Wednesday, August 24, 2022

NICHOLAUS KASANDA WA MIKALAY "DOCTOR NICO", ALIWAHI KUPEWA SIFA YA MUNGU WA GITAA

 

Dr Nico

Dr nico alikuwa mpiga gitaa la solo na mtunzi mzuri sana, alizaliwa tarehe 7 Julai 1939 katika eneo la Mikalay, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakati huo ikiitwa Belgian Congo. Alisoma na hatimae akafuzu kuwa mwalimu wa mambo ya ufundi. Aliacha kazi hiyo na kujiunga na muziki  na kutokea kuwa kati ya wapiga solo bora waliowahi kutokea katika nchi hiyo ya Kongo. Mwaka 1953 akiwa na umri wa miaka 14 tu akajiunga na kundi maarufu la African Jazz chini ya mkongwe Joseph Kabasele. Toka akiwa mdogo ubora wake katika kupiga gitaa ulionekana, wapenzi awali wakampa jina la Nico Mobali au Mwanaume Nico, baadae ndipo akapewa jina la Dr Nico linaloendelea kudumu mpaka leo kwenye vichwa vya watu walioupenda muziki wake.  Mwaka 1960 wakati Kongo imo katika harakati za mwisho za kupata uhuru, bendi ya African Jazz ilitoa kibao kilichoitwa Independence Cha Cha, Dr Nico akiwa anapiga gitaa la solo wakati kaka yake Dechaud akiwa kwenye gitaa la rithimu, kibao hicho murua kilikuja kuwa kama ndio wimbo wa Taifa wa Uhuru wa kongo. Wakati Dr Nico anajiunga na African Jazz mwaka 1953 walikuweko wanamuziki wengine waliokuja kutoa mchango mkubwa katika kutambulika kwa muziki wa Kongo. Walikuwemo akina Isaac Musekiwa, huyu alikuwa na asili moja na King Michael Enoch.  Musekiwa alisema alitoka Southern Rhodesia, nchi inayojulikana sasa kama Zimbabwe na Michael Enoch alisema alitoka Northern Rhodesia inayojulikana sasa kama Zambia. Walikuwepo pia akina Roger Izedi, Balonji Tino Baroza, Charles Mwamba Dechaud kaka yake na Dr Nico,Tabu Ley, Joseph Mulamba Mujos, majina yaliyokuja kutawala muziki wa Kongo katika miaka ya sitini na sabini. Wanamuziki wengi wa miaka hiyo hapa Tanzania walijiita majina haya, Mujos, Baroza na kadhalika. Mwaka 1963, kundi kubwa la wanamuziki wa African Jazz wakajitenga kutoka kwa Joseph Kabasele na kuanzisha kundi lao la African Fiesta Orchestra. Dr Nico akiwa kwenye solo na Tabu Ley akiongoza kwenye uimbaji, moto mkali uliwashwa Africa nzima. Muziki wa kipindi hicho mpaka leo bado unapendwa, nyimbo kama Bougie ya Motema, Salam Aleikum, Biatondi na kadhalika bado zinakonga nyoyo za watu hadi leo, Afrika nzima. Mwaka 1965 Novemba 16  kukatokea mpasuko mkubwa, African Fiesta ikameguka na kukatokea makundi mawili, African Fiesta Sukisa chini ya Dr Nico na African Fiesta National chini ya Tabu Ley. Dr nico akabaki na kaka yake Charles Mwamba "Dechaud", Pierre Bazeta, AndrĂ© Lumingu "Zoro", Victor Kasanda "Vixon", Joseph Mingiedi "Jeff", Pedro "Cailloux. Josky Kiambukuta, na  Lucie .

Mwaka 1966 kundi hili lilifanya ziara Tanzania, na kupiga muziki Dar es Salaam katika ukumbi wa Arnatogro na pia kulifanyika onyesho Morogoro. Kundi hili lilipoenda Morogoro lilifanya uhuni  na kukatisha dansi mapema baada ya wanamuziki kupata wasichana wapenzi. Mkuu wa mkoa wakati huo aliingilia kati na kuwalazimisha waendelee kupiga muziki mpaka saa tisa ya usiku au la angewaweka ndani. Wakalazimika kuendelea na dansi, baada ya dansi wakasindikizwa na polisi mpaka Chalinze, RPC wakati huo alikuwa marehemu mwanasheria maarufu Mzee Al Maamry.

African Fiesta Sukisa pia ililirekodi nyimbo kadhaa katika studio za RTD, ukiwemo wimbo wa TANU Yajenga Nchi na wimbo uliokuwa ukiongelea kumbukumbu ya Lumumba Homage ya Lumumba. Mwanzoni mwa miaka ya 70 kundi la African Fiesta Sukisa lilikuwa kati ya makundi pendwa ya muziki wa Kongo.

Pamoja na kuanzisha staili mpya ya kupiga gitaa la second solo lililokuwa likipigwa na kaka yake Nico, pia bendi hii inasifika kwa kuanzisha mtindo wa Mutwashi, mtindo uliotokana na ngoma ya kabila la Wakasai ambalo ndilo kabila lake Dr Nico.

 

 Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 80 nguvu ya kundi hili ilianza kufifia na hasa baada ya afya ya Dr Nico nayo kuanza kuyumba. Agosti 1985 hali ya Dr Nico ilikuwa mbaya sana kiasi cha Rais Mobutu kutoa amri ya mwanamuziki huyo kusafirishwa kwenda kutibiwa Ubelgiji. Muda mfupi baada ya kupokelewa hospitali ya  St Luc ya Brussels. Nicholaus Kasanda wa Mikalay akakata roho, tarehe 22 septemba mwaka 1985. Hakika mpaka leo upigaji gitaa la solo wa Dr Nico haujapata mpinzani, kuna wakati Wakongo walifikia mpaka kumuita Mungu wa gitaa. Siku moja wakati kundi hili likipiga muziki jijini Paris, mwanamuziki mpiga gitaa maarufu duniani Jimi Hendrix aliwahi kumfuata Dr Nico  nyuma ya jukwaa kumsalimia kwa kuheshimu ujuzi wake. Na Hendrix alikuwa ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika duniani kote kwa umahiri.

 

 

 

No comments:

Post a Comment