Patrick Balisidya, nyuma yake Salim Willis
Mwaka 1974
mwezi wa sita, ulikuwa mwezi wa furaha kwangu na wenzangu wa Operesheni
Ukombozi pale Ruvu JKT.
Tulikuwa tumemaliza miezi sita ya kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa ‘kwa mujibu wa sheria’. Mafunzo ya miezi sita yaliyoanzia kambi ya Mafuleta kule Handeni na kukakamilika katika kambi kubwa ya Ruvu, mkoa wa Pwani. Miezi sita iliyojaa visa na vituko vingi vya ujana, marafiki wapya, na shughuli nyingi za kujenga ukakamavu, kama vile mchakamchaka kila asubuhi, paredi, route march na mazoezi mbalimbali ya kivita na kazi mbalimbali zikiwemo kilimo cha mpunga, ufugaji wa kuku na ng’ombe, hakika hakukuweko muda uliokosa shughuli. Hatimae siku ya mwisho ilifika tukafanya paredi kubwa ya kumaliza mafunzo, chini ya Mkuu wa Kambi Marehemu Meja Jenerali Rashid Makame.
Baada ya paredi ya 'Pass Out', kulikuwa na shamra
shamra nyingi za kumaliza mafunzo zilizoishia na dansi lililoporomoshwa na bendi ya Afro 70.
Pamoja
na kuwa nilikuwa nafahamu habari za bendi hii na pia nilishaanza kununua
santuri zao toka mwaka 1973, siku hiyo ilikuwa siku ya kwanza kuiona bendi hiyo
ikiwa jukwaani. Ilikuwa furaha juu ya furaha. Furaha ya kumaliza muda wa kulitumikia
Jeshi la Kujenga Taifa juu yake furaha ya kuiona Afro70, bendi tuliyozowea
kuiita Afrosa, kutokana na jina la mtindo wa muziki wake.
Dansi lilianza kama
saa tatu usiku hivi baada ya chakula cha jioni, Afro 70 hawakutuangusha, na nyimbo zao zilizokuwa maarufu
ziliporomoshwa usiku kucha, Dirishani, Weekend, Dada Rida, Pesa, Tausi na
nyingine nyingi, pia bendi ilipiga nyimbo za wanamuziki waliopendwa miaka hiyo
akina Clarence Carter, Otis Redding, James Brown, Aretha Franklin, ilikuwa raha
kubwa. Sharti la muziki wa siku hii ya mwisho ilikuwa ni bendi kupiga muziki
mpaka jua litakapochomoza kwani mabasi yalikuja mapema ili kuondoka na askari
tuliokuwa tumemaliza muda kurudi makwetu. Alfajiri tulitoka kwenye muziki na
masunduku yetu na kuingia kwenye mabasi kurudi makwetu.
Nimekumbuka sana siku
hii kwa kuwa mwezi huu tunatimiza miaka
kumi na nane toka tulipo mzika Patrick Balisisdya, mtunzi, muimbaji, mpiga
gitaa na kiongozi wa bendi ya Afro 70 pale makaburi ya Buguruni Malapa.
Patrick Pama
Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 April 1946. Mama yake alikuwa anapiga
kinanda kanisani hakika Patrick angeweza
kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake. Alianza kushiriki katika mambo ya
muziki mapema na hata kuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake pale Dodoma
secondary School. Alipomaliza shule ya sekondari akajiunga na Chuo cha Ufundi
Dar es salaam, maarufu wakati huo kwa jina la Dar Technical, baada ya kumaliza
mafunzo Dar Tech, alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga
muziki Dar Es Salaam Jazz B.
Bendi hii ilikuwa inafanya kazi nzuri sana hivyo kuanza kuwa tishio kwa bendi
kongwe Dar es Salaam Jazz Band yenyewe ( Majini wa bahari), na hivyo uongozi wa
Dar Jazz ukaamua kuivunja bendi hiyo ndogo kabla haijaipoteza kabisa bendi kaka.
Patrick hakufurahishwa na hatua hiyo, kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa
ameanzisha kikosi chake mwenyewe kilichoitwa Afro70, kikiwa na mtindo wake
Afrosa. Mkongwe Shebby Mbotoni aliwahi nihadithia jinsi walivyokuja na
wazo la kuanzisha bendi ya Afro 70, bendi iliyokuja kumtambulisha Patrick
ulimwenguni. Shebby alisema siku moja alikuwa kwao akipiga gitaa, ndipo Patrick
alipomkuta wakati akiwa anamtafuta rafiki yake aliyekuwa amepanga nyumba hiyo
aliyokuwa akiishi Shebby. Basi alijitambulisha na wakaanza urafiki na ndipo
likaja wazo la kuanzisha bendi, na
hatimae ikazaliwa Afro 70,
Patrick alikuwa mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu
alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho
hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, hata bendi aliyokuwa akipigia, Dar es
Salaam Jazz Band ilikuwa katika mkumbo huo wa kuiga bendi za Kikongo. Msimamo
wa Patrick uliyumba baada ya kukutana na Franco wakati bendi ya TP OK Jazz ilipofanya
ziara yake ya kwanza nchini mwaka 1973,
Patricka akaanza kuiga staili ya upigaji gitaa wa Franco. Wimbo wake wa Umoja
wa kinamama, ulikuwa wazi umeiga sehemu kubwa wimbo wa Georgette wa TP OK Jazz.
Afro70 ilipata
bahati kuwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos,
Nigeria. (FESTAC festival 1977). Bahati hii ilikuja baada ya Afro 70 kushinda
mashindano ya bendi yaliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, kwa ajili ya kupata
muwakilishi wa kwenda kwenye Tamasha hilo.
Baada ya mashindano, bendi ilipata fursa ya kuzunguka sehemu mbalimbali
nchini kuonyesha kilichowafanya washinde na pia kupata mazoezi zaidi kabla ya
safari ya kwenda Lagos. Lakini bahati
mbaya wakati wa kurudi Dar gari lao lilipata ajali na vyombo vya bendi vyote viliharibika.
Wakati huohuo Wizara ya Utamaduni
ilikuwa imenunua vyombo vipya kwa ajili ya kuanzisha bendi yake, vyombo hivyo
ilikabidhiwa Afro 70 kuvitumia FESTAC. Baada ya kurudi kutoka Nigeria Afro 70
waliamuliwa kurudisha vyombo vile serikalini, na pia baada ya kurudi Festac bendi ilianza
kusambaratika haikufanya onyesho tena kama Afro 70. Afro 70 ikafa rasmi.
Vyombo vile viliporudishwa serikalini vilitumika kuanzisha bendi ya Wizara ya
Utamaduni iliyoitwa Asilia Jazz Band. Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na
kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado
Kidogo. Patrick pia alipitia Orchestre Safari Sound, (Masantula) na kupiga
piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie siri’, alipitia pia bendi iliyoitwa
Rainbow Connection, nakumbuka kukutana nae nilipotaka kujiunga na bendi hiyo
wakati ikipiga pale New Africa Hotel, lakini Patrick akanishauri nisijiunge
kwani alisema kuwa hakuwa anaona maendeleo yoyote katika bendi ile. Utabiri
ambao ulikuja kuwa kweli bendi ilikuja kusambaratika.
Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi, Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa,
Nakupenda kama Lulu, Ni mashaka na mahangaiko, Afrika, na nyinginezo nyingi.
Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004 na kuzikwa 12 Agosti katika makaburi ya
Buguruni Malapa.
MUNGU AMLAZE
PEMA PATRICK BALISDYA