TINO MASENGE MWENYE MIC MBELE AKIWA NA WENZIE WA SIKINDE
Tino Joakim Masenge, kwa wengi alijulikana kama Tino Masinge
Arawa, alizawa kijijini Maharo, wilaya
ya Rombo mwaka 1961. Mwaka 1969 alianza shule Mkuu Extendes Primary school na mwaka 1972, na akajiunga Kawe Primary
School, akajiunga na Mzizima Secondary na kumaliza kidato cha nne 1980.
Alianza kuimba kwaya primary na pia alikuwa anapiga
accordion. Babu yake alikuwa mpiga mbiu au chombo kijulikanacho kama iranda.
Baba yake mdogo Francis Petro Masenge alikuwa mpiga accordion maarufu na kila
mara alikuwa akikodishwa kusindikiza harusi kule kwao Rombo, pia alikuwa mtunzi
wa nyimbo zilizogusa matatizo ya jamii yake na hivyo kupendwa katika jamii yake. Kuna wakati
aliwahi kumtungia wimbo binamu yake ambaye ni Baba wa Wabunge wawili maarufu
akiimba kuwa mzee huyo akafungwe Sumbawanga kutokana na tatizo la kifedha
lililotokea pale kijijini kwao. Wakati huo kufungwa Sumbawanga ilikuwa jambo
kubwa na baya kwa mwenyeji wa Rombo. Wimbo ulipata umaarufu katika jamii pale
Rombo.
Bendi ya kwanza ya
Tino ilikuwa Dar International Orchestra, alijiunga 1983 na kukaa nayo mpaka
1985. Alivutiwa na Marijani na akaanza kuimba nyimbo zake kabla hata ya
kujiunga na Dar International. Na hii ilimrahisishia hata kuingia katika bendi
hii na pia kuachiwa kuimba nyimbo nyingi za Marijani. Hakujiendeleza katika
vyombo alitaka ajikite zaidi katika uimbaji.
Katika kipindi cha Dar International alijikuta amekuwa simulizi kiasi cha
kwamba baada ya Fresh Jumbe kuondoka JUWATA alifuatwa ili kujaza pengo la
Fresh. Katika bendi ya Dar International alishiriki kurekodi nyimbo kama Masudi,
Ubaya wa Jirani na kadhalika.
Alikaa JUWATA JAzz kwa muda wa miaka mitano 1985 -1990, kati
ya nyimbo zilizorekodiwa alizoshiriki ni Solemba. Tino alikuja kufuatwa na OSS
Ndekule na kusaini mkataba wa miaka miwili lakini akadumu kwa mwaka mmoja
kutokana na hali ya kutokuelewana na wenye bendi. Kwa kadri ya Tino katika
mazungumzo yake, alisema kuwa kulikuwa
ni maslahi madogo na maelewano madogo kati ya wanamuziki na uongozi. Alipohama Ndekule
akajiunga na Sikinde mwaka 1991. Akiwa
na kundi la Sikinde ndipo alipotunga kibao cha Arawa, kibao kilichompa umaarufu
na hata kubakia na jina jipya la Arawa maisha yake yote. Akiwa Sikinde pia
alitunga wimbo ulioitwa Jino la embe si dawa ya pengo. Tino na wenzie
walianziasha bendi ambayo haikudumu muda mrefu iliyoitwa Super Sikinde
Academia.
Baada ya hapo yeye na wenzie kadhaa walijikusanya na kuanzisha kundi la TZ
Brothers.
Tino aliwahi kusema moja wapo ya kitu
kilichomfanya ahame Sikinde ni hali ya kuona kabanwa sana kiusanii akashindwa
kuonyesha uwezo wake wote, na kujiona ni mtu wa kuitikia tu katika nyimbo licha
ya kuimba na watu kama Marijani Rajabu
na Niko Zengekala.
Kundi la TZ Brothers lilipata ufadhili mkubwa kutoka kwa Simon
Sewando, mwanamuziki wa zamani wa bendi za Kwiro na Mkwawa Secondary, ambaye ni
mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mlimani ambaye alitoa vyombo na kuwaeleza wanamuziki
kuwa wajitegemee wakati huohuo wakimpa sehemu ya mapato katika kumrudishia
gharama za kununua vifaa.
Walioanzisha TZ Brothers walikuwa Tino Masenge, Henry Mkanyia, Julius Mzeru
Gaspar Kanuti, Kejeli Mfaume, Kalamazoo Nyembo, Siraji Lumumba, na Mzee Sewando
Mwenyewe (ukitaka kujua hadith ya Mzee Sewando BONYEZA HAPA. Kati ya kibao
kilicho tikisa sana cha bendi hii kilikuwa kibao Blandina Stanley au maarufu
Funga Mtaa, kilichoanza kwa rumba lililoimbwa vizuri sana na Tino na kumalizika
na mtindo wa Vanga. Bahati mbaya bendi ya TZ Brothers ilisambaratika.
Tino Masinge nae alishatangulia mbele za haki, hatunae tena duniani MUNGU
AMLAZE PEMA ARAWA
No comments:
Post a Comment