Dada Rida, Pesa, Tausi na nyingine nyingi, pia bendi ilipiga nyimbo za wanamuziki waliopendwa miaka hiyo akina Clarence Carter, Otis Redding, James Brown, Aretha Franklin, ilikuwa raha kubwa. Sharti la muziki wa siku hii ya mwisho ilikuwa ni bendi kupiga muziki mpaka jua litakapochomoza kwani mabasi yalikuja mapema ili kuondoka na askari tuliokuwa tumemaliza muda kurudi makwetu. Alfajiri tulitoka kwenye muziki na masunduku yetu na kuingia kwenye mabasi kurudi makwetu.
Nimekumbuka sana siku hii kwa kuwa mwezi huu tunatimiza  miaka kumi na nane toka tulipo mzika Patrick Balisisdya, mtunzi, muimbaji, mpiga gitaa na kiongozi wa bendi ya Afro 70 pale makaburi ya Buguruni Malapa.

Patrick Pama Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 April 1946. Mama yake alikuwa anapiga kinanda kanisani  hakika Patrick angeweza kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake. Alianza kushiriki katika mambo ya muziki mapema na hata kuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake pale Dodoma secondary School. Alipomaliza shule ya sekondari akajiunga na Chuo cha Ufundi Dar es salaam, maarufu wakati huo kwa jina la Dar Technical, baada ya kumaliza mafunzo Dar Tech, alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga muziki Dar Es Salaam Jazz B.
Bendi hii ilikuwa inafanya kazi nzuri sana hivyo kuanza kuwa tishio kwa bendi kongwe Dar es Salaam Jazz Band yenyewe ( Majini wa bahari), na hivyo uongozi wa Dar Jazz ukaamua kuivunja bendi hiyo ndogo kabla haijaipoteza kabisa bendi kaka. Patrick hakufurahishwa na hatua hiyo, kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa ameanzisha kikosi chake mwenyewe kilichoitwa Afro70, kikiwa na mtindo wake Afrosa.
Mkongwe Shebby Mbotoni aliwahi nihadithia jinsi walivyokuja na wazo la kuanzisha bendi ya Afro 70, bendi iliyokuja kumtambulisha Patrick ulimwenguni. Shebby alisema siku moja alikuwa kwao akipiga gitaa, ndipo Patrick alipomkuta wakati akiwa anamtafuta rafiki yake aliyekuwa amepanga nyumba hiyo aliyokuwa akiishi Shebby. Basi alijitambulisha na wakaanza urafiki na ndipo likaja wazo la kuanzisha bendi,  na hatimae ikazaliwa Afro 70,
 Patrick alikuwa  mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, hata bendi aliyokuwa akipigia, Dar es Salaam Jazz Band ilikuwa katika mkumbo huo wa kuiga bendi za Kikongo. Msimamo wa Patrick uliyumba baada ya kukutana na Franco wakati bendi ya TP OK Jazz ilipofanya ziara yake ya kwanza  nchini mwaka 1973, Patricka akaanza kuiga staili ya upigaji gitaa wa Franco. Wimbo wake wa Umoja wa kinamama, ulikuwa wazi umeiga sehemu kubwa wimbo wa Georgette wa TP OK Jazz.  

Afro70 ilipata bahati kuwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos, Nigeria. (FESTAC festival 1977). Bahati hii ilikuja baada ya Afro 70 kushinda mashindano ya bendi yaliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, kwa ajili ya kupata muwakilishi wa kwenda kwenye Tamasha hilo.  Baada ya mashindano, bendi ilipata fursa ya kuzunguka sehemu mbalimbali nchini kuonyesha kilichowafanya washinde na pia kupata mazoezi zaidi kabla ya safari ya kwenda Lagos. Lakini  bahati mbaya wakati wa kurudi Dar gari lao lilipata ajali na vyombo vya bendi vyote viliharibika. Wakati huohuo  Wizara ya Utamaduni ilikuwa imenunua vyombo vipya kwa ajili ya kuanzisha bendi yake, vyombo hivyo ilikabidhiwa Afro 70 kuvitumia FESTAC. Baada ya kurudi kutoka Nigeria Afro 70 waliamuliwa kurudisha vyombo vile serikalini, na  pia baada ya kurudi Festac bendi ilianza kusambaratika haikufanya onyesho tena kama Afro 70. Afro 70 ikafa rasmi.
Vyombo vile viliporudishwa serikalini vilitumika kuanzisha bendi ya Wizara ya Utamaduni iliyoitwa Asilia Jazz Band. Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado Kidogo. Patrick pia alipitia Orchestre Safari Sound, (Masantula) na kupiga piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie siri’, alipitia pia bendi iliyoitwa Rainbow Connection, nakumbuka kukutana nae nilipotaka kujiunga na bendi hiyo wakati ikipiga pale New Africa Hotel, lakini Patrick akanishauri nisijiunge kwani alisema kuwa hakuwa anaona maendeleo yoyote katika bendi ile. Utabiri ambao ulikuja kuwa kweli bendi ilikuja kusambaratika.
Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi,  Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama Lulu, Ni mashaka na mahangaiko, Afrika, na nyinginezo nyingi. Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004 na kuzikwa 12 Agosti katika makaburi ya Buguruni Malapa.

MUNGU AMLAZE PEMA PATRICK BALISDYA