Mpiga saksafon maarufu Afrika,
Verckys amefariki dunia jana Alhamis tarehe 13 Oktoba 2022, baada ya afya yake
kuwa tete kutokana na kupata stroke ndogo miezi michache iliyopita. Verckys
ameacha watoto 32.
Georges Kiamuangana Mateta
maarufu kwa jina la Verckys alizaliwa Kisantu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo terehe 19 Mei,1944.
Alijipa jina la Verckys kimakosa kwani alitaka kujiita jina la mpiga saksafon
maarufu wa Kimarekani wakati ule aliyeitwa King Curtis. Kwa bahati mbaya alisikia
jina "Curtis" kama "Verckys." Na wote mpaka leo tunamfahamu kama Verckys.
Baba yake Verckys alikuwa mfanya biashara tajiri, hivyo Verckys aliweza kupata
elimu nzuri kabisa. Mapema kabisa alionyesha umahiri kipaji chake cha muziki
kwani alikuwa akifahamu kupiga vyombo kadhaa vya kupuliza kama vile filimbi na clarinet,
hatimae alianza kujifunza saksafon alipokuwa kwenye kikundi cha madhehebu
yaliyokuwa chini ya mchungaji maarufu wa Kikongo aliyeitwa Nabii Simon Kimbangu.
Mwaka 1962 alijiunga na bendi
iliyoitwa Los Cantina, baadae akahamia Jamel Jazz na mwaka huohuo safari yake
ikamfikisha kwenye kundi la Conga Jazz lililokuwa chini ya mkongwe mwingine
maarufu katika muziki wa Kongo aliyeitwa Paul Ebengo, maarufu zaidi kwa jina la
Dewayon. Mwaka 1963 akahamia O.K. Jazz in 1963, kundi lililokuja kumtambulisha
rasmi katika ulimwengu wa muziki. Alikuwa mpuliza saksafon mzuri sana kiasi
cha kupewa sifa ya kuwa ‘Mtu mwenye
mapafu ya chuma’, akawa mtu wa karibu sana na Luambo Luanzo Franco Kiongozi wa
OK Jazz.
Mwaka 1968, Franco akapata ziara ya kwenda Ulaya,
akachukua baadhi ya wanamuziki na kwenda nao, huku nyuma Verckys na muimbaji Youlou Mabiala wakakusanya wenzao na kufanya
mazoezi ya haraka na kuingia studio na kurekodi nyimbo nne. Kasheshe kubwa
lilizuka baada ya Franco kurudi kutoka ziara yake na hatimae tarehe 5 April
1969, Verckys alilazimika kuacha OK Jazz
na kuanzisha kundi lake mwenyewe aliloliita
Orchestre Veve.
Kundi hili likuwa na waimbaji vijana machachari sana, kati yao walikuweko Matadidi Mabele maarufu kwa jina la Mario, Marcel Loko maarufu kwa jina la Djeskain, and
Bonghat "Sinatra" Tshekabu aliyekuwa maarufu kwa jina la Saak Saakul.
Vijana hawa baadae walikuja kumkimbia Verckys na kuanzisha kundi lao lililokuja
kutikisa mpaka bendi kongwe za wakati huo, kundi hili liliitwa Orchestra
Sosoliso na umoja wao walijipa jina la Trio Madjesi .
Turudi kwa Verckys, yeye na kundi lake la
Orchestre Veve lilikuja kurekodi nyimbo nyingi sana maarufu, nyimbo zake pendwa
za kwanza zilikuwa Mfumbwa, Bankonko Baboyi na wimbo ambao ulikuwa utunzi wa
Saak Saakul ulioitwa Fifi Solange. Mafanikio makubwa aliyokuja kuyapata Verckys
yalimuwezesha kuingia rasmi katika
biashara ya muziki kwa kuanzisha label yake na kuingia mikataba na bendi
mbalimbali maarufu wakati ule. Baadhi ya bendi zilizotoa nyimbo ambazo kwa lebo
hiyo ambazo zilikuja kutikisa Afrika
nzima zilikuwa, Les Grand maquisards, Orchestra Kiam ambayo jina lake Kiam
lilikuwa ni ufupisho wa jina Verckys la Kiamuangana, Orchestra Bella Bella ya
wale ndugu wawili waimbaji, Soki Vangu na Soki Dianzenza, Orchestra Lipua
lipua, Les Kamale, na Empire Bakuba ya Pepe Kalle.
Mwaka 1972 Verckys alifungua studio yake
katika kituo alichokiita Veve Center. Alianza kufanya mambo mengi
makubwa katika muziki, hili liliwezesha mwaka 1978 apate kuchaguliwa kuwa rais
wa wanamuziki wa Zaire, baada ya Franco
Makiadi kumaliza muda wake.
Historia ya Verckys kwa kifupi imejaa mafanikio makubwa kimuziki. Akiwa na miaka 18 alijiunga na
kundi konwe la OK Jazz, alipofikia umri wa miaka 25 alifungua studio yake ya
kurekodi muziki. Mwaka 1972 alimshirikisha
Pepe Kalle kuimba kwenye
nyimbo Sola, Mbuta wakishirikiana na
Bella Bella, na kumshirikisha na Nyboma
Mwandido kwenye wimbo Kamale uliopigwa na Orchestra Lipua Lipua .Verckys ndiye
chanzo cha Orchestres Baya Baya, Lipua Lipua na
Kiam, matokeo yake ni nyimbo tamu maarufu kama Amba, Mombasa, Niki bue,
Mbale, Kamiki, Bomoto na nyingine nyingi sana. Huwezi kumuweka pembeni Verckys
utakapotaja mafanikio ya mtindo wa Cavasha, mtindo ulioishika Afrika nzima
miaka ya sabini.
Mwaka 1976 Verckys alibadili jina la label yake kutoka Editions Veve kuwa ZADIS, ambayo
ilikuwa kifupi cha Zaire disc. Kwa lebo
hii mpya Orchestra Veve ikatoa nyimbo mbili ambazo zingali zinagusa nyoyo za
wapenzi wa muziki wake mpaka leo, nyimbo
hizo ni Papy Baluti na Muana Mburu. Wakati huo Orchestra Veve ilikuwa na
wanamuziki wafuatao Tino Muinkwa, Djo Roy, Nejos Tusevo, Pepitho Fukiau kwenye
uimbaji, Lambion akiwa anapiga gitaa la solo, Aladji Baba kwenye gitaa la rhythm, Ndolo na Celi Bitsou wakiwa wapiga bezi. Kwenye drums
alikuweko Bayard, Ponta Vickys kwenye congas, yeye mwenyewe Verckys, Dibuidi na
Sax Matalanza wakipuliza Saksafon,
Makamba akiwa anapuliza trombone. Ni kiasi cha kusikiliza nyimbo hizo mbili ili
uweze kujua umahiri wa wanamuziki
waliotajwa.
Mwaka1978 alimrekodi kijana mdogo aliyeitwa Koffi
Olomide, hadithi ya Koffi kwa sasa kila mtu anaijua.
MUNGU AMLAZE PEMA NGULI HUYU
ALIYELETA FURAHA KWA MAMILIONI YA WATU KATIKA UHAI WAKE
Ni Majonzi Makubwa
ReplyDelete