Ahmad Kipande |
Ahmad Kipande
alizaliwa Kilwa na alipokuwa kijana akaamua kutafuta maisha nje ya Kilwa. Mwaka 1953 aliamua kuingia jiji la Dar es Salaam.
Alipofika Dar es Salaam kati ya mambo aliyoyakuta ni teknolojia ya gramafoni,
chombo ambacho kiliweza kupiga santuri na muziki ukasikika. Miaka hiyo kulikuwa
na santuri nyingi za vikundi kutoka Cuba. Santuri hizi zilikuwa na majina ya
bendi na nyimbo ambazo ziliandikwa Kispanyiola, lakini pia zilikuwa na namba
zilizoanzia herufi GV, Kiingereza ziliitwa GV series. Ahamad alianza kuzisikiliza
nyimbo za wanamuziki hawa wa Cuba, pia akaanza kusikiliza santuri za wanamuziki
wa Afrika ya Mashariki kama akina Fundi Konde. Harry Makacha na Frank Humplink
na dada zake. Taratibu akaanza kuwa na hamu ya yeye pia kuwa mwnamuziki.
Kwa msisimko
alioupata Kipande akaanza kujifunza mwenyewe vyombo mbalimbali likiwemo gitaa,
ukulele, banjo na violin na hatimae saxaphone ambayo ndio ilikuja kumpa
umaarufu mkubwa. Ahmad alianza muziki
kwa kujiunga katika kundi la Tanganyika
Jazz Band. Tanganyika jazz lilikuwa kundi la mtu binafsi na wakati huo muziki
ulikuwa ukipigwa kama kitu cha kujiburudisha na kuendeleza fani kwa wanamuziki,
haikuwa ajira wala njia ya kupata fedha. Bendi hiyo ilikuwa na vidhaa
vifuatavyo magitaa, violin, ngoma, trumpet na saxophone.
Mwaka 1958
akamua nae kuunda bendi yake, na ndipo wazo
la Kilwa Jazz Band lilipozaliwa. Taratibu akaanza kununua vifaa vya kuunda
bendi, akanunua saxaphone , magitaa ambayo hayakuwa yakitumia umeme, na kisha
kutengeneza ngoma , wakati huo ngoma zilikuwa zikitengezwa kwa kutumia mapipa
na ngozi ya ng’ombe au mbuzi.
Kati ya wanamuziki wa kwanza wa bendi hii alikuweko Mzee Zuberi Makata ambaye
alifundishawa kupiga sax na Mzee Kipande mwenye. Mzee Makata alikuja kufariki
kwa ajali ya ajali ya gari uzeeni. Baadae
wakaingia akina Duncan Njilima na Omari Omari. Wakati huo bendi ambazo
tayari zilikuwepo katika jiji la Dar es Salaam na zilikuwa zikivuma zilikuwa
Homeboys Jazz band, Dar es Salaam Jazz band, na Cuban Marimba Branch, hili
lilikuwa tawi la Cuban Marimba ya Morogoro. Bendi hii ya Cuban Marimba ya
marehemu Salum Abdallah ilikuwa na matawi mengi kwa mfano kulikuweko pia Cuban
Marimba Branch ya Kilosa.
Kilwa Jazz ilianza muziki ikawa inapiga nyimbo zake kwa mitindo mbalimbali
ikiwemo rumba, samba, bolelo na chacha.
Bahati mbaya katika zama hizi mitindo hiii yote imebebeshwa jina moja tu la
rumba.
Kilwa ikaja
kuwa moja ya bendi tishio jijini Dar es Salaam,
wimbo wenye maneno haya;
Napenda nipate lau nafasii,
Nipate kusema nawe kidogo aah mamaa aah
Rohoni
inaumiaa,
Hakika lakufanya bado sijaliona,
Nimeona leo bora nikuimbee,
Huenda punde roho yako ikadundaa
Ikaja siku ukaja nipoza moyo ooh mama
rohoni naumia…
Huo ni wimbo
wa Kilwa Jazz Band, japo muziki waliuchukua kutoka wimbo wa Mokolo nakokufa wa
bendi ya African Fiesta ya Kongo. Ahmad Kipande na bendi yake ya Kilwa Jazz
ilishiriki katika mambo mengi makubwa ya
Kitaifa. Kilwa Jazz Band ilikuwa moja ya vikundi vilivyotumbuiza siku
Tanganyika inapata Uhuru Decemba 09, 1961, na iliporomosha wimbo maalumu wa
kusifia Tanganyika kupata Uhuru. Wimbo huo ulikuwa na maneno haya;
“Ewe mola tunakuomba,
Uibariki Tanganyika,
Uhuru tumeshaupata
Llakini nyoyo zinasikitika,
Wenzetu wanateseka,
Wakoloni wamewashika…”
Kilwa Jazz Band iliheshimika sana, ndiyo iliyoteuliwa na serikali kushiriki
sherehe za Uhuru wa Malawi na Uganda.
Wimbo wake
mmoja ulitokana na meno aliyoyatamka Mwalimu Nyerere ulipata kupendwa sana
wimbo huo ulikuwa una maneno ya Kiingereza, ‘It can be done , play your part’
Kilwa Jazz
band ilikuwa na nyimbo nyingi sana ziolizopendwa na zinazoendelea
kupendwa, kati ya hizo ulikuweko wimbo
ulioitwa Kifo cha penzi. Kifupi mtunzi anasema kifo cha penzi ni kitu kibaya
usijiombee kifo cha penzi, na katika wimbo huo tunakumbushwa mambo mawili ya
kihistoria, mstari mmoja unasema, ‘Heri ufe kwa kugongwa na basi la ghorofa
liendalo Ilala’, miaka hiyo kulikuweko na usafiri wa mabasi ya ghorofa. Mstari
mwingine unasema ‘Heri ufe kwa kugongwa na gari la terela liendalo Zambia’.
Kabla ya kujengwa kwa bomba la TAZAMA Pipeline, na reli ya TARAZA, mizigo
na mafuta kuelekea Zambia yalikuwa
yakipelekwa na malori yenye materela.
Mapenzi
yananivunja Mgongo, Kifo cha Pesa, Dolly, Nacheka cheka Kilwa, Enyi vijana
tujenge nchi yetu, Rose wauwa ni baadhi ya nyimbo za bendi hii iliyokuwa ni
ndoto ya Ahmed Kipande.
Mwaka 1973
Kilwa Jazz Band ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa
dansi, Franco na bendi yake ya T.P.OK. Jazz lililofanyika Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Ahmed Kipande
alifariki dunia Aprili 27, 1987 baada ya
kusumbuliwa na ugonjwa wa kuharusi kwa kipindi kirefu, lakini ataendelea kukumbukwa
kwa mazuri aliyoyaacha katika Taifa hili Mungu Amlaze Pema Ahmad Kipande.
AHMAD KIPANDE, was born in Kilwa, in 1953 he moved to Dar es Salaam where he first heard different kinds of music from the gramophone. Spanish Vinyl records of the GV series, and East African musicians like Fundi Konde, Harry Makacha and Frank Humplick really caught his interest, and he also decided to be a musician. And that's how the great Kilwa Jazz band was born.
No comments:
Post a Comment