Tuesday, March 29, 2011

Wakongwe katika muziki wa dansi

Wakongwe wa muziki wa dansi katika picha moja ya kumbukumbu, kutoka kushoto waliosimama ni Capt Mstaafu John Simon, huyu ni mwimbaji ambaye alikuweko katika miaka ya kwanza ya NUTA, yeye pamoja na wenziwe wakatumwa na marehemu Mzee rashid Kawawa kwenda kuanzisha bendi ya JKT pale Mgulani, na akiwa kama kiongozi JKT ilikuja juu na kujulikana kama JKT Kimbunga kutokana na staili yao ya Kimbunga, kati ya tungo zake maarufu ni wimbo Sakina. Anaefuata ni Mzee Shem Karenga, mpiga solo na kiongozi wa Tabora Jazz, ndiye aliyepiga solo nyimbo kama Asha, Alhamdulilah, Lemmy, Chakula kwa jirani, na nyimbo nyingine nyingi zilizotikisa Afrika ya Mashariki na Kati, anaefuata si mwingine ila ni yule mwimbaji maarufu, Mjomba, Mzee Muhidin Gurumo, alisikika enzi za NUTA, JUWATA, OTTU, Mlimani Park, OSS Ndekule, na sasa Msondo Group nani asiyemjua? anaefuata alikuwa mtunzi na mwimbaji maarufu  wa Cuban Marimba Marehemu Juma Kilaza, alikuwa bingwa wa kwanza wa kurap katika nyimbo, enzi hizo muziki wake ukikolea utasikia, 'Pwaga pwaga pwaga weka ngoma chini', na staili zake Ambianse, Subisubi alileta upinzani mkubwa kwa bendi nyingine kali kutoka Morogoro wakati huo, Morogoro Jazz chini ya mkongwe mwingine Mbaraka Mwinshehe. Anafuata Ally Rashid-Mwana Zanzibar, huyu ni mpuliza saxophone maarufu aliyetokea Zanzibar miaka nenda rudi na kupitia bendi kama Urafiki , Bima, Shikamoo, na hatimae Msondo ngoma, kutokana na afya yake amekuwa adimu katika maonyesho ya bendi hiyo. Mzee Kassim Mapili, Sergeant wa polisi mstaafu, mpiga gitaa wa miaka nenda rudi ambae katika enzi zake bendi ya polisi ilikuwa juu sana na staili yao ya Vangavanga, amewahi kwa muda mrefu sana kuwa mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania(CHAMUDATA). Anaefuata ni Mzee Salum Zahoro, kiongozi wa bendi ya Kiko Kids toka Tabora, bendi ambayo wakati nyingine ziliingia mtindo wa kupiga gitaa la solo, bendi hii iliendelea kutumia Mandolin, nyimbo kama Sili sishibi silali, ni moja ambayo mandolin ndio imeshika nafasi ya gitaa la solo, pia Mzee huyu ni mwimbaji mahiri, kama anavyosikika katika nyimbo hizo na hata katika nyimbo kama mwamtetea nini, kwa sasa ni kiongozi wa Shikamoo jazz na bado sauti yake iko palepale licha ya kuwa na umri wa zaidi ya miaka sabini. Alikuwa rafiki mpenzi wa marehemu Salum Abdallah wa Cuban Marimba. Waliochuchumaa mpiga solo gitaa maarufu Nguza Viking aliyeingia nchini na bendi ya Marquis du Zaire, na mwishoni kuwa na bendi yake Achigo Sound, ambapo alipigia mpaka alipokutwa na hatia ya kubaka watoto wadogo anatumikia kifungo cha maisha. Mzee Majengo, mpiga saxophone mwingine wa miaka mingi aliyewahi kupigia bendi kama Maquis enzi za umaarufu wake, kwa sasa yuko na Shikamoo Jazz. Na mwisho ni Mzee John Kijiko, mpiga gitaa aliyewika sana katika bendi ya Atomic wakati huo wakipiga vibao kama Mado, Masikini Suzy, kwa mtindo wa Kiweke na kuleta upinzani mkubwa kwa bendi nyingine ya Tanga, Jamhuri Jazz. Mzee John Kijiko(RIP), pia alipitia bendi ya UDA na hata Magereza Jazz Band wana Super Mnyanyuo

11 comments:

  1. Mkuu Kitime asante sana kwa kutuletea habari hizi nzuri za wazee wetu wanaopaswa kupewa heshima tele katika ulimwengu wa muziki wetu wa dansi Tanzania,kwa kuongezea tu naona umemsahau mzee wangu mzee John Kijiko hapo chini,kwa walio chuchumaa mwisho kulia.Huyu mzee(marehemu)sitomsahau
    kwa kunipa moyo wa kuendelea na muziki aliponipokea Uda Jazz 1981
    RIP.
    Abbu Omar,Prof.Jnr(Mwanamuziki)Tokyo,Japan

    ReplyDelete
  2. Shukrani sana kwa hii picha,-Mimi naomba kujua juu ya Twahiri, mpuliza saxophone wa OSS nyakati zile,-je!! huyu bwana yupo hai?

