>
Josephine James akitumia brush kwenye drums, na Lea Samwel kwenye Bongos |
Historia ya bendi ya wanawake inaanzia pale Rais wa Guinea ya Conakry, marehemu Sekou
Toure alipotembelea Tanzania mwaka 1965. Rais huyu alipenda sana utamaduni wa nchi
yake na kama ilivyokuwa kwa Mobutu alisisitiza kurudia uasili katika shughuli
za utamaduni na akaufadhili kwa hali na mali, hata kuanzisha label ya muziki ya
serikali. Na ilikuwa wakati wa Rais huyu mpenda sanaa vilipoanzishwa vikundi vya sanaa vya mikoa nchini mwake na kutokana na vikundi hivyo alitengeneza vikundi
vya Taifa vya sanaa mbalimbali.
Mfano mzuri sana ambao wapenzi wa muziki wa dansi wa zamani
watakumbuka ni Bembeya Jazz, bendi iliyopiga wimbo maarufu wa Whisky Soda, hii
ilikuwa ni bendi ya mkoani lakini ikashinda mashindano na kuhamishiwa mkao
makuu ya nchi na kufanywa bendi ya Taifa. Bendi hii iliyoanzishwa mwaka 1959 bado iko hai mpaka leo na inafanya maonyesho Guinea na nje ya nchi hiyo, inawezekana ndio
bendi kongwe Afrika ambayo iko hai. Mwaka 1961 ilianzishwa bendi ya muziki
ya polisi wanawake hukohuko Guinea, bendi hiyo ikaitwa L’Orchestre Feminin De La
Gendarmerie De Guinee, wakati wa Sekou
Toure ikabadilishwa jina na kuitwa Les Amazones De Guinee na kuwa na wadhifa wa bendi ya Taifa. Wakati wa misafara yake Rais Sekou Toure alisindikizana na vikundi vya sanaa,
na alipokuja Tanzania ndege yake ilikuwa na wasanii wengi kuliko wanasiasa,
katika msafara huo alikuja na bendi hiyo ya kina mama Les Amazones.
Les Amazones de Guinée wakiwa kazini
Hiyo bendi ilipotua nchini, baadhi ya mabinti
wa TANU Youth League, ndio wakapewa kazi ya kuwa wenyeji wa wanamuziki hawa wa
kike. Baada ya siku chache Rais Sekou Toure na wasanii wake wakaondoka lakini wakawa wamepanda wazo la
vikundi vya sanaa vya Taifa na pia wazo la bendi ya wanawake. Wale mabinti
waliokuwa wakizunguka na wanamuziki, wengi wao walikuwa ni wafanyakazi Government
Press wakaazimia nao kuanzisha bendi ya wanawake, japo walikuwa hawana ujuzi wa chombo chochote cha muziki,
lakini nia yao ilikuwa kuwa na bendi kama Les Amazones.
Chini ya ufadhili wa
TANU Youth League mabinti hawa wakaanza kuhudhuria mafunzo ya muziki, pale
Police Mgulani chini ya mwanamuziki mahiri wa Polisi Mzee Mayagilo, baadae
wakawekwa chini ya kitengo cha Polisi Jazz Band, ambako huko wakamkuta marehemu
Mzee Kassim Mapili ambae akawa ndiye mwalimu wao mkuu. Hayawi hayawi yakawa hatimae tarehe
31 Mei 1966, bendi ya kwanza ya wanawake Tanzania, ikaingia katika studio za
Redio Tanzania Dar es Salaam na kurekodi nyimbo, wakiwa wanapiga na kuimba
nyimbo walizotunga wao wenyewe. Nyimbo hizo zilikuwa; Tumsifu Mheshimiwa, Leo Tunafuraha,
Mwalimu Kasema, Women Jazz, Sifa nyingi tuwasifu viongozi na TANU yajenga nchi.
Kundi zima lililoingia studio lilikuwa na wanamuziki wafuatao kumi na tano:
1. Mary Kilima- Mwimbaji
2. Juanita Mwegoha-Mwimbaji
3. Siwema Salum- Mwimbaji
4. Rukia Hassan- Mwimbaji
5. Kijakazi Mbegu- Solo Guitar
6. Mwanjaa Ramadhan-Bass Guitar
7. Chano Mohammed-Rhythm Guitar
8. Tatu Ally-Alto Sax
9. Mina Tumaini-Tenor Sax
10. Anna Stewart-Alto Sax
11. Rukia Mbaraka-Tenor Sax
12. Lea Samweli-Bongos
13. Josephine James-Drums
14. Zainab Mbwana-Maracass
15. Tale Mgongo-Timing.
Baada ya hapo bendi ilianza kupata umaarufu mkubwa watu wakishangaa kuona
kundi la wanawake wakiporomosha dansi bila sura ya mwanaume, bendi ikaanza
kufanya maonyesho kwenye hafla mbalimbali za serikali na chama, na pia kuanza
kuzunguka mikoa mbalimbali wakifanya maonyesho yaliyokuwa yakijaza kumbi. Sifa
zikavuka mipaka na wakajikuta wakipiga na kujaza watu kwenye kumbi mbalimbali Nairobi na Mombasa. Kutokana na
urafiki uliokuwepo wakati huo kati ya Tanzania na China, ikafikia hatua ya bendi hii kuonekana ni muhimu kwenda
kufanya ziara China, lakini wakati wa matayarisho ya safari hiyo, bendi
ikasambaratika. Kilichofanya bendi isambaratike ilikuwa ni kudhurumiwa mapato.
Akina mama hawa walikuwa wakifanya maonyesho na yalikuwa yakiingiza fedha,
lakini walikuwa hawapati chochote kutokana na maonyesho yao zaidi ya umaarufu.
Ni bahati mbaya majina ya waliokuwa wakitumbua fedha za bendi hii bila
kuwagawiya wanamuziki hawa kipato chao halali, ni wanaume wenye majina maarufu
katika historia ya siasa za nchi yetu. Kufikia hatua hiyo wanamuziki hawa wakaona ni
heri kurudia kazi yao ya awali
Government Press kuliko umaarufu uliokosa fedha, jambo ambalo lilianza
kuwaletea matatizo katika familia zao bila kuwa na sababu za msingi bendi
ikasambaratika. TANU youth League ikachukua vyombo vyake na kuvihifadhi, hatimae
vyombo hivi vikawa ndivyo vyombo vilivyotumika kuanzisha Vijana Jazz band chini
ya Mzee John Ondolo miaka kadhaa baadae. Karibu akina mama wote wa bendi hii
kwa sasa ni marehemu Mungu awalaze pema, lakini hakika walio hai wanastahili
kupewa tuzo katika maazimisho ya siku za akina mama.
Sikiliza wimbo wao wa Tumsifu Mheshimiwa hapa
No comments:
Post a Comment