Kati ya
wanamuziki maarufu ambao waliteka masikio ya wapenzi wa muziki wa Kenya katika
miaka ya 60 mmoja wao ni Daudi Kabaka Masika, maarufu kama Mtoboa Siri, alipewa jina hili kutokana na tungo zake zilizokuwa na vituko vilivyoweka wazi ukweli.
Daudi kabaka
alizaliwa Kyambogo Uganda mwaka 1939. Baba yake alimpa jina la Daudi Kabaka
kutokana na jina la Kabaka Daudi Chwa aliyekuwa mfalme wa Wabaganda aliyefariki
mwaka 1939. Mwaka 1950, Daudi alihamia Nairobi kumfuata baba yake aliyekuwa
mfanya kazi wa shirika la reli la East African Railways and Harbours,na akajiunga na shule ya msingi ya St. Peter
Clavers PrimarySchool. Alipokuwa na umri wa miaka 12 baba yake akawa anaishi jirani na
vijana waliokuwa na magitaa hapo ndipo akaanza kupata elimu yake ya muziki
iliyokuja kumfanya aje kujulikana Afrika ya Mashariki yote. Kabaka alijifunza
gitaa na miaka miwili tu baadae akiwa na umri wa miaka 14 alirekodi wimbo wake
wa kwanza ulioitwa Mie Kabaka Naimba.
Mwaka 1959 alianza kufanya kazi
Equator Sound Studio na muda si mrefu akawa mwanamuziki wa bendi ya studio iliyoitwa Equator Sound Boys ambayo
ilikuwa na mabingwa wengine kama Nashil Pichen, David Amunga, Charles Sonko,
Frida Sonko, na Fadhili William.
Sauti ya
Daudi Kabaka na gitaa lake vilisikika katika nyimbo maarufu kama Malaika na Taxi Driver za Fadhili William, Pole
Musa akiwa na Peter Tsosi na Nashil Pichen, na alikuwemo pia katika wimbo
maarufu wa Lunch Time wa marehemu
Gabriel Omolo.
Daudi Kabaka
alitunga nyimbo nyingi sana za twist kiasi cha kupewa sifa ningine ya kuitwa Mfalme wa
Twist. Siku moja aliwahi kusema wimbo wa
Mmarekani Chubby Checker Let's Twist Again, ndio uliomfanya aanze
kutunga nyimbo kwa mtindo huo. Kati ya
nyimbo zake za twist zilizokuwa maarufu sana ni Bushbaby Twist ambapo aliimba akisema hata wanyama wa mwituni
wanapenda kucheza twist, pia alitunga African
Twist, Bachelor Boy Twist, Taita
Twist na nyinginezo nyingi. Twist ulikuwa ndio mtindo wa vijana katika
miaka ya sitini na ulionekana ni mtindo wa uchezaji wa kihuni ambao
ulisababisha vijana wengi kupata adhabu kwa kukutwa wanacheza twist.Hakika
Kabaka alikuwa na nyimbonyingine nyingi ambazo hazikuwa twisti na kati ya hizo
nyimbo,kama Ambulance Mlangoni, Sisi
wanaume, Msichana wa sura nzuri zilikuwa zikiongea mambo ambayo yalikuwa si
rahisi kuongea hadharani na hivyo kumpa jina la Mtoboa Siri
Wimbo wa
Kabaka ulioitwa Harambe Harambe
ulikuwa maarufu sana Kenya kwani ulikuwa kama wimbo wa vijana wakisifia Taifa
lao na kwa miaka mingi ulipigwa kila siku katika redio ya Taifa hilo na
kujulikana na kila mtu. Mwaka 1967 kundi
la Uingereza la The Tremeloes lilichukua kipande cha kibwagizo cha wimbo Helule Helule wa Daudi Kabaka, na
kuurekodi, wimbo huo ukapata umaarufu na kufikia namba 14 katika Top Ten za
Uingereza, miaka mingi baadae Kabaka alisema hakupata hata senti kutokana na
mirabaha ya mauzo ya wimbo huo, japo alipewa fedha za awali kwa ajili ya
kutumia tu wimbo huo.
Mwaka 1972
Kabaka na wenzie wakaiacha Equator Sound na kuanzisha kampuni yao ya muziki
walioiita African Eagles Recording, Ltd, wakaunda bendi ya studio waliyoiita African
Eagles Lumpopo ambayo pamoja na kutoa nyimbo kadhaa ilifanya ziara katika nchi
za Zambia, Malawi na Uganda. African Eagles Recording, Ltd hatimae ikafa na
Daudi aliamua kupumzika kidogo.
Kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi katika
muziki mwaka 1995, Chuo Kikuu cha
Kenyatta, kilimtunukia mkongwe huyu tuzo ya Kenyatta University's Distinguished Service
Award. Na kutokana na historia yake,
Kabaka alipata kazi ya kufundisha kama Creative Arts instructor katika chuo
hicho kwa miaka kadhaa iliyofuata. Kabaka alipata tena ari ya kufanya maonyesho
akawa anafanya maonyesho kadhaa na wakongwe wenzie akina Fadhili William, John
Nzenze katika onyesho waliloliita Oldies Nite. Kabaka pia akaanzisha kundi
lililokuwa na vijana wadogo aliloliita Wazalendo Eagles Band. Urithi wa Kabaka unaendelea hata hapa kwetu
Tanzania,bendi kadhaa bado zinapiga nyimbo za Daudi Kabaka jukwaani na watu bado
wanaendelea kufurahia tungo za mkongwe huyu.
Kwa
mwanamuziki mtunzi au anaetaka kujifunza kutunga moja ya shule nzuri ni
kusikiliza nyimbo za Kabaka kuanzia miaka ya 50 mpaka kifo chake. Alitoa
mafunzo, ushauri, alichekesha, alifundisha uzalendo, na nyimbo zake ziliweza kusikilizwa
na kuchezwa na watu wa rika zote bila kuwa na ukakasi.
Daudi Kabaka
alifariki tarehe 26 Novemba 2001 zikiwa zimebaki siku mbili aweze kutimiza umri
wa miaka 62. Akazikwa nyumbani kwake
Muhudu, Tiriki Magharibi ya Kenya tarehe 15 Disemba 2001. Inasemekana mzee
alifariki akiacha watoto 47.
No comments:
Post a Comment