Mzee Mapili akiburudisha katika jukwaa la Maquis Du Zaire kwenye sherehe za mwanamizchezo bora 1986 |
Wakati wa uhai wake Mzee Kassim Mapili alikuwa akitania na kusema kuwa siku akifariki, maiti yake iagwe katika uwanja wa Mnazi Mmoja, na kisha jeneza lake libebwe na wapenzi wake bila kutumia gari hadi Kisutu ambapo ndipo azikwe. Alipofariki ni sehemu tu ya maneno ya Mzee huyu yaliyoweza kutimia. Shughuli ya kuagwa Mnazi Mmoja haikuwezekana, lakini Mzee Mapili alizikwa makaburi ya Kisutu kama alivyowahi kutabiri.
Jambo lililofanya Mzee Mapili asipate heshima ya kuagwa Mnazi Mmoja ni kutokana na mazingira ya kifo chake. Siku ya tarehe 23 Februari 2016 ilikuwa Jumanne, na siku hiyo kulikuwa na mechi kati ya Arsenal na Barcelona, Mzee Mapili alikwenda kuangalia mechi hiyo jirani na nyumbani kwake, aliporudi aliingia nyumbani kwake, na ilionekana kuwa alipatwa na tatizo la moyo ambao ulikuwa ukimsumbua muda mrefu na akafariki. Bahati mbaya baada ya kufikwa na mauti, mwili wake uligunduliwa Alhamisi jioni, tayari mwili ulishanza kuharibika hivyo haikuwezekana kutimiza nia ya marehemu ya kuagwa Mnazi Mmoja.
Mzee Mapili alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu, Tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937. Hivyo umauti ulimkuta Mzee Mapili akiwa na umri wa miaka 79. Alipata elimu ya msingi huko kwao Lipuyu, sambamba na kupata elimu ya dini na mwenyewe aliwahi kusema alianza kupata mapenzi ya kuimba wakati alipokuwa Madrasa akighani Kaswida. Mwaka 1958 alijiunga na White Jazz Band iliyokuwa na masikani Lindi. Mwaka mmoja baadae akahamia Mtwara na kujiunga na Mtwara Jazz Band, lakini mwaka 1962 akajiunga na Honolulu Jazz Band ambayo nayo ilikuwa hapo hapo Mtwara. Mwaka 1963, Mzee Mapili akachukuliwa na TANU Youth League ya mjini Lindi, na kujiunga na bendi ya Jamhuri Jazz Band ya hapo Lindi. Mwaka 1964 Mzee Mapili akachaguliwa kuanzisha bendi ya TANU Youth League ya Tunduru. Mwaka mmoja baadae alihamia Kilwa Masoko na kujiunga na Lucky Star Jazz Band ya mji huo. Baada ya hapo ndipo Kassim Mapili akatua katika jiji la Dar es Salaam na kujiunga na Kilwa Jazz Band iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande. Kama ilivyokuwa sera ya wakati ule ya kuanzisha vikundi vya sanaa katika sehemu za kazi, majeshi yetu pia yalianzisha bendi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nalo likaanzisha bendi na Mzee Mapili alikuwa mmoja ya waanzilishi wa bendi ya JKT Kimbunga Stereo mwaka 1965. Polisi nao kama majeshi mengine nayo pia ikaanzisha bendi na Mzee Mapili akajiunga na Police Jazz Band, 15 Desemba 1965. Mzee Mapili ndie aliyekuwa mwalimu wa bendi ya kwanza ya wanawake nchini Women Jazz Band iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka 1965.

Ni katika bendi ya Polisi katika mtindo wao wa Vangavanga ndipo jina la Mzee Mapili lilikuja julikana na sana, na hasa kutokana na tungo zake kama Dunia ulioimbwa na Moshi William, na Hayati Mzee Diwani. Baada ya miaka 16 katika bendi ya Polisi, tarehe 5 Mei 1981, Mzee Kassim Mapili alistaafu jeshi la Polisi.
Baada ya kustaafu Mzee Mapili alijiunga na bendi ya Tanzania Stars iliyokuwa na makao yake katika hoteli ya Margot. Hoteli na bendi zilikuwa zikimilikiwa na Jumuiya ya Ushirika iliyojulikana kama Washirika na hatimae bendi hiyo ilikuja julikana kama Washirika Tanzania Stars.
Mwaka 1982 baada ya semina ya wanamuziki iliyofanyika Bagamoyo Mzee Mapili alikuwa mmoja wapo wa wanamuziki walioanzisha Chama Cha Muziki wa dansi Tanzania, na akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho. Akiwa Mwenyekiti wa chama hicho mwaka 1986, aliweza kukusanya kundi la wanamuziki 57 ambao walitengeneza kund lililoitwa Tanzania All Stars. Kundi hili lilirekodi muziki ambao mpaka leo umekuwa katika kipimo cha juu ambacho hakijafikiwa na wanamuziki wa sasa. Wakati wa uongozi wa Mzee mapili kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM, Radio Tanzania, BASATA na CHAMUDATA waliweza kufanya shindano la bendi ambalo aina yake haijawahi kurudiwa tena, shindano hili lililoitwa Top Ten Show lilishirikisha bendi kutoka karibu kila wilaya hapa nchini. Uongozi huu aliendelea mpaka mwaka 1990. Mwaka 1993 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz Band na katika bendi hii alitunga wimbo wa Eva uliokuwemo katika album ya kwanza ya bendi hii. Alipoacha bendi hii Mzee mapili alipitia Super Matimila, Gold All Stars, na hata kujiunga na binti wa Mbaraka Mwinshehe katika bendi yake ya Volcano Stars, na kipindi cha karibuni alikuwa akishirikiana na Mrisho Mpoto na wasanii mbalimbali katika muziki. Mzee Mapili ameacha watoto watatu. Hakika Mzee Mapili alikuwa mtu wa watu.

Apumzike Kwa Amani Mzee Mapili.Hakika kusini mwa Tanzania pametokea wanamuziki wengi wazuri.
ReplyDelete