Orchestra Lipua Lipua, ni moja ya bendi za kutoka Kongo ambayo ilipendwa sana na wapenzi wa muziki hapa Tanzania. Nyimbo zao zilianza kusikika nchini kupitia redio na santuri mwanzoni mwa miaka ya 70.
Lipua Lipua ilitokana na bendi iliyoitwa Orchestra Bella Bella kujitoa
kwenye lebo ya Veve, lebo ambayo ilikuwa mali ya mwanamuziki mkongwe
Kiamangwana Mateta Verckys. Bella Bella walipoondoka, kundi jipya la wanamuziki
wakiwemo waimbaji Pepe Kalle na Nyboma Mwandido, Tonton Ricos Kinzunga mpiga
gitaa la solo, Kevin Kayembe Zeus, Mbubi
Malanda, walikuwepo pia Tagar Mulembu Tshibau na Assossa Tshimanga katika jopo la waimbaji, Pierre Bissikita alikuwa mpiga gitaa la rhythm ambaye alipohama
nafasi yake ikachukuliwa na Vata Mombassa, vijana hawa wakaanzisha kundi la Lipua Lipua. Nyimbo zao za kwanza Massale, Lusamba,
Nkoleta, na hasa Mombassa, zilitikisa anga za wapenzi wa muziki wa Kongo hapa nchini kwetu. Wimbo wao ulioitwa Kamale,
ukachaguliwa kama wimbo bora wa Zaire mwaka 1973. Jina la Lipua Lipua
lilitokana na wimbo ulioitwa Lipua Lipua ambao uliimbwa na Orchestra Bella
Bella kabla haijajitengana na Verckys.
Lipua Lipua na Orch Bella Bella
Pamoja na bendi hiyo kuanza vizuri, wanamuziki Pepe Kalle, Makosso, Pierre Bissikita na wenzie wakaihama Lipua Lipua. Pepe Kalle na Makosso wakarudi na kuendelea na bendi yao ya awali ya Empire Bakuba na Bissikita akaenda kuanzisha bendi yake. Na wakati huohuo Lipua Lipua ikampata mpiga gitaa la rhythm mpya aliyekuja kubadili mengi katika upigaji wa gitaa hilo, si mwingine alikuwa Vata Mombassa. Baada ya bendi hiyo kutoa vibao kama Niki Bue na Fuga Fuga, pengo la Pepe Kalle na wenzie walioondoka likasahaulika kabisa na Lipua Lipua ikaendelea na umaarufu wake kwa kutoa nyimbo nyingi nzuri. Mwaka 1975 Lipua Lipua ikapata pigo jipya. Mulembu Tshibau, Tonton Ricos, Nyboma Mwandido, Tchimanga Assosa wakaaicha bendi hiyo na kuanzisha Orchestra Les Kamale. Ikumbukwe jina la Kamale lilitokana na wimbo ambao Orchestra Lipua Lipua iliuimba mwaka 1973.
Kamale na Orchestra Lipua Lipua
Kuondoka kwa wanamuziki hao mabingwa hakukuiteteresha Lipua Lipua, wanamuziki wengine waliokuja kutetemesha anga za muziki walijiunga na bendi hiyo. Kiloto Toko, Luswama Aspro, Santana Mongoley. Lakini mtu aliyekuja kung’aa zaidi alikuwa mwanamuziki aliyeitwa Paul Nzayadio maarufu zaidi kwa jina la Nzaya Nzayadio. Nzaya ndie akawa muimbaji kiongozi wa Lipua Lipua. Nyimbo kali sana kama Mbondo, Matoba, Sekizenge, Namona Ya Wapi, and Mfueni ziliipaisha Lipua Lipua, nyimbo hizo zilisindikizwa na sauti nzito ya Nzaya Nzayadi, na kubembelezwa na Vata Mombassa kwenye gitaa la rhythm, hakika wapenzi wa muziki huo mpaka leo bado wanafurahia vibao hivyo.
Kuanzia
mwaka 1980 bendi ikaanza kupoteza umaarufu, hapa kuna somo kubwa kwa wanamuziki
maarufu kuwa hawatakuwa maarufu milele. Wapenzi wa Lipua Lipua wakahamisha
upenzi wao kwenye bendi kama Empire Bakuba, Viva La Musica, Zaiko Langa Langa
na bendi nyingine za vijana wakati huo. Lipua Lipua iliendelea kupiga muziki lakini kufika mwaka
1984 bendi ikasimama rasmi. Nimalizie kumbukumbu hii kwa kumkumbuka muimbaji wa
sauti ya kwanza aliyekuweko Orchestra Bella Bella na kisha kuwa mwanzilishi wa
Orchestra Lipua Lipua japokuwa baadae aliiacha bendi hiyo na kuwa mwanzilishi
wa bendi ya Orchestra Kamale nae ni Nyboma Mwan'dido.
Nyboma alizaliwa kijiji cha Niokoi kilichoko Maindombe nchini Kongo, tarehe 24 Disemba 1952, siku moja kabla ya Krismas. Alipofika umri wa miaka 16 akaanza kuimbia bendi ya Negro Success, lakini kifo cha kiongozi wa bendi hiyo Bavon Marie Marie kilisababisha bendi hiyo kusambaratika taratibu. Nyboma akajiunga na Orchestra Bella Bella na mwaka 1972, Nyboma akarekodi wimbo wa Mbuta, wimbo ambao ulikuja kuwa wimbo wa mwaka nchini Zaire mwaka 1972.
Kama nilivyohadithia
hapo juu, mwezi Machi mwaka 1973, Nyboma na wenzie wakawa waanzilishi wa
Orchestra Lipua Lipua.
Wapiga gitaa
la rythm wengi wa miaka ya 70 hukiri kuwa walitumia nyimbo za Lipua Lipua
zilizopigwa na Vata Mombassa kama darasa lao la kujifunza kupiga gitaa hilo.
Bendi nyingi ziliiba vipande vya gitaa la rhythm vilivyopigwa na Vata Mombassa
na kuviunganisha kwenye nyimbo zao. Pia Vata Mombassa alifanya wapiga gitaa
hilo la rhythm kubadili upigaji kwa kufunga nyuzi za gitaa lao katika mtindo wa
kufunga uzi namba moja badala ya namba nne katika gitaa hilo na kuleta aina
mpya ya sauti katika upigaji wa gitaa la rhythm.
Lipua Lipua
ilikuwa na wapiga gitaa la solo wazuri sana wawili, Tonton Ricos Kinzunga,
ambaye baada ya kuhama bendi hiyo nafasi yake ikachukuliwa na Luswama Aspro,
staili ya upigaji wa wanamuziki hawa wawili iliigwa na wapigaji wengine Afrika
nzima. Nyimbo nyingi zilitungwa na
vipande vya solo zilizotungwa na mabingwa hawa wawili zilinakiliwa na kuingizwa
kwenye nyimbo nyingi za bendi mbalimbali Afrika. Hakika hakuna sifa kubwa zaidi
kuliko hiyo kwa bendi ya Lipua LIpua.
No comments:
Post a Comment