Friday, August 26, 2022

UTAMADUNI WA WANAUME KUIMBA NAFASI ZA WANAWAKE UENDELEE USIENDELEE?

 

jOHN KITIME AKIWA TANCUT ALMASI ORCHESTRA 1988

Mume wangu Jerry – Mlimani Park Orchestra, Mfaume – Mlimani Park Orchestra, Mfaume- Orchestra Makassy, Nimemkaribisha nyoka- Tancut Almasi Orchestra,  Mabruki- Maquis, Mke Mkubwa – Vijana Jazz, Rehani-Oss Ndekule, Kalubandika- Maquis, Ndoa ya Mateso – Dar es Salaam International Orchestra hii ni orodha ndogo sana ya nyimbo nyingi za bendi tofauti lakini zina kitu kimoja ambacho kinafanana. Waimbaji  walikuwa wanaume, walikuwa wakiimba nafasi za wanawake. Hebu tuangalie baadhi ya maneno katika nyimbo hizi.  Wimbo Mfaume wa Orchestra Makassy uliimbwa na Issa Nundu na Kyanga Songa ulikuwa na maneno haya,

Ewe Mfaume umefikaa nyumbani kwetu

Mimi bado nasoma mama,

Ukanieleza kwamba unataka tufunge

Pingu za maisha pamoja

Nami nikakweleza subiri

Nikimaliza shule ewe Mfaume

Kwa kuwa siwezi kuolewa  bado ningali mwanafunzi oyoo.

Sehemu ya wimbo wa Tancut Almasi Orchestra Nimemkaribisha Nyoka ulioimbwa na Kasaloo Kyanga ulikuwa na maneno yafuatayo.

Mume wangu alipotoka kazini,

Nikamuelezea mambo yote mama

Naye pia akakubali  kama ni dada yake ambaye wamezaliwa tumbo moja

Basi tukaendelea kuishi kama mtu na wifi yake ndani ya nyumba

Marijani Rajabu akiwa na Dar es salaam International nae aliimba maneno haya katika wimbo Ndoa ya Mateso;

Niulizieni enyi walimwengu, huyu mwanaume anavyonitesa

Hii ndio haki au ni mateso, hii ndio haki au ni mateso,

Kanitoa kwetu kwa baba na mama, Kwa vigelegele na heshima nyingi,

Tizameni sasa anavyonigeuka, Tizameni sasa anavyonigeuka

Ananipa mateso huku ugenini sina hata ndugu wa kunisaidia

Nami nina watoto jamani tabu gani

Nami nina wayoto jamani tabu gani

Kwani kuolewa ni jambo la ajabu au kuolewa sawa na utumwa

Kama ndivyo hivyo mimi nimeshindwa

Kama ndio hivyo mimi nimeshindwa

Natoa ushhidi kwako we mjumbe, mwambie huyo bwana anipe talaka yangu

Nisije kuondoka ikawa maneno, nisije kuondoka ikawa maneno

Wimbo ulioitwa Masikitiko wa Tancut Almasi Orchestra ulikuwa na maneno haya,

Kinachonisikitisha ni kuona kwamba nakosa mume, wa kunioa mama,

Nami nijisikie kama wenzangu waliobahatika kuolewa iyooo iyoo

 Nyimbo hizi zilitungwa na kuimbwa na wanaume na ni nyimbo ambazo bado hazijapoteza umaarufu  japo nyingine zina zidi ya miaka 40 toka zilipoanza kusikika. Haikuwa kitu cha ajabu kwa wanaume kuimba kuhusu matatizo na maisha ya wanawake hapo zamani. Moja ya sababu ilikuwa ni kukosekana kwa waimbaji wa kike katika muziki wa bendi za dansi, lakini hata pale ambapo bendi zilikuwa na waimbaji wa kike bado nyimbo zilizohusu wanawake zilitungwa na kuimbwa na wanaume bila kuweko na shida yoyote. Ulikuwa usanii wa kiwango cha juu sana. Siku hizi ni nadra sana kusikia sanaa ya aina hii, na hakika ilipigwa vita na hata viongozi kadhaa ambao waliona ni kosa wanaume kuimba nafasi za wanawake. Pengine kitu kilichofanya watu waanze kuona kama ni tatizo wanaume kuimba maneno ya wanawake ni pale utamaduni wa ushoga ulipoanza kujitokeza  hadharani. Lakini jambo hili si geni kabisa katika sanaa, Tyler Perry ni muigizaji maarufu ambaye moja ya sifa yake kubwa ni kuigiza nafasi ya mwanamke  Mabel ‘Madea’ Simmons, na ameweza kutengeneza sinema nyingi akiigiza kama mwanamke Madea, na hakika ukiangalia simema hizo utaona jinsi alivoweza kuvaa nafasi yake. Hata hapa kwetu msanii Joti amekuwa na mafanikio makubwa katika kuigiza nafasi ya mwanamke katika vichekesho vyake vingi, na ndivyo ilivyokuwa kwa watunzi na waimbaji wengi wa bendi wa zamani. Siku hizi kuna waimbaji wengi sana wa kike, lakini je wanazungumza matatizo ya wanawake kwa uzito uliokuwa unabebwa na wanaume katika nyimbo za dansi zilizotajwa? Kuna waimbaji wa kike mashuhuri kwa ‘mipasho’,  hizi ni tungo ambazo mara nyingi ni kuwasema wanawake wengine na hasa katika kugombea penzi la wanaume. Kundi jingine la waimbaji wa kike wamejikita zaidi katika kuimba nyimbo za mapenzi  za  kujisifia jinsi watakavyowafurahisha wanaume tu, hivyo pengo la nyimbo zinazoongelea matatizo ya wanawake limekuwa kubwa  zaidi, pengine inasubiriwa wanaume waanze tena kutunga na kuimba nyimbo kwa kuvaa  matatizo ya wanawake. 
Katika kuongea na baadhi ya waimbaji wa kiume wa siku hizi wengi walisema wanaona aibu kuimba nyimbo ambazo wanaimba kama ‘ mke wa mtu’, kubwa likiwa ni kuogopa kuhisiwa kuwa si mwanaume kamili.  Hakika hapa nalazimika kushangaa kidogo, kwani mwanamuziki huyohuyo ambaye ameamua kutoga masikio na kuvaa heleni na kutinda nyusi huku amesuka vizuri nywele zake, na suruali kashusha kuonyesha nguo yake ya ndani anasema anaona aibu kuimba nyimbo zenye maneno ya wanawake kwani atahisiwa vibaya!!!

Nadhani usanii huu wa wanaume kuimba nyimbo zenye ujumbe kwa wanawake, bado unanafasi katika sehemu kubwa ya jamii yetu ambayo haina hisia mbaya, na pia kwa kuwa waimbaji wa kike wenyewe hawataki kubeba jukumu lao la kuelezea ulimwengu matatizo yao na ya wanawake wenzao. Nimalize kwa kuandika maneno ya wimbo Nirudishe Kwetu uliopigwa na NUTA miaka ya 70, na kuimbwa na akina Hassan Rehani Bitchuka na Mzee Muhidini Gurumo..

Mume wangu nirudishe kwetu, Nyumba yako imekwisha nishinda

Sababu watoto wako sielewani nao, kila nisemalo wasema mimi mama wa kambo

Kumbuka nilikueleza usimuache mama watoto wako

Kumbuka nilikueleza usimuache mama watoto wako

Watoto wengi mmekwisha zaa nae mmrudishe mama watoto wako.

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment