Wednesday, September 14, 2022

JOHN ONDOLO CHACHA - MIAKA 14 BAADA YA KIFO CHAKE ALBUM YAKE YATOLEWA UPYA MAREKANI

 

John Ondolo katika sehemu ya chuo chake Shekilango

Wiki hii kampuni ya Mississippi Records imezindua mauzo ya santuri ya marehemu John Ondolo yenye nyimbo 12. Santuri yenye nyimbo nyingi hivyo huitwa album.
Album hiyo imekuwa gumzo kwenye mitandao ya wapenzi wa muziki wa gitaa kavu ‘Acoustic guitar’, kutokana staili ya upigaji gitaa wa nguli huyu.
Nilikutana na Mzee John Ondolo Chacha kwa mara ya kwanza mwezi  Aprili mwaka 1993, mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Kwa kuwa tulianza kazi bila ofisi,  Mzee Ondolo akatukaribisha kwenye eneo lake Sinza Shekilango, ili tuweke masikani yetu pale. Wakati huo Mzee Ondolo alikuwa ameanzisha kituo cha kufundisha sanaa ambacho alikiita Kituo Cha Sanaa Kuu. Kamati husika ya  CHAMUDATA ilimshukuru lakini sikumbuki sababu, iliamua kutokuweka ofisi zake mahala pale. Hilo halikumzuia Mzee Ondolo kuendelea kutoa mawazo mbalimbali kuhusu uendelezaji wa muziki wa dansi, alikuwa mhudhuriaji mzuri wa mikutano yote ya CHAMUDATA. Kati ya mawazo aliyowahi kutoa ni kuishauri CHAMUDATA  kuanzisha mafunzo kuhusu mambo mbalimbali katika tasnia ya muziki, ikiwemo masomo ya nadharia ya muziki, elimu ya Hakimiliki, ikumbukwe kuwa wakati ule kulikuwa hakuna hata sheria ya Hakimiliki iliyopo.
John Ondolo Chacha
alizaliwa mwezi  Machi mwaka 1917  katika kijiji cha  Kirumi wilaya ya Musoma. Kwa kabila alikuwa Mkurya. Kutokana na jina lake la Chacha, ni wazi alikuwa mtoto wa kwanza kuzaliwa. Baba yake aliitwa Joas Aliongo Mwaka na mama yake aliitwa Norah Alionga Muroka. Miaka michache baada ya wazazi wake kuoana wakaamua kuhamia Kenya kutafuta maisha, wakati huo Afrika ya Mashariki ilikuwa kama nchi moja kwa vile eneo lote lilikuwa chini ya utawala wa Uingereza, hivyo kulikuwa hakuna haja ya passport wala vibali vyovyote kuhama toka sehemu moja kwenda nyingine.
Baada ya familia kuhamia Kenya, Mzee Joas akapata kazi katika shamba la chai lililoitwa Majani Mingi, John Ondolo akaanza masomo katika shule ya msingi ya kimisionari ya Mukumu
iliyokuwepo Kakamega.  
Mwaka 1928 familia hiyo ikahamia Nairobi  na John Ondolo akajiunga na shule ya St Peter Claver. Hii ilikuwa shule ya wamisionari Wakatoliki. St Peter Claver ilifunguliwa mwaka 1923 na inasemekana ndio ilikuwa shule ya kwanza Kenya iliyokuwa na wanafunzi wa makabila mchanganyiko.
John Ondolo alipokuwa shule hii ndipo kipaji chake kilianza kugundulika, alijifunza kupiga gitaa, piano na vyombo vingine.   Bahati mbaya uwezo wa wazazi wake ukawa mdogo wakashindwa kuhimili ada ya shule hii hivyo akafukuzwa shule.

Mwaka 1942  John Ondolo alijiunga na jeshi la Waingereza, lililoitwa King’s African Rifles kwa kifupi KAR, watu wa kawaida waliwaita askari wa jeshi hilo askari Kea. Alipokuwa jeshini ndipo akagundulika kuwa pia anakipaji kikubwa cha kuchora, kipaji hiki kilifanya hata atambuliwe na malkia wa Uingereza kwa kazi hiyo. Mwaka 1947 aliacha jeshi na mwaka 1948 akaanza kufanya kazi kwa mtu mmoja muhimu sana katika historia ya muziki wa Afrika Mashariki, mtu huyo aliitwa Peter Colmore. Colmore akamuajiri Ondolo kuwa mtunza store ya vyombo vyake vya muziki.
Niongee kidogo kuhusu huyu
Peter Colmore. Colmore alizaliwa Uingereza mwaka 1919, mwaka 1938 akahamia Kenya ili afanye kazi kwenye kampuni ya ndege ya Wilson Airways, lakini ilipoanza tu vita ya pili ya dunia mwaka 1939, mali zote za Wilson Airways zikataifishwa na jeshi la Uingereza, Peter nae akalazimika kujiunga na KAR. Baada ya vita Peter akishirikiana na mtu mwingine mashuhuri katika historia ya muziki wa Afrika ya Mashariki, Ally Sykes, wakaanzisha  Colmore African Band. Huyu Mzee Sykes ni babu wa mwanamuziki Dully Sykes. Ni wakati huu huu ndipo John Ondolo Chacha akapata kazi ya kutunza stoo ya vyombo vya muziki vya Peter Colmore.

Baadae Peter Colmore  akaanza kazi ya ‘uproducer’ wa muziki na kuwa na lebo yake ambayo ilikuja kutoa santuri zaidi ya 250, lebo hiyo  iliitwa His Master’s Voice (HMV) Blue Label.
Colmore pia akanzisha kampuni ya promosheni ya bidhaa iliyoweza kuwagundua wanamuziki wengi akiwemo John Mwenda Bosco na Edward Masengo.

Pamoja na kuwa Ondolo alifanya kazi kwa Colmore, hakuna kumbukumbu kuwa aliwahi kutoa nyimbo zake katika lebo ya Colmore kwani kati ya nyimbo zake za kwanza ni Wazazi Musilie, iliyotoka mwaka 1959  chini ya lebo ya Galotone ya Afrika ya Kusini.

 Baada ya hapo John Ondolo  alitoa nyimbo kadhaa zikiwemo, Ukiwa Na Bwana We Bibi, Safari Ya Kilimanjaro  akiwa na the Jolly Trio Band, Olalekanga  akiwa na  Jolly Quartet Band nyimbo hizi zilitoka mwaka 1961. Mwaka 1962 alirekodi Yunie Mpenzi We akishirikiana na Jolly Quartet Band na wimbo Kenya Style  aliopiga peke yake.

Mwaka huohuo 1962 John Ondolo aliingia jiji la Dar es Salaam kwa mara ya kwanza. Akajiwekea makazi yake eneo la  Sombrelo, Ubungo. Sombrello ilikuwa ‘night club’ maarufu wakati huo na bendi nyingi zikipiga hapo, club hiyo ilikuwa pembeni tu mwa jengo la Ubungo Plaza, kwa sasa eneo hilo kumejengwa kanisa kubwa.  Ondolo aliweza kupata umaarufu mkubwa kiasi cha kuchaguliwa kuwa Katibu wa wa eneo lile katika muda mfupi sana.

Mwaka unaofuata alirudi tena Kenya ambako pamoja na kuoa mke wake wa kwanza alianza tena kutoa nyimbo. Mwaka 1963 alirekodi wimbo wa  Tucheze Selele, mwaka 1964 akatoa Tumshukuru Mungu  na  Kenya Twist, mwaka 1965  Siri ya  kijana, mwaka 1967,  Kwela Wangu  na mwaka 1968 akishirikiana na Ngambotano Boys Band akatoa wimbo wa Haukutoka Mbinguni.
Mwaka huo huo  1968, akarudi Tanzania akisindikizana na watoto wake watatu. Aliweza kupata kazi katika shamba la Mawingi huko Moshi ambako akafanya kazi mpaka mwaka 1970, ndipo  akapata mwaliko wa kurekodi nyimbo kwa ajili ya kuhamasisha utalii na akatoa nyimbo mbili, Kilimanjaro and Mbuga zetu . Nyimbo hizi alirekodi katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Baadae akaajiriwa hapohapo redio kama mtayarishaji wa vipindi vya biashara. Mwaka 1972 akaajiriwa na Umoja wa Vijana wa TANU  (TYL) kama Katibu Mwenezi. Na ilikuwa ni hapo kwa kutumia vyombo ambavyo viliachwa na bendi ya wanawake Women Jazz band, akashirikiana na Hamza Kalala kuanzisha Vijana Jazz Band.

KWA MAELEZO ZAIDI YA SANTURI HII INGIA HAPAAA

Tarehe 21 Machi 2008  ilikuwa ni Ijumaa Kuu,  John Ondolo alienda kanisani kusali, katikati ya misa alidondoka, akakimbizwa hospitali lakini alipofika hospitali John Ondolo Chacha alikuwa amekwishapoteza uhai.

 John Ondolo alizikwa Dar es Salaam, akiwa ameacha watoto kumi na moja.

 

No comments:

Post a Comment