    ReplyDelete
  3. Mdau umeulizia kuhusu Twahir Mohamed,bahati mbaya ndugu yetu alifariki siku nyingi sina uhakika kama haikutangazwa huko Tanzania,alifariki 29/Jan/2004 mjini Nairobi Kenya,alizikwa katika makaburi ya waislam yaliyopo
    Kibera(Makina)kifo chake kilisababishwa na kuumwa.Kabla ya kifo chake niliwahi kupiga nae ktk bendi ya Simba Wanyika,pia alipitia
    Virunga ya Samba Mapangala,bendi moja ya reggae,pia alikuwa akipiga part time miziki ya hotel katika Hotel Intercontinental Nairobi,pia aliweza kuanzisha kundi lake la Bora bora pamoja na marehemu Shabani Dogo dogo,Msichoke Kombo nk.Baadae alibadilisha jina la bendi yake na kuiita Golden Sound hadi kifo chake.Katika Simba Wanyika tulishirikiana nae ktk kurekodi album tatu "Baba Asia"Haleluya"na Kipenzi tulia,hii album ya Kipenzi ndiyo ilikuwa album yetu ya mwisho kushiriki
    (mimi na Twahir)ktk Simba Wanyika kabla Wilson na George Peter kufariki,mimi nilihamia Japan mwisho kabisa wa 1992.Mkaburi aliyozikiwa Twahir ndipo alipozikiwa Wilson Peter,Wison katika maisha yake alikuwa akifuata madhehebu na maisha ya kiislam na jina lake lilikuwa Juma,ila aliendelea kutumia jina la Wilson Peter kwa kuwa lilifahamika sana kisanii napia katika rekodi nyingi alizorekodi.Tumepoteza wanamuziki mahiri Tanzania na Afrika.Pia mwingine ni Mohamed Shaweji,huyu aliwahi kuimbia Vijana Jazz miaka ya nyuma huyu nae nadhani watu hawana habaru za kifo chake kamili,yeye alifariki(sina uhakika ni lini)alifia mjini Kakamega na siyo Kisumu kama watu wanavofahamu,alipata mwanamke huko akaamua kuishi nae huko huko hadi alipougua na kufariki.Mungu awalaze pahali pema peponi ndugu
    zetu hawa. Abbu Omar,Prof.Jr,(mwanamuziki)Tokyo,Japan.

    ReplyDelete
  4. Tunashukuru bw.Abbu Omar kwa kutupa habari zinazo onekana kuwa na uhakika kabisa,kuna wanamuziki wengi mashuhuri wa kitanzania ambao
    walitoa mchango wao mkubwa katika fani hii nchini na kwa bahati mbaya hupotea kimya kimya na pengine huwa wametangulia mbele za haki,tatizo linakuja kuwa huwa hakuna njia nzuri au mfumo mzuri wa kuwaenzi wanamuziki hawa,fikiria watu kama Twahir ni mwanamuziki mkubwa sana katika bara letu zima la Afrika hata Ulaya/Marekeni nk.anajualikana,lakini cha kusikitisha ni vyombo vyetu vya habari hapa bongo sijui kama huwa vina puuza au kutokuwa na njia nzuri za kutafuta habari??mimi nashauri tu kuwa vyombo vinavyohusika kama wizara ya utamaduni,Chamudata,Cosota nk.viwe na system ya kutoa au kuwaenzi wanamuziki wetu hasa wakongwe,tunaona vyombo vya habari vimelalia sana ktk bongo movies na muziki wa kizazi kipya,jamani tujaribu kuwa organised ili kuleta maendeleo katika fani hii ya sanaa hasa upande wa muziki wetu wa dansi.
    Albert Katsenga,Oysterbay,Dar

    ReplyDelete
  5. Mdau anasema kweli kabisa mimi ushauri wangu mkubwa uwe kwenye hizi redio za siku hizi kama cloud nk,Hawa watangazaji chipukizi wanajiona ni watangazaji wa kimataifa na kuziona redio zao ni bora,cha kushangaza hawajifunzi historia ya muziki wa nchi yetu,wao tangu waanze kutangaza na kuijua redio wanajua bongo fleva tu.Mfano ukipita katika stesheni nyingi za redio hizo uwaulize hao watangazaji maswali rahisi tu km.je?Unawajua mf.Ahmad Kipande,Dunkan Njilima,Wema Abdallah,Juma Mrisho,Abel Bartazal,Maneti na wengineo ???Utakuta wengi wa hawa watangazaji wamjui hata mwanamuziki mmoja labda majina ila bendi walizopigia hawatajua,huu ndio u mbumbumbu wa hali ya juu,kama mtangazaji inabidi usome historia ya mambo mengi ya dunia km nuziki wa nchi yako na wa nje pia.Mimi bado naiheshimu redio Tanzania na wakongwe wote watangazaji enzi zile kama akina Nyaisanga,Msoud Masoud nk.walikuwa wanazijua bendi pamoja na wanamuziki wote wa Tanzania hata wa
    kikongo.Naziomba redio ndogo ndogo hizi za mitaani zijiffunze na kuwaenzi wanamuziki wetu.
    mpenzi wa muziki Tanga.

    ReplyDelete
  6. Du !!!hiyo ni kweli kabisa,haya kazi kwenu watangazaji wa redio "mbao" inabidi mjifunze zaidi na siyo kuridhika na kazi yenu ilhali mnashindwa hata kujua historia ya muziki wa nchi yenu,inatia huruma.

    ReplyDelete
  7. Naomba kusahihisha kidogo. Chakula nakula kwa irani aliyepiga solo gitaa ni marehemu Athuman Tembo

    ReplyDelete
  8. Uko sahihi kabisa, kuna posting humu ambayo inaonyesha picha ya Tabora Jazz band wakati wa enzi ya Chakula kwa Jirani. Aksante kwa masahihisho

    ReplyDelete
  9. Naomba wimbo wa Mwamtetea nini uwe uploaded kwa kumuenzi mzee salum zahoro

    ReplyDelete
  10. Msanii gani wa kizazi kipya ambae baba ake alitumikia jazz bandi

    ReplyDelete
  11. Kina viongozi wangapi wa jazz band na majina yao nataka kuyajua

    ReplyDelete