Monday, August 29, 2022

SHAKILA NA BABU NJENJE WALIZALIWA SIKU MOJA, MJI MMOJA NA WAKANYONYA ZIWA MOJA

 

Mabruk Khamis(Babu Njenje), Tatu Said (Shakila)

Tumetimiza miaka sita sasa toka alipotutoka Bi Tatu Saidi Msengi, maarufu kwa jina la Bi Shakila.Ilikuwa siku ya Ijumaa, tarehe 19 Agosti mwaka 2016, Bi Shakila, muimbaji maarufu wa Taarab, alianguka ghafla nyumbani kwake Mbagala Charambe, na alipokimbizwa hospitali moja jirani Bi Shakila alikata roho.Mwezi huu tunatimiza miaka sita toka kukatika kwa sauti ya muimbaji huyu mahiri.Bi Shakila alikuwa mzaliwa  peke yake kwa baba na mama yake, japokuwa alikuwa na kaka na dada zake kadhaa kutoka ndoa nyingine ya mama yake.  
Bi Shakila alipozaliwa kule Pangani tarehe 14 June 1947 alipewa jina la Tatu. lakini tarehe hiyohiyo katika mji huo huo wa Pangani pia alizaliwa mtoto mwingine aliyekuja kuwa muimbaji mashuhuri nae ni marehemu Mabruk Khamis wa Kilimanjaro Band, aliyejulikana sana kwa jina la Babu Njenje. Mama yake Mabruk alipata tatizo la kutoa maziwa hivyo mama yake Tatu akaanza kumnyonyesha pia mtoto huyo wa jirani. Mabruk Khamis alianza maisha  kwa kunyonyeshwa titi moja na  Tatu Said.

Tatu alikuja kupewa jina la kubandika la Shakila kutoka na muigizaji mmoja wa sinema za Kihindi katikati ya miaka ya 50, hivyo jina hilo la kubandikwa likaja kuwa maarufu kuliko jina lake halisi la Tatu, kama ilivyokuwa kwa mwenzie aliyepachikwa jina la Babu NJenje na likawa maarufu kuliko jina lake halisi.
Baba yake Tatu,  Mzee Said Khamis, alikuwa mtu wa kutoka Singida ambaye alikwenda Pangani kumtafuta mjomba wake aliyepotelea Pangani miaka mingi kabla na huko akakutana na mama yake Shakila, Bi Khadija Mohamed Chagutwi. Mzee Said alikuwa dobi na Bi Khadija alikuwa msusi maarufu.

Kwa kadri ya maelezo yake mwenyewe Bi Shakila alianza muziki akiwa na miaka 6, alipokuwa na umri wa miaka 12, aliteuliwa kumuimbia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipotembelea Pangani, wakati wa kutafuta Uhuru. Na ni baada ya hapa ambapo aliweza kusikika na Bwana Khatibu, ambaye pia alikuwa dereva wa basi la Nashuu lililokuwa likisafiri kati ya Pangani naTanga mjini. Bwana Khatibu ndie pia aliweza badae kumshawishi Shakila kujiunga na kundi la Taarab lililokuwa pale Pangani lililoitwa Taarab Kijamvi, hakukaa sana katika kundi hilo akalazimika kuhamia Tanga kumfuata Bwana Khatib ambaye sasa walikuwa wameoana. Katika ndoa yao walikuja kubahatika kupata watoto watano.
Huko Tanga yeye na mumewe walijiunga na kundi la Shaabab Al Watan, katika kikundi hiki aliwakuta wakongwe wakina Asmahani, Bi Kirua, Binti Sefu, tatizo katika kundi hili ni kuwa Shakila alijikuta akiimba mazoezini tu, hakupata nafasi ya kuimba katika kadamnasi, hivyo baada ya muda si mrefu Bi Shakila akiambatana na mumewe walihamia kundi jingine lililokuwa likimilikiwa na fundi baiskeli maarufu Mzee Kiroboto, kundi hilo  liliitwa Young Noverty.
Bi Shakila aliweza kupata uzoefu mkubwa wa kuimba mbele za watu, lakini kundi hili lilikuwa ni la kutumbuiza bure katika vikao vya kahawa tu. Hatimae kundi hili lilikufa na zaidi ya nusu ya wasanii kujiunga na kundi la Black Star. Black Star Musical Club ilikuwa  ikimilikiwa  na Mwarabu mmoja aliyekuwa anafanya kazi bandarini aliyeitwa Hassan Awadh. Ni katika kundi hili ndipo Bi Shakila alipoanza kufahamika na  kuaminika kwa kupewa nyimbo za kuimba kama Jongoo Acha Makuu, Mpenzi Amini, Majuto Yamenipata. Shakila akanza kufahamika sana kundi likawa linaalikwa kwenye hafla za kisiasa, sherehe za harusi, akawa kati ya waimbaji mashuhuri katika jiji la Tanga.
Mwaka 1972 tajiri mwingine Mwarabu aliyeitwa Sudi Said akanunua vyombo vipya vizuri na kuanzisha kundi lililoitwa Lucky Star Musical Club.  Bi Shakila na wenzie tisa walihama Black Star na kuhamia Lucky Star. Kwa kuwa kundi lilianzishwa wakati Bi Shakila alikuwa mja mzito, mtoto aliyezaliwa alimuita Lucky.

 Nyimbo nyingi zinazofahamika hadi leo za Bi Shakila zilirekodiwa wakati yuko kundi hili. Mapenzi Yamepungua, Kifo cha Mahaba. Macho Yanacheka na kadhalika. Bi Shakila aliendelea na kundi hili hadi mwaka 1984.
Shakila alikuja kuhamia Dar es Salaam baada ya wito wa kikazi kuja kujiunga na kundi la JKT Taarab. Shakila alianza kazi katika mtindo wa kujitolea na hatimae akaajiriwa kama zilivyo taratibu za JKT. Kazi ya Shakila ilikuwa kuwajenga wasanii wa kundi la Taarab katika maadili ya waimbaji bora  wa taarabu. Kati ya waimbaji waliopitia mikono ya mama huyu ni , Elizabeth Sijila ambaye nae ni marehemu, Mwajabu Kitale, Anna Mussa, Asha Dagula na wengineo.
Katika muda wake JKT Taarab, Shakila aliweza kutunga nyimbo nyingi zikiwemo Kiyangayanga, Gari, Siwezi Tabu, na nyingine nyingi. Hakika Shakila ametuachia hazina kubwa ya nyimbo zake ambazo watu wengi bado wanazipenda.

Mungu Amlaze Pema Shakila Tatu Saidi Msengi.

No comments:

Post a Comment